Friday 30 December 2016

Jinsi ya kuishi na Watu wenye Tabia Ngumu

Ni ngumu na kamwe siyo rahisi kumbadilisha mtu mwenye tabia ngumu awe rafiki. Badiliko hili lawezekana ikiwa mhusika (mwenye tabia ngumu) atadhamiria na kuwatayari kushughulika ili kubadilika.

Kwa hiyo kama ni ngumu au haiwezekani kumbadilisha basi jaribu kubadili mtazamo wako na jinsi unavyoishi naye au nao, kwasababu mara nyingi wewe ndiye unaye kwazika au kuumizwa wakati yeye (yule anayekuudhi) anafanikiwa na anaendelea na furaha yake tu.

Mawasiliano baina yetu na watu wengine yanajumuisha jinsi tunavyowafanyia wengine na jinsi wao wanavyotufanyia sisi (reaction and counter reaction). Kwa kubadili jinsi sisi tunavyowatendea wengine inaweza kubadili jinsi wao wanavyotutendea sisi. Hata kama ni kwa muda au kitambo kidogo tu. Hata kama hali hii haibadili hali kwa kudumu ila inaweza kurahisisha mazingira ya kuishi na mtu au watu wenye tabia ngumu.

Kila wakati lazima uwe na akili sana katika kuishi na watu wenye tabia ngumu, kama hutoweza kujizuia, na ukaanza kuwabwatukia basi itakuwa unaleta tatizo hasa pale ambapo mwenye tabia hii ngumu ni bosi wako. Je, utaropoka au kutukana kama ulivyozoea?

Hata kama mtu au watu wenyetabia hii wako ndani ya familia na yamkini ni wadogo kwako kiumri, bado kuropoka na kuwapayukia siyo suluhisho, hali hii yaweza kukugharimu.

Najua kila mmoja wetu anajinsi anavyofanya kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Wote hatuna namna moja, mmoja anaweza kuwa ni mkimya na mwenye ujasiri hata anapoudhiwa, mwingine hupayuka na kumjibu yule anaye muudhi, mwingine anaamua kulia tu anapoudhiwa, wako wanaozira na kuamua kutozungumza tena na aliyewaudhi, wapo ambao husambaza habari mbaya kuhusu huyo mwenye maudhi, wako ambao huamua kumwambia uso kwa uso jinsi walivyo kwazika, sijui staili yako ni ipi.

Ni rahisi sana kuumizwa au kuudhiwa na maneno au matendo ya mwingine, na mara mtu huyo anapojua kuwa unaumia yeye hupata nguvu, hii huwa ndiyo silaha yake muhimu pale mnapopambana.

Unachotakiwa kufanya ni kuwaachia wakati wote wao wawe washindi, kamwe usitafute kushindana nao, utaumia mwenyewe. Njia pekee ni kujitahidi kuwa mjanja na mwenye akili kuliko yeye na pia kuwa na ushawishi katika yale wanayotaka kuyatenda hata pasipo wao kugundua.

Je, unawajibu vipi watu hawa (How do you react?)
Ni jambo jema kuanza kujitazama jinsi unavyowatendea wengine na jinsi tunavyoshughulika na wale wanaotukwaza. Kumbuka kuwa jinsi unavyoikabili hali hiyo katika mazingira fulani inawezekana isiwe hivyo katika mazingira mengine.

Watu wenye tabia ngumu na zinazotatiza mara nyingi huweka mitego ya maneno au matendo na kwa kiasi kikubwa unaweza kunaswa na kuwaruhusu wakuchezee jinsi watakavyo, na kati ya vitu wanavyo vipenda na kuvitamani ni kukuona unalia na kuumia na kuchanganyikiwa. Kwahiyo fikiri kwanza kabla hujafanya chochote mbele yao.

Watu watabia hii mara zote huwachukulia na kuwatendea watu wote sawa kwa hiyo usifikiri kila alichosema au alichofanya kwako ni cha kibinafsi sana na alikikusudia kwako. Angeweza kufanya au kusema hivyo hivyo hata kwa mwingine aliye karibu naye wakati ule. Kwa kufahamu hili itakusaidia kupunguza maumivu yanayoletwa na hisia zako kwake.

Hembu jiulize ni jinsi gani umewahi kukabiliana na mtu au watu wa jinsi hii, na je ilikuwa ni kwa jinsi ya kuumiza au kuelemisha? Fahamu kwamba kujibu kwa kupayuka, kutukana au kubishana haisaidii, bali kunakushusha chini ya miguu ya yule aliye kusababishia maumivu hayo, na sasa atakuwa anafurahia na kukuona wewe mjinga.

Ni chaguo lako, la ni jinsi gani utakabiliana na mtu au watu wa aina hii, ingawa unaweza kuchagua njia bora itakayoweza kukusaidia kukuimarisha na kupunguza udhaifu wako, zaidi ya kuamua kuchagua njia ambayo itakuacha umeumia, umechoka, umekatishwa tamaa na umejeruhika moyo.

Hii haimaanishi uwe mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu na kila mtu, na haimaanishi kuwa hutakiwi kukasirika HAPANA, hasira ni asili na haina tatizo lolote hapa, ila tu matokeo ya hasira hiyo ndiyo yanayoweza kuleta shida. Je ni jinsi gani unakabiliana na hasira yako na unaionyeshaje? Kwa fujo, kupayuka kubishana, kulia, kuvunja vitu, kunyamaza n.k.

Ili Kujua jinsi watu wenye tabia ngumu wanavyokuathiri. Jiulize maswali yafuatayo:

Je, ni unataka kutawaliwa na wengine?
Najua jibu ni kwamba hakuna nayetaka kutawaliwa na mwingine, na ndiyo maana unaweza kujikuta unabishana au kushindana na huyo anaye kukwaza.

Tatizo ni kwamba mwisho wewe ndiyo unaumia na yeye anabaki kufurahia kwa kukushinda mfano; tazama fujo za madereva barabarani hususan wale wa daladala.
Nikweli unahasira naye, lakini je hiyo ni njia muafaka ya kumkabili? kumbuka mwishoni atakayeumia ni wewe.

Fikiri kama unatatizo la shinikizo la damu kama utakubali kuyumbishwa kihisia na tabia mbovu za mwingine wewe ndiyo utabaki unaumia na siyo tu kama hutoweza kufanya vile moyo wako utakavyo bali pia utaachwa ukijihisi kuchoka, kuumizwa kwa hisia zako mwenyewe na kukatishwa tamaa na tabia yako wewe mwenyewe.

Nini Mwitikio wako pale unapoudhiwa? (Haswa na yule mwenye hasira na wewe)

  • Je, unalipa hasira kwa hasira?
  • Je, unajitetea na kuukimbia ukweli (being defensive)
  • Au unajificha kutoroka au kumkwepa?

Njia zote hizi hapa juu siyo nzuri.
Hata kama una haki ya kukasirika, lakini bado atakayeumia unabaki kuwa ni wewe. Na siyo tu utaumizwa na kukasirishwa kwa tabia yake mwenye kukuudhi bali utaumizwa moyoni mwako kwa vile wewe ulivyotenda, dhamiri itakushtaki zaidi (guilty conscious).

Je, unajizumgumziaje wewe mwenyewe, vibaya au vyema?
Mfano: Ukweli mimi najichukia haswa ninapofikia kipindi cha mitihani au usaili.
Hivi mimi nikoje?
Hivi kwa nini nimeumbwa hivi?
Kamwe mimi siwezi kufanya lolote jema!
Wakati wote mimi ni mtu wa bahati mbaya tu!

Wala huhitaji kujichukia unapofikia wakati wa mitihani au usaili, unachohitaji kufanya ni kujiandaa mwenyewe vizuri na kuwahi mapema katika eneo la tukio.
Hisia potofu na zisizojenga ambazo tunajiwazia wenyewe mara nyingi hutupotezea muda na mara tunapoziruhusu hutuharibia siku yetu nzima.

Unafanya nini unapopingwa? (what do you do when you are criticized)
Wako watu wanaopendelea kupinga wengine katika kila kitu, hata katika vile visivyostahili kupingwa,hakuna chochote chema kinachoweza kusemwa na yeyote, bali yeye peke yake. Hata kama kilichosemwa kina ukweli kwa asilimia kubwa basi mtu huyu atajitahidi walau kurekebisha hata lugha tu, ili mradi kisipite hivihivi bila yeye kukipinga japo kidogo (hawa ndiyo wale wenye tabia ngumu).

Hali hii huwapa kufurahi na kujijengea nguvu kwa jinsi wanavyopinga wengine.
Ni kweli upinzani mwingine ni wa ukweli na unajenga lakini hapa nakazia wale wanaopinga ili tu kujifurahisha nafsi zao na kuwafanya wale wanaowapinga waumie mioyo.

Je, unapopigwa, unajibuje?
Je, unajitetea au unajishusha na kukubali kila kinachopingwa kwa kuamini kwamba anayekupinga yuko sawa na kwa hiyo unayameza maoni yako yote, bila kuchambua kwa kina mapingamizi hayo.

Kuna jinsi ambavyo unaweza kumkabili au kumjibu anayekupinga na ikawa kama umeweka petroli kwenye moto, upinzani utawaka na hata kuleta ugomvi, lakini pia iko njia ambayo unaweza kumjibu mtu huyu na ukanyamazisha fukuto lote.

Je, una mtazamo hasi (mtazamo usiofaa) na wa kudumu katika kitu fulani?
Mfano; Labda unasema “Mambo yangu hayaendelei tangu nihamie katika nyumba hii, au mambo yangu yanakwama tangu nimuoe au niolewe na huyu, ni matatizo tu tangu tuoane, watoto hawa hasara tupu.” n.k.

Mtazamo huu hasi, waweza kukugharimu siyo tu kukunyima raha bali pia waweza kuharibu hisia zako na za wengine pia.

Ukijikuta katika hali hii ni vyema kujifahamu na kujitahidi kuelewa nini tatizo husika na jitahidi kubadilisha mtazamo wako.

Tafuta vile vitu ambavyo unaweza kuvitazama katika mtazamo chanya hata kama ni vidogo. Tafuta kuviongelea vile unavyovipenda zaidi ya vile usivyovipenda.
Je, unazimeza hisia zako zote, nzuri na mbaya?

Je, unaona ni ngumu sana kusema “nakupenda” “umependeza” “umeniudhi” n.k. labda unaweza kusema neno moja tu na siyo lingine. 
Wengi wetu tumekuzwa katika mazingira ambayo tunahofu kusema chochote ili tu tusije tukamkwaza mtu, hata kama tunaumizwa au tunajisikia vyema kusema kitu fulani, lakini tunajizuia.

Badala yake tunakwenda kusemea pembeni. Yamkini kunyamaza kunaweza kuwa na faida katika baadhi ya mazingira lakini siyo hata katika kukubali vitu visivyofaa. Hakuna ubaya wowote katika kuelezea jinsi unavyojisikia moyoni mwako ili mradi tu unaeleza kila unachokihisi kwa hali njema na siyo kwa hasira au shari. Katika hali hii kamwe hutowapoteza marafiki zako, na kama kuna yeyote aliye rafiki atasumbuliwa na hili basi usihofu, kubali tu kumpoteza kwa kuwa hakuwa wa muhimu au wa msaada sana kwako.

Hali ya kujifanya hujaumia au hujakwazika na wakati umekwazika na unalia ndani kwa ndani inaumiza na kufanya ujisikie vibaya sana. Inakufanya uzidishe mazingira ya msongo wa mawazo (stress) hasa pale unapojiwazia wewe mwenyewe zaidi ya kushughulika na wale waliokuudhi.

Mtazamo wako jinsi unavyojiona wewe mwenyewe huathirika sana, na pia waweza kujisababishia tatizo hasa pale wale wenye tabia ngumu watakapo kugundua kuwa huwezi kusema chochote hata ukiumizwa na hii itawafanya wakugeuze mpira wa kuchezea.

Je, wewe ni kati ya wale wanaojiamini kusema chochote wanachokifikiri bila kujali matokeo yake?
Hebu fikiria jinsi unavyojisikia pale ambapo mtu au watu wengine wangefanya hivyo hivyo kwako. Je, unataka kuwasababishia wengine maumivu ya moyoni? Kusema chochote kinachoshuka toka kichwani mwako kupitia kinywani mwako bila kufikiri juu ya matokeo au athari zake kwa wale wanaokusiliza au waliokuzunguka kunaweza kukupotezea marafiki na kuishusha hadhi yako kwa urahisi sana.

Mara nyingi mtu wa jinsi hii huweza kujikuta akiwa pweke na anayepingana na ulimwengu (kila mtu anamchukia). Hii ni kati ya hisia za kuhuzunisha na kuumiza sana muda wote, lakini pia huumiza zaidi pale unapogundua kuwa ni maumivu uliyojitakia mwenyewe. Peke yako unajikuta umetengwa na mtego wa kihisia na kukuzamisha usipoweza kujikwamua tena.
Share:

Feri wanasa 13 waliovua samaki kwa mabomu

UONGOZI wa Soko la Samaki la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam umewakamata watu 13 wanaohusishwa kuvua shehena ya samaki 473 karibia tani 1.3 wenye thamani ya Sh milioni 13 kwa kutumia mabomu.

Samaki hao aina ya kolekole, jodari, changu, pono, sehewa na nguru waliingizwa sokoni hapo Desemba 16, mwaka huu na baada ya ukaguzi, ikabainika kuingizwa kwa samaki hao, huku wahusika wakidaiwa kutoroka.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya soko hilo, kupitia upya mfumo wa mapokezi, ulinzi na usimamizi ili kujiridhisha kama uko safi. Kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa hao,

Meneja wa Soko hilo, Eliakim Mniko alisema jana kuwa, walikamatwa sokoni hapo na wamefikishwa polisi kutoa maelezo na kufunguliwa kesi itakayoanza kusikilizwa mapema mwakani.

Akiwa katika ziara sokoni hapo Desemba 19, 2016, Dk Tizeba alisema ni aibu kwa kitendo hicho kufanyika meta chache kufika Ikulu na kwamba kama suala la ukaguzi limewashinda, Bodi ya soko iachie jukumu hilo kwa mamlaka nyingine ifanye kazi sokoni hapo.

Pia aliagiza wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kutangazwa kuwa ndio wanaoharamisha uvuvi na kulitia hasara taifa.
Share:

Mto Ruaha Mkuu wakauka

MTO Ruaha Mkuu unaopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa) umekauka maji. Hali hiyo inatishia uhai wa wanyama waliopo katika hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini.

Gazeti hili lilitembelea hifadhi hiyo wiki iliyopita na kushuhudia wanyama wakihangaika kutafuta maji huku samaki, viboko na mamba ambao maisha yao yanabebwa na mto huo, wakiathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali hiyo.

Baadhi ya miti inayoelezwa kuwa na majimaji ilishuhudiwa ikiwa imeanguka ndani ya hifadhi hiyo na maelezo yaliyotolewa na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Runapa, Moronda Moronda ni kwamba imeharibiwa na Tembo wanaotumia miti hiyo kutuliza kiu ya maji.

Baadhi ya wadau wa mto huo, wamekosoa utekelezaji wa mikakati ya kuunusuru mto huo, wakisema haileti tija pamoja na kurejewa mara kwa mara.

Ofisa wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Malima Mbigima aliiomba serikali iingilie kati kwa kuyashughulikia masuala yote yanayosababisha mto huo ukauke.

Mbigima alisema nje ya hifadhi hiyo, mto huo umekuwa tegemeo kwa wakazi wengi ambao wamekuwa wakitumia maji yake kwa shughuli za uvuvi na kilimo.

“Hali kadhalika uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu unategemea maji ya mto huu. Licha ya umuhimu huo, kiwango cha maji katika mto huo kimeendele kupungua siku hadi siku,” alisema.

“Mto Ruaha Mkuu wenye urefu wa kilomita 475 unaanzia katika Mlima Kipengere wilayani Makete mkoani Njombe, ukimwaga maji katika ardhi oevu ya Usangu wilayani Mbarali mkoani Mbeya kupitia Runapa hadi katika Mto Rufiji. Mto huu unachangia asilimia 22 ya maji ya Bonde la Rufiji ukiwa na zaidi ya aina 39 za samaki,” alisema.

Alitaja sababu kubwa ya mto huo kukauka kuwa ni shughuli za kibinadamu zinazofanywa kandokando ya vyanzo vya maji ya kwenye vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika mto huo.

Hivi karibuni, wadau wa mto huo waliafikiana katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kupanga mpango wa pamoja utakaotekelezwa kwa pamoja kurejesha mtiririko wa maji katika mto huo kwa mwaka mzima.

Katika Kikao hicho kilichofanywa kwa ushirikiano na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira na Mali Hai Duniani (WWF), kwa mara nyingine wadau hao walikiri ni hatari kubwa kwa mto huo kuachwa uendelee kukauka.

Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Mtera, Lewis Loiloi alisema ikiwa Mto Ruaha utakauka kabisa, basi gridi ya Taifa itaondokewa na megawati 284 za umeme.
Share:

New AUDIO | Aslay - Rudi | Download

Share:

MAGAZETI YA LEO IJUMAA DEC TAREHE 30.12.2016

Share:

Thursday 29 December 2016

Bodi ya Mikopo yaja na mbinu nyingine ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia mwanzoni mwa Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa sugu kwenye vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kuanzia wale wa miaka 10 iliyopita.

Bodi hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30, mwaka huu, kwa wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika kulipia gharama za kuwasaka na kuendesha kesi.

Pamoja na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi cha kuhakiki waajiriwa wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB, na adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa muda huo wa siku 30 walioutoa, wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa hawajajisalimisha wenyewe kwa hiari, kulipa madeni yao wataanikwa hadharani na picha zao.

“Tumeamua kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua wadaiwa hawa wa bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka ili waturejeshee fedha zetu,” alisema Badru.

Aidha, alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni kuutangazia na kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi wengine kukosa fursa ya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha iliyopo bado haitoshelezi.

Alisema bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na baadaye kuwaongezea tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka huu, hivyo kinachofuata ni utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia fursa hiyo ya kujisalimisha.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa kushindwa kulipa madeni yao, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usumbufu wa kuwatafuta.

Alisema utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi zaidi, kupata fursa ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni vyema wanafunzi wote wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa muda muafaka uliowekwa kisheria.

Badru alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo, imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na mikopo kutoka miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga na kutafuta ajira.

Aidha, alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa waajiriwa walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya mishahara yao hadi asilimia 15.

“Tunawashukuru sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija kwenye sheria hii katika eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato kifikie hadi asilimia 30 na zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo wa wabunge walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,” alisema.

Alisema ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo hiyo aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi hiyo imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kupitia marekebisho hayo ya sheria.

“Tumeunda kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali nyeti, kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka huu, ya kuhakiki kila ofisi ya waajiri sugu ili kubaini kama ama wamewasilisha majina ya wanufaika wa mikopo hii au wanawakata bila kuwasilisha michango hiyo kwa bodi,” alisema.

Alisema waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa kutoisaidia bodi kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato yao, wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua makato hayo waliyoshindwa kuyawasilisha na endapo watashindwa watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha muda wa miezi 36 jela.

“Lakini pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha wanapeleka wenyewe taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa makato, yeyote atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye atawajibishwa,” alisisitiza.

Halikadhalika, Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa wanufaika wa mikopo hiyo ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira, ambao nao wanatakiwa kurejesha kiasi kisichopungua Sh 100,000 kila mwezi.

Akizungumzia mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa sugu kulipa wenyewe madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya fedha, yameongezeka kutoka Sh bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh bilioni nane.

Alisema tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza wenyewe kwa hiari na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote na wengine wakiyapunguza.

Hadi sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva, inazozidai kwa wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140 pekee ndio zimelipwa.

Kwa mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu ianzishwe Juni, mwaka 1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa wanafunzi hao.

Jumla ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na mikopo ya HESLB, wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi cha Sh trilioni 1.4, baada ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria kuisha.
Share:

Hapi Aishika Pabaya Kampuni Ya ZanteL,Yalipa Mapato Zaidi Ya Milioni 687 Ndani Ya Siku 7 Ilizopewa

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zantel Tanzania imelipa zaidi ya Sh milioni 687 baada ya kupewa siku saba na halmashauri hiyo iwe imelipa fedha hizo ambazo zilikuwa za kodi ya pango inazodaiwa na manispaa hiyo.

Fedha hizo zililipwa Desemba 21 na mkataba huo wa zamani unaisha Januari mwakani ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema wanaandaa mpya wenye viwango vya malipo vya sasa.

Aidha halmashauri hiyo imeamua kuelekeza fedha hizo ambayo ni sh 687,931,040 katika ujenzi wa vyumba vya madarasa 40 katika halmashauri hiyo kwamba kama itaonekana inawezekana kujenga shule nyingine mpya ya sekondari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Hapi alisema fedha hizo zimelipwa baada ofisi yake kubaini mchezo mchafu uliokuwa umefanywa na watendaji wa halmashauri yake waliokuwepo huko nyuma ambao walificha mkataba kati yake na Zantel.

Aidha aliipongeza Zantel kwa kutii maagizo waliyopewa na kulipa fedha hizo na tayari wamepewa risiti kuonesha kupokea fedha hizo na kwamba watu wote waliohusika katika jambo hilo watachukuliwa hatua za kisheria. 
Alisema baada ya malipo hayo, ameelekeza Manispaa kutumia fedha zote hizo kujenga vyumba vya madarasa katika halmashauri hiyo.

“Takwimu zinaonesha mwaka huu watoto 19,000 walifaulu katika Halmashauri ya Kinondoni waliochaguli kujiunga na Sekondari ni 12,889 na hadi sasa wanafunzi 3,169 hawajapata nafasi katika shule zetu kwasababu ya ufinyu wa madarasa,” alisema Hapi.
Share:

Waziri Mkuu Achangia Mabati Ujenzi Wa Zahanati

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani Ruangwa waharakishe kufyatua matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye atawachangia mabati.

Ametoa ahadi hizo jana (Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na Chibula na viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. 
Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.Alisema sera ya Serikali ni kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na kwamba umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya jimbo hilo inayosema “Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”

Katika kuhimiza ujenzi wa zahanati hizo, alichangia mabati kati ya 50 na 150 kwa kila kijiji na akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi wa maboma ili aweze kutimiza ahadi yake ya mabati.

Alisema katika awamu iliyopita, alikazania sana suala la elimu kwa kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa na madarasa ya kutosha. Pia alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika baadhi ya shule.

“Kuanzia awamu hii na miaka minne iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia upatikanaji wa maji safi na suala la kuboresha sekta ya afya katika jimbo zima nikishirikiana na uongozi wa Halmashauri yetu,” alisema.
Pia alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe anawasiliana na viongozi wa vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar Specialist, Bw. Ansi Mmasi alisema atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts 300 pamoja na nyaya zake kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji cha Namilema.
Alisema anaishukuru kwa kuwapa kazi makandarasi wazawa na akawataka wakandarasi wenzake watumie vifaa bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa huduma na taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.

“Tujitahidi kufanya kazi hizi kwa weledi na tutumie vifaa bora na imara ili watu wanaotarajia huduma zetu waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani na wakandarasi wazawa kwamba tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora unaotakiwa,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alisema atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Namilema. Pia alichangia mifuko 100 kwenye zahanati ya kijiji cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Chikundi.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Share:

Watu 7 Wafikishwa Mahakamani kwa kumchoma mkuki mdomoni mkulima

POLISI mkoani Morogoro imewafikisha mahakamani watu saba kati ya 12, kujibu tuhuma za kumjeruhi kwa kumchoma mkuki mdomoni hadi kutokea shingoni, Augustino Mtitu (35).

Walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa huku wengine watano, wote wakazi wa kitongoji cha Upangwa wilayani Kilosa wakisubiri kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana alipokuwa anazungumzia msako uliofanywa na polisi na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao baada ya kutokea kwa tukio hilo Desemba 25, mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi eneo la kitongoji cha Upangwa, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata na Tarafa ya Masanze wilayani Kilosa.

Kamanda Matei alisema katika msako huo, watu 12 walikamatwa na saba kati yao tayari wamefikishwa mahakamani. Wengine watano watafikisha mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

Hata hivyo, Kamanda huyo aliwataja majeruhi wa tukio hilo mbali na Mtitu ambaye bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kuwa ni George Andrew (68) aliyejeruhiwa kichwani.

Wengine ni Yohana Wisa (26) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Mathayo Elia (34) aliyejeruhiwa kichwani na bega la kushoto, Josephat Mtitu (55) aliyejeruhiwa begani na shavuni na mwingine ni Paulo Thomas (56) aliyejeruhiwa mbavu na mkono wa kushoto.

Wote ni wakazi wa kijiji cha Dodoma Isanga na wanaendelea vizuri. Hivi karibuni, baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai waliwashambulia kwa silaha za jadi na kuwajeruhi watu sita akiwemo Mtitu mara baada ya kukamata mifugo ya mtu mmoja aitwaye Ngoyoni Kimang’ati, iliyokuwa ikiharibu mahindi shambani.
Share:

Mapya Yaibuka Sakata la Kijana Aliyefariki Baada ya Nyoka wake Kuuawa na Wananchi

Share:

Mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya yaongoza kwa maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI

Kutokana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kupungua kwa asilimia 50 duniani kote na kupelekea watu milioni 2.1 tu kuambukizwa Virusi vya Ukimwi katika mwaka 2015,kumeibua matumaini mapya ya kuwa na watu wasio na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko aliwaambia waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam kuwa, nchini Tanzania maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi nayo yameshuka kwa asilimia 20 ambapo watu 54,000 wameambukizwa virusi hivyo kwa mwaka 2015 pekee.

Dkt. Maboko alisema, Ukimwi bado ni janga kubwa duniani na taifa kwa ujumla huku akitaja kundi la wanawake kuwa ndilo lina kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU huku mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya ukiwa na kiwango cha juu cha maambukizi hayo kitaifa.

Aidha, alisema serikali imejiwekea mikakati kuhakikisha kuwa waliogundulika kuwa wameathirika wanaanzishiwa dawa, kuhimiza matumizi ya mpira wa kiume, kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 29 na kutoa elimu kwa wanawake wanaojihusisha na ngono, kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Share:

Wassira akimbilia Mahakama ya Rufaa kumpinga Bulaya

WAZIRI mwandamizi wa serikali ya Tanzania kwa awamu nne za uongozi, Stephen Masato Wassira, kupitia kwa wafuasi wake watatu, amekata rufaa Mahakama ya Rufaa, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kuhalalisha ushindi wa Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema).

Wassira (71 ) alikuwa waziri kwa mara ya kwanza tangu Desemba 07, 1973 akiwa naibu waziri wa Kilimo na ameendelea kuwa kiongozi mwandamizi wakati wa serikali ya Mwalimu Julius Nyerere, akarithiwa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, baadaye Rais Benjamin Mkapa na hatimaye uongozi wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete.

Tayari wafuasi hao wa Wassira; Magambo Masato, Matwiga Matwiga na Ascetic Malagaila, wamefungua kesi hiyo na imesajiliwa katika ofisi za mahakama ya rufaa jijini Mwanza tarehe 16 Desemba, 2016 na itakuwa ni kesi ya rufaa namba 199 ya mwaka 2016.

Katika rufaa hiyo iliyoandikwa na wakili wao, Constatine Mutalemwa, wametoa sababu kadhaa kama hoja zao za kukata rufaa.

Kwanza, wanadai kwamba jaji hakuzingatia makosa yaliyofanyika baada ya zoezi la kupiga kura.

Pili, Wassira au wakala wake wanadai hakuitwa kwenye majumuisho kujulishwa siku, mahali wanafanyia majumuisho.

Tatu, wanadai kuwa jaji hakutilia maanani kesi zinazofanana na hii zilizotolewa kama mfano mahakamani.

Nne, Jaji alikosea kutoa uamuzi kwa misingi ya maoni binafsi badala ya kuzingatia mambo ya maana.

Wanadai kuwa jaji alisema wananchi wa Bunda ni maskini waachwe wafanye shughuli za maendeleo kwa sasa.

Tano, wanadai jaji alikosea kuamua kuhusu sheria ya viapo na matamko iliyotajwa katika kanuni za kuendesha kesi za uchaguzi.

Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitoa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wassira (CCM).

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, mkoani Mara.

Mahakama hiyo ilieleza kutoridhishwa na ushahidi wa kupinga matokeo hayo uliowasilishwa na upande wa walalamikaji, hivyo ikamthibitisha Bulaya kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.

Kesi ya kupinga matokeo hayo ilifunguliwa na wafuasi wa Wassira ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuondolewa kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Katika kesi ya msingi, walalamikaji ambao ni wakazi wa Bunda walidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kwakuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanaemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.

Katika kesi hiyo, Bulaya alitetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
Credit: FikraPevu
Share:

Bodi ya Mikopo yawatosa Watanzania wanaosoma China

Watanzania waliopata ufadhili wa kusoma nchini China, hawatapata mikopo baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwaondoa kwenye orodha ya wanufaika. 
Taarifa iliyotolewa na HESLB, ikijibu Ubalozi wa Tanzania nchini China, kuhusu madai ya kuchelewa kwa fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaosoma nchini humo imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwamba wanafunzi wote wanaopata ufadhili kutoka nchi rafiki watajitegemea ikiwamo gharama za tiketi za ndege.

Barua hiyo ya Desemba 20, 2016 iliyomnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Razaq Badru inaeleza kuwa mwaka huu wanafunzi hao hawatanufaika na mikopo kama ilivyokuwa ikitolewa miaka ya nyuma.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari, Badru aliitambua barua hiyo huku akisita kutolea ufafanuzi wake kwa madai ilikuwa ni majibu kwa wanafunzi hao wa China.

Hata hivyo, alisema endapo kutakuwa na madai kutoka kwa wanafunzi hao watalazimika kutolea ufafanuzi.

Akizungumzia suala hilo Naibu Waziri Elimu, Stella Manyanya alisema ni hekima zaidi kuangalia au kusaidia wanafunzi wa ndani wasiokuwa nacho kuliko wanaopata ufadhili wa nje ya nchi.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger