Friday, 7 February 2020

Makondo Ataka Mabadiliko Ya Kiutendaji Wizara Ya Ardhi

...
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo amewataka watumishi wa sekta ya ardhi katika Wizara hiyo kushirikiana ili kuibadilisha Wizara na kuwa na utendaji bora utakaokidhi mahitaji ya wananchi.

Makondo alisema hayo jana wakati akizungumza na watumishi wa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipowasili kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.

Makondo alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Dorothy Mwanyika aliyestaafu kwa mujibu wa Sheria. Kabla ya Uteuzi huo Makondo alikuwa Kamishna wa Ardhi kwenye Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Alisema, mategemeo ya watumishi wa Wizara ya Ardhi mara baada ya kuteuliwa kwake ni makubwa lakini msisitizo wake ni watumishi hao kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma ili kuweza kuibadilisha Wizara.

‘’Kauli ya Wizara kuwa ina ‘madudu’ siyo nzuri hivyo tukimbie ili tuwe na sekta ya ardhi iliyobadilika’’ alisema Makondo.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitaka kuthaminiwa kwa mchango wa kila mtumishi wa Wizara hiyo kwa kuwa ndiyo njia pekee itakayoleta mabadiliko na mafanikio ya utendaji kazi wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Makondo, Kampuni ya utengenezaji magari ya Toyota imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye biashara zake kutokana na kutumia mfumo wa Kaizen unaothamini mchango wa kila mmoja katika utendaji kazi.

Makondo amewataka pia watumishi wa Wizara ya Ardhi kuweka miakakati ya pamoja kwa lengo la kuibadilisha wizara hapo ilipo ili kuonesha kuwa wizara hiyo imebadilika katika utendaji wake.

Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi walioneshwa kufurahishwa na uteuzi wa Katibu Mkuu huyo kwa kuwa ametokea Wizara hiyo na anaijua sekta ya ardhi vizuri pamoja na watumishi wake.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger