
Na Lydia Lugakila-Bukoba
Vijana Katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wametakiwa kuachana na makundi mbali mbali yasiyofaa ikiwemo ikiwemo kujiingiza katika tamaa za kujipatia fedha za mkato bila kuwajibika, kukaa vijiweni, kujihusisha na madawa ya kulevya.
Kauli hiyo imetolewa na Mchungaji Peter Mayengo wa Kanisa la Moravian Jimbo la Ziwa Tanganyika muda mfupi kabla ya semina ya ujasiliamali iliyolenga kuwanoa watu wa rika zote hasa vijana iliyofanyika kanisani hapo.
Mchungaji Mayengo amesema vijana wanatakiwa wajifunze neno la Mungu na kufanya kazi huku akikili kuwepo kwa vijana wavivu ambao wamejikuta kutamani vitu vingi kwa wakati ambapo sio sahihi kwa namna yake.
"Vijana pia wamejikuta wakitoa lugha za matusi, wapo pia wanaoingia kwenye madawa ya kulevya na wana makundi ya ajabu yasiyoleta mafanikio katika Taifa"amesema mchungaji Mayengo.
Mtumishi huyo wa Mungu ameongeza kuwa inaumiza kuona vijana wengi wa Bukoba wanakaa katika vijiwe vya Kahawa na Wazazi hawawakemei jambo linalosababisha kutengeneza vijana na Taifa ambalo linaenda kuharibika.
Amesema ni wakati sasa Wazazi na Watumishi wa Mungu kusimama vizuri katika kurekebisha vijana hao ki maadili ili kuwa naTaifa bora.
Aidha amesema malalamiko juu ya Vijana kukengeuka ki maadili ni mengi huku jamii ikishindwa kuelewa chanzo ni nini.
"Wazazi wanatakiwa kuwatengeneza vijana katika maadili pia Watumishi wa Mungu kuchukua nafasi ya pekee katika kutoa mafunzo ya neno la Mungu ili hofu iwe ndani yao"amesema Mayengo.
Hata hivyo amewahimiza vijana kujikita katika masuala ya ujasiriamali ili wapate ujuzi utakao wasaidia kwa maisha ya baadae huku akiiomba Serikali pia kuona namna ya kuwasaidia vijana wenye ujuzi ili kuwa na Taifa lenye wataalam wengi.
0 comments:
Post a Comment