Friday, 7 February 2025

MAFUNZO YA URAIA, UTAWALA BORA YAHITIMISHWA KILIMANJARO

...



Na Dotto Kwilasa, KILIMANJARO

Hatimaye timu ya wataalam wa mafunzo ya Uraia na utawala bora imehitimisha ziara yake mkoani Kilimanjaro safari iliyoanzia mkoani Mtwara.

Wakili wa Serikali Mkuu na Mratibu wa Mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Prosper Alexander Kisinini,amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa walengwa.

Amesema washiriki wote wameonesha kwamba walikuwa na kiu ya mafunzo na wamevutiwa na ufanisi wa mafunzo yaliyofundishwa.

Kisinini amesema lengo kuu la mafunzo haya ni kuhakikisha kila raia anapata elimu kuhusu haki zake, wajibu wake, na namna ya kushiriki kikamilifu katika ulinzi na usalama.

Akieleza tathmini ya jumla kuhusu mafunzo hayo, Kisinini amesema yataenda kuwajengea uwezo washiriki kwa kujituma na kuwa na ari ya kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuelimisha wananchi kuhusu misingi ya utawala bora na umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali.

"Washiriki wa mafunzo wametuahidi kuibadilisha jamii kupitia mafunzo haya,hii ni ishara ya kwamba walengwa watatekeleza mafunzo hayo kwa vitendo na hivyo kukuza utamaduni wa utawala bora miongoni mwa jamii, " amefafanua

Halikadhalika amesema washiriki hao wameonesha kuwa na kiu ya mafunzo na wameishauri Wizara hiyo kuwa mafunzo hayo yawe endelevu kwa kutanua wigo wa mafunzo kwa viongozi wengi zaidi wakiwemo madiwani, watendaji wa vijiji na Wenyeviti wa Vijiji.

"Tumewasisitiza kwamba maoni yao tumeyapokea na tutayawasilisha ili kuhakikisha mafunzo haya yanaendelea kuwafaidisha watu wengi ziaidi, " ameongeza Kisinini.

Pia amewashukuru wadau ambao wameshirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuanzia Mkoani Mtwara hadi kuhitimishwa kwake mkoani Kilimanjaro wakiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Tume ya Haki za Binadamu, kwa kuunga mkono juhudi za kuhamasisha ujenzi wa utawala bora na uwajibikaji.

Miongoni mwa watoa Mada katika mafunzo hayo, Wakili wa Serikali ASP Nicholas Mhagama amesema kwa tathmini kabla ya mafunzo, wengi wa Watendaji hawakuwa wanafahamu wajibu wao wa kisheria kwenye suala la ulinzi na usalama.

"Ni wacheche waliokuwa na uelewa na baada ya mafunzo kila mtu ana uelewa wa ulinzi na usalama na wote kwa pamoja wameahidi kushirikisha jamii na kuwa na jamii salama," ameeleza Mhagama.

Naye Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Agness Mabago, ameeleza kuwa Watendaji wa Serikali wanatakiwa kufahamu kuwa waajiri wao ni wananchi, kwa kuwa ndiyo walioiweka Serikali madarakani, hivyo wanayo haki ya kupata huduma nzuri.

"Na sasa tunaimani na Watendaji hawa kwa kuwa wamestawi na watashuka chini kuwahudumia Wananchi kwa haki, kwa kufuata kanuni, sheria na miongozo yao," amesema Mabago.

Kwa upande wake Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Julina Laurent, ameeleza kuwa kwa mikoa yote miwili, yaani Mtwara na Kilimanjaro, mafunzo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Amesema, "Ni matumaini yetu kwamba viongozi waliopata mafunzo haya wataenda kutenda haki katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii namna ya kujitoa kulinda usalama na hatimaye kuwa jamii inayojali na kutii usawa wa haki za binadamu."

Pamoja na Mambo mengine,mafunzo haya ya Uraia na Utawala Bora ni muhimu kwa kuboresha ushiriki wa wananchi katika utawala wa nchi, huku wakisisitiza misingi ya uwajibikaji, usawa, na haki za binadamu.

Ifahamike wakakati wa mafunzo washiriki walijidhatiti kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii zao, huku wakitambua kwamba ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kudumisha utawala bora na ulinzi wa haki za kila mmoja.





Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger