Wednesday, 15 January 2025

WIZARA YA NISHATI YAWASILISHA UTEKELEZAJI WA BAJETI 2024/2025 KATIKA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI

...
📌 Maeneo ya kipaumbele yaliyotekelezwa kwa mwaka 2024/2025 yaelezwa

📌 Ni pamoja na hali ya uzalishaji na upatikanaji wa Nishati ya Umeme nchini

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (Mb) ameongoza Menejimenti ya Wizara ya Nishati kuwasilisha taarifa utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2024/2025 katika Kipindi Cha Julai hadi Desemba 2024 katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Taarifa hiyo imewasilishwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Nishati Petro Lyatu ambaye ameeleza kuwa Wizara ya Nishati  imetekeleza bajeti katika maeneo mbalimbali  ikiwa ni yale ya kipaumbele na kimkakati pamoja na kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji ,usafirishaji na usambazaji wa Umeme Ili kuufikisha gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia.

Amesema Wizara imeendelea kupeleka nishati Vijijini ikiwemo kusambaza umeme katika vitongoji Tanzania Bara pamoja na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwa ni sambamba na mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika.

Amesema Wizara ya Nishati inaendelea kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaokidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii, ikiwa ni pamoja  na kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa na kuongezeka kufikia Megawati 3,091.71 mwezi Desemba,2024.

Amesema ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali hususani Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Julius Nyerere ambapo hadi Desemba 2024 mitambo mitano (5) kati ya tisa ilikuwa imekamilika na inazalisha umeme na kuingizwa katika Gridi ya Taifa.

Vile vile, Lyatu amebainisha kuwa Wizara imekamilisha Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati (2024/2025) mwezi Novemba 2024 ambao ulizinduliwa Desemba 3, 2024 wakati wa Kongamano la Kikanda katika Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) la Matumizi Bora ya Nishati, Mkakati ambao  pamoja na masuala mengine unalenga kuendelea kuhakikisha Watanzania kutumia Nishati kwa ufanisi Ili kupunguza gharama za Matumizi pamoja na kuendelea kuimarisha upatikanaji na Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia. 

Mwenyekiti wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini  Dk. David Mathayo David baada ya kupokea taarifa amesema kuwa  "Wizara Haina budi kuendelea  kuunga mkono Sera ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia kwa Watanzania,kwa kuendelea kufanya tafiti, kuhamasisha watumiaji, kutoa elimu na kuanzisha sheria ya kulinda miundombinu mbalimbali ya nishati ya kupikia na kuhakikisha gesi kwa watumiaji inapatikana kila Kona ya Tanzania".

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger