Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara ndg Mobutu Malima akizungumza na wajumbe wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara 

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Masasi Mohamed Lawa
Bi Mariam Kasembe Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya Masasi
Na Regina Ndumbaro - Masasi.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Ndg. Mobutu Malima, amewataka wanachama wa CCM wilaya ya Masasi kuepuka siasa za makundi ndani ya chama, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Masasi, Malima amesisitiza umuhimu wa mshikamano na umoja ndani ya chama ili kuhakikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao.
Ameonya kuwa siasa za makundi zinaweza kudhoofisha chama na kuhatarisha mafanikio yake.
Katika hotuba yake, Malima pia amewataka wanachama kuwa waangalifu na wale wanaotangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwa ni pamoja na ubunge na udiwani akisemavbaadhi ya watia nia wamekuwa wakizunguka majimboni na kuwalaghai wanachama, jambo ambalo halikubaliki.
Amewatahadharisha watia nia hao kuacha mara moja tabia hizo, kwani tayari wamebainika na chama hakitasita kuchukua hatua kali dhidi yao.
Amesema CCM ina taratibu zake za kupata viongozi na hakuna haja ya kufanya kampeni za chinichini kabla ya wakati rasmi.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi, Bi Mariam Kasembe, amemshukuru Katibu wa Mkoa kwa hotuba yake yenye maelekezo mazuri kwa wanachama akisema lengo ni kujenga chama.
Bi Kasembe amewataka wanachama wa CCM wilayani Masasi kuwa waaminifu kwa Chama na kufuata taratibu zilizowekwa ili kudumisha mshikamano.
Amesema chama hakiwezi kuvumilia vitendo vinavyoweza kusababisha migawanyiko.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama katika ngazi ya wilaya na kata, ambapo walionesha mshikamano na kueleza dhamira yao ya kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopata nafasi ya kuzungumza wameonyesha kuridhishwa na hotuba ya Malima na kuahidi kushirikiana kwa karibu na uongozi wa chama ili kuhakikisha wanatekeleza maagizo yaliyotolewa kwa manufaa ya chama na jamii kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment