Tuesday 7 July 2020

Bodi ya Mkonge Kuanzisha Vitalu vya Miche, Kuwawezesha wananchi kupata fursa ya zao hilo.

...
Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO
Serikali kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini ambako zao la mkonge linalimwa imesema itaanzisha vitalu vya zao hilo ili kuwawezesha wananchi kupata mbegu baada ya kuwepo na mwamko wa wananchi kutaka kulima zao hilo.

Akizungumza katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA), Afisa Maendeleo ya Masoko wa Bodi ya Mkonge Tanzania, David Maghali alisema kuwa mwamko wa wakulima kulima zao hilo sasa ni mkubwa ndiyo maana Serikali imefikia uamuzi wa kuzalisha miche mingi ili kuwawezesha wananchi kupata fursa katika kilimo cha zao hilo.

“Mwamko wa kuongezeka kwa wakulima wa zao la Mkonge kumekuja baada ya kuongezeka kwa matumizi ya zao hilo hasa kwenye sekta ya ujenzi, kwani mkonge hutumika kutengeneza gypsam na vifaa vya Magari kwa hiyo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku”, Alisema Maghali.

Alisema kuwa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam(SABASABA), yameleta mwamko mkubwa wa wananchi wengi kujua na kujifunza fursa zilizoko kwenye zao la mkonge, ikiwemo kupata elimu juu ya kulima zao hilo, uvunaji wa zao hilo, ajira zinazoweza kutengenezwa katika zao hilo na matumizi ya zao hilo ambayo kwa sasa ni makubwa duniani, lakini pia wameweza kujifunza bidhaa mpya, matumizi mapya na fursa za uwekezaji viwanda katika eneo hilo.

Aidha Maghali aliongeza kuwa Bodi ya Mkonge Tanzania iko tayari kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ambako zao la mkonge linalimwa, kwa kushirikiana na Halmashauri TSB inaendesha zoezi ya kutengeneza vitalu ili kurahisisha upatikanaji wa miche kwa  wananchi wenye uhitaji kupata miche hiyo kwa urahisi.

Kwa Upande wake Afisa Mipango wa TSB, Fredrick Sospeter alisema kuwa zao la Mkonge lina fursa nyingi na linadumu kwa muda mrefu ambapo linamuwezesha mkulima kuvuna kwa miaka 12 mara mbili kwa mwaka baada ya kupanda na kuanza mavuno baada ya miaka mitatu.

“Ulimaji mkonge ni mzuri kwa sababu zao hili linakomaa kwa muda wa miaka mitatu na baada ya hapo mavuno yake yanachukua hadi muda wa miaka 12 kwa mkulima akiwa anavuna mara mbili kwa mwaka, maana yake akiwa anavuna baada ya miezi sita”, 

Alieleza kuwa zao hilo lina faida nyingi sana ikiwemo  mizizi yake ambayo hutumika kutengenezea madawa ya binadamu, mifugo na mimea, shina ambalo hutumika kutenegeneza juisi yenye sukari (asali) ambayo hutumiwa kwa wingi na wagonjwa wenye matatizo ya kisukari.

Vilevile majani ya mkonge hutumika kutengenezea nyuzi, Kamba, mazulia, magunia, Gypsam, karatasi za kutengenezea fedha(noti), gesi, mbolea pamoja na chakula cha wanyama.

“Zao la Mkonge lina fursa nyingi kwa hiyo wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi karibuni muwekeze katika viwanda vya kutengeneza madawa ya binadamu, mifugo, mimea, juisi yenye sukari (asali), nyuzi, Kamba, mazulia, magunia, Gypsam, karatasi za kutengenezea fedha(noti), gesi, mbolea pamoja na chakula cha wanyama ili kujenga uchumi mzuri kwa wananchi kupata ajira na wengine kulima zao hili”, Alisema Sospeter.

Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger