Sunday, 5 February 2017

Mawaziri: Mageuzi ya Rais Magufuli Yanazaa Matunda

...


Dodoma, Jumamosi, 4 Februari, 2017
Serikali imesisitiza kuwa, utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha robo ya kwanza yanaakisi dhamira ya kimageuzi iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano. 
Wakijibu hoja zilizotokana na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na maoni ya Wabunge Bungeni leo, Mawaziri wa sekta mbalimbali wamesisitiza kuwa kuna mabadiliko makubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Dhamira ya Rais Iko Wazi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. January Makamba, amesema kuwa ikiwa ni miezi 15 tu madarakani, kuna mabadiliko makubwa katika kila eneo la utendaji wa Serikali ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Alisema hali hiyo inatokana na dhamira safi na ya wazi ya Mhe. Rais Magufuli kuenzi misingi aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 
Waziri Makamba amesema miezi 15 baadaye, na Bunge likiwa linajadili takwimu za robo ya kwanza tu ya Bajeti ya sasa, hata kama wapo watu ambao huenda wameumizwa na mageuzi yanayoendelea, kwa vyovyote vile, hakuna hoja wala ushahidi wa kulalamika kuwa nchi inarudi nyuma.
Biashara Zashamiri
Wizara ya Fedha imetoa takwimu kuonesha kuwa biashara nchini zinashamiri tofauti na baadhi ya watu wanaotumia takwimu za kufungwa kwa baadhi ya biashara hizo. Wakichangia hoja, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Phillip Mpango na Naibu wake, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, wamefafanua kuwa mapato ya Serikali yameongezeka na hali ya biashara inakwenda vyema. 
Akifafanua kuhusu kushamiri kwa biashara nchini, Naibu Waziri Dkt. Ashatu amesema wakati takwimu zinaoonesha kuwepo kwa biashara 4,183 tu zilizofungwa, watanzania wengi zaidi wamefungua biashara. Amesema kuwa takribani biashara 139,554 zimefunguliwa katika mwaka mmoja uliopita. 
Idadi ya Watalii Yaongezeka
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe amesema kuwa,ubunifu wa kodi mpya zilizoanzishwa na Serikali haujapunguza idadi ya wataliinchini. Alisema sekta hiyo inayochangia asimilia 17.5 ya pato la Taifa kwa mwaka
baada ya kuanza kukata kodi mpya ya ongezeko la thamani katika sekta hiyo. 
“Mheshimiwa Spika pamoja na Tanzania kuanza kutoza kodi hii mpaka sasa ninayofuraha kuwajulisha kuwa hatujaona ushahidi wa kodi hii kupunguza idadi ya watalii wanaokuja nchini,” alisema Prof. Maghembe.
Mfumo Mpya wa Mbolea
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Tate Ole-Nasha, amesema Serikali itaanzisha mfumo mpya utakaosaidia kuboresha upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini. 
Amedokeza kuwa, katika mfumo mpya, Serikali itaanza kununua mbolea kwa ununuzi wa pamoja kama ilivyo katika ununuzi wa mafuta. Ameongeza kuwa pia Serikali imebaini changamoto ya kuwepo kwa tozo nyingi katika sekta ya kilimo na kuahidi kuwa itawasilisha Bungeni hoja ya kupunguza baadhi ya kodi hizo. 
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger