Baraza
la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tumepokea kwa
mshtuko mkubwa taarifa kuwa utawala huu wa Serikali ya CCM, chini ya
Rais John Magufuli zaidi ya nusu ya wanafunzi waliodahiliwa kwa ajili ya
masomo ya elimu ya juu mwaka wa masomo 2016/2017, wako katika hatari ya
kukosa fursa ya kupata elimu hiyo kwa sababu ambazo hazieleweki hadi
sasa.
Kwa
mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na vyanzo vingine, Tume ya Vyuo
Vikuu Nchini (TCU) imeweza kudahili takriban wanafunzi wapya 58,000 kwa
ajili ya elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu
wa masomo.
Lakini
katika hali ambayo tunajua itaumiza vijana wengi na kuwasikitisha
Watanzania, taarifa ambazo zimethibitishwa na Serikali ya Rais Magufuli
kupitia kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo, ni kwamba zaidi ya nusu ya
idadi hiyo ya waliodahiliwa na TCU kusoma elimu ya juu, hawatapata
mikopo!
Hivyo
ndoto za kutafuta mafanikio yao, kwa ajili ya jamii zao na taifa letu
kwa ujumla zinaelekea kukatiliwa. Hili ni jambo kubwa na zito kwa sababu
linagusa moja ya misingi muhimu ya taifa lolote lenye ndoto ya kutaka
kuendelea, achilia mbali kuwa taifa lenye uchumi wa kati unaotegemea
viwanda.
Kwa
mujibu wa Gazeti la The Guardian la Oktoba 18, mwaka huu, Serikali ya
CCM, chini ya Rais Magufuli imesema itawakopesha wanafunzi wapatao
24,000, idadi ambayo haifiki hata nusu ya wanafunzi wote waliodahiliwa
na TCU.
Hata
hivyo kauli hiyo ya Mkurugenzi wa Bodi, tumeichukulia kuwa si ya kweli
hata kidogo, bali ya mtu anayejaribu kuficha mambo kwa ajili ya “nusu
shari kuliko shari kamili”.
Tunasema
hivyo kwa sababu hadi sasa Bodi hiyo hiyo, imeshatoa mikopo kwa
wanafunzi 3,966 tu. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 6 tu kati ya
wanafunzi wote waliopata udahili wa kusoma elimu ya juu kwa mwaka huu.
Maana
yake ni kwamba kuwakopesha vijana wapatao 24,000 ili wasome elimu ya
juu bado nayo ni ahadi tu ya maneno, lakini uhalisia uliopo kwa vitendo
hadi sasa ni kwamba Serikali ina uwezo wa kuwakopesha vijana wake 3,966
pekee nchi nzima.
Idadi
hiyo ambayo serikali imeweza kuwakopesha mikopo, haifiki hata nusu ya
jumla ya wanafunzi wanaopaswa kudahiliwa na mojawapo ya vyuo vikuu
vikubwa nchini, mathalani Chuo Kikuu Dar es Salaam.
WAMEKOPESHWA CHAKULA NA KULALA, SI KUSOMA!
Aidha,
kwa muda mrefu sasa, walau tangu kuanza kwa utaratibu wa serikali
kuwakopesha wanafunzi kwa ajili ya elimu ya juu, inaeleweka kuwa HESLB
imekuwa ikitoa mikopo kwa ajili ya vitu vitatu; ada, malazi na chakula.
Katika
hali ambayo inazidi kushangaza na kuibua maswali kuwa kuna jambo kubwa
ambalo linafichwa, BAVICHA tunazo taarifa kuwa hata hao wanafunzi
asilimia 6 ambao bodi inadai imeshawapatia mkopo, katika vyuo vingi
wamepata fedha kwa ajili ya CHAKULA NA KULALA tu.
Hawajalipiwa fedha ya ada (tuition fees hadi sasa).
Kwa
mantiki hiyo ni kwamba, Serikali ya CCM, chini ya Rais Magufuli hadi
sasa wiki ya tatu tangu vyuo vifunguliwe si tu kwamba imeshindwa
kuwakopesha wanafunzi wote wanaostahili kupata mkopo kwa ajili ya elimu
ya juu, bali hata imeshindwa hata kulipa fedha za ada kwa wanafunzi
ambao tayari imeshawakopesha. Hali hii ikiendelea tutegemee kuona vyuo
vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu vikifungwa kwa sababu vitakuwa
haviwezi kujiendesha.
Taarifa
hizi za Bodi ya Mikopo zinapaswa kulishtua taifa letu na kila Mtanzania
aone jinsi ambavyo Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli
haijajipanga na wala haijui inachokifanya katika kuhakikisha inatoa
elimu bora kwa Vijana wetu.
Lakini
pia zinathibitisha kuwa Serikali ya Rais Magufuli iko katika hali mbaya
ya kifedha na hivyo inahitaji msaada wa fikra mpya nje ya CCM kuikwamua
vinginevyo tujiandae kwa mwendelezo wa janga kubwa zaidi katika sekta
ya elimu.
Tunamtaka
Rais John Magufuli kujitokeza hadharani, na kuueleza umma wa Watanzania
hatma ya Vijana waliokosa mikopo, na kama ahadi zake alizozitoa wakati
wa Kampeni zilikuwa ni ulaghai au ghiliba za kutafuta kura?
Pia
Rais Magufuli anapaswa kuwaeleza watanzania ikiwa ameshindwa
utekelezaji wa ahadi zake ikiwemo Elimu bora, au akubali kuwa yeye ni
Muongo kwa sababu wakati wa kampeni alisema nanukuu; “ETI NIWE RAIS
HALAFU NISIKIE WANACHUO WAMEKOSA AU WAMECHELWESHEWA MIKOPO YAO,
WATANIJUA MIMI NI NANI, KITU CHENYEWE KINAITWA MIKOPO HALAFU
UNACHELEWESHA” Mwisho wa kunukuu.
Tunawataka
Viongozi wa serikali za wanafunzi katika Vyuo Vikuu vyote nchini,
kuungana pamoja ili kudai haki ya wanafunzi wenzao, tukitambua kuwa,
baadhi ya Viongozi wa shirikisho la serikali za wanafunzi wa elimu ya
Juu (TAHILISO) wamekuwa wakitumika kwa ajili ya CCM badala ya maslahi
mahsusi ya wanafunzi na hivyo kuidhoofisha taasisi hii muhimu ya wasomi,
hivyo umoja wao ni muhimu katika kuipata haki hii.
Tunatoa
wito kwa taasisi mbalimbali za kutetea haki za vijana, asasi za vijana
pamoja na mtandao wa wanafunzi Tanzania, kujitokeza hadharani na
kuwapigania vijana hawa katika kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi
ya elimu.
Imetolewa leo Jumatano,19.10.2016
Patrobas Katambi
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa
0 comments:
Post a Comment