Wednesday, 20 September 2023

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO SEPTEMBA 20,2023

 










































    Share:

    Tuesday, 19 September 2023

    SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI KITUO CHA AFYA KISORYA, BUNDA


    Wakazi wa Kijiji cha Kisorya wakiwemo wanawake wajawazito katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wameondokana na adha ya kutembelea umbali mrefu kufuata huduma za afya hususani upasuaji baada ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kuboresha Kituo cha Afya Kisorya.


    Awali wakazi hao walilazimika kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 42 hadi Kibara na Kasahunga wilayani Bunda ama kuvuka maji katika Ziwa Victoria hadi Nansio wilayani Ukerewe kufuata huduma za afya hususani wakati wa kujifungua.


    Mmoja wa akina mama katika Kijiji hicho, Kasenda Kaguba amesema maboresho katika Kituo cha Afya Kisorya yaliyojumuisha vifaa tiba na uwepo wa madaktari wawili pamoja na manesi wanane umewaondolea adha ya upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo ya upasuaji ambayo haikuwepo tangu Kituo hicho kipande hadhi kutoka Zahanati mwaka 2018.


    Kaguba amesema mwezi Aprili mwaka 2021 alifika katika Kituo cha Afya Kisorya kujifungua watoto mapacha ambapo mtoto wa kwanza alijifungua salama lakini akakumbana na uchungu pingamizi kwa mtoto wa pili na kulazimika kupelekwa katika Kituo cha Afya Kibara na kujifungua kwa upasuaji.


    Kutokana na changamoto hiyo, mwezi Disemba mwaka 2022 Serikali ilipeleka mashine ya usingizi, mashine ya oksjeni, kitanda cha upasuaji ambapo kwa kushirikiana na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH iliwajengea uwezo watoa huduma katika Kituo cha Afya Kisorya hatua iliyosaidia kuanza kutoa huduma za upasuaji katika Kituo hicho.


    Jitihada hizo zimewanufaisha wakazi wa Kijiji cha Kisorya wakiwemo wanawake wajawazito kupata huduma za afya katika Kituo hicho akiwemo Kabuga ambaye Disemba 30, 2022 alijifungua kwa upasuaji katika Kituo cha Afya Kisorya ikiwa ni mara ya kwanza huduma hiyo kutolewa katika Kituo hicho.


    Akizungumzia maboresho hayo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kisorya, Dkt. Hemedi Hassani amesema tangu huduma ya upasuaji ianze kutolewa katika Kituo hicho Disemba mwaka jana, zaidi ya wanawake 20 wamejifungua katika Kituo hicho, kati yao watano wakijifungua kwa upasuaji.


    “Wananchi pia wameongeza imani ya kuja hapa kupata huduma za afya ambapo idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 45 hadi 50 kwa siku na kufikia 80 hadi 100 kwa siku. Tunaishukuru Serikali kwani kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH imetujengea uwezo, sasa tuna uzoefu wa kutoa huduma bora ikiwemo upasuaji” amesema Dkt. Hassani.


    Naye Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Vijijini, Hellen Magare amesema jitihada za Serikali na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH zimesaidia kiwango cha ubora wa huduma kwa Halmashauri hiyo kuongezeka kutoka asilimia 3.5 hadi 4.1 ambapo lengo ni kufikisa asilimia 5 ambazo ni kipimo cha juu kwa Halmashauri kwa utoaji huduma bora za kitaifa.


    “Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana vyema na wadau wa afya hususani mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH na kuboresha huduma za afya katika Halmashauri yetu, jitihada hizi zitasaidia kufikia asilimia tano za ubora katika utoaji huduma za afya” amesema Magare.


    Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabrone Masatu amesema mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH umesaidia kuwajengea uwezo wataalamu pamoja na kuimarisha huduma za afya ikiwemo upasuaji katika Vituo 30 vya afya na hospitali 18 mkoani Mara.


    Kwa Mkoa wa Mara, mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH umesaidia kupunguza vifo vya uzazi kwa akina mama kutoka 46 kwa zaidi ya wanawake elfu 90 waliojifungua mwaka 2022 hadi kufikia vifo 32 kati ya wanawake zaidi ya elfu 60 waliojifungua hadi kufikia mwezi Septemba mwaka 2023.


    Jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya Kisorya Wilaya ya Bunda mkoani Mara zimezaa matunda kwa ushirikiano wa karibu na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya ya mama, mtoto na vijana balehe ukitekelezwa katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.


    Mikoa hiyo ni Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga, Simiyu, Tabora , Katavi, Manyara, Dodoma, Tanga na Dar es salaam kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022/27 kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na kutekelezwa na shirika la JHPIEGO kama mdau mkuu.


    Mashirika mengine yanayoshirikiana na JHPIEGO kutekeleza mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH ni Tanzania Communication and Development Centre, Benjamini Mkapa, Amani Girls Home, The Manoff Group na D-Tree International.
    Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
    Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabron Masatu akizungumza ofisini kwake kuhusiana na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya kuboresha huduma za afya katika Vituo vya Afya na Hospitali ili kukabiliana na vifo vya uzazi kwa akina mama na watoto.
    Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabron Masatu akizungumza na timu ya wataalam wa afya mkoani Mara.
    Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Vijijini, Hellen Magare akieleza namna Serikali ilivyoboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya Kisorya kwa kushirikiana na wadau kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH.
    Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kisorya, Dkt. Hemedi Hassani akionyesha vifaa tiba mbalimbali kikiwemo kitanda cha upasuaji, mashine ya dawa ya usingizi na mashine ya Oksijeni vilivyonunuliwa katika Kituo cha Afya Kisorya.
    Mmoja wa wakazi wa Kisorya wilayani Bunda, Kasenda Kaguba aliyepata huduma ya kujifungua kwa njia ya upasuaji katika Kituo cha Afya Kisorya akitoa shukurani kwa Serikali kuboresha huduma za afya katika Kituo hicho.
    Share:

    Monday, 18 September 2023

    SERIKALI YATOA FEDHA KWAAJILI YA MIRADI YA MAENDELEO CHALINZE




    Makao makuu ya halmashauri ya Chalinze

    NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE

    HALMASHAURI ya Chalinze Mkoa wa Pwani, imepokea jumla ya shilingi 2,222,000,000 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.

    Taarifa kwa umma iliyotolewa mapema wiki hii na  kitengo Cha mawasiliano  katika halmashauri hiyo, kiasi hicho cha fedha kimelengwa katika ujenzi wa Madarasa , Vyoo vya shule, vituo vya afya, zahanati na vifaa tiba.

    Katika fedha hizo jumla ya shilingi 208,000,000 ni kwaajili ya Ujenzi wa Madarasa na vyoo katika shule kongwe za msingi.

    Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa Madarasa na vyoo vya shule za Sekondari(464,000,000/=), ujenzi wa uzio wa shule ya msingi Chalinze shilingi 30,000,000 na ujenzi wa nyumba mbili za wakuu wa idara zenye thamani ya shilingi 320,000,000.

    Halmashauri hiyo pia imepokea shilingi 100,000,000 kwa ajili ya umaliziaji zahanati, Shilingi 700,000,000 kwaajili ya uendelezaji wa hospitali ya Wilaya, Shilingi 300,000,000 kwaajili vifaa tiba katika vituo vya afya na shilingi 100,000,000  zimeelekezwa kwenye vifaa tiba vya zahanati katika halmashauri hiyo.
    Share:

    TAASISI YA OMUKA HUB YAFUNGUA MKUTANO KUANGAZIA SUALA UKATILI WA KIJINSIA MTANDAONI KWA WANAWAKE KATIKA SIASA


    Taasisi ya OMUKA HUB ambayo imejikita katika masuala ya maendeleo na ujumuishi wa kidijitali ikiwemo kuhamasisha matumizi ya mtandao kwa wanawake katika siasa, imefungua mkutano wake jijini Dar es Salaam wenye lengo la kuangazia suala la ukatili wa kijinsia mtandaoni kwa wanawake katika siasa.

    Akizungumza katika hafla hiyo leo Septemba 18,2023 Jijini Dar es Salaam, Mwanzilishi wa Taasisi hiyo Mhe.Neema Lugangila amesema ukatili wa kijinsia katika siasa una shabiana na ukatili wa wanawake katika habari.

    "Tumekuwa na majidiliano mazuri ya namna gani tunaweza kuimarisha uwakilishi na ushiriki wa wanawake katika siasa za mtandaoni na tumekubalina tutaandaa kamati ambayo itaenda kudadavua suala hili ili tuje na mpango kazi ambao tutakapo kwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wanawake wataweza kushirik katika mitandao ya kijamii kunadi sera zao bila bughudha". Amesema.

    Amesema anaelewa kadhia ambayo wanapitia wanawake wanasiasa katika mitandao hivyo wao kama wabunge wanawake wameamua kubeba ajenda hiyo kusemea wanawake katika siasa lwasababu wanatambua umuhimu wa kushiriki katika mitandao

    "Sasa kwa kushirikiana na wanawake katika vyombo vya habari tunaamini tunaweza kushirikiana. vzuri na kupaza sauti kubwa ili kuweka mazingira sawia na wezeshi ili wanawake katika siasa waweze kushiriki ipasavyo katika mitandao ya kijamii".Amesema

    Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali Mhe.Gerson Msigwa amesema ukatili haukubaliki uwe wa kwenye vyombo vya habari, bungeni au mahali pengine popote hivyo serikali imekuwa ikishiriana na wadau kuhakikisha kwamba kunakua na kampeni mbalimbali za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake.

    Aidha amesema kuwa zipo sheria mbalimbali ambazo vitendo vyote vya ukatili havikubaliki na ni makosa kwa mujibu wa sheria hivyo wanaangalia kama wanaweza kuja na uwanja mpana zaidi wa kisheria wa kukabiliana na hayo majukumu.

    Pamoja na hayo amempongeza Rais Samia Suluhu kuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaongoza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake katika maeneo mbalimbali na kuwawezesha wanawake wenyewe.

    "Rais Samia ameandaa Wizara Maalumu ya kukabiliana na vitendo hivi ambayo ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, ambapo moja ya kazi ya Wizara hii ni kutoa Elimu kwa jamii juu ya kutambua vitendo vya ukatili,kuviripoti na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria". Amesema

    Wadau walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Wabunge wanawake,wawakilishi wa UNESCO Makao Makuu, na UNESCO Dar es salaam wawakilishi kutoka Habari Maelezo, IPU,TAMWA,Wabunge wanawake kutoka Ghana,Kenya,Uganda na Malawi.


    Share:

    MKURUGENZI MANISPAA YA TABORA AMPA SIKU TATU MKUU WA KITENGO CHA TAKA NGUMU KUONDOSHA TAKA ZOTE ZILIZOLUNDIKANA MAENEO YA KUKUSANYIA TAKA



    Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndugu Elias M. Kayandabila amemtaka Mkuu wa Kitengo cha Taka Ngumu Ndugu Adamu Baleche kuhakikisha kuwa ndani ya siku tatu awe ameondosha taka zote zilizopo maeneo yote ya kukusanyia taka na kuzipeleka dampo.

    Kanyandabila ameyatoa maelekezo hayo leo Septemba 18, 2023 wakati wa Ziara fupi ya Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) ya kukagua hali ya usafi katika viunga vya Manispaa ya Tabora.

    Aidha Ndugu Kayandabila ameunda timu ndogo itakayoshirikiana na Kitengo cha Taka Ngumu katika kuratibu na kusimamia kazi zote za usafi mjini hapo, lengo kubwa ikiwa ni kuongeza ufanisi wa shughuli za usafi katika Manispaa yetu.

    Wajumbe wa CMT nao baada ya kujionea hali mbaya katika maeneo ya kukusanyia taka, wameafiki kwa pamoja umuhimu wa timu hiyo ndogo ambayo itaongeza nguvu kwenye kitengo cha taka ngumu.

    Share:
    Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

    Popular Posts

    Unordered List

    Pages

    Blog Archive


    Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger