Sunday, 20 March 2022

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI MACHI 20,2022



Share:

Saturday, 19 March 2022

MASHIRIKA YANAYOTETEA HAKI ZA WAFUGAJI WAOMBA SERIKALI KUFANYA MAZUNGUMZO YA PAMOJA ILI KUMALIZA MGOGORO WA LOLIONDO SALE NA NGORONGORO


Katikati ni mkurugenzi wa mtandao wa wafugaji Tanzania( TPCF), Joseph Parsambei akitoa tamko la mashirika zaidi ya 20 juu ya mgogoro wa ardhi wilayani Ngorongoro.

Na Rose Jackson,ARUSHA

Zaidi ya Mashirika ishirini ya kiraia yanayotetea haki za wafugaji wa asili Tanzania wameiomba serikali na wananchi wilayani Ngorongoro kukaa kwa pamoja katika meza ya mazungumzo ili kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo katika wilaya hiyo.

Akitoa tamko hilo kwa niaba ya mashirika hayo katika mkutano wa mashirika hayo ,Mkurugenzi wa Mtandao wa Wafugaji Tanzania ,Joseph Parsambei amesema kuwa wamekutana ili kufanya tathmini na kuelimishana juu ya mgogoro huo na namna ya kuutatua.

Amesema kuwa wao wakiwa kama mashirika ya kutetea haki za wafugaji wanaomba pande zote mbili kukaa kwa pamoja huku wakiomba mashirika hayo ya kiraia kuhusishwa ili waweze kutoa ushauri wao kwa kuwa nao ni sehemu ya jamii..

"Tumelazimika sisi mashirika kukutana kufanya tathmini ya mgogoro kutokana na taarifa wanazozisikia na kwamba wanatoa tamko katika eneo la Loliondo na Sale pamoja na mgogoro uliopo eneo la Ngorongoro na lengo letu ni kuomba meza huru iwepo ili kumaliza tatizo hili",aliongeza

Amesema kuwa wanatambua umuhimu wa uhifadhi na wanatambua haki za wananchi hivyo haki isikiukwe katika kutafuta uhifdhi.

Aidha amesema wanaunga mkono juhudi za kumaliza mgogoro huo huku kwa eneo la Loliondo Sale wanasisitiza kuwepo kwa matumizi sahihi ya ardhi kwani ndiyo suluhisho la mgogoro huo.

Parsambei ameomba kila upande uheshimu sheria za nchi haki za binadamu na utawala wa kisheria huku wakitaka wadau wote kujielekeza katika meza huru ya majadiliano ili kumaliza mgogoro bila kuchochea upande wowote.

Kwa upande wake Msaidizi wa Kisheria kutoka Shirika linalotoa msaada wa kisheria bi Agnes Marmo amesema kuwa wanaomba hatua zote zinazochukuliwa na serikali katika eneo la Loliondo Sale zishirikishwe kwa jamii husika ili kufikia muafaka .

Amesema kuwa kwa upande wa eneo la Loliondo Sale ni km za mraba elfu 1500 ambao mgogoro wake ni baina ya wananchi na wawekezaji huku mgogoro wa Ngorongoro ukiwa ni kati ya serikali na wananchi kwa madai ya ongezeko la watu na mifugo.

Aidha ameomba serikali na jamii kukaa meza huru ya majadiliano na wakubaliane na kwamba wadau wajikite katika mgogoro huo ili maslahi yote yalindwe.

Amesema wao kama mashirika ya utetezi wataendelea kuwa macho na karibu na sakata hilo ili kuhakikisha matumizi ya ardhi endelevu yanalindwa

Naye Afisa mipango kutoka Shirika la Masae Pastoralism Development Organization , Amani Sekilo amesema mgogoro wa tarafa ya Ngorongoro Ina sheria yak maalum hivyo kuna umuhimu sheria hiyo itumike vizuri kwani inatambua kuna wafugaji na uhifadhi.

Amedai kuwa Ngorongoro ni eneo la matumizi mseto na kwamba utatuzi wa migogoro hiyo na kwamba wao wanataka mbinu mbadala ya serikali kufanya mazungumzo ya pamoja ili wasiumizane.


Share:

MAJI TARIME YAWACHEFUA DC, KATIBU CCM, MBUNGE WAITARA, WASISITIZA MAJI YA ZIWA VICTORIA


Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara akiwa kwenye chanzo cha maji Nyakonga
Meneja RUWASA wilaya ya Tarime Malando Masheku
Mkuu wa wilaya ya Tarime Michael Mtenjele
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)wilaya ya Tarime,Valentine Maganga

Na Dinna Maningo,Tarime
UKOSEFU wa Maji Safi na Salama katika mji wa Tarime mkoani Mara umekuwa ni kero kwa wananchi na kuwa karaha kwa kuwa maji wanayoyatumia ni machafu yanayobadilisha rangi halisi ya nguo nyeupe  na kupoteza muonekano wake licha yakwamba kila mwisho wa mwezi watumiaji wa maji wanalipa bili za maji serikalini.

Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele amesema kuwa upatikanaji wa maji katika halmashauri ya mji Tarime ni asilimia 45, lakini bado si safi na salama ni tope kwakuwa chujio linalochuja maji ni dogo halina uwezo wa kuchuja maji kipindi cha mvua ambapo kiwango cha maji ya tope uongezeka kwenye vyanzo vya maji.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari waliofika wilayani humo kutembelea baadhi ya miradi ya maji inayojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),Mtenjele amesema kuwa katika halamshauri ya wilaya ya Tarime kiwango cha upatikanaji wa maji ni asilimia 70.

"Wakati mwingine ukiingia bafuni unajiuliza nioge au nisioge,maji nikama tope hutamani hata kuvaa shati nyeupe,hali ya maji bado haipo vizuri si safi yanakuja yakiwa vumbi hasa wakati wa mvua chujio ni dogo linazidiwa,tukipata maji kutoka Ziwa Victoria yatatusaidia sana’’,amesema Mtenjele.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kuna mradi  wa maji yatakayotoka Ziwa Victoria na maji kufika Tarime na kwamba Serikali bado inaendelea na mchakato kuhakikisha mradi huo unafika Tarime ambao ndiyo utakuwa suluhisho na kwamba mbali ya chujio la maji kwenye vyanzo vya maji kuzidiwa uwezo wa kusafisha maji bado vyanzo vingine vya maji vimeathiriwa  na shughuli za binadamu.

"Pamoja na changamoto ya maji tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha nyingi kutekeleza miradi ya maji  wilayani hapa miradi mingine imekamilika na mingine inaendelea na ujenzi,kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria zinafanyika taratibu za kitaalamu kisha mkandarasi  ambaye atafanya kazi na mradi uwe mzuri ,hatuwezi kukaa kuusubiri huo mradi tunaendelea na ujenzi wa miradi mingine ya maji",amesema Mtenjele.

Ameiomba RUWASA kuendelea kuongeza miradi ya maji safi na salama  kwa kile alichoeleza asilimia 46 ya ya maji mjini Tarime ni kidogo ikilinganishwa na uhitaji wa huduma ya maji  lakini pia kufanya jitihada kuhakikisha chujio kubwa linanunuliwa na kuweka dawa kwenye maji ili kuwanusuru wananchi wanaotumia maji machafu yasiyo safi na salama kutoka chanzo cha maji cha mto Nyanduruma.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Tarime Valentine Maganga amesema kuwa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaopita wilaya ya Rorya hadi Tarime ni wa muda mrefu  nakwamba kuchelewa kwa mradi huo ni kuchelewa kutimiza hazma ya Chama cha Mapinduzi.

"Lengo la Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha Serikali inatekeleza ilani ya chama ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani kwa maana yakufikisha maji kwenye jamii,hii hali ya kuchimba visima vifupi na virefu hatutafikia malengo makubwa,ni vizuri zaidi kulifanya ziwa victoria kuwa chanzo cha maji,mradi ukikamilika silimia 98 ya wana Tarime watakuwa wanatumia maji safi na salama’’,amesema Valentine.

Katibu huyo wa CCM ameeleza kuwa awali miradi ya maji ilipokuwa chini ya halmashauri baadhi haikufanyika vizuri kutoka na halmashauri kuwa na Idara nyingi  na hivyo usimamizi kuwa mdogo katika Idara ya maji na kutopewa kipaumbele hali iliyosababisha Serikali kuanzisha RUWASA na kazi imeonekana.

"RUWASA wamefanya kazi kubwa na miradi inaonekana japo bado safari inayoendelea ni ndefu kuna miradi mizuri kama mradi wa Sirari ila wajaribu kuwasiliana na taasisi zingine kama TANESCO ule mradi unahitaji umeme tusipofunga transifoma hatutafika  maana wanalazimika wasukume maji usiku  ambapo watumiaji wa umeme wanakuwa wamepungua  kwa sababu mchana umeme unatumika sana.

"Kitu kikiwa kizuri siyo kwamba kinakosa changamoto,mfano mradi wa Kibasuka umekamilika kwa asilimia 97 wamefanya kazi kubwa huu mradi awali ulijengwa ukakamilika lakini haukutoa maji wamekuja RUWASA wameuendeleza na maji yanatoka,mradi kata ya Manga haujakamilika ila wamefanya kazi nzuri",amesema. 

Valentine ameitaka RUWASA kutoa elimu kwa kamati za Jumuiya za watumiaji wa maji vijijini kwa kile alichoeleza kuwa kamati hizo zimeundwa  lakini hazina elimu yakutosha ikiwemo ya usimamizi wa miradi ya maji na uendeshaji wake na matumizi ya fedha zinazolipwa na wananchi wanapokuwa wakichota maji ya bomba huku akiisisitiza Serikali kutoa fedha kwa wakati kutekeleza miradi kwa kile alichoeleza kuwa kuna baadhi ya miradi ujenzi umefikia asilimia 50 lakini pesa bado hazijafika kukamilisha miradi.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara amesema kuwa  maji ya Tarime ni machafu kutokana na baadhi ya vyanzo vya maji likiwemo lambo la maji kijiji cha Nyakonga kata ya Nyakonga kutofanyiwa usafi wala kuweka dawa ya kutibu maji kwenye tenki zinazohifadhi maji na kusababisha wageni wanaofika Tarime kushindwa kuyatumia maji na wenyeji nao wakihangaika kutafuta maji safi na salama.

Waitara ameongeza kuwa hali hiyo inashusha sifa ya wilaya kutokana na tatizo la maji yasiyo safi na salama kupigiwa kelele kwa miaka mingi,aliiomba Serikali kuharakisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao umekuwa ndiyo hitaji kubwa la watumiaji wa maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tarime Malando Masheku amesema kuwa ili kutekeleza lengo la Serikali la kuwapatia huduma ya maji wananchi waishio vijijini kwa asilimia 85 ifikapo 2025,wilaya ya Tarime upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 47.1 mwaka 2016/2017, hadi wastani wa asilimia 70 kufikia Desemba 2020/2021.

"Mahitaji  ya maji vijijini kwa sasa ni 11900m3/d,lakini uzalishaji uliopo kwa vituo vinavyotoa maji hadi sasa ni 8,330m3/d ikiwa ni asilimia 70, upatikanaji wa huduma ya maji mjini mahitaji ya maji kwa sasa ni 6000m3/d,lakini uzalishaji uliopo kwa vituo vinavyotoa huduma ya maji hadi sasa ni 15000m3d,ikiwa ni asilimia 45 nakwamba miradi ya Sabasaba na Gimenya ikikamilika upatikanaji wa maji utafikia asilimia 56’’,amesema Masheku.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetoa Bilioni 4.33 kutekeleza miradi 9 ya maji zikiwemo Milioni 998,750,000.00 fedha za UVIKO-19 zinazotekeleza miradi miwili ya maji nakwamba miradi yote itakamilika ifikapo Juni,30,2022.
Share:

WANAKIJIJI BUTIAMA WAKACHA KUCHOTA MAJI YA BOMBA WADAI SH. 50 NI PESA NYINGI

Mwananchi wa kijiji cha Masurura akichota maji yasiyo safi na salama
Mashine yakusukuma maji kijiji cha Masurura


Na Dinna Maningo,Butiama

Ugumu wa Maisha unatajwa kuwa ni moja ya sababu inayosababisha baadhi ya wananchi katika kijiji cha Masurura kata ya Bwirege wilaya ya Butiama mkoani Mara,kuacha kuchota maji ya bomba na kuendelea kuchota maji katika visima vya asili na mito ambayo siyo safi na salama kwa kile walichoeleza kuwa malipo ya shilingi 50 kwa ndoo moja ya maji ni pesa nyingi nakwamba wao wamezoea kuchota maji bila malipo.


Licha ya Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutoa fedha za kujenga,kukarabati na kupanua miradi ya maji katika wilaya hiyo kama njia ya kupunguza tatizo la ukosefu wa maji safi na salama vijijini,bado wananchi wanatumia maji yasiyo salama huku wengine wakidai tatizo ni ukosefu wa elimu juu ya umuhimu wa kutumia maji safi na salama.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kutembela miradi ya maji katika wilaya hiyo,mkazi wa kijiji hicho Ester John alisema "Watu wanakwepa kuchota maji ya bomba kwasababu ya gharama sh.50 kwa maisha ya hapa kijijini kwetu ni pesa nyingi,ardhi yetu yenyewe ni changamoto hata kupata mazao ya uhakika uuze upate pesa ni shida.

“Sisi tunategemea kilimo ukivuna mazao ukauze ili upate pesa ya kununua mboga na mahitaji mengine bado tena ununue maji na kwa maisha ya kijijini kuna familia zina watu 10 kwa siku wanatumia maji mengi hata zaidi ya ndoo 10 kila siku hiyo 500 itatoka wapi ?na haya maisha yetu ya kijijini tunayoishi kwa kutegemea kilimo kwakuwa hatuna pesa tunatumia maji ya visima kwakuwa yenyewe tunachota bure bila malipo”,alisema Ester.


Raheli Mugesi alisema "Pesa yakununua mafuta ya kula,nyanya au vitunguu ili uunge mboga hakuna tunakula mboga chukuchuku hiyo pesa ya kulipa kila siku inatoka wapi?tunakunywa uji hauna sukari siyo kwamba tunapenda hapana!nikwasababu ya ugumu wa maisha na pesa kuipata ni kazi hakuna biashara huku zakutuingizia fedha alafu wanatuuzia maji!.

"Kwani ni biashara?hii ni huduma hatukupaswa kutozwa tena fedha ,serikali kama imeamua kutusaidia wananchi wa vijijini tupate maji bure au tulipe kwa mwezi sh.2,000 kama tunavyolipa kwenye visima vya watu wengine vinginevyo maji ya bomba watakuwa wanatuona wakati wa kiangazi visima vinapokauka’’,alisema Mugesi.

Bhoke Wambura alisema "Maisha ya watu wa vijijini ni magumu siyo kama watu wanaoishi mjini ambako kuna fursa nyingi zakutafuta pesa,tunafurahi kutupatia mradi unatusaidia hasa wakati wa kiangazi lakini tatizo bado halitaisha kama watu wataendelea kutumia maji yasiyo safi na salama kwasababu ya fedha.


"Watu wakiacha kuchota maji mradi hautakuwa na tija ukizingatia mradi wenyewe jamii ndiyo inauendesha kifaa kikiharibika fedha za maji ndiyo zitengeneze licha yakwamba mjini matengenezo ya mradi yanasimamiwa na MUWASA na ajira wanalipa wao lakini sisi huku vijijini wanategemea makusanyo ya pesa za maji ndiyo watu walipwe asilimia 10’’,alisema Bhoke.


Naomi Juma alieleza "Yaani nitoe pesa kuchota maji bombani wakati kuna maji ya bure kisimani! maji yenyewe mpaka upange foleni wakati kisimani ukifika unachota maji unaondoka zako bombani mpaka usubiri zamu kituo kimoja cha maji wanachota kitongoji kizima inasababisha watu wachote kisimani kwa sababu yak uogopa foleni,foleni kubwa wakati mwingine watu wanapigana wanagombania maji mwenye nguvu ndiyo anachota haraka”,alisema Naomi.

Maseke Marato alisema kuwa watu wanachota maji visimani ili kuepuka gharama "Watu wanatumia maji ya visima na mto kwa kufua,kuosha vyombo,kunywesha mifugo ili kuepuka gharama anayetumia maji machafu ni kwa sababu ya ugumu wa maisha pesa inakosa hata ya kununua kiberiti,bombani wanaenda tu kufuata maji ya kunywa.

"Awali huu mradi ulikuwa unaendeshwa kwa mafuta ya dizeli na tulichota bure bila kulipia sema kulikuwa na changamoto ya maji tulikaa hata miezi mitatu bila kupata maji ya bomba kwasababu mashine ilikuwa inafanya kazi mara chache yakitoka yanakaa muda ndiyo yatoke,tulichota maji machafu,ila baada ya mradi huu kurekebishwa mashine inaendeshwa kwa umeme’’,alisema.

Maseke alisema kuwa watu hawana uelewa wa umuhimu wa kutumia maji safi na salama nakwamba wakihamashishwa na kupewa elimu itawasaidia kutoendelea kutumia maji machafu"kinachohitajika ni elimu kuna watu watoto wao hawavai nguo utawaona matumbo wazi lakini nguo zipo sh.1000 hawanunui watoto wanakaa uchi,unakataa kutoa sh. 50 unatumia maji machafu ukiugua unatibiwa kwa zaidi ya 20,000 yote ni kwasababu tu ya uelewa mdogo watu waelimishwe’’alisema.

Elizabeth William mkazi wa kitongoji cha senta alisema kuwa mradi huo wa maji umewasaidia na kwamba kabla ya mradi huo walichota maji kwenye malambo ambayo si safi na salama hivyo watu kukwepa maji ya bomba na kwenda kwenye visima ambavyo baadhi maji siyo safi ni kutokana na uelewa mdogo wa umuhimu wa kutumia maji safi na salama.

Josephu Mugendi alisema kuwa mradi huo umesaidia kupunguza wimbi la watu kutumia maji yasiyo safi na salama kwakuwa yanapatikana bombani lakini aliiomba RUWASA kuhakikisha inasambaza maji katika vitongoji vyote na kuhakikisha maji hayakatiki kwakuwa wakati mwingine maji hukosa kwa siku tatu.

Mwenyekiti wa kamati ya Jumuiya ya watumiaji wa maji Masurura (CBUSO) Jacob Hezekia, alisema kuwa kitendo cha wananchi kukwepa kuchota maji ni mazoea na jambo hilo linarudisha nyuma mapato yatokanayo na mradi "mradi ukishakamilika unakabidhiwa kwa wananchi kuusimamia na kuuendesha kifaa kikiharibika fedha za maji ndiyo tunachukua na kurekebisha na pesa hizo hizo bado tumlipe mlinzi na mhasibu hazitoshi.


‘’Mradi ulianza 1981 uliendeshwa kwa mafuta ya dizeli wakati huo wananchi walichota maji bure ,tangu mwaka jana mashine inatumia umeme watu wanalipa sh. 50 kwa ndoo moja fedha ambazo ni kwa ajili ya uendeshaji wa mradi.

"Bomba zinapasuka ovyo,ili kuzuia chngamoto ya wizi wa maji chemba za DP ziwekewe mifuniko ya bati ili tufunge kufuri kuzuia wizi wa maji lakini hizi ni za zege watu wanatoa na kuchota maji,tuna DP 20(vituo vya kutoa huduma ya maji) zinazofanya kazi ni DP 18 moja bado haijakamilika ni nyingine tuliifunga baada ya kukosa msimamizi”,alisema.

Jacob alisema kuwa hadi sasa kuna makusanyo ya fedha za maji sh.135,000 zilizopo benki "fedha zinazopatikana ndiyo zinatumika kwenye matengenezo ya mradi,tunalipa umeme na tunamlipa mlinzi,Mhasibu na katibu asilimia 10 ya malipo ya maji,kuna shida ya getivalvu hakuna bomba likiharibika maji yanamwagika hakuna namna ya kuyazuia inabidi ufunge tenki au laini ya maji iliyopasuka.

Alisema kuwa baadhi ya wananchi hawajafikiwa na mradi wa maji wakiwemo wa kitongoji cha Bumagwa,Sei,Malama,Nyakangara,Taho na Kumunya wanatembea umbali zaidi ya km 3 kutafuta maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini( RUWASA)wilaya ya Butiama,Mafuru Dominico alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha kutekeleza miradi saba ya maji kiasi cha Bilioni 2.4,vijiji vilivyonufaika na miradi ya maji ni kijiji cha Biatika kata ya Buhemba,Nyasirori kata ya Masaba.

Aliongeza kuwa miradi mingine ni ya fedha za UVIKO-19 kijiji cha Nyamikoma kata ya Kyenyari,kijiji cha Mwibagi kata ya Kyenyari,Buswahili kata ya Buswahili,Kyankoma kata ya Nyamimange na mradi wa uboreshaji wa visima vya pampu ya mikono kwa kufunga sora za umeme katika vijiji vinne ambavyo ni kijiji cha Mmazami,Kyatungwe,Masurura na Nyambili na itakamilika juni 30/2022.
Share:

BARRICK YAKABIDHI MASHINE ZA KUPIMIA UVIKO -19 HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (katikati) akikata utepe wakati Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation kupitia Migodi yake ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation kupitia Migodi yake ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi imekabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya Dola 50,000 sawa na shilingi za Kitanzania 115,000,000/= katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga.

Mashine hizo zimekabidhiwa leo Jumamosi Machi 19,2022 na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Mashine za Kupimia COVID – 19, Meneja Mkuu wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare amesema Mashine hizo zitasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na hivyo kuwezesha utambuzi UVIKO – 19 kwa haraka zaidi.

“Kampuni ya Barrick kupitia Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi inaendelea kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO -19. Tunakabidhi mashine hizi mbili za kisasa za kupimia UVIKO – 19 ambapo kila mashine ina gharama ya Dola 25,000”,amesema Sangare.

Naye Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra amesema mashine hizo zina uwezo wa kupima Sampuli nne ndani ya saa moja hivyo kuwahamasisha wananchi kufika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya UVIKO- 19 .

Akipokea Mashine hizo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema ameishukuru Kampuni ya Barrick ameishukuru kwa kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO – 19.

“Barrick hamjawa nyuma,mmekuwa kimbilio letu kila wakati, serikali inapokuwa na jambo,mmekuwa mkifungua mikono yenu. Asanteni sana kwa kuiunga mkono serikali kwa jambo hili jema la kuleta vifaa ambavyo ni vya kisasa zaidi vitakavyoweza kupima mgonjwa na kubaini kama amepata maambukizi ya UVIKO – 19. Hapa Kahama kuna mwingiliano mkubwa wa watu hivyo zitasaidia kupima watu wengi”,amesema Mjema.

Mjema ameutaka uongozi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama kutumia mashine hizo kwa matumizi stahiki ili viweze kuwasaidia wananchi.

“COVID – 19 bado ipo. Mmepata vifaa hivi, watangazieni wananchi kuhusu uwepo wa mashine hizi waje wapime kwani mashine hizi zinatoa majibu ndani ya saa moja tu. Zitasaidia kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma ya vipimo vya UVIKO – 19 katika Viwanja vya ndege au Jijini Dar es salaam”,amesema Mjema.


Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Mzee ameishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuwapatia mitambo hiyo ya kupimia UVIKO – 19 kwani Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa imeathiriwa na COVID – 19 katika wimbi la tatu hivyo kuahidi kutunza mashine hizo na kuhakikisha zinatumika kama inavyopaswa.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare (kulia) akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya Shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumamosi Machi 19,2022. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema. Katikati aliyevaa kofia ni Meneja Mkuu wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (katikati) akikata utepe wakati Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation kupitia Migodi yake ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. Kulia ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare, kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen.
Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra akimwelezea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) kuhusu Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 zilizotolewa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) akizungumza wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga.  Kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare akifuatiwa na Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra.
Muonekano wa Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 zilizotolewa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. 
Muonekano wa Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 zilizotolewa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. 
Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra (kushoto) na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Mzee wakikagua vifaa vya kupimia UVIKO - 19 vilivyotolewa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) akizungumza wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen akifuatiwa na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare. Wa kwanza kulia ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama Dkt. David Lucas akifuatiwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Mzee.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) akizungumza wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. Walioketi kulia ni Wafanyakazi wa Kampuni ya Barrick.
Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra akizungumza wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Mzee akizungumza wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen akifuatiwa na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare na  Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare (wa tatu kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115. Wa kwanza kulia ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama Dkt. David Lucas akifuatiwa na Katibu Tawala wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Share:

Friday, 18 March 2022

KAMATI YA BUNGE 'LAAC' YATEMBELEA MRADI WA MACHINJIO YA KISASA MANISPAA YA SHINYANGA...YAAGIZA WAONGEZE MIFUGO YA KUCHINJA


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi akizungumza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga na kuuagiza Uongozi wa Manispaa hiyo kufanya jitihada za maksudi kuimarisha eneo la Masoko kwa kuongeza idadi ya ng’ombe na mbuzi wanaotakiwa kuchinjwa ili mradi ulete tija.

Akizungumza baada ya Wajumbe wa LAAC waliombatana pia na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange kutembelea Mradi huo leo Ijumaa Machi 18,2022, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi amesema licha ya kukamilika kwa mradi huo lakini wamebaini kuwa idadi ya ng’ombe wanaotakiwa kuchinjwa haitoshi ukilinganisha na uwezo wa machinjio hiyo.

“Tumeona mradi umekamilika na umeanza kufanya kazi lakini tulichobaini ni kwamba mradi ni mkubwa, una uwezo mkubwa lakini kwa sasa hakuna ng’ombe na mbuzi wa kutosha kufikia kiwango cha uzalishaji kilichopo.

Kamati inafahamu kwamba hii miradi ya kimkakati ambayo fedha zilitoka Benki ya Dunia ambapo halmashauri nyingi ikiwemo hii ya Manispaa ya Shinyanga ilipata na kuanzisha miradi na nyinyi Shinyanga mlianzisha Mradi wa machinjio ya kisasa lengo lake lilikuwa Halmashauri itengeneze miradi ili hiyo miradi igeuke kuwa vyanzo vya mapato”,amesema Zedi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukene mkoani Tabora.

“Sasa mradi wa Machinjio umekamilika, ushauri wetu ni kwamba zifanyike jitihada za maksudi, lazima mpate watu wa masoko wazuri wanaoweza kuisukuma vizuri, wapite huko na huko ili mpate ng’ombe na mbuzi wa kutosha wa kuchinja kwa sababu mradi huu una uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 kwa siku lakini sasa mnachinja ng’ombe 20 kwa siku na pia wanatakiwa kuchinjwa mbuzi 1000 lakini sasa mnachinja mbuzi 38 kwa siku”,amesema Zedi.

Ameongeza kuwa lengo la miradi ya kimkakati ni kuzifanya halmashauri zijitegemee ziwe na vyanzo vya mapato hivyo kuutaka uongozi wa Manispaa ya Shinyanga kuongeza ubunifu ili mradi huo uwe na manufaa zaidi.

“Tunajua Menejimenti, Mkurugenzi wa Manispaa na timu yako, Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa huu mradi mmeukuta kwa jinsi mlivyojieleza, kamati ina imani na utendaji kazi wenu, tunajua mna uwezo wa kuibadili hii hali ya machinjio hii ili ilete tija.Tunakupongeza Mkurugenzi kwa kushirikisha Waheshimiwa Madiwani na hata kwenye hii ziara wapo tunajua haya tuliyoyaacha waheshimiwa madiwani wataendelea nayo”,amesema Zedi.

Naye Mjumbe wa Kamati ya LAAC, Mhe. Rashid Shangazi ambaye ni Mbunge wa Mlalo mkoani Tanga ameushauri uongozi wa Manispaa ya Shinyanga kubuni miradi mingine jirani na machinjio hiyo ya kisasa ili kuongeza mapato.

“Haya mapungufu ya mradi wa machinjio siyo jambo dogo,Mkurugenzi najua umerithi haya matatizo ya mradi tumia ubunifu mpya kuendeleza mradi huu na kutengeneza miradi mingine ikiwemo viwanda vidogo katika eneo hili la machinjio. Hii njia tuliyopotea tusiendelee kupotea zaidi”,amesema Shangazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Mrisho Satura amesema wameyapokea maelekezo ya Kamati ya Bunge (LAAC) ikiwa ni pamoja na kuimarisha eneo la masoko na kurekebisha kasoro zilizokuwepo ili kuleta mabadiliko na mradi ulete tija.

Akisoma taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi, Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim amesema ujenzi ulianza rasmi Mei 26,2017 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 2018 hata hivyo ujenzi haukukamilika kwa wakati hivyo ulisogezwa mbele hadi Novemba 31,2021.

Amesema kwa sasa ujenzi wa miundo mbinu ya machinjio umekamilika kwa asilimia 100 na jumla ya fedha zilizotumika mpaka sasa ni shilingi 5,969,863,980.29.

“Tangu kuanza kwa uchinjaji hadi hadi tarehe Machi 11,2022, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imekusanya jumla ya shilingi 93,540,000/= sawa na wastani wa shilingi 26,107,000/= kwa mwezi. Aidha gharama za uendeshaji ni shilingi 15,205,588.79 kwa mwezi ambazo zinahusisha malipo ya vibarua 31, BAKWATA, ulinzi, umeme na maji”,amesema Chamzhim.

“Mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji iliyopo ni pamoja na kuchimba kisima kirefu na kuweka tenki ili kuwa na maji yanayoweza kutumika katika machinjio na kuweka mfumo wa kuvuna maji ya mvua”,amesema.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi (katikati aliyevaa koti la bluu) akiwasili leo Ijumaa Machi 18,2022 katika Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wajumbe wa LAAC. Kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Muonekano wa sehemu ya Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi (wa tatu kulia aliyevaa koti la bluu) akiwa katika eneo la kupumzikia mifugo kwenye Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wajumbe wa LAAC. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Jomaary Satura akifuatiwa na Mjumbe wa Kamati ya LAAC Rashid Shangazi ambaye ni Mbunge wa Mlalo mkoani Tanga ,Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko. Wa kwanza kulia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko akifuatiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),Selemani Zedi (katikati aliyevaa koti la bluu) akizungumza baada ya kuwasili katika Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
 Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim akisoma taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi wakati Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilipotembelea mradi huo.
 Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim akionesha Mitambo ndani ya Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kwa wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea mradi huo.
Wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wakiangalia mitambo ndani ya Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza jambo wakati wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
 Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim akionesha chumba cha Ubaridi ndani ya Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kwa wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea mradi huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi akizungumza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga na kuuagiza Uongozi wa Manispaa hiyo kufanya jitihada za maksudi kuimarisha eneo la Masoko kwa kuongeza idadi ya ng’ombe na mbuzi wanaotakiwa kuchinjwa ili mradi ulete tija.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe.Rashid Shangazi  akizungumza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Share:

LAAC YAIPONGEZA HALMASHAURI YA MANISPAA YA KAHAMA

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imempongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Festo Kiswaga na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Anderson Msumba kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi yake katika Halmashauri hiyo.

Makamu Mwenyekiti Mhe. Selemani Zedi aliyasema hayo wakati akihitimisha ziara ya kamati ya siku mbili Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.

Mwenyekiti alisema amefurahi kuona asilimia kumi iliyotengwa kwenye fedha za Halmashauri zinaenda kwa akina mama na walemavu kama ilivyokusudiwa.

Kamati ilishauri wanufaika wa saccos za kina mama waongezeke na pia Mkurugenzi aangalie utaratibu wa kuwapa mikopo vijana ili waweze kujiendeleza kibiashara.

Pia Kamati iliridhishwa na kasi ya mradi wa Hospitali ya OPD- Hospitali ya Manispaa ya Kahama ambayo ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95 na kuahidi kukabidhi ndani ya siku 13.

Kwa upande wa vijana wa Sacco wamemshukuru sana Mhe. Rais Mama Samia kwa mikopo hii wanayoletewa kwa wakati na Mkurugenzi kuahidi kuwaongezea fedha za mikopo hiyo.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger