Na Salvatory Ntandu - Kahama
Tatizo la kufuata huduma za matibabu umbali mrefu kwa wakazi wa kata ya kinamapula katika halmashauri ya Ushetu limetajwa kuchangia akinamama wajawazito kujifungulia njiani hali ambayo huhatarisha usalama wao na watoto wao.
Kauli hiyo imetolewa na Magdalena bundala mkazi wa kijiji butibu mbele ya kamati ya siasa ya Chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya kahama mkoani shinyanga ambayo imefika katika kijiji hicho kwa lengo la kukagua ujenzi wa zahanati mpya ya kijiji hicho uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 174.
“Akinamama wengi hujifungulia njiani kutokana na kutembea umbali mrefu wa kilomita 12 kwenda zahanati kijiji cha kisuke kupata matibabu na wakati mwingine hulazimika kukodi pikipiki kwa shilingi elfu 10000 kwa nyakati za usiku na kwa kipindi cha mvua za masika bei hupanda zaidi alisema”alisema bundala.
Alisema kuwa Kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia kuondoa adha hizo walizokuwa wanazipata pindi wanapokuwa wanahitadi huduma za matibabu hususani kwa akinamama na watoto ambao ndio mara nyingi hukumbwa na magojwa mbalimbali.
Nae Elizabeth Maziku mkazi wa kijiji cha Butibu alisema kuwa kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wamekuwa wakipata shida kwenda kufuata dawa kutokana na umbali mrefu na wakati mwingine hulazimika kuacha dozi kama wanavyoelekezwa na wataalam.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kusikiliza kilio chetu cha muda mrefu cha kupata zahanati tunaimani tutapata huduma zote za kitabibu hapa ikiwemo dawa za watu wanaishi na virusi vya ukimwi ambazo tulikuwa tunalazimika kuzifuata katika zahanati ya kisuke ambayo ni mbali”alisema Maziku.
Kwa upande wake Kaimu mganga mkuu wa Halmashauri ya Ushetu Dk Nikodemas Senguo alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo umegharimu shilingi milioni 174 na unatarajiwa kukamili mwezi wa tatu mwaka huu fedha ambazo zimetolewa na serikali ya watu wa Japan.
“Niwatoe hofu wananchi wa kijiji hiki pindi ujenzi huu utakapo kamilika tuanza kutoa huduma za matibabu mara mmoja ili kuwasogezea huduma karibu wananchi “alisema Dk Senguo.
Nae katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya kahama Emanuel Mbamange alimtaka mkandarasi anayejenga zahanati hiyo kuhakikisha anajenga kwa kuzingatia ubora ili majengo hayo yaweze kudumu kwa muda mrefu na huduma kwa wananchi zianze kutolewa.
“Serikali ya awamu ya Tano chini ya Dk John Pombe Magufuli imelenga kusogeza huduma karibu na wananchi ndio maana sisi wasimamizi wa Ilani ya CCM tuko hapa kuangalia utekelezaji wake katika miradi mbalimbali ya maendeleoa katika halmashauri hii”alisema Mbamange.
Aliongeza kuwa Mwaka huu CCM inadhimisha miaka 43 ya kuzaliwa kwake kwa kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yote iliyoainishwa kwenye Ilani yake katika maeneo mbalimbali ili kuona utekelezaji wake.
Maadhimisho ya miaka 43 ya CCM yanakwenda na kauli mbiu isemayo “tumeahidi,tumetekeleza na tunaahidi tena kuchapa kazi kwa juhudi,ubunifu na maarifa zaidi”.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment