Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
TANESCO Shinyanga imetoa onyo kwa wakulima na wananchi wilayani Kahama kuacha kulima mazao kwenye njia kuu ya umeme huku ikiwapa wiki moja wale waliolima kuondoa mazao yao kwenye njia kuu ya umeme ili kuepuka madhara ya umeme.
Hii ni sehemu ya juhudi za TANESCO kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza miundombinu ya umeme, ili kuepusha madhara na kuongeza usalama.
Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Bw. Paul Maisori, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa za watu wanaohujumu miundombinu ya umeme, hususan wale wanaoharibu kwa kuiba vyuma na nati kutoka kwenye nguzo za umeme.
Amewahimiza pia wakulima kuondoa mazao yao haraka, akieleza kuwa maagizo ya awali yalishatolewa, lakini bado baadhi ya wananchi wamekuwa wakikaidi.
“Watakaobainika kuwa bado na mazao yao kwenye maeneo hayo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani,” amesema Bw. Maisori.
Kwa upande mwingine, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Victory Senge, amesisitiza kuwa miundombinu ya umeme ni muhimu na inahitaji uangalizi wa pamoja.
Amefafanua kuwa wananchi walishalipwa fidia kwa maeneo yao, hivyo wanapaswa kuzingatia maagizo ya serikali na kuacha kulima kwenye njia kuu ya umeme ili kuepusha madhara.
TANESCO inasisitiza ushirikiano wa wananchi katika kutunza miundombinu ya umeme, na wale watakaokiuka maagizo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
0 comments:
Post a Comment