Thursday, 27 February 2025
KIKAO CHA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA LISHE CHAFANYIKA RUVUMA
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza na watumishi wa sekta mbalimbali ikiwemo Afya waliokuja kwenye kikao hicho cha mpango harakishi na shirikishi wa tathmini ya mpango wa bajeti ya lishe
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Louis Chomboko akiwasilisha mpango harakishi na shirikishi wa kupunguza udumavu na utafiti wa hali ya udumavu na viashiria vyake
Afisa lishe Mkoa Joyce Cosmas Kamanga akitoa taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2024
Baadhi ya Watumishi wa serikali kutoka sekta za afya na viongozi wa serikali wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pichani hayupo kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai-Disemba 2024.
Na Regina Ndumbaro - Songea Ruvuma.
Kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024 kimefanyika katika Ukumbi wa Chandamali, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, ambaye alithibitisha ajenda za kikao hicho.
Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kutathmini hali ya lishe katika mkoa huo, hususan kwa watu wanaokabiliwa na tatizo la udumavu, na kuweka mikakati ya kupunguza changamoto hiyo.
Katika kikao hicho, takwimu za hali ya lishe ziliwasilishwa kwa kila wilaya ya mkoa wa Ruvuma.
Mkoa huu una jumla ya wilaya tano, zikiwemo Manispaa ya Songea, Tunduru, Mbinga, Nyasa, na Namtumbo.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa Manispaa ya Songea ina mashine tatu za usindikaji wa lishe, viwanda 34, na shule mbili za sekondari—Songea Girls na Songea Boys.
Halmashauri ya Tunduru ina mashine moja, Madaba mashine moja, wakati Mbinga Mji na Nyasa hazina mashine za usindikaji wa lishe na Wilaya ya Namtumbo, ambayo awali haikuwa na mashine, sasa ina mashine tatu.
Sababu mbalimbali zinazoathiri lishe na kusababisha udumavu katika mkoa wa Ruvuma zilijadiliwa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, kikao kilielekeza juhudi za kufanya tafiti za kina katika kila wilaya ili kubaini chanzo halisi cha tatizo.
Matokeo ya tafiti hizo yatasaidia kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha hali ya lishe na kupunguza udumavu katika jamii.
Afisa Lishe wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Joyce Cosmas Kamanga, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024.
Taarifa hiyo ilihusisha tathmini ya hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha lishe pamoja na changamoto zilizopo.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo katika kupambana na tatizo la udumavu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Louis Chomboko, amewasilisha mpango harakishi na shirikishi wa kupunguza udumavu katika mkoa huo.
Pia, amewasilisha utafiti wa hali ya udumavu na viashiria vyake, akibainisha maeneo yanayohitaji uingiliaji wa haraka ili kuboresha hali ya lishe kwa watoto na makundi mengine yaliyo hatarini.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa, Victory Nyenza, amewasilisha taarifa ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).
Programu hiyo imelenga kuhakikisha kuwa watoto wanapata lishe bora na malezi sahihi tangu utotoni ili kudhibiti tatizo la udumavu na madhara yake ya muda mrefu.
Kikao kilihitimishwa kwa majadiliano kati ya washiriki, ambapo maswali yaliulizwa na kujibiwa na wataalamu wa lishe, afya, na ustawi wa jamii.
Hatimaye, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, alifunga rasmi kikao hicho huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kutekeleza mipango ya lishe kwa maendeleo ya jamii na afya bora ya wananchi.
BALOZI NCHIMBI AWASILI NAMIBIA MSIBA WA SAM NUJOMA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasili nchini Namibia, akiongoza ujumbe wa CCM kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Namibia na Baba wa Taifa hilo, Dkt. Sam Shafiishuna Nujoma, yatakayofanyika tarehe 1 Machi, 2025.
Balozi Dkt. Nchimbi pamoja na msafara wake aliongozana nao, ambao pia yumo Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Abdalla Hamid, aliwasili Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Hosea Kutako, jijini Windhoek, na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Mhe. Caesar Waitara, tarehe 26 Februari 2025.
Balozi Nchimbi atashiriki ratiba mbalimbali za utoaji wa heshima za mwisho na kumuaga Dkt. Sam Nujoma, kuanzia tarehe 27 Februari 2025, ambapo Chama Tawala cha Namibia, SWAPO, ambacho ni rafiki wa kihistoria wa CCM, kimeandaa shughuli kwa ajili ya heshima ya mwasisi wake huyo.
Baada ya hapo, Balozi Nchimbi atashiriki ibada ya kitaifa ya kumuaga Hayati Dkt. Nujoma iliyopangwa kufanyika tarehe 28 Februari 2025, kabla ya shughuli ya mazishi ya kitaifa itakayofanyika tarehe 1 Machi 2025, katika eneo la makaburi ya mashujaa, yaliyoko makao makuu ya nchi hiyo, jijini Windhoek
Uhusiano kati ya Namibia na Tanzania, halikadhalika CCM na SWAPO na watu wa nchi hizo mbili, ni wa kihistoria, ukiwa umejengwa katika misingi imara tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru dhidi ya wakoloni na makaburu.
Itakumbukwa kuwa Hayati Dkt. Nujoma na viongozi na wanachama wengi wa SWAPO na Namibia waliishi maeneo mbalimbali uhamishoni nchini Tanzania, tangu miaka ya 1960, wakishiriki mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao, ambako pia ndipo walipoanzisha Chama cha SWAPO ili kuendesha shughuli za kuikomboa nchi yao kisiasa, hadi walipopata uhuru mwaka 1990.
Wednesday, 26 February 2025
WILDAF YAWAOKOA NA VITENDO VYA UKATILI ZAIDI YA WASICHANA 700 KUTOKA MIKOA YA SHINYANGA NA MARA, CANUCK YAAHIDI KUSHIRIKIANA NAO
Mkuu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center) Father John akipokea zawadi kutoka kwa wahitimu wa mahafali ya 25 ya chuo hicho.Shirika la Wanawake katika sheria na Maendeleo Barani Afrika(WilDAF) kwa kushirikiana na UN-FPA kwa ufadhili wa serikali ya Finland, kupitia mradi wa ‘Chaguo langu haki yangu’ limefanikiwa kuwaokoa mabinti balehe na vijana wamama zaidi ya 700 kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Afisa mradi wa mradi wa chaguo langu haki yangu Joyce Kessy katika mikoa ya Mara na Shinyanga amesema mradi huo unalenga kuwafikia mabinti balehe na wanawake vijana kati ya umri wa miaka 10-19 na 15 – 24, kuwalinda dhidi ya ukatili, ndoa na mimba za utotoni pamoja na ukeketaji kwa mkoa wa Mara.
Ameyazungumza hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo mabinti balehe na wanawake vijana zaidi ya 270 wamehitimu na kutunukiwa vyeti vyao tayari kwa kujiajiri/kuajiriwa.
Bi Kessy amesema mradi huo pia umelenga zaidi wenye ulemavu katika makundi hayo kwani wanaonekana kusahaulika zaidi na jamii, huku likiwa katika uhatarishi mkubwa wa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema WiLDAF kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la idadi ya watu ulimwenguni UNFPA kwa ufadhili wa serikali ya Finland, iliona suala kubwa ni kutoa nafasi kwa wale waliopo nje ya shule kujiunga na vyo vya VETA ikiwemo VTC Mwakata ili kujifunza fani tofauti tofauti ili wawe na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa ili kujikwamua kiuchumi hali itakayowasaidia kuepukana na vitendo vya ukatili.
“Kama tunavyofahamu kwamba uchumi duni unachangia kwa kiasi kikubwa sana vitendo vya ukatili, kwa hiyo sisi tunamwezesha binti kiuchumi, tunampa ujuzi, ili aweze kuinuka kiuchumi kama nyenzo ya kujikwamua dhidi ya vitendo vya ukatili” Alisema Kessy
Amesema wahitimu hao baada ya mafunzo wanawapatia vifaa kulingana na fani walizosomea ili waweze kutekeleza ujuzi wao kwa vitendo na kubadilisha maisha yao, na kwamba mabinti hao 787 wamefikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi wa “Chaguo langu, haki yangu” uliotekelezwa katika wilaya mbili za mkoa wa Mara(Butiama na Tarime) na mbili za mkoa wa Shinyanga (Kishapu na Kahama).
Kati ya mabinti hao 263 wameshapatiwa vifaa na kwamba waliobaki wanakwenda kupatiwa vifaa vyao hivi karibuni kulingana na fani husika baada ya awamu hii ya mwisho kuhitimu, na kueleza kuwa mambo haya yote yanafanyika kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya serikali ya manispaa ya Kahama, wakati wa mahafali hayo, afisa ustawi wa jamii kutoka manispaa hiyo Swahiba Chemchem alisema kuwa, serikali iko tayari kuwaunga mkono mabinti hao hata wanaporejea mtaani, sambamba na kuwaunganisha na fursa mbalimbali zitakazojitokeza.
Baadhi ya wahitimu Vaileth Charles mhitimu wa fani ya ushonaji kutoka Kishapu, aliishukuru WiLDAF kwa kuwawezesha kutimiza ndoto zao na kuwaomba waongeze muda zaidi wa utekelezaji wa mradi huo kwa mabinti wengi bad oni wahanga wa ukatili haswa mimba na ndoa za utotoni, sambamba na wao kutokuwa tegemezi.
Awali akisoma risala ya wahitimu kwa niaba ya wahitimu wenzake, kwa mgeni rasmi, ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu – Canuck Clarence Haule, mhitimu Debora Martin amelishukuru shirika la WiLDAF, uongozi wa chuo pamoja na serikali kwa kuwapatia fursa hiyo, ambayo imewasaidia kupata ujuzi mbalimbali, utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa, huku wakiomba zinapotokea fursa mgodini hapo basi viongozi wasisite kuwapa kipaumbele.
Kwa upande wake Mwalimu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center) Mwalimu Monica Daniel akisoma historia ya chuo hicho alisema kimeanzishwa mwaka 2003, na kilianzishwa na padreJoseph Elian aliyekuwa mkuu wa chuo chini ya mkuu wa shirika la Mt Fransisco wa sales.
Mwalimu Monica alisema chuo kimefanikiwa kuwajengea uwezo mzuri wanafunzi wao ikiwemo tabia njema za kiroho na kuishi katika hofu ya Mungu, lakini pia chuo kimefanikiwa kuwatafutia wanafunzi wao maeneo ya kujifunza kwa vitendo baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Akizungumza kwenye mahafali hayo, mgeni rasmi ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule, kwa niaba ya meneja mkuu wa kampuni hiyo ameahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji, kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa uzio wa chuo hicho, ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo dhima ya kurejesha sehemu ya faida yake kwenye jamii inayozunguka mgodi (CSR).
Haule amesema uwepo wa uzio chuoni hapo, utasaidia usalama kwa wanafunzi, mali za chuo na kuondoa migogoro itokanayo na mwingiliano kati ya wanakijiji na chuo, huku akiutaka uongozi wa chuo kuainisha aina za mashine na gharama zake ili mgodi uone namna ya kusaidia kufanikisha jambo hilo.
Akizungumzia changamoto ya maji inayokikabili chuo hicho pamoja na maeneo jirani, Haule amesema tayari mgodi umeanza mchakato wa kupata maji safi na salama kutoka ziwa Victoria, na chuo hicho ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika zaidi na ujio wa maji hayo, na kwamba yameshafikishwa kwenye mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama – KUWASA, na sasa wanasubiri utekelezaji wao.
“Tunatambua kuwa hapa kijijini swala la upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na jamii na jamii bado ni tatizo, hivyo kampuni inawaomba wote kwa ujumla tuwe na subra kwa maana kampuni imekwishafikisha ombi la kufikishiwa huduma na KUWASA” Alisema Haule
Baadhi ya wanafunzi na wahitimu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center), wakitoa burudani, wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho

Mkuu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata , Father John akizungumza wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francis Vacation Center) ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule kushoto, akiwa na mmoja wa wazazi wa wahitimu, wakiwatunza watumbuizaji.

mkurugenzi wa WiLDAF akizungumza na wahitimu pamoja na wazazi kwenye mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata

Wahitimu wa fani ya umeme katika chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francis Vacation Center) wakionyesha kwa vitendo kile walichojifunza wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho mbele ya mgeni rasmi ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francis Vacation Center) ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule kulia akitoa vyeti kwa wahitimu.

Matron wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francia Vacation Center) Magreth Alimosa, akiongoza zoezi la ukataji wa keki ya mahafali ya 25 ya VTC Mwakata kwa wahitimu na wageni waalikwa.























