Friday, 12 July 2024

MISA TAN YATOA TAMKO MWANDISHI DICKSON NG’HILY KUNYANYASWA AKIPIGA PICHA WANAFUNZI WAKISOMEA CHINI YA MTI


 TAARIFA YA KUPINGA HATUA ZA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI NA UNYANYASAJI DHIDI YA MWANDISHI DICKSON NG’HILY. 

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA TANZANIA),imepokea taarifa za kupigwa kujeruhiwa,kunyang'anywa simu na kuharibiwa simu yake Mhariri wa Habari wa Biashara na Mkuu wa Kitengo cha Digital cha Kampuni ya The Guardian Limited, Bw. Dickson Ng’hily. 

Mhariri huyo ambaye ni mwandishi wa habari alikuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kazi za uandishi wa habari kwa kupiga picha wanafunzi wa shule ya msingi Kwembe,Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, waliokuwa wanasomea chini ya mti. 

Katika tukio hilo, mwandishi alishambuliwa na wanafunzi ambao walipata maelekezo kutoka kwa mwalimu wao jambo ambalo halikuwa sahihi. 

Katika dunia ya ukuaji wa tekonolojia kuzuia mwandishi wa habari kupiga picha ni sawa na kuzuia mabadiliko kwa kuwa picha zinaweza kupigwa kwa namna nyingi bila muhusika kufika eneo husika.

 MISA TANZANIA tunakemea uamuzi wowote wa kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa ni kinyume cha sheria. 

Pia licha ya mwandishi huyo kujitambulisha na kuonesha vitambulisho vyake lakini bado aliendelea kushambuliwa kama mhalifu. Kitendo hiki hakikubaliki kwa kuwa kinakwenda kinyume na sheria na kusigina uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari. 

Tunatoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kumpiga na kumjeruhi binadamu,lakini mamlaka za serikali zilizohusika na ukamataji kuhakikisha haki inatendeka. 

Pia tunawakumbusha waandishi wa habari kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu za nchi.

 Imetolewa na MISA TANZANIA.

 Julai 12, 2024 Dar es Salaam.

Share:

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKOSHWA NA MIRADI YA AFYA MKALAMA



KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, Godfrey Mnzava amempongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kupambania  afya za watanzania kwa kuboresha miundombinu ya sekta ya afya.

Mnzava ametoa pongezi hizo Julai 10,2024 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru ulipofika katika hospitali ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida, kuangalia vifaa tiba vilivyowezeshwa na Rais Dk. Samia.

"Mheshimiwa Rais Dk. Samia ameendelea kujenga miundombinu mingi sana ambayo ni rafiki na  yakisasa kutolea huduma za afya, Hapa pia mmeletewa vifaa hivyo, tumekagua na kuona namna ambavyo vinaendelea kufanya kazi, kwa kweli tunampongeza na kumshukuru  sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan

Amedokeza Rais ameyafanya hayo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa na hawapati changamoto ya kuzifuata mbali na makazi yao na pia ameendelea kuboresha maslahi ya watumishi ili kuhakikisha tufikia malengo tulijiwekea kama taifa.

"Ameleta vifaa ambavyo vinasaidia kutafsiri changamoto za wagonjwa na mifumo ya hewa tiba kwa lengo la kuwasaidia watu wenye changamoto ya kupumua na upatikanaji wa hewa ndani ya miili yao ili waweze kupata unafuu," amesema.

Awali akiwasilisha taarifa fupi ya vifaa vya kisasa walivyovipata, Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya Mkalama, Dkt. Nicas Leonart amesema wanamshukuru Rais kwa kuwapatia vifaa ambavyo wanaamini vitawanufaisha wananchi wilayani Mkalama pamija na wilaya za Jirani ambazo ni Meatu, Mbulu, Manyara na Iramba.

Aidha, ameeleza serikali iliwapatia fedha za kujenga jengo la wagonjwa wa dharura kupitia mradi wa mapambano ya UVIKO-19 mwaka 2021. Amesema mradi huo, uligharimu sh millioni 300 kutoka serikali kuu huku katika mwaka 2023 hadi 2024 wakipokea  vifaatiba vyenye thamani ya sh milioni 450.5.

Daktari Leonart amevitaja vifaa hivyo kuwa ni Portable x-ray, Oxygen Port, ventilators, Control ya Mfumo wa hewa tiba, Maniford Control (Mfumu wa hewa tiba), vitanda vya umeme vitano na vifaa vingine,"Vifaa hivi lengo lake ni kuboresha huduma kwa wagonjwa wa dharura," amesisitiza.

Share:

Thursday, 11 July 2024

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA JULAI 12, 2024

Share:

DUWASA YASHUKURU WANANCHI NZUGUNI WALIOJITOLEA MAENEO YA MRADI


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amesema kukamilika kwa asilimia 98 ya mradi mkubwa wa maji wa Nzuguni uliyogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 4.3 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi tangu Disemba 23, 2023 ni mafanikio yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wananchi waliyojitolea maeneo yao ili mradi huo uweze kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Nzuguni.

Mhandisi Aron amewashukuru wananchi wa Nzuguni katika Mkutano wa Hadhara uliyoitishwa na Mbunge wa Jimbo wa Dodoma Mjini, Mhe. Antony Mavunde Julai 10, 2024 ukiwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

Hata hivyo, Mhandisi Aron ameendelea kuwasisitiza wananchi wapatao 33 kati ya 58 ambao hawajajitokeza kutambuliwa kwa ajili ya kupata fidia za maeneo yao kujitokeza ili zoezi hilo likamilike kabla ya malipo ya fidia zao kuanza kulipwa.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Aron ameutambulisha Mradi wa kusaidia Kaya zisizo na uwezo kuunganishiwa huduma ya maji na DUWASA (WFL)kwa gharama nafuu ya shilingi Elfu Thelathini tu baada ya kufanyika utambuzi wa kaya hizo kwa ushirikiano na viongozi wa mitaa na kata katika Kata za Ntyuka(Chimala), Ndachi na Nzuguni (Nzuguni A) utakaoanza mwezi Agosti, 2024 ambao unagharimu kiasi cha shilingi Milioni 970.
Share:

Wednesday, 10 July 2024

WANAHARAKATI WAIPONGEZA SERIKALI KWA MAFANIKIO DIRA YA TAIFA 2025


WANAHARAKATI wa masuala ya Jinsia na Maendeleo wameipongeza Serikali kwa uwajibikaji mkubwa kwenye Dira ya taifa ya miaka 25 iliyopita katika nyanja ya elimu ,afya pamoja na sekta ya habari na mawasiliano.

Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 10,2024 Mabibo -Jijini Dar es salaam,kwenye semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika kila jumatano TGNP-Mtandao,

Akizungumza wakati katika semina hiyo, Mdau wa Jinsia na Maendeleo Mwl.Vivian Ugurumo amesema elimu bure kwa wote, ujenzi wa madaraja, zahanati kila kata pamoja na barabara ni mafanikio kwa miaka 25 iliyopita ambapo awali havikuwepo vyote vilivyofanyika.

"Kuna masuala kama jamii tunaona tumefanikiwa sasa hivi tunaona watoto wanasoma kuanzia shule ya msingi hadi vyuo,tunaona mabinti nao wanasoma, kumekuwa na redio za mtandaoni,televisheni za mtandaoni ambapo kipindi hicho hazikuwepo"Amesema.

Aidha Vivian ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita ya dira ya taifa kwenye nyanja ya afya maboresho makubwa yamefanyika kwa kuingizwa vifaa vya kisasa kwenye matibabu pamoja na upatikanaji rahisi wa dawa.

Amesema kwenye sekta ya afya huduma kwa wazee pamoja na huduma ya mama na mtoto bado ni changamoto kwani bado kuna malalamiko kwamba wanalipishwa kwa ajili ya kupata matibabu.

Pamoja na hayo Vivian ameomba Dira ijayo kila sekta iingize masuala ya mlengo wa kijinsia pamoja na makundi yote,bila kuwaacha nyuma walemavu kwa aina zake.

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia,Jasmine Mohamed amesema mafanikio yaliyooatika kwa miaka 25 ni makubwa ambapo amegusia suala la miundombinu ya maji ya Sasa ukilinganisha na miaka 25 iliyopita kunatofauti kubwa ingawa bado kuna changamoto ammbazo zinatakiwa kufanyiwa ufumbuzi.

Aidha Jasmine ameshauri yafanyike maboresho katika dira mpya inayokuja kwa kuongeza idadi ya walimu mashuleni pamoja na kusimamia vyema miundombinu iliyoanzishwa kwa upande wa maji na usafirishaji.

Share:

TANROADS DAR ES SALAAM YASAIDIA VITU VYA MILIONI 2 KWA WAHITAJI WA KITUO CHA MAMA THERESA MBURAHATI



Na Mwandishi Wetu

Watumishi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam jana wametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa binadamu katika kituo cha Furaha na Amani cha Mtakatifu Thereza cha Mburahati jijini Dar es Salaam.

Akiongoza watumishi hao Meneja wa Mkoa huo, Mhandisi John Mkumbo amesema mahitaji hayo ya vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 2,030,000/= yamewasilishwa ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka nchini.
“Tunashukuru umetutembeleza kila mahali wanapoishi watoto wa umri mbalimbali, wazee wasiojiwe na watoto wenye changamoto ya kimwili, tumejionea mazingira yalivyo na hata uhitaji ninaamini kuna siku Mungu atatuongoza tutakuja tena kutoa mahitaji yanayostahili,” amesema Mha. Mkumbo.

Naye Mhasibu Mwandamizi wa TANROADS Dar es Salaam, Bi. Neema Mtengula amesema mbali na kuwa ni wajenzi wa barabara ili zipitike vizuri lakini pia wamekuwa wakitoa misaada kwa jamii zenye uhitaji katika vituo vya kulea wazee na watoto.

“Kwanza nakupongeza sana Sista kwa kazi ya utume unayofanya ya kuwalea watoto ni nadra sana kwa mama ambaye hana mtoto akaweza kumlea mtoto mwingine mwenye changamoto kwa mapenzi makubwa, nakupongeza sana kwa moyo wa upendo ambao Mungu ameuweka ndani yako,” amesema Bi. Mtengule.

Kwa upande wake Sista, M. Gonzalo M,C amewashukuru wafanyakazi hao wa TANROADS kwa majitoleo yao kwa ajili ya kituo hicho, amewaomba wasiwachoke na wafike mara kwa mara kuwasaidia maana bado wanauhitaji wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto na wazee wanaolelewa hapo.

Sista amesema kuwa wanawapata watoto wa kuanzia umri wa sifuri hadi miaka miatatu kutoka kwenye ofisi za Ustawi wa jamii wakiwa wengine wametelekezwa na wazazi wao hawajulikani, na wengine wanachangamoto za ulemavu wa viungo.


“Ninashukuru sana kwa moyo wenu mkuu mmeweza kutembelea nyumba yetu ya wahitaji mmejionea wenyewe wapo watoto wadogo sana jumla tuna watoto 34, wazee wasiojiweza 42 na watoto wenye changamoto mbalimbali za viungo wapo 22 bado tunahitaji misaada kutoka sehemu mbalimbali maana tuna watoto wadogo sana na wazee wengi hawajiwezi,” amesisitiza Sista Gonzalo.
Share:

TUMIENI MFUMO WA e-MREJESHO KUWASILISHA KERO ZENU SERIKALINI: e-GA



Na Dotto Kwilasa,DODOMA

WANANCHI wametakiwa kutumia mfumo wa kupokea maoni, malalamiko au pongezi Serikalini (e-Mrejesho), ili kuwasilisha maoni yao na Serikali iweze kuyafanyia kazi kwa wakati.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za Mamlaka jijini Dodoma.

Ndomba amebainisha kwamba, mfumo wa e-Mrejesho ambao hivi karibuni umeshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Ubunifu katika Huduma za Umma kwa mwaka 2024 ‘UN Public Service Innovation Awards’ unadhihirisha kuwa ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya serikali na wananchi .

“e-Mrejesho umetambuliwa kimataifa kama jukwaa linalowezesha serikali kukusanya maoni na malalamiko ya wananchi kwa njia ya kidijitali, na hivyo kufanya maamuzi ya sera na utekelezaji kwa wakati.” Ameeleza Mhandishi Ndomba.

Ameongeza kuwa, Tanzania ilikuwa moja kati ya nchi mbili tu za Afrika zilizotunukiwa tuzo hiyo, nyingine ikiwa ni Afrika Kusini kati ya nchi 73 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoshiriki, ambapo mifumo 400 iliwasilishwa wakati mifumo 15 pekee ndiyo ilishinda tuzo mbalimbali ukiwemo mfumo wa e-Mrejesho.

Amesema, tuzo hizo za Umoja wa Mataifa kuhusu Huduma za Umma zinalenga kuhamasisha ufanisi, uwazi na ushirikishwaji katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, na kuthamini mchango wa taasisi za umma katika kukabiliana na mahitaji ya kijamii, kiuchumi na mazingira ya jamii.

“ Mfumo wa e-Mrejesho unasaidia kuongeza uwajibikaji, kwani lalamiko linapofika kwenye taasisi litaonekana kwenye ngazi zote za uongozi wa taasisi hiyo na kila Afisa, aliyelifungua ama kulifanyia kazi ataonekana", amesema Ndomba na kuongeza kuwa,

“Pia mfumo huu unafanya uchambuzi wa taarifa na kumuwezesha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais UTUMISHI na Katibu Mkuu Kiongozi kuona malalamiko yaliyowazi, yanayoshughulikiwa na yale yaliyokamilika".

Kuhusu utambulisho wa mtoa malalamiko katika mfumo wa e-Mrejesho, Mhandisi Ndomba amebainisha kwamba mfumo haumlazimishi mwananchi kuandika taarifa zake binafsi kama jina au anuani yake au namba ya simu.

“Siyo lazima kuandika jina lako kama hutaki kufanya hivyo, lakini ni muhimu kuandika taarifa zako ili maoni au malalamiko yako yanapofanyiwa kazi upate majibu yake kwa haraka zaidi.” Amesema Mhandisi Ndomba

Machi 13 mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, aliwataka viongozi wa umma kutumia Mfumo e-Mrejesho ili kupokea maoni ya wananchi kuhusu Serikali na pia kutoa mrejesho kwa wananchi kupitia mfumo huo ili kuimarisha uwajibikaji kwa viongozi wa umma.

Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya emrejesho.gov.go.tz.

Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), unasimamiwa na kuendeshwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Share:

TBS YAENDELEA KUTOA ELIMU YA VIWANGO SABASABA

Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Francis Mapunda akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya ya  48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja Vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa huduma kwa wajasiriamali ,wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Viwango katika Maonesho ya  48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba ambapo wamekuwa wakiwapa taarifa ya huduma ambazo wanazitoa ikiwemo uandaaji wa viwango,usajili wa bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi.

Akizungumza na Waandishi wa habari Julai 9, 2024 kwenye maonesho hayo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Francis Mapunda amesema wameweza kupata wadau mbalimbali wakiwemo wajasirimali wadogo ambao wameweza kupata elimu namna ya bidhaa zao zinavyotakiwa kuthibitishwa ubora na Shirika hilo kupitia SIDO.

“Katika maonyesho haya pia tunatoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaeleza kuhusu huduma tunazozitoa ikiwemo kuthibitisha ubora wa bidhaa, mifumo ya kimenejimenti, upimaji, kufanya usajili wa vyakula na vipodozi" amesema 

Aidha amesema kupitia Maonesho hayo wanapokea wajasiriamali wadogo waliosajiliwa na kutambulishwa kwao na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ambao wanawapatia huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bila malipo.

Amesema baada ya kwenda SIDO watafanyiwa tathimini na kuandikiwa barua ya utambulisho kwenda TBS ambako watahudumiwa bure kwa miaka sita wakati wakiwa wanaendelea kukuwa kibiashara. 

Pamoja na hayo Mapunda ametoa wito kwa wafanyabiashara na walaji kuhakikisha kwamba bidhaa wanazozinunua ziwe zimethibitishwa na kuwa na alama ya ubora ya TBS, na wanaofanya biashara ya chakula na vipodozi wasajili majengo yao.

Watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakiendelea kuwahudumia wananchi waliotembela banda la TBS katika Maonesho ya ya  48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja Vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam

Watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakiendelea kuwahudumia wananchi waliotembela banda la TBS katika Maonesho ya ya  48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja Vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam

Watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakiendelea kuwahudumia wananchi waliotembela banda la TBS katika Maonesho ya ya  48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja Vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger