Vurugu na mvutano mkali
umeibuka jana kati ya mgambo wa jiji la Mwanza na wamachinga wanaofanya
biashara katika eneo la Makoroboi baada ya kutakiwa kuondoka mahali
hapo.
Eneo hilo lipo katikati ya msikiti unaomilikiwa na watu wenye
asili ya Asia wa Swaminarayan na Shule ya watoto wadogo ya Tample.
Uamuzi huo umekuja wakati tayari Rais John Magufuli alishaonya
kutowavumilia viongozi wa mikoa watakaowaondoa wamachinga kwenye maeneo
yao, kabla hawajawatafutia maeneo mbadala ya kufanyia biashara.
Katika
vurugu hiyo iliyotokea asubuhi jana inadaiwa kuwa mgambo mmoja
alijeruhiwa baada ya kushambuliwa na wamachinga hao wakipinga kuondolewa
eneo hilo.
Hata hivyo, walipotafutwa viongozi husika kuzungumzia tukio hilo hawakupatikana kwa madai wapo kwenye
vikao.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la
Mwanza, Kiomoni Kibamba aliwatangazia wamachinga wote ambao wapo katika
maeneo yasiyo rasmi waondoke kufikia Februari 9, mwaka huu na kwamba
atakayekaidi ataondolewa kwa nguvu.
Wakizungumza katika eneo la tukio,
baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema hatua hiyo ilijitokeza baada
ya kutakiwa kuondoka katika eneo hilo.
“Tulipofika hapa asubuhi tulikuta, sehemu tunayopanga bidhaa zetu kuna mgambo wa jiji wakisema hakuna
mtu kuingia wala kufungua biashara eneo hilo, mgambo walianza
kutufukuza,” alisema Ally Erick.
Shuhuda mwingine alisema kutokana na
hasira waliyoipata watu hao walilazimika nao kujihami kwani mgambo hao
walishindwa kutumia busara baada ya kutaka kuwaondoa kwa kuwapiga
virungu.
Alisema baada ya kuzidiwa walilazimika kuomba nguvu mpya kutoka
kwa askari wa kutuliza ghasia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
alisema yupo kwenye kikao na Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Hosiana
Kosiga alisema naye yupo kwenye kikao.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,
Merry Tesha alisema hayupo eneo lake la kazi badala yake atafutwe Mkuu
wa Wilaya ya Ilemela anayekaimu nafasi hiyo, Dk Leonal Masale,hata hivyo
alipopigiwa simu iliita bila kupata majibu.
0 comments:
Post a Comment