Tuesday 7 July 2020

Serikali Kufuta Ada Ya Usajili Kwa Watoa Huduma Ya Msaada Wa Kisheria Ili Kusogeza Huduma Kwa Wayonge

...
NA TIGANYA  VINCEN
SERIKALI inafanyia kazi wazo la kufuta ada ya usajili kwa watoa huduma ya watoa  msaada wa kisheria na Wasaidizi wa Msaada wa kisheria ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia  wananchi wanyonge kwa wingi mahali walipo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inawafikia wananchi wanyonge walipo na wanapata haki zao kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa  jana Mkoani Tabora na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Amon  Mpanju wakati akizindua Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa.

Alisema pamoja na wazo hilo ni  lazima watoa huduma hao  wakaendelea kuzingatia taratibu nyingine zilizoanishwa katika Sheria na kanuni ili waweze kuwafikia wananchi wanyonge.

Mpanju alisema ni vema watoa huduma hizo zikasaidia kutatua kwa haraka migogoro ya wananchi wanyonge ili watumie muda mwingi katika uzalishaji badala ya kuwa Mahakamani.

Alisisitiza kuwa Watoa huduma za Msaada wa Kisheria na wasaidizi wa msaada wa Kisheria ni sawa na viongozi wa dini ambao wanatakiwa kutoa huduma kwa wananchi wanyonge ambao hawawezi kulipa gharama za Mawakili bila malipo.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora (Utumishi na Utawala) Hamis Mkunga alisema kuzinduliwa kwa Kamati hiyo kutasaidia kutatua migogoro ambayo wakazi wa Mkoa huo wamekuwa wakikabiliana nayo ambao kipato chao ni kidogo.

Aliongeza kuwa wapo wengi walikuwa wakipoteza haki zao na kudhulumiwa mali zao kama vile mashamba kwa sababu ya ukosefu wa fedha na kulipa Wakili na wengine kwa sababu ya kuishi mbali na vyombo vya utoaji haki.

Msajiri Msaidizi (LAPS) Mkoa wa Tabora Panin Kerika alisema katika wiki ya Sheria ya Mwaka 2018/19 , Mkoa ulikuwa na jumla ya mashauri 358 ambayo yaliweza kusikilizwa.

Alisema kati ya hayo 181 yalihusu migogoro ya ardhi, 62 matunzo ya watoto, 58 masuala ya mirathi, ukatili wa kijinsia matatu, migogoro katika ndoa yalikuwa 21, madai 15, migogoro katika masuala ya kazi 8 na jinai 10.

Mwisho


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger