Saturday, 22 March 2025

ACHENI MIGOGORO NDANI YA CHAMA, CHAPENI KAZI – ODDO MWISHO

...
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza na wananchi na wanachama Kata ya Namiungo Wilayani Tunduru

Na Regina Ndumbaro  - Tunduru .

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amewataka viongozi wa chama hicho kuacha migogoro na badala yake waelekeze juhudi zao katika kuwahudumia wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Tarafa ya Nakapanya, Wilaya ya Tunduru, Oddo amesisitiza umuhimu wa mshikamano ndani ya chama ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi.

Ziara hiyo ilihusisha mazungumzo na wanachama wa CCM kutoka kata nane, ambapo aliwataka viongozi wa chama kuwaelimisha wanachama kuhusu umoja na ushirikiano kwa ajili ya ustawi wa chama na wananchi.

Katika hotuba yake, Oddo Mwisho ametoa rai kwa viongozi wa chama kushirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wananchi.

Amewakumbusha wenyeviti wa vijiji na mitaa kuwa na vikao vya mara kwa mara kwa mujibu wa taratibu, huku akisisitiza kuwa madiwani wana wajibu wa kusimamia mikutano hiyo.

Aidha, amewataka viongozi wa kata kuwahimiza watendaji wa vijiji kufanya mikutano na kuhakikisha haki na sheria vinafuatwa katika uongozi.

Pamoja na kuhimiza mshikamano ndani ya chama, Oddo Mwisho ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu, huduma za afya, maji, na umeme.

Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, akitolea mfano ujenzi wa madarasa, madawati, na vyoo safi katika shule za msingi, kama vile Shule ya Msingi Ligoma.

Pia amewahimiza wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na kuzilinda kura zake katika uchaguzi ujao.

Katika mkutano huo, wananchi wamepata nafasi ya kueleza changamoto zao, miongoni mwao Yasin Omar aliuliza kuhusu ubovu wa barabara ya Mindu-Ngapa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma amejibu kuwa watawasiliana na mamlaka husika, ikiwemo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ili kuhakikisha barabara hiyo inafanyiwa matengenezo.

Aidha, Ausi Mohamed ameuliza kuhusu changamoto ya mikopo kwa wananchi, ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Hairu Musa, ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto katika upatikanaji wa mikopo hiyo, lakini amesisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wananchi ili waweze kunufaika na fursa hiyo.

Oddo Mwisho amewataka wanachama wa CCM kufikiria maendeleo badala ya kugombania nafasi za uongozi kwa sasa.

Amesisitiza kuwa huu si wakati wa malumbano, bali ni kipindi cha kujenga mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo katika jamii.

Pia amewahakikishia wananchi kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa suluhisho kwa wakati.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza na wananchi na wanachama Kata ya Nakapanya Wilayani Tunduru

Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger