MWANDISHI WETU MUSOMA
Wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Mara wameelezea kero mbalimbali zinazochangia kukwamisha ukuaji wa uwekezaji mkoani humo ikiwemo tatizo la umeme na wengine kueleza changamoto za utitiri wa kodi.
Wameeleza changamoto hizo Februari 24, 2020 wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara wa mkoa wa Mara uliohusisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka Sekta mbalimbali ikiwemo Viwanda na Biashara na masuala ya Fedha wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki uliofanyika Wilaya Musoma Mjini katika Mkoa wa Mara.
Lengo la mkutano huo lilikuwa kusikiliza changamoto na kero wanazokabiliana nazo katika maeneo yao ya biashara na uwekezaji na kuzitatua, ambapo wameeleza namna utitiri wa kodi na kukatikatika kwa umeme kunavyochangia uzorotaji kwa ukuaji wa uchumi na kuiomba Serikali kushughulikia tatizo hilo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Wafanyabiashara hao walieleza kuwa, kukosekana kwa umeme wa uhakika umekwamisha shughuli za uzalishaji ikiwemo zile za viwandani.
Kufuatia hali hiyo wameiomba Serikali kutatua kero hiyo huku wengine wakibainisha hasara wanazopata katika changamoto hiyo.
Akieleza changamoto za uwekezaji Dkt. John Changwa alieleza kuwa, TANESCO imechangia kukwamisha uzalishaji katika viwanda kutokana na umeme kukatika mara kwa mara pamoja na kutofika kwa wakati katika viwanda vidogo kwa kuhusisha changamoto ya miundombinu hafifu ikiwemo barabara.
“Ni kweli kabisa TANESCO hamtutendei haki kwani mmekuwa mnatukwamisha kwa muda mrefu na mmeshindwa kufika kwa wakati hasa katika maeneo vinavyojengwa viwanda huku vikiwa vihitaji huduma za umeme hivyo ni vyema mkabadili utaratibu na kuona namna ya kutufikia kwa wakati,”Alieleza Dkt. Changwa
Akijibu baadhi ya kero hizo kwa kushirikiana na mawaziri wengine Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki ametumia fursa hiyo kuzikumbusha Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maamuzi ya Serikali kwa kuhakikisha changamoto zilizoainishwa ikiwemo utitiri wa kodi, uwepo wa riba kubwa zinazotozwa na benki, ucheleweshwaji wa vibali vya ajira, ukosefu wa ajira kwa vijana, na uvuvi wa kutumia vyavu zisizokidhi mahitaji halisi na bei elekezi kuwa juu.
‘’Ni wakati sahihi kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha tunatatua na kumaliza kero zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara ili kuendelea kuwa na maendeleo katika nchi yetu na niwahakikishie Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwa na tija inayotakiwa,”alisema Waziri Kairuki.
Sambamba na hilo alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na Serikali katika ulipaji wa kodi mbalimbali kwa utaratibu uliopo na kuhakikisha wanachangia katika ukuaji wa pato la taifa.
“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inasisitiza ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya watanzania na taifa kwa ujumla hivyo lazima tuzingatie na kutimiza wajibu wetu ili kuepuka kuingia katika makosa yasiyo ya lazima na kupelekea uwekezaji wenu kuwa wa hasara”,alisisitiza Waziri Kairuki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima alimhakikishia Waziri kuendelea kutatua kero na changamoto katika mkoa wake ili kuwahakikishia mazingira rafiki ya uwekezaji wao huku akiahidi kuendelea kusimamia sheria zote zinazowahusu ili kuwa na tija katika kuwekeza mkoani humo kwa kuzingatia fursa zilizopo.
“Mkutano huu umekuwa wa faida sana kwa kuzingatia umetoa fursa kubwa kwa kuwakusanya wafanyabiashara na wawekezaji 400 kwa pamoja na kuweza kuzieleza kero zao, tunaahidi kero ambazo hazijapatiwa majibu kwa siku ya leo zitatatuliwa haraka iwezekanavyo,”Alisisitiza Mhe. Malima.
0 comments:
Post a Comment