Friday, 20 February 2015

MPYA:SERIKALI KUAJIRI WALIMU 35,000 MWAKA 2015/2016 – WAZIRI MKUU

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Februari 19, 2015) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kiwere, mara baada ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu kwenye shule ya sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.

Waziri Mkuu alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji yaliyokwishawasilishwa na kwamba watakapopata mgao wao
hawana budi kuziangalia kwanza shule zenye miundombinu iliyokamilika kama ilivyo kwa shule hiyo.

Akifafanua kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara Waziri Mkuu alisema: “Mkoa mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318 na zilizo tayari mpaka sasa ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika,” alisema.

“RC inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo bado hazijaanza kujengwa zikamilike kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameelekeza. Alisema hataongeza tena muda wa ujenzi,” aliongeza.

Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN).

Waziri Mkuu aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.

Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Elimu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Leonard Msigwa alisema ujenzi wa nyumba hizo nne ambazo zina pande mbili (four duplex houses) umegharimu sh. milioni 323.2. Alisema nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala, sebule na jiko, zina uwezo wa kubeba familia nane.

Bw. Msigwa alisema ujenzi wa nyumba ulifanywa shirika la DESWOS la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na wananchi. Pia walisaidiwa kujengewa tenki la maji na mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 112 kila moja kwa ajili ya wasichana.

Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Afisa Elimu huyo alisema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na Baiolojia lakini bado viko kwenye hatua ya kupaka rangi. Alisema mfumo wa gesi na maji umekwishafungwa ndani ya vyumba vya maabara.

“Ujenzi wa maabara hadi sasa umekwishagharimu sh. milioni 52.8/- na katika kipindi cha Februari 2015, tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya samani za maabara yaani meza 24 na stuli 96 zenye thamani ya sh. 8,940,000/-,” alisema.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger