Sunday, 16 February 2020

Watumishi Wa Maliasi Watakiwa Kuhamishia Ofisi Katika Maeneo Ya Hifadhi Ili Kulinda Maliasili

...
NA TIGANYA VINCENT
WATUMISHI wa Mamlaka na Wakala zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wametakiwa kuhamia katika maeneo ya hifadhi ili kulinda na kuzuia uharibifu wa maliasili kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.

Kauli hiyo imetolewa  na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Tabora , Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori(TAWA), Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi na Hifadhi za Taifa(TANAPA) kwenye ziara yake ya kikazi.

Alisema Taasisi zote zinahusika na usimamizi na ulinzi wa  maliasili zinatakiwa kujenga Ofisi ndani ya Hifadhi na watumishi kuhamia huko ili iwe rahisi kukabiliana na uharibifu wowote unaotaka kufanyika.
Dkt. Kigwangala aliongeza katika Ofisi zilizopo nje ya hifadhi wabaki watumishi wachache ikiwemo Watendaji wakuu na waliobaki waende porini kwa kuwa tayari walishapata mafunzo ya jinsi ya kupambana na waharibifu wa maliasili.

"Hatuwezi kulinda maliasili tukiwa maofisini ...ni lazima tujenge post kwenye hifadhi zetu na watumishi wahamie huko wakalinde maliasili zetu , ofisi wabaki wachache ikiwemo viongozi wa Kanda... wao watakwenda kukagua utendaji kazi wa watumishi wanaowasimamia" alisisitiza

Alisema ni jukumu lao kuhakikisha maliasili zilipo ikiwemo wanyamapori , ndege na mimea inalindwa kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho na kuhakikisha wanazuia uharibifu wowote ndani ya Hifadhi nchini.

Waziri huyo alisema kuwa Kanda ya Magharibi ndio pekee imebaki na mistu mingi ya asili ni vema watendaji wanaohusika kulinda na kuhifadhi wakahakikisha haiendelei kuharibiwa.

Katika hatua nyingine Dkt. Kigwangala ametoa siku 14 kwa Taasisi zilizopo chini Wizara ya Maliasili na Utalii katika kanda ya Magharibi kukaa pamoja na kuanisha mipaka halisi ya Hifadhi mpya za Taifa, mapori ya akiba na Hifadhi ya Mistu  na maeneo ya wananchi ili kuondoa mwingiliano na migogoro.

Alisema kumekuwepo na mlingiliano ambao umetokana na baadhi ya maeneo ya hifadhi moja kusomeka katika eneo jingine la hifadhi na kuleta utata.

Aidha Dkt. Kigwangala alizitaka Taasisi hizo kuhakikisha wanaweka upya mipaka katika Msitu wa Hifadhi wa Ulyankulu ambapo kuna sehemu ambayo wananchi wameshavamia na kufanya makazi na kujenga huduma mbalimbali.

Alisema mipaka hiyo itasaidia wananchi kuendelea kuingia katika msitu huo na kuendesha shughuli mbalimbali ambazo zinatishia uendelevu wa msitu huo.

Mwisho


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger