NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido Mkoani Arusha,Dkt Steven Kiruswa amewataka viongozi wa Milla wa Jamii ya Kimasai maarufu kwa jina la Malaigwanani kukemea tabia ya jamii hiyo kutaka kuchagua viongozi wa kichama na kiserikali kwa kufuata makundi ya Uko na rika na kusema kuwa hiyo itawanyima watu demokrasia ya kuchagua viongozi bora na kutoa mwanya kuchaguliwa viongozi wasiokuwa bora na sifa na hivyo kusababisha makundi na migogoro ndani ya jamii.
Kiruswa alisema hayo wakati akizindua Baraza Kuu la Malaigwani la Wilaya ya Longido lililohudhuriwa na Malaigwanani zaidi ya 60. Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Mkuu wa wilaya ya Longido,Salum Kalli, Mwenyekiti wa Wilaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Papa Nakuta, viongozi wastaafu wa chama na serikali wilaya na Mkoa akiwemo Lekule Laizer, Joseph Sadira na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido,Simon Oitesoi.
Alisema Malaigwanani ni kiungo muhimu kati ya serikali na jamii ya kifugaji katika suala la kuhamasisha maendeleo na wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea hilo kwani tabia hiyo ikijengeka itazaa viongozi wasiokuwa na sifa na kutapelekea kupata viongozi wasiostahili na kuwa chimbuko kwa jamii kukumbwa na migogoro ya mara kwa mara yanayotokana na makundi ya rika,uko na ukanda, kitu ambacho ni hatari kwa ujenzi wa jamii bora yenye mshikamano na umoja.
Alisema hilo lilijitokeza katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2024 wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wilayani Longido katika baadhi ya maeneo na kuwataka viongozi wa Milla kukemea hilo kwa nguvu zote lisijirudie katika chaguzi zijazo kwani linawagawa wananchi na kuathiri demokrasia kwa kuwa baadhi ya waliochaguliwa walipatikana kupitia mihemuko ya kirika na koo.
Naibu Waziri Kiruswa alisisitiza Malaigwanani kuhakikisha wanahimiza na kuhamashisha wananchi kushiriki kazi za maendeleo ikiwa ni pamoja na kupeleka watoto shule, kusimamia
Nyanda za malisho na kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa wao ni nguzo ya jamii ya kimasai na wanaheshimika katika jamii hivyo watumie nafasi hiyo kuiongoza vyema jamii na sio vinginevyo.
Alisema huu Mwaka ni mwaka wa uchaguzi Mkuu hivyo viongozi wa Milla wanawajibu wa kutoa elimu kwa jamii kuchagua viongozi bora na waadilifu wanaoweza kuongoza jamii kwa kuhamashisha na kufanya kazi za maendeleo kwani Malaigwanani ni kiungamishi cha serikali na jamii na wana wajibu huo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido,Salum Kalli alisema yeye ana miezi minne tu toka amehamia Longido na amepata ushirikiano mkubwa toka biongozi wa Milla hivyo kurahisisha kazi yake ya kusimamia ulinzi wa usalama wa raia na mali zao ndani ya wilaya.
Kalli alisema Malaigwanani wanawajibu wa kusimamia amani na mshikamano kwa kushirikiana na serikali na amewashukuru viongozi hao kuwajibika kwa hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwani Wilaya ya Longido, Laigwanani Simon Melau Ole Mepurda alisema kikao hicho ni muhimu kwa jamii hiyo kwani kimeshirikisha wajumbe kutoka katika kata zote 19 za jimbo la Longido na akasistiza kuwa baada ya Baraza kuzinduliwa wana wajibu wa kuelimisha jamii inayowazunguka kuheshimu sheria za nchi na milla ya jamii hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha wafugaji Wilayani Longido,Joseph Sadira aliwataka viongozi wa milla kuhimiza ufugaji bora na kuuza mifugo yao katika kiwanda cha nyama kilichopo Longido kwani ndio kiwanda kinachoingiza mapato katika Halmashauri ya Longido hivyo kinapaswa kuungwa mkoano na sio vinginevyo.
0 comments:
Post a Comment