Tuesday, 18 February 2020

Kampeni Ya Elimu Kwa Mlipakodi Yawafikia Wafanyabiashara Iringa

...
Na Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea na kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambapo kwa sasa inafanya kampeni hiyo katika Mkoa wa Iringa na wilaya zake ikitoa elimu ya kodi kwa kuwatembelea wafanyabiashara mbalimbali kwenye biashara zao.

Akizungumzia kampeni hiyo, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi Bi. Rose Mahendeka alisema kuwa TRA imejipanga kuwafikia wafanyabiashara mahali walipo ili kuwapatia elimu ya kodi ikiwa ni pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

“Leo tumeanza kampeni ya elimu kwa mlipakodi hapa mkoani Iringa na tumeanza na Wilaya ya Kilolo na baadae tunaelekea Mufindi na Iringa mjini. Licha ya kuwaelimisha wafanyabiashara masuala mbalimbali ya kodi lakini pia tunapokea maoni yao, mrejesho na changamoto za ulipaji kodi walizonazo kwa lengo la kuzitatua”, alisema Bi. Mahendeka.

Bi. Mahendeka aliongeza kuwa elimu inayotolewa katika kampeni hiyo ni pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za biashara, ulipaji wa kodi ya pango kwa mfumo wa kodi ya zuio, kodi ya majengo, makadirio ya kodi na faida za kulipa kodi kwa ujumla.

“Tunataka kuongeza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari na ili kujenga ridhaa hiyo ni muhimu tuwafundishe wafanyabiashara sheria, wajibu na haki zao kuhusu ulipaji kodi ikiwa ni pamoja na namna ya kutunza kumbukumbu za biashara zao, kuzia kodi ya pango na kuiwasilisha TRA, kulipa kodi ya majengo kwa wakati n.k. Tuna uhakikia hii itawaongezea uelewa wa masuala ya kodi na hatimaye wataweza kulipa kodi stahiki kwa hiari”, Aliongeza.

Timu ya Maafisa wa TRA imepanga kuyafikia maeneo ya Miomboni, Migoli na Mtera yaliyopo Iringa mjini, na kwa upande wa Wilaya ya Kilolo maeneo ya Kilolo mjini, Kidabaga, Ilula na Ruaha - Mbuyuni yatafikiwa wakati katika Wilaya ya Mufindi kampeni ya elimu kwa mlipakodi itawafikia wafanyabiashara wa maeneo ya Mgololo, Igowelo, Nyororo na Mafinga mjini.

Kampeni hiyo ya elimu kwa mlipakodi katika Mkoa wa Iringa imeanza leo tarehe 17 na inatarajia kumalizika tarehe 22 Februari, 2020 ambapo TRA imepanga kuwafikia wafanyabiashara 1000 katika mkoa huo.

Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger