Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kuanza kupanga maeneo ya uwekezaji katika sehemu ambazo miji inakuwa kwa kasi.
Dkt Mabula alisema hayo jana katika mkutano wa Mashauriano baina ya Serikali na sekta binafsi kuhusiana na changamoto za uwekezaji katika mkoa wa Simiyu.
Alisema, kuna maeneo mengi nchini ambayo miji inaendelea kwa kasi hivyo halmashauri kupitia Wakurugenzi wake zinapaswa kuhakikisha zinatenga maeneo ya uwekezaji kwa lengo la kumuwezesha Mwekezaji atakapopatikana asipate tabu.
‘’Ni vizuri katika kipindi hiki ambacho baadhi ya miji inakuwa kwa kasi halmashauri zikatenga maeneo ya uwekezaji na kuyahaulisha kwa lengo la kuwarahisishia wawekezaji watakapokuja kuwekeza katika halmashauri husika’’ alisema Mabula
Aidha, Naibu Waziri Mabula amezitaka pia halmashauri kuhakikisha zinapanga miji maeneo yaliyopo pembezoni kwa kuanishwa matumizi yake kama vile kilimo, ufugaji na maeneo ya kuchezea kwa kutumia watendaji wa ngazi za chini badala ya kusubiri wataalamu wa mipango miji.
Alisema, upangaji miji mapema kwa kutumia watendaji wa ngazi za chini utasaidia wataalamu wa mipango mijini watakapokuja baadaye kutopata shida katika kupanga maeneo hayo hasa katika ile miji inayokuwa kwa kasi kwa kuwa miji hiyo itakauwa imepangwa na kuainisha matumizi mbalimbali.
‘’Hawa watendaji wa chini wakipewa elimu wataweza kuipanga miji yao kama ilivyokuwa wakati wa vijiji vya ujamaa maana sasa hivi mtu anaweza kujenga kiwanda katikati ya makazi ya watu’’ alisema Mabula.
Katika mkutano huo Manaibu Mawaziri kutoka sekta mbalimbali walitolea ufafanuazi baadhi ya changamoto zilizowasilishwa kwao kwa lengo la kurahisisha ufanyaji biashara itakaokuwa na tija.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Ashatu Kijaji alitoa ufafanuazi wa riba kubwa kwa taasisi na fredha na kubainisha kuwa serikali ya awamu ya tano imesikia kilio hicho na imekuwa ikisisitiza taasisi hizo kupunguza riba kufikia asilimia kumi na moja.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Musa Sima alisema lengo la serikali si kufungia biashara bali ni kutafiuta njia itakayowawezesha wawekezaji kufanya biashara katika mazingira mazuri na kubainisha kuwa mtendaji wa ofisi yake atakayekwamisha jitihada hizo basi taarifa itolewe ili hatua zichukuliwe.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa alisema, wizara yake inafanya jitihada kubwa kuunganisha mikoa katika masuala ya miundombinu sambamba na kushughulikia maeneo korofi ili wawekezaji wafanye kazi zao kwa urahisi.
Mnaibu Mawaziri wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Viwanda na Bishara Stela Manyanya, Maliasili na Utalii Constatntine Kanyasu na kiongozi wa mkutano huo Angela Kairuki Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji.
PICHA: Wizara ya Ardhi
PICHA: Wizara ya Ardhi
0 comments:
Post a Comment