MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali hainunui korosho wala mazao mengine bali inaweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa masoko.
“Serikali hainunui korosho, Serikali hainunui pamba, wala hainunui chai au kahawa. Kazi ya Serikali ni kutengeneza fursa ili wanunuzi waje. Mtu asitumie zao la korosho ili kujipatia umaarufu wa kisiasa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Likongowele na Kibutuka wilayani Liwale ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na madiwani 20 wa kata za jimbo hilo.
“Mwaka 2018, kuna wafanyabiashara waliungana na wakagomea kununua korosho kwa sh. 1,800. Rais Dkt. Magufuli akasema hakuna kununua korosho za wakulima kwa bei hiyo, ndipo akatoa sh. bilioni 900 ili zitumike kununua korosho kwa bei isiyopungua sh. 3,000 kwa kilo.”
“Fedha hizo zimetumika kuwalipa wakulima, wasafirishaji, wenye magunia, kulipia usimamizi wa maghala na sasa imebakia kuwalipa Halmashauri ambao wanadai ushuru wa asilimia 5, na hao ni Serikali wenzetu kwa hiyo watalipwa tu. Kama kuna wakulima waliobakia ni mmoja mmoja sana, hao wanafuatiliwa na Wizara husika.”
Amesema korosho siyo zao pekee lililoathiriwa na kuporomoka kwa bei bali mazao mengine kama pamba, chai, kahawa na tumbaku nayo yameathiriwa na kushuka kwa bei mwaka huu.
“Korosho ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini yaliyokosa soko msimu uliopita baada ya mataifa ya Ulaya kufunga mipaka yao kutokana na ugonjwa wa corona na hivyo wanunuzi hawawezi kuja nchini.”
“Korosho, pamba, tumbaku, chai na kahawa hayakuwa na bei nzuri kutokana na corona si vinginevyo. Serikali hainunui mazao, kazi yake ni kutengeneza mazingira mazuri ya soko asije mtu akawadanganya na kutumia bei za mazao ili apande chati kisiasa,” alionya.
Akitoa mfano, Mheshimiwa Majaliwa amesema: “Bei ya pamba imeshuka kutoka sh. 1, 200 hadi sh. 800 kwa kilo; kahawa imeshuka kutoka sh. 1,800 has sh. 1,200 kwa kilo, na tumbaku imeshuka kutoka sh. 1,700 hadi sh. 1,400.”
“Wanunuzi wakubwa wa korosho wanatoka China, Singapore, Vietnam na India. Hawa wenzetu sasa hivi bado wameelemewa na ugonjwa huu, hawawezi kutoka na kusafiri. Tuwaombee nchi zao ziondokane na corona ili na sisi tuweze kufanya biashara na nchi nyingine,” alisisitiza.
(mwisho)
0 comments:
Post a Comment