Saturday, 23 September 2023
DKT.MGOGO AONGOZA MAHAFALI YA 3 YA DARASA LA SABA SHULE YA AWALI NA MSINGI KOM YA FANA,MKURUGENZI KOM ATANGAZA OFFA KWA WAZAZI NA WALEZI WENYE WATOTO WALIO HITIMU DARASA LA SABA SHINYANGA
Na Mwandishi wetu Malunde Blog Shinyanga
Dkt.Agatha Mgogo ambaye ni Mkurugenzi chuo kikuu huria cha Tanzania mkoa wa Shinyanga ameongoza Mahafali ya Tatu ya darasa la saba 2023 katika Shule ya awali na Msingi Kom tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.
Mahafali hayo yamefanyika leo Jumamosi September,23 ,2023 katika shule hiyo iliyopo eneo la Butengwa kata ya Ngokolo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ambapo jumla ya wanafunzi 43 wamehitimu elimu ya darasa la saba na wanafunzi zaidi ya 60 wamehitimu elimu ya awali na sasa wataingia darasa la kwanza mwaka 2024.
Akizungumza, na wazazi na walezi Pamoja na Wahitimu Dkt.Agatha Mgogo amesema serikali na wanaShinyanga wanajivunia uwepo wa shule ya Awali na Msingi Kom ambayo imekuwa ikiupa sifa nzuri mkoa wa Shinyanga kwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa.
“Shule hii imekuwa ikitutangaza vizuri kitaifa katika matokeo ya mtihani jitihada ambazo tunatakiwa kuziunga mkono ”,amesema Dkt.Mgogo.
“Ninawapongeza pia kwa kukuza vipaji vya watoto, watoto hawa wana vipaji lakini pia darasani hawakamatiki, Kusoma na burudani pamoja na mazoezi lazima vyote vifanyike kwa ajili ya makuzi ya watoto. Nawapongeza sana kwa kulea watoto na kuwa bora”,ameongeza Dkt.Mgogo.
Aidha Dkt. Mgogo amewataka wazazi na walezi kuendelea kutilia mkazo suala la elimu kwani elimu inatengeneza watalaamu mbalimbali na watoto wanataka kutimiza ndoto zao huku akiwahimiza wazazi kuwasimamia watoto na kuwapeleka shule kwani hakuna urithi mzuri zaidi ya elimu.
“Tukiwapeleka shule watakwenda kujitegemea, wataenda kusoma kwa bidii ili wawe na vipato , wasiwe tegemezi, pelekeni watoto shule, tuwafundishe uzalendo, tuwafundishe utamaduni pia, haya lazima wakue nayo ili waje watumikie taifa lao”,amesema Dkt.Mgogo.
“Shule hii ina uongozi thabiti, walimu wanajituma na wanajitahidi kulea na kusimamia watoto hawa, ambao ni wanyenyekevu na nidhamu kwa sababu wamefundishwa shuleni”,amesema Dkt. Mgogo.
“Sisi wazazi tuna wajibu wa kuwalinda watoto hawa waliomaliza shule wasiwe wazururaji kwenye mitaa yetu na wazazi tuwaleee vizuri. Kwenye shule zetu wapo ambao kwa kiasi kikubwa kuna changamoto, naomba wazazi tujinyime na kujitahidi na kulipa ada, tulipe ada”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule za Msingi na Sekondari Kom Jackton Koyi ameishukuru serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa shule hiyo .
Aidha Koyi amewashukuru wazazi na walezi kwa kuiamini shule hiyo na kupeleka watoto katika shule za Kom.
Koyi amewataka wahitimu wa darasa la saba kuwa watoto wazuri kwa familia, jamii na mahali popote watakapokwenda huku akiwasihi wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kuwaendeleza kwa kuwapeleka sekondari huku akitoa offa kwawazazi na walezi kuwapeleka watoto wao walio hitimu elimu ya msingi kufanya mtihani wao Kom Sekondari Tarehe 29 Mwezi September ili waweze kujiunga na wenzao mwezi January Tayari kwa kuanza elimu ya Kidato cha kwanza.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Kom Derick Okech amewaomba wazazi na walezi kuendelea kushirikiana na walimu katika kulea wanafunzi ili kutimiza ndoto zao huku akiwakumbusha kulipa ada kwa wakati.
Mkurugenzi wa shule za Msingi na Sekondari Kom Jackton Koyi akiwa na meneja Magreth Koy wakifurahi na watoto
Dkt.Agatha Mgogo ambaye ni Mkurugenzi chuo kikuu huria cha Tanzania Shinyanga akizungumza na wazazi na walezi.