Na John Mapepele
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi amesema Serikali haitamfumbia macho mdau yoyote wa utoaji wa huduma ya afya ambaye atafanya kazi kwa mazoea bila kuzingatia sheria na taratibu za utoaji huduma na kwamba kuanzia sasa Serikali itakaa na kupanga kwa pamoja ili kuwapatia wananchi huduma bora wakati wote kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla.
Dkt. Lutambi amesema wakati akifungua mkutano wa maandalizi ya mpango kabambe wa afya, ustawi wa jamii na lishe Mkoa wa Singida ambapo kwa sasa kwenye Mkoa wa Singida umekuwa na wadau wengi wanaotoa huduma za afya kutokana na Serikali kuweka mazingira wezeshi lakini changamoto kubwa ni kuwa hakuna uelewa wa pamoja wa mdau gani anafanya nini katika eneo moja la utoaji wa huduma za afya.
Amesema Mkoa wa Singida ni kitovu cha nchi yetu ambapo watu kutoka sehemu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi hufika na kupita hivyo ni muhimu huduma inayotolewa katika mkoa huu kuwa katika kiwango cha kimataifa.
Aidha, amesema Mkoa wa Singida kuwa jirani na makao makuu ya nchi ni lazima uwe mkoa wa mfano katika utoaji wa huduma za afya ambapo amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida kuboresha huduma ili ifanane na hali halisi ya sasa.
Alisema ili kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na John Pombe Magufuli kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025 lazima sekta afya iratibiwe vizuri na wadau wote washirikiane na kupata namna ya utoaji wa huduma za afya ili wananchi waweze kupata afya bora.
“Ni kwa sababu hii ndiyo maana Serikali imeamua kuwakutanisha ili kujua namna bora ya kufanya shughuli hizo kwa manufaa ya taifa” alisema Katibu Tawala.
Alisema baada ya mkutano huu kila mdau atafahamu jinsi bora ya kufanya kazi baina yake na mwingine ambapo pia Serikali itatambua na kupanga ushiriki mzuri baina ya Serikali na wadau wote wa afya katika Mkoa wa Singida.
Dkt. Lutambi alisisitiza kuwa mpango huu ni nyenzo inayotumiwa na Timu ya uendeshaji wa afya mkoani Singida katika kupanga, kutekeleza, kusimamia na kutathmini shughuli mbalimbali za afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Halmashauri zote na vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya Jamii kila mwaka.
Akizungumzia ya baadhi ya mafanikio ya mpango huo kwa mwaka 2019, Mratibu wa ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi kwenye upande wa Afya Mkoa wa Singida, Dkt. Abdallah Balla alisema kumekuwa na kuongeza kiwango cha wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka 86% (2018) hadi 99% (2019) kulingana na takwimu za NBS,kuongezeka kwa wateja wapya wa njia za kisasa za uzazi wa Mpango kutoka 27.4% (2018) hadi 32% (2019).
Dkt. Balla alisema kumekuwa na kupungua kwenye kiwango cha udumavu kutoka 34% (2014) hadi 29% (2018) Kuongeza kiwango cha uchanjaji kutoka 106% (2018) hadi 117% (2019).
Aidha, upimaji wa virusi vya UKIMWI ngazi ya jamii, kwa mwaka 2019 jumla ya wananchi 35,973 walipimwa na kati yao wateja 602 (46%) ya wagonjwa wapya waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na kuunganishwa na vituo vya kutolea huduma.
Aliongeza kuwa huduma ya tohara kinga kwa wanaumie ilitolewa kwa wanaume 31008 sawa na 94% ya lengo la mwaka, ikihusisha Halmashauri zote za Mkoa wa Singida.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida Victorina Ludovick alimshukuru Dkt. Lutambi na kumhakikishia kuwa ataendelea kusimamia kikamilifu utolewaji wa huduma bora za afya katika Mkoa wa Singida.
0 comments:
Post a Comment