Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene leo amezungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, na kutangaza kuwa kuanzia tarehe 14 Januari hadi terehe 24 Februari, 2025, usaili wa kada za Ualimu utaendeshwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (UTUMISHI); Ofisi ya Rais (TAMISEMI); Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Afya; Tume ya Utumishi wa Walimu; Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma.
"Usaili huu una lengo la kujaza nafasi elfu kumi na nne mia sita na arobaini na nane (14,648) zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini.
Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwasihi sana wale wote walioitwa kwenye usaili wajiandae vyema kwa usaili huo kwani nafasi hizi ni za ushindani.
"Vilevile, kulingana na mahitaji yetu ya elimu kwa sasa, tutaajiri wataalamu wa fani za Amali. Hivyo, nawasihi sana wale wote watakaopata nafasi ya kuajiriwa, wawe tayari kujiendeleza ili kuweza kukidhi matakwa ya ajira zao katika Utumishi wa Umma." alisema Waziri Simbachawene.
Mhe. Simbachawene amesema kuwa usaili huu wa kada za Ualimu utafanyika katika Mkoa ambao kila msailiwa anaishi. Lengo kuu la utaratibu huu ni kuwapunguzia gharama za kusafiri na mambo mengine. Sekretarieti ya Ajira ilitoa matangazo kumtaka kila msailiwa kuhuisha taarifa zake katika akaunti yake ya Ajira Portal sehemu iliyoandikwa ‘current physical adress’ kwani ndipo tumewapangia vituo vya usaili kulingana na anuani walizojaza.
Aidha Mhe. Simbachawene amesema kuwa Usaili wa awali wa kuandika (Mchujo) kwa kada za Ualimu utafanyika kwa njia ya kuandika kwa mkono kwa kada zote na ngazi zote za elimu.
"Ninapenda kuwakumbusha wale wote watakaokwenda kwenye usaili wahakikishe wanabeba vyeti vyao Halisi kikiwemo Cheti cha Taaluma na Cheti cha kuzaliwa. alisema Mhe. Simbachawene
Vilevile, wasailiwa wanapaswa kuja na namba zao za usaili walizotumiwa kwenye akaunti zao za ajira portal pamoja na kuzingatia Ratiba kama ilivyopangwa na Sekretarieti ya Ajira.
Kwa wale ambao kwenye vyeti vyao vya kitaaluma wanatumia majina mawili wakati kwenye cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha NIDA kuna majina matatu (3), au wale ambao majina yanatofautiana katika vyeti, wanapaswa kuwa na hati za kiapo (Affidavit au Deed Poll) ili kuthibitisha majina yao na vyeti husika.
Wasailiwa wanapaswa kuwa na kitambulisho halisi kwa ajili ya utambuzi, Kitambulisho kinachotambuliwa ni pamoja na Kitambulisho cha Taifa (NIDA); Hati ya Kusafiria; Leseni ya Udereva; Kitambulisho cha Mpiga Kura; Kitambulisho cha Mkaazi; Kitambulisho cha Kazi; au Barua ya Utambulisho kutoka ofisi ya Serikali ya Mtaa unaoishi au Shehia.
"Ninapenda kusisitiza kwamba ni muhimu sana msailiwa kuhakikisha anakwenda katika kituo alichopangwa kwa ajili ya usaili na si vinginevyo kwani mahitaji yake yatakuwa katika kituo alichopangwa." Alisema Mhe. Simbachawene.
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 ambacho kinaelekeza kuwepo kwa chombo maalumu cha kushughulikia mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma. Pamoja na Sheria hii kutungwa Mwaka 2007, Sekretarieti ya Ajira ilianza utekelezaji wa majukumu yake rasmi tarehe 01 Machi, 2010 baada ya maandalizi muhimu kukamilika. Aidha, iliweza kuendesha usaili wa kwanza Mwezi Juni, 2010.
0 comments:
Post a Comment