Rwanda imepinga shinikizo kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kutaka uchunguzi huru kufanywa kuhusu kifo cha msanii maarufu wa muziki wa kiinjili Kizito Mihigo, ambaye alifariki katika kituo cha polisi Jumatatu asubuhi.
Alifariki siku tatu baaada ya kukamatwa karibu na mpaka wa Burundi, polisi wakimtuhumu kwa jaribio la kutaka kutoroka nchi na kujiunga na la waasi linalopigana dhidi ya serikali ya Rwanda.
Bw. Mihigo alipigwa marufuku kuondoka nchini Rwanda kutokana na mashitaka yaliyopita dhidi yake.
Msemaji wa shirika la upelelezi la Rwanda, Marie Michelle Umuhoza, ameiambia BBC kwamba "Rwanda ni nchi huru inayojitawala na ambayo ina uwezo wa kuchunguza kitu chochote".
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch, Amnesty International na Commonwealth Human Rights Initiative yamekuwa yakishinikiza kufanyika kwa uchunguzi huru wa kubaini mazingira yaliyosababisha kifo cha mwanamuziki huyo aliyekuwa na miaka 38- amabaye alizoa umaarufu kutokana na ujumbe wake wa amani na maridhiano.
Siku ya Jumatatu, polisi ya Rwanda ilitangaza kuwa alijinyonga akiwa kizuizini.
Afisa wa Human Rights Watch ameiambia BBC kwamba uchunguzi huru utaangalia kamera za siri katika eneo ambalo msanii huyo alikuwa anazuiliwa.
Lakini Umuhoza amesema Rwanda tayari inafanya uchunguzi kuhusu kifo chake.
"Sioni haja ya kufanyika kwa uchunguzi huru, katika nchi huru", alisema
0 comments:
Post a Comment