Monday, 8 August 2022
Sunday, 7 August 2022
NAIBU WAZIRI MARY MASANJA AFUNGA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA WANYAMAPORI
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akimkabidhi cheti cha pongezi Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Robert Mande (kulia) kwa kushiriki katika utoaji mafunzo ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akifunga mafunzo ya siku tano ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Robert Mande (kulia) akizungumza na washiriki wa mafunzo ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akimkabidhi cheti cha pongezi Afisa Uwajibikaji na Mkurugenzi wa Haki wa Taasisi ya Grace Farm Foundation Rob Khattabi (kulia)kwa kushiriki katika utoaji mafunzo ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Robert Mande (kushoto)Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani)akifunga mafunzo hayo leo jijini Dar es Salaam.
*********
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amefunga mafunzo ya siku tano ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mhe. Masanja amesema kuwa mafunzo hayo yametoa mbinu za kuhakikisha hifadhi zinahifadhiwa vizuri ili kulinda wanyamapori na kuendeleza utalii.
“Wataalamu wa masuala ya uchunguzi wamejifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi katika nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka (Lusaka Agreement)”.
Amesema mafunzo hayo yameshafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na Tanzania itaendelea kushiriki kama nchi mwanachama ili kuzilinda hifadhi na wakati huohuo kuendeleza utalii.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Robert Mande amesema kuwa mafunzo hayo yataendelea kufanyika ili kutekeleza sera za Serikali za kuendeleza uhifadhi.
“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona na waweze kuwa na usalama”Mande amefafanua.
Ameongeza kuwa washiriki zaidi ya 21 kutoka nchi wanachama wamejengewa uwezo katika masuala ya uchunguzi, upelelezi, intelijensia na uendeshaji mashitaka ili waweze kufikia viwango vya umahiri mkubwa kwa sababu makosa ya ujangili yanavuka mipaka ya nchi na yanahitaji ushirikiano na vyombo vingine vya nje ya nchi.
Kwa upande wake Mshiriki wa Mafunzo kutoka nchini Kenya, Bw. Jami Yamina amesema mafunzo hayo yametoa mbinu mbalimbali za kutumia ili kuwakamata majangili na kuzikamata mali zao na kuziwasilisha mahakamani.
“Tukiweza kuwakamata hawa majangili tutakuwa tumefanikiwa kuzuia biashara hii haramu ya wanyamapori ” amesisitiza.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wataalamu wanachama wa Lusaka Agreement (unaojihusisha na kuzuia uuzaji, usafirishaji wa wanyamapori pamoja na mimea) Grace Farm Foundation, US Homeland Security na washiriki kutoka nchini Uganda, Kenya na Tanzania
MWAROBAINI KUPAMBANA NA FUNZA WA VITUMBA WACHEMSHWA TARI
Funza wa vitumba
***
Na Mwandishi wetu
Imeelezwa kuwa Funza wa Vitumba ni tishio kwa mazao mengi kutokana na kwamba anaanza kushambulia mazao pale yanapoanza kutoa maua.
Hayo yamesemwa na Mtafiti wa Wadudu waharibifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru, Romana Cornel kwenye Maonesho ya Nane Nane yanayoendela katika viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza.
Amesema Funza wa Vitumba ni hatari kwani anaanza kushambulia mazao pale yanapoanza kutoa maua.
“Kwa upande wa pamba ni wiki ya nane lakini pia anaharibu mazao mengine, anashambulia mahindi na kama unavyoona hawa tumewatoa kwenye dengu na mtama pia wanashambulia. Ni vyema wakulima wakatumia mitego hii kuwatega. Watumie mabaki ya Sukari yaani Molases na huu mtego tuliouweka hapa na tumeweka juu yake harua, hapa vipepeo dume wote wamenaswa. Hivyo vipepeo majike hawataweza kutaga mayai”, amesema mtafiti huyo.
“Kwa sasa bado tupo kwenye utafiti wa njia nzuri zaidi kupambana na wadudu hawa na mwaka ujao matokeo yatakuwa tayari hivyo itakuwa ni nafuu kwa wakulima kwani funza huyu atakuwa amepatiwa suluhisho”,amesema Cornel.
Funza wa vitumba anachukuliwa kuwa mmoja kati ya wadudu wasumbufu muhimu zaidi duniani kote, wanaoshambulia zaidi ya aina 200 za mimea.
TARI YAALIKA OFISI ZA HALMASHAURI KUPELEKA MAAFISA UGANI KUPIGWA MSASA
Mfano wa kifaa cha kupimia afya ya udongo
**
Na Mwandishi wetu - Mwanza
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru imewataka Maafisa Ugani kutoka kwenye Halmashauri za wilaya kwenda kupigwa msasa kwenye kituo hicho jinsi ya kutumia vifaa vya kupimia udongo (Soil Test Kit) walizopewa kwa ajili ya kupima afya ya udongo kwenye maeneo yao.
Akizungumza kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza ,Mtafiti kutoka Idara ya Udongo TARI Ukiriguru, Hainess Msuya amesema endapo maafisa ugani hawatapata mafunzo Soil Test Kit hiyo haitaleta matokeo yanayotarajiwa.
“Maafisa ugani waje wapewe semina ya jinsi ya kutafsiri taarifa zinazopatikana baada ya kupima udongo kuna uhakika wengi wao itakuwa vigumu kutafsiri taarifa hizo kutokana na ukweli kwamba wengi wametoka Chuo siku nyingi na wengine hawajawahi hata kukutana na hizo Soil Test Kit",amesema Mtafiti huyo.
Mtafiti huyo alisema tunapima udongo ili kujua afya ya udongo na vipimo hivyo ndiyo vitatusaidia kwenye eneo husika ni nini tunahitaji kupanda na ni mbolea gani tuweke kwenye udongo huo
“Vifaa ni vizuri nashauri Halmashauri ziwapeleke maafisa ugani kwenye vituo vya TARI wapewe mafunzo ya muda mfupi. Huku Kanda ya Ziwa Magharibi waje Ukiriguru na wa Kanda zingine waende kwenye vituo vya TARI vilivyopo kwenye maeneo yao ili wawahi msimu wa mvua huu kabla ya kilimo kuanza”,amesema
Saturday, 6 August 2022
MZEE MWENYE WATOTO 34 KUTOKA KWA WANAWAKE 20 AZUA GUMZO
Video ya mzee wa miaka 78 imeleta hisia mseto mitandaoni huku ikinasa ufichuzi wa kusisimua aliotoa kuhusu maisha ya jamii yake.
Mkulima huyo alifichua kuwa kwa sasa anaishi na mwanamke mwenye umri wa miaka 35 ambaye wamejaliwa watoto watano, amezaa watoto 34, lakini ni 32 pekee ambao wako hai.
Kulingana naye, watoto 20 kati yao ni wa mama 20 tofauti, na bado anaendelea kujifungua
Kwenye video iliyotamba mitandaoni mzee huyo aliwarai wanaume wengine kuufuata mfano wake akisema watoto ni baraka
Alipoulizwa kilichomsukuma kujifungua idadi kubwa ya watoto, mzee huyo alisema ‘utukufu’ wote ulitoka kwa Mungu kwa kumbariki.'
"Mke wangu wa sasa ana umri wa miaka 35 na tuna watoto watano lakini bado hatujamaliza kujifungua. Tutakuwa na wengine," alisema.
Prince Ko Fi alisema: "Mtu mmoja peke yake watoto 32 na serikali inapaswa kumsaidia kuwalipia wanawe karo ya shule. Ninaamini kunapaswa kuwa na idadi ya watoto ambayo mtu anapaswa kujifungua. Mtu mmoja anafaa kuwa na mtoto mmoja au wawili."
Shaibu Sahada alisema: "Anadhani hilo ni mzaha Lakini hii ni mojawapo ya matatizo ya Ghana. Angewezaje kulea watoto 32 ifaavyo? Watoto hao kuna uwezekano mkubwa wa kukosa malezi yoyote bora, na kwa pamoja wanakuwa mzigo kwa jamii nzima. Ni watu masikini tu ndio watafurahia kitu kama hiki."
Dyer Tsoeke alitaja: "Huyu hamshindi Togbe Asilenu ambaye ana watoto 100+. Kwa kweli Shaibu Sahada aliibua baadhi ya hoja halali ambazo tunapaswa kuzingatia kwa kina."
Katika hadithi sawa na hiyo, mwanaume aliyetambulika kwa jina la Nana ana watoto zaidi ya 200 na wake zake 43 katika Mkoa wa Juu Mashariki mwa Ghana.
Wafanyakazi wa Kipindi cha Asubuhi cha Angel TV (Anopa Bofo) wakiongozwa na Kofi Adomah walisafiri hadi Tenzuku, kijiji ambacho kiko umbali wa saa 13 kwa gari kutoka Accra, ili kuwahoji baadhi ya watoto kuhusu familia hiyo kubwa.
Ingawa mwanaume huyo mwenyewe hakuwepo, msemaji wake alionyesha kuwa makadirio ya idadi ya wake na watoto ilikuwa chini ya takwimu halisi.
TBS YAENDELEA KUTOA HUDUMA KWENYE MAONESHO NANE NANE ARUSHA
Afisa Usalama wa Chakula (TBS), Bw.Edward Mwamilawa akimsaidia mteja kuingia kwenye mfumo kwa ajili ya kupata huduma ya kitaalum ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi. Kaimu Meneja wa Kanda ya Kaskazini ( TBS) Bw. Deogratius Ngatunga akimuelimisha mdau kuhusu masuala ya viwango katika maonesho ya 28 ya 88 mkoani Arusha.
*********************
TBS imeshiriki maonesho ya 28 ya 88 jijini Arusha yanayofanyika katika viwanja vya 88 Njiro.Kauli mbiu Agenda 10/30:Kilimo ni Biashara, Shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Maonesho hayo yameanza rasmi tar 01/08/2022 na kufunguliwa rasmi tarehe 03/08/2022 na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. John Mongela.
TBS ni wadau wakubwa ukizingatia lengo moja wapo ni kuwezesha biashara.
Tumewatembelea wajasiriamali kujua changamoto zao sambamba na kuwapa elimu ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao haswa ukizingatia kwa sasa kwao ni bure, Serikali inatenga kati ya 150M -200M kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia. Mpaka sasa zaidi ya wajadiriamali wadogo 600 kutoka mikoa mbalimbali wamepata leseni chini ya mpango huu wa bure.( Bw Deogratius Ngatunga, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini)
Meneja alisema TBS ipo viwanjani hapo pia kwa ajili ya kuwapa msaada wateja wapya na wazamani kwa kuwaelekeza jinsi ya kufanya maombi ya usajili wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi pamoja na maombi ya kupata leseni ya kutumia alama ya ubora.
Bw. Ngatunga alitoa wito kwa wateja na wananchi kutumia fursa hiyo kwa kutembelea banda la TBS lililopo ndani ya viwanja hivyo na watakaoshindwa wasisite kuwasiliana na TBS kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba ya bure 0800110827.
Maonesho haya yanatarajia kufungwa tarehe 08/08/2022 .
Friday, 5 August 2022
RAIS SAMIA ARIDHISHWA NA UJENZI JENGO LA OFISI YA MKUU WA MKOA WA MBEYA
OR-TAMISEMI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ameridhishwa matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya lililogharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.7
Ametoa kauli hiyo leo Agosti 05, 2022 wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo hilo kwenye ziara yake ya siku Nne ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini Mbeya.
Amesema kuwa katika suala la utawala bora Serikali ya awamu ya sita inaboresha maeneo ya wananchi wanapoenda kupata huduma kuwe na mazingira mazuri ya kuhudumiwa na wale wanaotoa huduma kuweza kutoa huduma bora kwa jamii wakiwa kwenye mazingira mazuri.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha na kujenga majengo ya Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Majengo ya Halmashauri, nyumba za wakuu wa Wilaya, lengo likiwa ni kuboresha mazingira ili kuweza kutoa huduma bora kwa jamii.
“Utafiti unaonyesha kuwa tunapofanya kazi kwenye mazingira mazuri, utoaji wa huduma hutolewa vizuri hivyo Serikali imeamua kutumia fedha nyingi kujenga Ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha, Mheshimiwa Samia amesema Serikali itaendelea kujenga majengo kama hayo katika Mikoa yote hasa katika maeneo ya Kikanda
Mheshimiwa Samia amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo niwatake Madiwani kuhakikisha wanasimamia fedha hizo ili ziweze kutekeleza miradi iliyokusudiwa na Serikali.
Jengo la Ofisi ya Mkuu w Mkoa lina urefu wa mita 84.2 na upana wa mita 33.5 ambapo vyumba vya ofisi vipo 72, stoo moja kubwa, Maktaba mbili, kumbi mbili ndogo na ukumbi mmoja mkubwa wenye uwezo wa kuchukua watu 250.