Saturday 20 July 2019

Trump: Kwa sasa hatuna mapango wa kuiwekea vikwazo Uturuki

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa, kwa sasa serikali ya Washington haina mpango wa kuiwekea vikwazo Uturuki.

Trump ameyasema hayo  kufuatia mzozo ulioshtadi kati ya nchi yake na Uturuki na kuongeza kuwa, kwa sasa hana mpango wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Hayo yanajiri ambapo Ikulu ya Marekani White House siku ya Alkhamisi ilitangaza kuwa, kwa kuzingatia hatua ya Uturuki ya kununua mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia, ni suala lisilowezekana kuiuzia tena serikali ya Ankara, ndege za kivita aina ya F-35.

Aidha serikali ya Uturuki pia imetoa kauli   kufuatia msimamo huo wa Washington ambapo İbrahim Kalın, Msemaji wa Rais Recep Tayyip Erdoğan amenukuliwa akisema kuwa, Ankara haijafurahishwa na hatua ya Washington ya kuiondoa nchi hiyo kwenye orodha ya pamoja ya kuunda ndege za kivita za F- 35.

Kabla ya hapo yaani tarehe 16 Julai mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alisema kuwa, hatua ya Uturuki ya kununua ngao ya makombora ya S -400 ya Russia, imeifanya Washington kufuta mpango wa kuiuzia nchi hiyo ndege zake za kivita za F 35.

Mkataba wa mauziano ya ngao ya makombora ya S-400 wa kiasi cha dola bilioni 2.5 kati ya Russia na Uturuki, ulitiwa saini Disemba 2017.


Share:

Waziri Mkuu: Nitamtuma Waziri Mhagama Aje Makanya .....Ni Katika Mashamba Ya Mkonge, Apokea Kilio Cha Wafanyakazi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama aende Makanya, wilayani Same, kwenye mashamba ya mkonge akatatue kero za wafanyakazi.

“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, manake watumishi wameweka malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona wanaoendesha mitambo hawana gloves, wengine wamevaa kandambili badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu…” alisema Waziri Mkuu.

Ametoa ahadi hiyo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro, mara baada ya kukagua uzalishaji kwenye kiwanda hicho.

Alifikia uamuzi huo baada ya kusoma mabango yaliyokuwa yakitoa ujumbe juu ya hali mbaya kiwandani zikiwemo malipo ya sh. 3,800 kwa siku; mikataba mibovu ya kazi; wafanyakazi kutothaminiwa wanapougua na kutoridhika na mawakala wawili ambao ni UNIQUE na UPANI waliowekwa kusimamia uendeshaji wa shamba hilo. UNIQUE inasimamia wakata mkonge na UPANI inasimamia kazi ya upandaji na upanuzi wa mashamba.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alimweleza Meneja wa Mashamba ya METL likiwemo la Hasani, Bw. Ndekiwa Nyari kwamba uamuzi wa kuweka mawakala unawapunguzia wenye kampuni mzigo wa usimamizi kwenye mashamba lakini unaipa hasara kampuni yao.

“Kwa sasa unashughulika na watu watatu au wanne ambao ni mawakala wakati watu wote wanaokuzalishia wako hapa. Ni vema ungeajiri hao watu wanne, ukawasimamia kwa karibu na unaweza kuwapa motisha wakifanya vizuri au kuwafukuza wakiharibu. Lakini kwa sasa hawa mawakala huna mamlaka hayo, sababu ulishaweka mkataba nao,” alisema.

“Ni bora uwe na idara mbili za upandaji na uvunaji, kisha uweke wasimamizi watatu au wanne ambao watawajibika kwako moja kwa moja. Hii system uliyotumia ina walakini hasa kwenye maslahi ya wafanyakazi. Unawalipa fedha lakini haifiki yote kwa wafanyakazi,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyakazi hao.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Makanya wajipange na kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili nao waanze kulima mkonge ambao alisema watakuwa wanauuza kwenye kiwanda hicho.

“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji jirani ingieni kwenye kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na nje ya nchi. Tafuteni maeneo ya ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha mkonge sasa. Zao hili lipo kwenye mazao ya nyongeza ya mkakati ambayo ni chikichi na mkonge.”

“Na uzuri wake unalima mara moja tu, halafu kila mwaka unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji simamieni jambo hili,” alisisitiza.

Mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na korosho.

Mapema, akitoa taarifa juu ya uzalishaji kwenye kiwanda hicho, Bw. Nyari alisema shamba lote lina ukubwa wa ekari 2,453 na kwamba uzalishaji umekuwa ukiongezeka kidogo kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani za mkonge 713 na hadi kufikia mwka 2018 walifikisha tani 890 za mkonge. “Mwaka huu tunatarajia kufikisha tani 1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge limeongezeka,” alisema.

Alisema moja ya changamoto inayowasumbua ni tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge mchanga hali ambayo alisema inaua miche hiyo michanga.

Aliitaja changamoto nyigine kuwa ni ukosefu wa maji ya uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha singa za katani ambazo ni safi.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Waziri Mkuu Aagiza Same Sekondari Ipewe Gari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bi. Anna-Clare Shija apeleke gari haraka katika shule ya sekondari ya wavulana ya bweni ya Same ili kumsaidia mwalimu mkuu endapo kutatokea dharura.

“Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 800 lazima iwe na chombo cha usafiri kitakachotumika kwa dharura za kuwapeleka hospitali wanafunzi pale wanapougua. Sasa hivi mwanafuzi akiugua, Mwalimu Mkuu anafanyaje? Ni kama ameachiwa jukumu hili peke yake,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati alipotembelea shule hiyo na kuzindua mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya sekondari ya Same na kisha kuzungumza na wanafunzi, walimu na baadhi ya wazazi waliokuwepo.

Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bi. Shija na kumtaka atoe jibu hadharani kwamba ni lini atapeleka gari hilo shuleni hapo. Mkurugenzi huyo aliahidi kulipeleka gari hilo ifikapo Jumatatu jioni (Julai 22, 2019).

“Haya maelekezo ni kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wenye shule ambazo zina wanafunzi zaidi ya 700. Mnapaswa kuhakikisha kunakuwa na gari la shule ili ikitokea dharura, Mkuu wa Shule aweze kuingilia kati na kupata ufumbuzi.”

“Wakurugenzi mnatakiwa kutambua shule hizi ni zenu, kwa hiyo mnalo jukumu la kuzihudumia. Shule hii ya Same ina wanafunzi zaidi ya 800 na wanalala hapa hapa, ni lazima kuwe na gari la kuwahudumia hasa wakati wa dharura.”

Pia amemuagiza Mkurugenzi huyo atafute daktari na muuguzi mmoja na awapangie kwenye shule hiyo ili waweze kutoka huduma kwa wanafunzi na kuwapunguzia adha ya kwenda mjini kutafuta huduma hiyo.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kupokea changamoto zilizowasilishwa na kijana Omary Said wa kidato cha sita mchepuo wa PCB ambaye alisema shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji; uchakavu wa mabweni; ukosefu wa zahanati ya shule na uhaba wa walimu wa sayansi hasa wa masomo ya fizikia.

Mapema, akitoa taarifa ya ukarabati, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Hoza Mgonja alisema ukarabati huo ambao umegharimu sh. milioni 919, ulifanikisha ukarabati wa majengo saba ya madarasa yenye vyumba 22; maabara tatu, vyoo viwili vyenye matundu tisa; jengo moja la walimu; maktaba yenye vyumba viwili na ofisi mbili; vyoo viwili vyenye matundu manne na miundombinu ya umeme na majitaka.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 


Share:

Waziri Mkuu Amsimamisha Kazi Mhandisi Wa Maji Same

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Same, Mussa Msangi kwa kosa la kumdanganya kuhusu mradi wa maji aliouzindua leo katika kata ya Hedaru.

Amechukua uamuzi huo jana jioni (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Hedaru mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Lengeni-Hedaru, wilayani Same.

Waziri Mkuu alibaini kuwepo kwa tatizo wananchi walipoanza kuzomea wakati zikitolewa salaam za utambulisho kwa viongozi alioambatana nao. Kabla hajahutubia, aliamua kumuita Mhandisi huyo aelezee ukweli wa madai ya wananchi kwamba maji yametoka leo kutokana na ujio wake.

"Eleza ni kwa nini nilipofungua maji, hayakuwa na presha ya kutosha na wewe umesema upatikanaji wa maji umefikia zaidi ya asilimia 80?"

Alipoulizwa kwa mwezi wanakusanya kiasi gani cha fedha kutokana na mauzo ya maji hayo, Mhandisi Msangi alijibu kwa mwaka uliopita walikusanya sh. milioni saba tu.

"Haiwezekani kama maji yanatoka, wenye KAMATI wapate shilingi milioni saba. Ni ama maji hayatoki au wanakusanya hela na wanazila."

Alipoambiwa aelezee utendaji wa mradi huo wa maji na kama alikuwa akiufuatilia, alishindwa kutoa maelezo kamili, akidai kuwa leo maji yanatoka kidogo kwa sababu kuna hali ya mawingu. "Mbona kule ndani ulisema zile betri zinasaidia kuvuta maji na kubalance upatikanaji wa maji wakati hakuna jua la kutosha?" alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu aliamua kumuita mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji maji au Kiongozi mwingine yeyote aje atoe maelezo, lakini wote hawakuwepo kwenye mkutano huo. Ndipo akachukua uamuzi wa kuzivunja jumuiya hizo.

"Jumuiya zote za maji nazivunja kuanzia leo, na wahusika wote watafutwe na Jeshi la Polisi. Haiwezekani nipewe kazi ya kuzindua mradi ambao hauna maji," alisema Waziri Mkuu.

"Katibu Tawala wa Mkoa lete wakaguzi wa mahesabu kwenye huu mradi, pia leta Mhandisi mwingine asimamie huu mradi. Huyu arudishwe kwa Waziri wake," alisema.

Waziri Mkuu pia alimwagiza Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu abaki Hedaru na afuatilie utendaji wa mradi huo kisha ampe taarifa.

Wakati akimaliza kutoa maagizo hayo, Katibu wa Jumuiya ya watumiaji maji Hedaru-Masasi (HEWAUA), Bw. Francis Kazen Kiondo aliletwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi, lakini Waziri Mkuu alielekeza apelekwe kituoni akatoe maelezo.

Taarifa zilizothibitishwa zimebainisha kuwa Kata ya Hedaru inazo Jumuiya tatu za watumiaji maji ambao ni Hedaru-Masasi, Lung wana na Mradi wa Kati. Wakazi wa Hedaru wanakadiriwa kufikia 20,000.

Ilibainika kwamba wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Hedaru-Masasi, Bw. Clement Ngoka aliamua kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ya upinzani aliokuwa akipata kwa viongozi wenzake ambao pia wanadaiwa kuwaunganishia maji baadhi ya watu hadi majumbani kwao na fedha zilizolipwa hazijulikani zilipoenda.

Awamu ya pili ya mradi wa maji alioenda kuuzindua Waziri Mkuu, inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika korongo la mto Rangeni ambao ulikamilika Desemba 2018. Chanzo hicho cha mtiririko, kilitarajiwa kuzalisha lita 750,000 kwa siku ili kusaidia maji yanayozalishwa kwenye visima ambayo yana ujazo wa lita 7,500 kwa saa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Hali Ni Tete: Iran Nayo Yakamata Meli ya Mafuta ya Uingereza

Jeshi la Walinzi wa Kimapinduzi nchini Iran limesema limekamata meli  yenye bendera ya Uingereza katika lango la bahari la Hormuz baada ya kukiuka sheria za kimataifa za baharini. 

Hatua hii inakuja wakati kukiongezeka hali ya wasiwasi katika eneo hilo tete la bahari. 

Uingereza imesema Iran imekamata meli  mbili katika eneo la Ghuba huku waziri wake wa mambo ya nje Jeremy Hunt akionya hatua kali za kisasi iwapo suala hilo halitashughulikiwa mara moja. 

"Kutakuwa na 'madhara makubwa'' ikiwa Iran haitaachia meli ya mafuta ya uingereza wanayoishikilia" Amesema  Waziri wa mambo ya kigeni Jeremy Hunt .

''Tunajua wazi kuwa hali hii haitakuwa rahisi kuitatua, kutakuwa na madhara makubwa.

''Hatuangalii suluhu ya kijeshi.Tunatafuta suluhu ya kidiplomasia kutatua hali hii, lakini tunajua tunapaswa kushughulikia.''- Amesema

Amesema wafanyakazi ndani ya meli walikuwa wa mataifa tofauti tofauti lakini hakuna raia wa Uingereza aliyekuwa akifahamika kuwa ndani ya chombo hicho.

''Balozi wetu mjini Tehran anfanya mawasiliano na wizara ya mambo ya kigeni wa Iran kutatua hali hii na tunafanya kazi kwa karibu na washirika wetu wa kimataifa,'' amesema.

Mmiliki wa meli  ya Mesdar ambayo ni miongoni mwa zilizokamatwa amesema wanajeshi wenye silaha waliingia kwenye meli hiyo kwa muda kabla ya kuiruhusu kuondoka. 

Tukio hili linakuja baada ya jana rais Donald Trump wa Marekani kusisitiza kwamba manowari ya Marekani iliidungua ndege ya Iran isiyokuwa na rubani iliyokuwa ikitishia usalama wa meli na wafanyakazi katika lango hilo la Hormuz.


Share:

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Aiagiza TANAPA kupitia upya sheria ya tozo ya kiingilio kwa watalii wanapotoka nje ya Hifadhi

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ameiagiza Hifadhi za Taifa ( TANAPA) kupitia upya sheria ya tozo ya kiingilio kwa watalii wanapotoka nje ya Hifadhi  inayowalazimu kulipwa tena wanapoingia ndani ya Hifadhi maarufu kwa jina la Single Entry waiondoe kwenye maeneo yanayolalamikiwa kuwa imeua shughuli za Utalii kwenye  vijiji vinavyozunguka Hifadhi.

Aidha,Mhe. Kanyasu ameagiza TANAPA iangalie maeneo ambayo inadhani ni muhimu  kwa Single Entry iendelee kutumika  kuwa waweke mfumo wa kielektroniki wa utambuzi wa vidole ( Biometric Identity) utakaoweza kutumika kubaini udanganyifu endapo utafanyika.

Amesema mfumo huo utawalazimisha watalii kuweka kidole wakati wakiwa wanaingia na wakati wanapotoka nje ya Hifadhi.

Amesema hali hiyo itawasaidia Waongoza  watalii kutoka nje ya Hifadhi na Watalii wao kwa ajili kuzitembelea jamii zilizokaribu na Hifadhi na hivyo kuzisaidia jamii kunufaika moja kwa moja kupitia utalii wa kiutamaduni.

Hayo yamesemwa kupitia  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akifunga Maonesho ya 8 ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti mkoani Mara.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Single Entry kumepelekea madhara makubwa kwa baadhi ya maeneo yaliyo karibu na Hifadhi za Taifa kudumaa  kiutalii.

Ameyataja  maeneo hayo yaliyokaribu na yaliyoathirika moja kwa moja kuwa ni ukanda wa Magharibi katika geti la Ndabaka katika Hifadhi ya Serengeti na katika  Hifadhi ya Ruaha.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Maonesho hayo, Kanyasu amesema maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na kuwepo kwa Single Entry ni yale maeneo ambayo hayajapitiwa na barabara kuu pamoja na viwanja vya ndege.

Ametaja sababu zilizopelekea  kufa kiutalii maeneo hayo kuwa watalii walio wengi hulazimika kukaa ndani ya Hifadhi hadi muda wa masaa 24 yanavyoisha bila kutoka wakikwepa gharama endapo watatoka.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alimueleza Naibu Waziri huyo  kuwa wilaya yake asilimia 80 ni eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo kutokana na uwepo wa Single entry wilaya hivyo imeathirika sana kwa vile imekosa watalii wanaotembelea vijijini tofauti na ilivyokuwa mwanzo kabla ya kuanzishwa.

" Mhe.Waziri tunakuomba uliangalie suala  hili, utalii wa kiutamaduni uliosaidia kuajiri wananchi wengi umekufa kutokana na Single Entry" alisisitiza

Ameongeza kuwa  endapo itaondolewa itasaidia watalii kuweza kutoka nje ya Hifadhi kuembelea vituo vingi vya utalii ambavyo vipo nje ya Hifadhi.

Naye, Anaeli Kilemi aliyesoma risala mbele ya Waziri huyo amesema Single entry imewadidimiza wananchi wengi ambao walikuwa wamejiajiri kupitia utalii wa kiutamaduni, Hivyo anaiomba serikali itatue tatizo hilo.


Share:

Taasisi ya elimu ya watu wazima (TEWW) Yajidhatiti Kuwakomboa Vijana Waliokosa Elimu katika Mfumo Rasmi

Na Timoth Anderson - TEWW
Taasisi ya elimu ya watu wazima (TEWW) imesema imeweka mkakati wa masomo wa kitaifa ambao utakwenda sambamba na Mpango Changamani kwa Vijana Walio Nje ya mfumo Rasmi wa Elimu maarufu kama ‘IPOSA’ ili kuwafikia  Vijana wa kike na wa kiume ambao hawajawahi kwenda shule, wanafunzi walioacha shule za msingi, wanafunzi waliomaliza darasa la saba lakini hawajapata fursa ya kuendelea, wanafunzi waliohitimu masomo yao kupitia program ya MEMKWA, Wasichana walioacha shule kwa changamoto mbalimbali kama vile ujauzito na ndoa za utotoni

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Elimu kwa Umma Shule Huria, Bw. Placid Balige wakati alikuwa akizungumza na waandishi habari kwenye maonesho ya 14 ya Vyuo vya elimu ya juu sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja.

"taarifa ya tathmin ya Mpango wa Elimu Changamani baada ya msingi (MECHAM) ya mwaka 2015,Utafiti uliofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi ya Teknolojia wa mwaka 2015 na taarifa ya takwimu ya Elimu ya msingi zinaonesha watoto wa kati ya miaka 14-17 wapatao 2,256,940 hawapo shule japokuwa ilibidi wawepo shule hivyo TEWW, Wizara yetu, wakaanza kuandaa mpango ambao hapana mtoto atakaeachwa kupewa elimu” amesema Balige.

Ameongeza kuwa,  watoto walioingia katika ndoa na mimba za utotoni na kukatisha masomo yao wamepata mafanikio makubwa kwani TEWW kupitia miradi yake mbalimbali wamewafundisha stadi za maisha jambo lililopelekea kuwawezesha kujiajiri wenyewe hali ambayo itawawezesha wale wenye nia ya kurudi shuleni  kwa mfumo rasmi kurudi kwakuwa wameshapewa stadi za maisha juu ya kukabiliana na mazingira yao.

Aidha, Bw. Balige ameongeza kuwa , watoto hao wameweza kufungua maduka na kuweza kudhalisha bidhaa zao wenyewe ikiwemo kutengeneza sabuni, kusindika chakula jambo lililopelekea kupata mkopo wa asilimia 4 wa vijana unaotolewa na Halmashauri katika maeneo yao ili kuwakomboa vijana kiuchumi.

"Tumeweza kuwafikia vijana 3000 katika mkoa wa Dodoma,Rukwa na Lindi ambao walipata ndoa za utotoni na kukatisha masomo yao kwa sasa wameweza hata kujiunga Vikundi na kuweza kupata mkopo wa Manispaa wa asilimia 10 unatolewa nchi nzima " amesema Balige.

Aidha amesema, Taasisi hiyo ilianzishwa na Sheria ya Bunge Namba 12 ya Mwaka 1975 ambapo pamoja na majukumu mengine inatoa Mafunzo kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada katika eneo la Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelevu pamoja na Ustawi wa jamii kwa njia ya ana kwa ana na kwa njia ya masafa ili kuwaandaa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima hiyo ikiwa ni mtekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi na kwasababu ni mpango mahususi katika kuchagiza Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025


Share:

Benki Ya Dunia Yaijengea Tanzania Uwezo Wa Tathmini Baada Ya Maafa

Benki ya Dunia, kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia  Ofisi ya Waziri  Mkuu,  Idara ya Menejimenti ya Maafa, imeendesha mafunzo ya siku tatu juu ya namna ya kufanya Tathmini ya mahitaji baada ya maafa kutokea na namna ya Kuandaa Mipango wa kurejesha hali baada ya maafa kutokea, kwa wataalamu wa menejimenti ya maafa kutoka wizara, mikoa, Taasisi na  Idara za serikali pamoja na mashirika yasiyo  kuwa ya kiserikali.

Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo,  jijini Arusha  tarhe 19, Julai, 2019, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amefafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa na wataalam wa kutosha hapa nchini wa kufanya tathmini za Maafa kitaalam zenye kujikita katika athari za maafa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na maendeleo.

“Mafunzo haya yatatusaidia kutuongoza serikali na wadau wa menejimenti ya maafa  kuwa na mfumo  wa pamoja utakao wezesha kuwa na mtazamo wa pamoja katika  kuendesha shughuli ya Tathmini hususani kwa athari za kiuchumi kwa ngazi ya mtu binafsi, Taifa na Kimataifa, Uharibifu wa miundo mbinu na hapo tutaweza kuwa na mpango wa pamoja wa kurejesha hali ” amesema Matamwe.

Matamwe ameendelea kufafanua kuwa kutokana na wataalamu hawa kujengewa uwezo wa Kuandaa Mpango wa kurejesha  hali, utaalamu huo utaisaidia nchi yetu Tanzania kuwa na Takwimu za  urejeshaji hali  ambazo tutapata uwezo wa kurejesha hali itakayo saidia nchi yetu kuwa inarejesha hali wakati.

Akiongea katika mafunzo hayo  kwa niaba ya Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Mtaalamu wa Mawasiliano Benki ya Dunia Edward Anderson amefafanua kuwa  Benki hiyo imeamua kuendesha mafunzo hayo ili nchi ya Tanzania kuwa na  wataalam wenye uwezo wa kurejesha hali kwa wakati baada ya maafa kutokea.

“Tangu mwaka 2016 nilipofika hapa nchini nimeshuhudia athari za maafa yakitokea  ikiwemo tetemeko la ardhi mkoani Kagera, na mafuriko katika jiji la Dar es salaam mwaka 2016, hivyo maafa yanahitaji mfumo sahihi na Mpango bora katika kurejesha hali, na ninafurahi kuona Benki ya Dunia tupo tayari katika kutekeleza hayo” Amesema Edward.

Aidha, washiriki wa mafunzo hayo kwa nyakati tofauti wamefafanua mafunzo hayo yamewajengea uwezo katika kufanya Tathmini baada ya maafa kutokea na uuandaaji wa Mpango wa kurejesha hali hususani katika maeneo ya kuanisha gharama za urejeshaji, mbinu za kuanisha vyanzo vya rasilimali fedha wakati wa urejeshaji hali, kuainisha hasara na athari  zitokanazo na maafa  .

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia  tarehe  16 hadi 19 Julai, 2019,  liliwashirikisha wataalam wa usimamizi wa shughuli za maafa , kwa wataalamu wa menejimenti ya maafa kutoka wizara, mikoa, Taasisi na  Idara za serikali pamoja na mashirika yasiyo  kuwa ya kiserikali, limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa,  kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

MWISHO.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi 20 July



















Share:

Friday 19 July 2019

'FACEAPP' MITANDAO INAYODUKUA TAARIFA ZAKO HUKU UKICHEKELEA....'KIJANA ANAONEKANA MZEE'

Share:

RAIS MAGUFULI AREJEA DAR ES SALAAM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na wahudumu wa ndege iliyomchukua baada ya kuteremka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam asubuhi leo Ijumaa Julai 19, 2019 akitokea jijini Dodoma.

Share:

BENKI YA MAENDELEO YA WAKULIMA TADB YAJA NA NEEMA KWA WAKULIMA MKOANI KAGERA


Kaimu Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB Kanda ya ziwa, Izirahabi Jumanne akizungumza wakati akizindua kampeni ya kuhamasisha wakulima kutumia mfumo rasmi wa kibenki

Na Lydia Lukagila - Malunde1 blog Kagera

Wakulima mkoani Kagera walio katika mazao ya mikakati wametakiwa kufuata agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa la kupitia mifumo rasmi ya kibenki ili kukopesheka kwa urahisi.

Rai hiyo imetolewa  leo Julai 19 ,2019 na Kaimu Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB Kanda ya ziwa, Izirahabi Jumanne wakati akizindua kampeni ya kuhamasisha wakulima kutumia mfumo rasmi wa kibenki na kufungua akaunti zao ili kupata fursa mbalimbali zitakazo wawezesha kukopesheka kwa urahisi katika ofisi ya Chama cha Ushirika mkoani Kagera.

Jumanne amesema Waziri Kassim Majaliwa alitoa agizo kwa wakulima wote walio katika mazao ya mkakati kupitia mifumo rasmi ya kibenki ili kuwawezesha wakulima hao kupata fursa mbali mbali za mikopo itolewayo na Benki ya Kilimo.

Amesema huu ni msimu wa pili wa kuhamasisha wakulima kutumia mfumo jumuishi kwani msimu wa kwanza ulifanyika mwaka 2018 japo changamoto kubwa ilikuwa ni elimu jambo ambao lilisababisha wakulima wengi kupata pesa zao kwa kuchelewa.

"Mfumo huu una malengo mahsusi, kwani mkulima atakopesheka wa haraka na kupata fursa mbali mbali za mikopo kwa urahisi ikilinganisha na aliyezunguka kupitia ofisi za vyama vya ushirika",amesema.

Naye Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera Robert Kitambo amesema mfumo wa kulipia kupitia akaunti unampunguzia adha mpokeaji pesa na kutoa pesa anavyotaka tena kwa siri na kuepuka kusuala ya wavamizi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Vodacom kutoka Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera Muda Tito amewahimiza wakulima kutunza pesa zao kupitia simu za mkononi na kuwa na kumbukumbu za namba zao za siri kwani inakuwa ngumu pale mkulima anaposahau namba za siri.

Tito ameongeza kuwa kuhusu masuala yoyote yatakayoleta ugumu wakulima waonane na makarani ili kumaliza matatizo yao.

Ikumbukwe kuwa kampeni hii ya kuhamasisha wakulima kutumia mfumo wa kulipia kupitia akaunti itafanyika katika wilaya zote za mkoa wa Kagera ili kuwasaidia wakulima kukopesheka kwa urahisi na kupata fulsa mbali mbali za mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Kaimu Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB Kanda ya ziwa, Izirahabi Jumanne akizungumza wakati akizindua kampeni ya kuhamasisha wakulima kutumia mfumo rasmi wa kibenki. Picha zote na Lydia Lugakila - Malunde1 blog

Share:

Tanzania Wahitajika Kuwekeza Katika Afya Na Elimu Ya Vijana Wake–Ripoti Ya Benki Ya Dunia


 Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bi. Bella Bird akitoa neno la ukaribisho kwa wageni waalikwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa toleo jipya la jarida la Uchumi la Benki ya Dunia iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza kuhusu maono ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati kufikia mwaka wa 2025 na inawekezana kuhakikisha kuwa maono yanafikiwa kwa kuboresha huduma zetu za afya na miundombinu wakati wa uzinduzi wa wa toleo jipya la 12 la jarida la uchumi wa Tanzania la Benki ya Dunia katika hafla iliyofanyika  kwenye Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
 Mchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia na Mwandishi mwenza wa toleo la 12 la uchumi wa Tanzania, Quentin Wodon akizungumza na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa wa toleo jipya la 12 la jarida la uchumi wa Tanzania la Benki ya Dunia katika hafla iliyofanyika  kwenye Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisiliza kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa uzinduzi wa wa toleo jipya la 12 la jarida la uchumi wa Tanzania la Benki ya Dunia katika hafla iliyofanyika  kwenye Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. 
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. William Ole Nasha akizungumzia juhudi za serikali katika kuboresha elimu ya Tanzania wakati wa uzinduzi wa wa toleo jipya la 12 la jarida la uchumi wa Tanzania la Benki ya Dunia katika hafla iliyofanyika  kwenye Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Pichani juu na chini ni Baadhi ya wadau wa masuala ya uchumi kutoka mashirika na taasisi mbalimbali nchini walioshiriki hafla ya uzinduzi wa wa toleo jipya la 12 la jarida la uchumi wa Tanzania la Benki ya Dunia iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.

 Tanzania imetakiwa kuwekeza kwa haraka katika elimu na afya za watu wake hasa vijana kama itataka kuimarisha rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Kauli hiyo imo katika toleo jipya la jarida la Uchumi la Benki ya Dunia.
Imeelezwa kuwa katika miaka ya karibuni Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya binadamu ambapo imeweza kupunguza idadi ya vifo kwa watoto chini ya miaka mitano, kuongeza miaka ya wanafunzi kuwa shule kwa vijana wake na kuimarisha umri wa uhai kwa watu wazima.
Hata hivyo takwimu za urari wa uzalishaji wa binadamu yaani Human Capital Index (HCI) ya 0.40 inamaananisha kuwa watoto wanaozaliwa leo nchini Tanzania wanaweza kufikia asilimia 40 tu ya pato wanaloweza kulipata wakiwa na afya njema na elimu.
“Utajiri nchini Tanzania umeongezeka kwa asilimia 45 toka mwaka 1995 na haya ni mafanikio makubwa, lakini pia idadi ya watu imeendelea kuongezeka, na hivyo kupungua kwa pato halisi na hivyo kukosa uendelevu,” anasema  Bella Bird, Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Tanzania.
“Ili nchi iwe na ukuaji endelevu, inahitaji kuwekeza kwa watu wake, kwani raslimali watu ni muhimu sana kwa nchi yoyote ile.” 
Benki ya Dunia ilizindua HCI Oktoba 2018, kama mradi mpya wa kushawishi mataifa kuwekeza zaidi kwa wananchi wake.
Urari huo unaangalia vipengele vitano vyenye kuonesha kipato cha baadae: uhai wa watoto baada ya miaka mitano; Wastani wa miaka inayokamilishwa na  vijana kujipatia elimu; Ubora wa elimu katika shule;ni kwa miaka mingapi watu watafanyakazi, kama kipimo cha uhai wa mtu mzima utapitiliza miaka 60 na kuzuia udumavu kwa vijana na watoto. 
“Kuna mambo mengi kwa Tanzania na mataifa mengine kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa katika urari huo ( HCI ) nchi za Singapore, Korea Kusini, Japan, na Hong Kong.
Mataifa haya mafanikio yake yameelezwa kutokana na kuwekeza zaidi katika vijana, wakizingatia zaidi elimu na maendeleo ya utaalamu katika ngazi zote za makuzi yao,” anasema Quentin Wodon, Mchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia na Mwandishi mwenza wa  toleo la 12 la uchumi wa Tanzania.
Kwa kuangalia kiwango chake cha maendeleo, Tanzania haifanyi vyema miaka ya kijana kuwa shuleni na kuna hatari ya watoto chini ya miaka 5 kudumaa.
Ripoti zinaonesha pia  urari mbaya wa mapato kijinsia inakwamisha kuongeza ubora wa raslimali watu na hivyo pato la utajiri.
Ili kukabiliana na vikwazo vinavyozuia maendeleo ya raslimali watu, serikali imeshauriwa kuimarisha uwekezaji katika maeneo mengi kwa kutumia nguvu yake yote na kutoa huduma bora.
Pia mkazo umetakiwa kuwekwa kwa makundi yenye shaka hasa wasichana wanaokua na kwa kuangalia maeneo ambayo yapo nyuma.
Pia wametaka muda wa wanawake kufanyakazi wasizolipwa kama utunzaji wa familia upunguzwe, kwa kusambaza wajibu huo ili kuwawezesha kufanya kazi zaidi zinazowalipa.
Pia kuwapa nafasi zaidi wanawake kumiliki mali za kufanyia uzalishaji, kuangalia hali ya soko na mifumo ya kitaasisi inazuia fursa kwa wanawake.
Jarida hilo la sasa linaloelezea hali za uchumi pia limetoa maoteo ya hali ya uchumi kwa miaka michache ijayo. Kuangalia changamoto za mazingira ya nje ya biashara na uwekezaji kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku ikitambulika kwamba kwa Tanzania hali inakuwa bora zaidi.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema ukuaji huo utategemea utekelezaji wa mabadiliko katika sera. 
Pia hatua za serikali kuboresha mazingira biashara na kifedha ikiwamo kupunguza tozo, kurejesha fedha kwa wananchi hasa za kodi na kuweka kipaumbele kwa miradi ya uwekezaji inayolenga kuleta maendeleo na yenye fedha tayari za kumalizia miradi kwa wakati uliopangwa.


Share:

Waziri Mkuu Awafunda Watumishi Wa Umma.....Ataka Wawe Na Mipango Kazi, Asema Serikali Inapima Matokeo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wawe na mipango ya kazi ambayo itaweza kupimika na kutoa matokeo.

“Kila mtumishi anapaswa awe na mpango kazi katika sekta yake na ni lazima aende kupima matokeo. Awamu hii, tunataka kuona matokeo ya kazi zenu."

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Same kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, mjini Same.

“Watumishi mmeletwa kwenye wilaya hii ili muwahudumie wananchi. Tulioajiriwa, kazi yetu kubwa ni kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote uwe ni wa kabila, itikadi au rangi.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kwamba baada ya mchujo wa watumishi hewa, waliobakia wanapaswa kufanya kazi kwa bidii.

"Fanyeni kazi kwa bidii, msimamo wa Serikali hii ni kwamba hatumvumilii mtumishi ambaye si mwajibikaji, ni mwizi, mzembe au anaomba rushwa. Serikali hii hatuna muda wa kujadili matatizo ya watumishi, tunamalizana hapo hapo," amesema.

Amewataka watumishi hao wasimamie utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo chama tawala.

"Mtumishi angalia sekta yako inasema nini, ifanyie kazi. Kama ni maji, tafuta ni wapi yanapatikana, changanua zinahitajika shilingi ngapi, tafuta njia ya kupata hizo fedha ili wananchi wapate maji."

Kuhusu tabia ya kukaa ofisini, Waziri Mkuu amekemea tabia hiyo na kuwataka watumishi wote nchini waache tabia ya kukaa ofisini na badala yake waende vijijini kuwasikiliza wananchi.

"Watumishi wa umma msikae ofisini. Nendeni vijijini walau kwa siku nne za juma. Hizo mbili zinazobakia, zitumieni kuandaa taarifa. Nendeni huko ili wananchi wasipate usumbufu wa kuja hapa mjini kuwatafuta," amesisitiza.

"Mkuu wa Wilaya simamia zoezi la wakuu wa idara na wasaidizi wao kwenda vijijini. Wakienda vijijini ni lazima waonane na waheshimiwa madiwani, washirikiane kusikiliza kero na kutafuta majibu kwa wananchi. Huo ndiyo mshikamano wenyewe unaohitajika," amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma watambue mipaka yao na wajenge mahusiano baina yao na wengine.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Moshi, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

"Kila mmoja lazima atambue mipaka yake na mamlaka baina yake na wengine. Hapa mko wateuliwa, waajiriwa na wachaguliwa. Kila mtu ana nafasi yake ya kuwatumikia wananchi.

Aliwataka watumishi hao watambue falsafa ya Kiongozi mkuu wa nchi ambayo inahimiza uchapakazi. “Kwa hiyo tunaposema Hapa Kazi Tu, maana yake chapa kazi na tuone matokeo. Tunasisitiza kazi na tunataka kazi unayoifanya, itoe matokeo,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,       


Share:

DROO IMEPANGWA KUELEKEA AFCON 2021


Droo ya Kombe la taifa bingwa barani Afrika 2021 imefanyika Alhamisi mjini Cairo kabla ya michuano hiyo kufanyika nchini Cameroon.

Algeria, ambao wanakutana na Senegal Ijumaa hii katika fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika la mwaka mjini Cairo, watalazimika kusafiri umbali wa bara zia kwa ajili ya mechi za waliofuzu la mwaka 2021

Katika draw hiyo mbwa mwitu wa jangwani (Desert Foxes) wamepangiwa kucheza katika kundi H pamoja na timu tatu za kusini mwa Afrika , Zambia, Zimbabwe na Botswana.

Mahasimu wa Algeria, Senegal, katika fainali ya Ijumaa , watakuwa katika kundi feature in I dhidi ya Congo Brazzaville, Guinea-Bissau na eSwatini.

Madagascar, ambao kufuzu kwao kwa robo fainali kuliwashangaza wengi katika kombe la AFCON 2019, wamewekwa katika kundi K pamoja na Ivory Coast, Niger na Ethiopia.

Nigeria, waliowapiga Tunisia 1-0 siku ya Jumatano wakiwa katika nafasi ya tatu , watakutana na wenzao wa Afrika magharibi Benin na Sierra Leone pamoja na Lesotho.

Ghana na Afrika Kusini wako kundi C na wote watatakiwa kiufuzu kutokana na kutoshiriki kwa Sudan na washindi wa wa awamu ya kwanza watakutana na Mauritius na Sao Tome e Principe.

Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika 2021 kufanyika Cameroon.

Ingawa mwenyeji Cameroon ambaye anafuzu moja kwa moja kutokana na kwamba ndio inayopokea wageni, atalazimika kushiriki mechi ya ushindani na hivyo kuziacha Cape Verde, Msumbiji na Rwanda kushindana na kundi jingine la F.

Uganda, ambayo imekuwa ndio timu thabiti katika eneo la Afrika mashariki katika shindano la mwaka 2019 , wako pamoja na Burkina Faso, Malawi na Sudan kusini au Ushelisheli katika kundi B.

Michuano minne ya awali itachezwa mnamo mwezi wa Octoberna zile za makundi zitaanza mwezi utakaofuatia kwa raundi mbili.

Washindi na timu zitakazochukua nafasi ya pili kutoka kila kundi watafuzu isipokuwa Katika kundi F lenye Cameroon ambao wanafuzu moja kwa moja kama wenyeji .


Jinsi Droo kwa ukamilifu:

Raundi ya kwanza :

Liberia v Chad

South Sudan v Ushelisheli

Mauritius v Sao Tome e Principe

Djibouti v Gambia

Makundi:

A: Mali, Guinea, Namibia, Liberia/Chad

B: Burkina Faso, Uganda, Malawi, Sudan Kusini /Ushelisheli

C: Ghana, Afrika Kusini, Sudan, Mauritius/Sao Tome

D: Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Gabon, Angola, Djibouti/Gambia

E: Morocco, Mauritania, Jamuhuri ya Afrika ya kati, Burundi

F: Cameroon (wenyeji), Cape Verde, Msumbiji, Rwanda

G: Misri, Kenya, Togo, Visiwa vya Komoro

H: Algeria, Zambia, Zimbabwe, Botswana

I: Senegal, Congo Brazzaville, Guinea-Bissau, eSwatini (zamani ikiitwa Swaziland)

J: Tunisia, Libya, Tanzania, Equatorial Guinea

K: Ivory Coast, Niger, Madagascar, Ethiopia

L: Nigeria, Benin, Sierra Leone, Lesotho

Haikuingia: Eritrea, Somalia

CHANZO.BBC SWAHILI
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger