
Muonekano wa miundombinu ya barabara inayoendelea kutekelezwa na TANROADS Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Ruvuma.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, Saleh Juma, amewataka wananchi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutunza na kulinda miundombinu ya barabara, ikiwemo taa na alama mbalimbali.
Amesema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga barabara, hivyo wananchi wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu kwa muda mrefu.
Aidha, Saleh ameeleza kuwa TANROADS imebaini ongezeko la wizi wa alama za barabarani, ambazo zinauzwa kama chuma chakavu, hali inayohatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Amesema kuwa kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama Barabarani, wameweka mikakati ya kuwadhibiti wahalifu wanaoharibu miundombinu hiyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Pia, ametaja changamoto ya magari mazito yanayosafirisha makaa ya mawe kupitia barabara zisizo na uwezo wa kubeba uzito mkubwa, jambo linalosababisha uharibifu wa barabara na madaraja.
Ametoa mfano wa barabara ya Nangombo–Chiwindi, ambapo daraja la Nangombo limeanza kuchakaa kutokana na mzigo mkubwa wa magari yanayopita eneo hilo.
Wananchi wa Ruvuma wametoa wito kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaojihusisha na wizi wa alama za barabarani.
Ali Mselem, mfanyabiashara wa soko la Bombambili, amesema wizi huo unaweza kusababisha ajali, huku Baraka Komba akisema kuwa wahusika wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kudhibiti uhalifu huo.
0 comments:
Post a Comment