Kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa chama cha walimu Tanzania CWT utakao anza mapema mwezi Februari hadi Mei mwaka huu , Rais wa Chama hicho Mwalimu Leah Ulaya amewatahadharisha wanachama watakao gombea kujiepusha na vitendo vya rushwa na atakayekiuka maadili ya chama kuhusu uchaguzi atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kunyang'anywa ushindi
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Februari 16,2020 Jijini Dodoma katika Makao Makuu ya Chama hicho, Ulaya amesema kuwa chama kinapinga kwa nguvu zote matumizi ya fedha ,Rushwa na uvunjaji wa Maadili .
“Nitoe wito wanachama wote wa Chama cha Walimu Tanzania[CWT]kuwa ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika uchaguzi wa viongozi mbalimbali Wa CWT ila nitahadharishe tu katika masuala ya rushwa katika uchaguzi huu na rushwa ni adui wa haki hivyo ni lazima tupinge kwa nguvu zote,na kingine ambacho nataka niwasisitize Walimu wenzangu ni kuendelea kuilinda amani na uzalendo kwa nchi yetu”amesema.
Akitoa Ratiba ya Uchaguzi huo , Katibu Mkuu wa CWT Mwalimu Deus Seif , amesema kwa Mujibu wa katiba ya CWT chama kinawataka kufanya chaguzi zao kila baada ya Miaka mitano hivyo, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi kwa chama chao.
“Ngazi ya Tawi [sehemu ya kazi]utachaguzi unafanyika kuanzia tarehe 15-27 Februari ,2020 ,chaguzi hizi zitafanyika katika shule,vyuo vya ualimu[TTC],Vyuo vya maendeleo ya Jamii[FDC’s]Wizara na Taasisi mbalimbali zenye wanachama pamoja na taasisi zilizo ngazi ya wilaya zinazojumuisha ofisi za Elimu za wilaya na waratibu wa elimu ngazi kata”amesema.
Katika ngazi ya wilaya uchaguzi utafanyika kuanzia Tarehe 16 -27 Machi,2020 na ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu itapangwa na kamati ya uendeshaji ya wilaya husika.
Ameendelea kufafanua kuwa uchaguzi ngazi ya Mkoa utafanyika kuanzia Tarehe 20 -30 April,2020 na ratiba ya uchukuaji na kurejesha fomu itapangwa na kamati tendaji ya mkoa.
Akizungumzia kwa ngazi ya Taifa Seif amesema mkutano mkuu wa Taifa utafanyika Mei 27-28 mwaka huu,ambapo uchaguzi wa ngazi ya Taifa utafanyika tarehe 28 Mei mwaka huu na wagombea watajulishwa mahali pa mkutano kabla ya mkutano mkuu wa uchaguzi huku utaratibu wa kuwa na wawakilishi wa makundi Maalumu kama vile walimu wanawake na walimu wenye ulemavu watapewa kipaumbele zaidi.
Nafasi zinazogombewa ambapo ngazi ya tawi [sehemu ya kazi]katibu wa chama,ngazi ya Wilaya ni Mwenyekiti wa CWT Wilaya,Mweka hazina CWT Wilaya,mwakilishi wa walimu wanawake CWT Wilaya,mwakilishi wa Walimu wenye ulemavu CWT wilaya, mwakilishi vijana[miaka 18-35]CWT wilaya, na wawakilishi wa walimu wanaofundisha shule za awali,msingi,sekondari,shule/vyuo vya serikali,vyuo vya walimu,vyuo vya maendeleo ya jamii[FDC’s]na Taasisi za elimu za serikali zinazowajumuisha waratibu wa elimu kata,waratibu wa TRC’s na walimu maafisa ngazi za wilaya.
Nafasi zinazogombewa ngazi ya mkoa ni mwenyekiti CWT mkoa,mweka hazina CWT mkoa,mwakilishi wa walimu wanawake CWT mkoa,mwakilishi wa walimu wenye ulemavu CWT mkoa, mwakilishi wa vijana CWT mkoa,mwakilishi wa wenyeviti wa wilaya kwenye baraza la Taifa,mwakilishi wa mkoa kwenye kamati tendaji ya Taifa na wawakilishi wa CWT Kwenye vikao vya TUCTA .
Na nafasi zinazogombewa ngazi ya Taifa ni Rais wa Chama,Makamu wa Rais,Katibu Mkuu,Naibu katibu mkuu,Mweka Hazina wa Taifa,mwakilishi wa walimu wenye ulemavu kwenye kamati tendaji ya taifa ,mwakilishi wa walimu wanawake kwenye kamati tendaji ya Taifa,mwakilishi wa vijana[18-35] kwenye kamati tendaji ya taifa pamoja na pamoja na wadhamini watatu[3]wa chama.
Hivyo,CWT Kimetoa wito kwa wanachama wake hasa wanawake walimu na wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali huku wakiwashauri wanachama kusoma kwa makini katiba ya CWT Toleo la 6 la mwaka 2014,kanuni za chama Toleo la 4 la mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment