Tuesday, 18 February 2025

SERIKALI KUENDELEA KUVUTIA WAWEKEZAJI WILAYANI SONGEA

...

Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya Aviv Ltd inayojishughulisha na kilimo cha zao la kahawa katika kijiji cha Lipokela Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Hamza Kassim kushoto akiwaonyesha baadhi ya kampuni hiyo miche bora
Sehemu ya Shamba la Aviv Ltd lililopo katika kijiji cha Lipokela Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.
Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya Aviv Ltd Hamza Kassim akiwaongoza baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni.

Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 blog Songea 

Serikali Wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaotaka kuwekeza na kushiriki shughuli za maendeleo wilayani humo. 

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akitembelea shamba la kahawa la Aviv Tanzania Ltd lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 3,000 katika kijiji cha Lipokela.

Ndile amesema kuwa kampuni ya Aviv Ltd imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi tangu ilipoanza shughuli zake, ambapo mwaka jana pekee ililipa zaidi ya Shilingi milioni 700 kama mapato kwa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutokana na mauzo ya kahawa, fedha zilizotumika kufadhili shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.

Amebainisha kuwa kutokana na mafanikio hayo, serikali itaendelea kushirikiana na halmashauri zake kujenga mazingira mazuri kwa wawekezaji, kuhakikisha hawakumbwi na vikwazo vinavyoweza kuathiri ulipaji wa mapato na kusababisha halmashauri kushindwa kujiendesha.

Ndile amesifu ubora wa kahawa inayozalishwa katika shamba la Aviv, akisema ina ladha bora zaidi kuliko kahawa kutoka mikoa mingine nchini, na kuongeza kuwa Wilaya ya Songea ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa kilimo kutokana na ardhi nzuri na mazingira yanayofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Wilaya ya Songea, kwa mujibu wa Ndile, ni ghala kuu la hifadhi ya chakula nchini, hivyo akawahimiza wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo na uwekezaji. 

Amemtaja pia mwekezaji mwingine, kampuni ya Ndolela Farm katika Halmashauri ya Madaba, ambayo imepewa hekta 500 kwa kilimo cha mahindi na ngano inayotumika kama chakula na malighafi ya kutengeneza bia.

Meneja Uzalishaji wa Aviv Ltd, Hamza Kassim, amesema kuwa shamba hilo huajiri wafanyakazi kati ya 4,000 hadi 5,000 wakati wa msimu wa mavuno, hali inayochangia ajira kwa wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini na kuongeza mapato ya serikali kupitia halmashauri na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Baadhi ya wananchi waliopata ajira katika shamba hilo walisema limewasaidia kujikwamua kiuchumi. Yovitha Komba kutoka Ruvuma alieleza kuwa ajira aliyopata imemwezesha kusomesha watoto, kulipa michango na kujenga nyumba ya kuishi, huku akiitaka serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.

Rashid Mrope kutoka Masasi, Mkoa wa Mtwara, amesema anajivunia kufanya kazi katika Aviv Ltd kwani amepata fursa za kuboresha maisha yake na kujikwamua na umaskini kupitia ajira anayopata shambani hapo.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger