Wednesday, 14 August 2019

Msemaji Mkuu wa Serikali: Nchi 16 Zimethibitisha Kushiriki Mkutano Mkuu Sadc Tanzania 2019

Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO
Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimethibitisha kushiri Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika  Jijini Dar es Salaam, Tanzania  Agost 17 na 18 mwaka huu.

Akizungumza katika Kipindi cha 360 cha Clouds Tv, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi alisema maandalizi yamekalika na sasa Tanzania iko tayari kwa ugeni huo.

Dkt. Abbasi alisema kuwa mkutano huo ulitanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo Maonesho ya Wiki ya Viwanda kutoka nchi wanachama wa SADC, Vikao vya Maafisa Waandamizi kutoka SADC, Vikao vya Mawaziri kutoka SADC na Mikutano mbalimbali ya sekta za SADC, ambapo maeneo haya yote Tanzania inachukua uenyekiti wa Nchi Wanachama.

“ Katika mikutano yote iliyotangulia karibu nafasi zote za SADC kuanzia zile za kusimamia kamati, kusimamia mabaraza mbalimbali, Tanzania imechukua hatamu, kwani kuna sekta nyingi sasa zimeshachukua uenyekiti, Juzi Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania  alichukua kiti hicho cha  kwenye kamati ya wanachama wa SADC, vilevile Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania naye alichukua nafasi hiyo kwenye Kamati ya Mawasiliano SADC”, Dkt. Hassan Abbasi.

Dkt.Abbasi alisema kuwa kuelekea kwenye tukio lenyewe ambalo ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Wafalme kutoka Serikali 16 za nchi wanachama, zimethibitisha kushiriki mkutano huo na kuwa viongozi wao wataanza kufika nchini kuanzia tarehe 15 na kuendelea.

Aidha Dkt.Abbasi alisema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa Kitovu cha Amani kwa nchi za kusini mwa Afrika, kwa hiyo viongozi wengi wa nchi hizo watakuja Tanzania kama wanarudi nyumbani, ambako ni kituo cha ukombozi wa nchi zao, na kufanya mkutano ambapo Agost 17 na 18 Wakuu wa  Nchi Wanachama watasaini mikataba mbalimbali na kuhitimisha ajenda zao.

Aliongeza kuwa kabla ya kufika mkutano wa wakuu wa nchi kuna matukio mengine kama vile Mabalozi na wawakilishi wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali kuwasili nchini; ikiwa ni lengo la kushiriki Mkutano Mkuu ambapo pia wamepata wasaa wa kufanya ziara katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu  ya Tano.

“Kabla ya kufika Mkutano Mkuu, kuna matukio mbalimbali ambayo pia ni makubwa na ni muhimu sana kwa nchi yetu, leo tunatukio kubwa la Mabalozi 42 wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani wanatembelea mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project( JK HPP) na kesho watatembelea mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) na hawa wote wako nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa SADC”, Alisisitiza  Dkt.Abbasi.

Dkt.Abbasi alisema kuwa Mabalozi hao wamekwenda kuona kwa mfano, ni nini serikali yao inatekeleza ili wakirudi katika maeneo yao ya kazi wapate kuyatangaza waliyoyaona na kuweza kuleta wawekezaji watakao kuja kuwekeza nchini na kuleta mapato kwa taifa.

Pia, Dkt. Abbasi alisema kuwa leo Tanzania itampokea  Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye atawasili nchini kwa ziara ya siku mbili kabla ya Kusiriki Mkutano Mkuu, na ziara yake itajikita zaidi katika kutembelea eneo la wapigania uhuru Mazimbu, Mkoani Morogoro, ili kujenga kumbukizi ya Udungu kati ya Tanzania na Afrika Kusini.


Share:

Zaidi Ya Vijana 500 Nchini Tanzania Wanatarajia Kukutana Jijini Dodoma Agosti 15 Katika Kongamano La Vijana

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Katika kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa ya  vijana Duniani ambapo  huadhimishwa Agosti 12 kila mwaka ambapo kwa Tanzania Maadhimisho hayo  kwa Mwaka 2019 yamesogezwa mbele hadi Agosti 15 na  16,2019  ,Zaidi ya vijana 500 kutoka Tanzania  wanatarajia kukutana jijini Dodoma .
 
Akizungumza na Waandishi Wa Habari leo Agosti ,14,2019 Jijini Dodoma ,Meneja  Mradi wa shirika la Kimataifa la  idadi ya Watu  [ UNFPA]  kwa Tanzania , katika kitengo cha Maendeleo ya vijana Dkt. Majaliwa Marwa amesema mwaka huu itakuwa ni kutimiza miaka 20 tangu maadhimisho hayo kuanzishwa maadhimisho hayo 
 
Ametaja Malengo ya Maadhimisho hayo kuwa ni pamoja na kupanua wigo uelewa juu ya vijana pamoja na changamoto zinazowakabili na Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kasim Majaliwa na mada zitakazowasilishwa ni pamoja na na elimu ya uzazi kwa vijana pamoja na changamoto za ajira kwa vijana.
 
Kwa Upande wake,Mwakilishi wa Shirika linaloratibu masuala ya vijana Tanzania[Restless Development] Bw.Ridhione Juma amesema  shirika hilo litahakikisha  kuwa na ulinganifu kwa makundi ya watu maalum ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu huku katibu wa Asasi ya Vijana Tanzania [AFriYAN] akiishukuru Serikali ya Tanzania kwa Kutoa Elimu Bure.
 
Afisa  Mawasiliano  wa shirika la  Kazi Duniani [ILO]kwa Afrika Mashariki  Bw.Magnes Minja amesema utafiti uliofanyika mwaka 2014 ulibaini kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ilikuwa asilimia 11.7&  ikilinganishwa na ukosefu wa asilimia 10.3 % kwa ukosefu wa ajira kiujumla huku meneja mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa[UN]Bi.Stella Vuzo akisema ajenda kuu ya Umoja wa Mataifa ni Malengo ya Maendeleo endelevu.
 
Naye  Mwakilishi wa UN Kitengo cha Habari nchini Tanzania ,Dokta.Warren Bright Hasheem amesema elimu inatakiwa kuwa jumuishi pamoja na ajira kwa vijana  pamoja na Malengo endelevu  ya miaka 15 na malengo ya millennia ya miaka 15.
 
Maadhimisho ya vijana Dunia yalianza yalianzishwa mwaka 1999 katika mkutano mkuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo kauli mbiu mwaka 2019 ni Elimu.


Share:

Mhadhiri wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Samson Mahimbo Afikishwa Mahakamani Kwa Kuomba Rushwa ya Ngonoi Kwa Mwanafunzi Ili Amsaidie Kufaulu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Agosti 14, imemuachia kwa dhamana mhadhiri wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Samson Mahimbo anayekabiliwa na mashtaka ya kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake.

Mshtakiwa hayo amesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na Wakili kutoka TAKUKURU ambapo inaelezwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 12, 2017.

Imeelezwa kuwa mshatakiwa alitenda kosa hilo akiwa katika nyumba ya kulala wageni ya Com David iliyopo katika maeneo ya Mlalakuwa, Mwenge, kwa kumlazimisha mwanafunzi wake kutoa rushwa ya ngono kwa madai ya kwamba angemsaidia ufaulu katika masomo yake.

Mara baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana kutotenda kosa hilo na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuahirishwa hadi Septemba 17, 2019. Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.


Share:

Waziri Mhagama Akagua Miradi Ya PSSSF Na NSSF Mkoani Mwanza

Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameagiza watendaji wa Mifuko ya hifadhi ya Jamii yaani Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa wabunifu katika kuwekeza kwenye vitega uchumi vyenye kuleta tija na inayochochea maendeleo ya Taifa.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake Jijini Mwanza alipokuwa akikagua Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii ili kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji.

Alieleza kuwa kuwekeza katika miradi yenye tija ni jambo muhimu kwa kuwa miradi hiyo italeta maendeleo endelevu yatakayochangia katika ukuaji wa pato la taifa na ustawi wa mkoa huo.

“Mwanza ni miongoni mwa Mikoa yenye fursa nyingi za kibiashara kutokana na sehemu kubwa ya mkoa huo kuzungukwa na ziwa viktoria, hivyo kurahisisha ukanda huo kufikiwa kwa urahisi na soko la Afrika Mashariki,” alisema Mhagama.

Alifafanua kuwa ubunifu katika kutekeleza shughuli za mifuko ni pamoja na kutafuta masoko ya vitenga uchumi ya miradi hiyo kwa kuangalia fursa zilizopo kwenye kanda ya ziwa.

Aliongeza kuwa fursa ni pamoja na ujenzi wa daraja la Busisi litakalopita ziwa viktoria, Mbuga ya Wanyama ya Burigi pamoja na shughuli za uchimbaji madini zilizopo katika mkoa huo.

Katika Ziara hiyo Waziri Mhagama aliweza kutembelea linapojengwa Soko la Madini katika Jengo la Kibiashara la Rock City Mall. Pia alitembelea jengo la PSSSF Mwanza na alipata fursa ya kukagua shughuli za uwekezaji katika jengo hilo zinazoendeshwa na wawekezaji wazawa katika Hoteli ya Gold Crest.


Share:

Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Chatakiwa Kuwajengea Uwezo Maafisa Mipango

Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) kimetakiwa kutoa mafunzo ya takwimu rasmi za Serikali kwa maafisa mipango nchini ili kuwajengea uwezo wa kufuatilia na kufanya tathimini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka Mitano katika maeneo yao ya kazi.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na  Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya ziara katika Chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kufuatilia utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19  katika Chuo hicho.

Alisema kuwa mafunzo ya takwimu rasmi za Serikali yanatakiwa kutolewa kwa Maafisa Mipango  kuanzia ngazi ya Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa ili kuwezesha kufanya tathimini ya mipango ya maendeleo na kuweka mikakati yenye tija kwa taifa hususani kwa wananchi wa hali ya chini katika kukuza kiwango chao cha maendeleo katika nyanja ya uchumi, kijamii na masuala ya sayansi na teknolojia.

“Wizara ya Fedha na Mipango inayonafasi kubwa ya kuhakikisha Chuo hiki kinajiimarisha katika Sekta ya miundombinu na kuweza kutekeleza shughuli zake vizuri kwa maendeleo ya nchi”, alieleza Dkt. Kazungu

Aidha Dkt. Kazungu, amekitaka Chuo hicho kujikita katika ubunifu kwa kubuni program mbalimbali za kitaaluma zitakazowavutia wanafunzi, jambo litakaosababisha ongezeko la wanafunzi na kuimarika kwa kipato cha Chuo, hivyo kupunguza utegemezi kwa Bajeti Kuu ya Serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Dkt. Frank Mkumbo, alisema kuwa kuna utofauti kati ya takwimu rasmi zinazotolewa na chuo hicho na takwimu zinazotolewa na vyuo vingine, kwa kuwa EASTC hutoa takwimu rasmi za Serikali zikiwemo za mfumuko wa bei, idadi ya watu na hata kiwango cha uzalishaji wa bidhaa nchini.

Dkt. Mkumbo, ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kazungu, yakiwemo ya kutoa mafunzo kwa maafisa mipango na kuanzisha kozi zitakazo ongeza idadi ya Wanafunzi lakini pia kuendelea kushirikiana na wizara katika kutekeleza shughuli mbalimbali.

Mkuu huyo wa Chuo amesema, ziara ya Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kazungu, katika taasisi zilizopo chini ya Wizaya ya Fedha na Mipango, kikiwemo Chuo cha EASTC imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa utaimarisha upatikanaji wa mapato na kuongeza ufanisi wa utoaji elimu.

Mwisho.


Share:

Waziri Mabula Akemea Ucheleweshaji Utoaji Hati Za Ardhi

Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekemea ucheleweshaji utoaji Hati za Ardhi katika Manispaa ya Halmashauri ya Tabora mkoani Tabora na kueleza kuwa hali hiyo inachangia kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 13 Agosti 2019 wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua mifumo ya kodi kwa njia ya kielektronik na Masijala ya ardhi katika mkoa wa Tabora.

Kauli ya Naibu Waziri wa Ardhi inafuatia kubaini uwepo Hati za Ardhi 92 katika Manispaa hiyo ambazo hazijafanyiwa kazi kwa muda mrefu kwa maelezo kuwa baadhi ya majalada ya hati hizo yalikuwa na upungufu na wahusika wake hawapatikani.

Dkt Mabula alishangazwa na hali hiyo kwa kuwa baadhi ya maombi ya Hati za Ardhi yana zaidi ya miaka miwili katika Ofisi ya Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Tabora tangu mwaka 2016 bila kufanyiwa kazi jambo alilolieleza kuwa linawakatisha tamaa wananchi wanaoomba Hati.

Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru kumuandikia barua ya onyo Afisa Ardhi Mteule wa Daudi Msengi kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kwa sasa Wizara yake haitamvumilia Mtumishi yeyote wa sekta ya ardhi atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake na kusisitiza kuwa kuwa  upandishwaji vyeo kwa watmushi utazingatia utendaji kazi na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Amezitaka Halmashauri nchini kupanga malengo ya uandaaji Hati za Ardhi kwa watendaji wake ili kuelewa kwa siku moja zinaandaliwa Hati ngapi na kufafanua kuwa hiyo itazisaidia halmashauri kufikia malengo ya utoaji hati. Dkt Mabula alitolea mfano wa halmashauri ya Ilemela mkoani Mwanza kuwa imejiwekea malengo ya kuandaa hati tano kwa siku moja jambo lililoiwezesha kuandaa hati nyingi na hivyo kuwa moja ya halmashauri inayofanya vizuri kwa utoaji Hati za Ardhi.

Dkt Mabula alisema, manispaa ya Tabora imeshindwa hata kutimiza malengo yake ya kutoa hati katika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Manispaa hiyo ilijiwekea kutoa jumla ya Hati 2000 lakini ilifanikiwa kutoa 1200 tu.

Aidha, alitaka suala la kuandaa Hati za Ardhi lifanywe na Maafisa Ardhi kwa kuwa wote wana taaluma ya ardhi badala ya kumtegemea Afisa Ardhi Mteule ambaye wakati mwingine  amekuwa akichelewesha kwa kisingizio cha kutingwa na shughuli nyingi.

Ameitaka Manispaa ya Tabora kuongeza kasi ya utoaji Hati za Ardhi kwa wananchi  katika Manispaa hiyo ili kuwamilikisha na kuchangia mapato ya serikali kupitia kodi ya ardhi sambamba na kuhimiza Maafisa Ardhi kuwa na kauli nzuri kwa wateja  kwa lengo la kujenga mazingira mazuri ya utendaji.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewakabidhi wananchi kumi na tano wa eneo la Uledi katika Kata ya Mpera mkoani Tabora Hati za Ardhi kwa niaba ya wenzao takriban 2117 baada ya kukamilisha taratibu za kupatiwa hati.

Dkt Mabula alisema usalama wa miliki ya ardhi ni kupatiwa Hati ya Ardhi na kusisitiza usalama wa eneo siyo kuwekewa Beacons pekee bali wananchi wanahitaji kupatiwa hati ili ziweze kuwasaidia katika shughuli za uchumi ikiwemo kuchukua mikopo benki.

Ameagiza kukamatwa kwa wale wote waliohujumu alama za mipaka katika maeneo ya ardhi eneo la Uledi kwa kung’oa Beacons na kusisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na wote waliofanya kosa hilo wachukuliwe hatua ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya sheria

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera alisema upimaji ardhi katika Manispaa ya Tabora kwa sasa umeongezeka tofauti na miaka ya nyuma ambapo maeneo mengi yanapimwa na kupangwa na kubainisha kuwa ofisi yake itahakikisha wananchi wanamilikishwa na kueleza kila mwananchi mwenye eneo kufuatilia taratibu za kumilikishwa.


Share:

UPDATES: Majeruhi Wengine 6 ajali ya Moto Morogoro Wafariki Dunia Usiku wa Kuamkia Leo....17 Bado wako ICU

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminieli Aligaesha  amesema  Majeruhi 6 kati ya 38 wa ajali ya moto ya mkoani Morogoro ambao walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamefariki Dunia usiku wa kuamkia  leo hospitalini hapo. 
 
Aminiel amesema Majeruhi waliobaki ni 32 ambapo kati yao  Wagonjwa 17 Wako ICU huku wengine  15 wakiwa Wodi ya Kawaida.


Kwa takwimu hizi mpya zilizotolewa leo, Mpaka sasa idadi ya waliofariki kwenye ajali hiyo  itakuwa imefikia  watu 82.


Share:

Malinzi Atoa Utetezi Wake Mahakamani

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (59), amedai mahakamani kuwa wakati anaingia madarakani shirikisho hilo lilikuwa na hali ngumu kiuchumi iliyosababisha madeni makubwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha akaunti zake kufungwa kila wakati na kusema kuwa siku chache kabla ya kukamatwa, aliikopesha TFF Sh. Milioni 15.

Malinzi alitoa madai hayo jana wakati akijitetea dhidi ya mashtaka ya kughushi na kutakatisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Richard Rweyongeza, Malinzi alidai hali hiyo ilikuwa ikimlazimu kuikopesha TFF fedha zake binafsi na alikuwa akifanya hivyo kupitia akaunti waliyoifungua kati yake na shirikisho hilo.

 Amedai kiasi hicho cha sh. Milioni 15, zilikuwa ni kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa kufuzu fainali za Afrika kati ya Tanzania na Lesotho

Amedai akiwa Rais, alihakikisha shughuli mbalimbali za timu zinakwenda hadi kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa ambapo ili kufanikisha hilo, mara nyingine ilikuwa ikimlazimu kutumia fedha zake za mfukoni ili kuweza kuinusuru TFF .

Malinzi alidai kuwa aliikopesha TFF kutokana na hali ngumu ya kifedha iliyokuwa ikiikabili na hivyo kulazimika kutumia fedha zake binafsi, kukopa kwa watu binafsi ama kamati ya utendaji ili kunusuru hali hiyo hasa katika matukio muhimu yanayoikuta TFF na timu ya Taifa Taifa Stars.

Akiendelea kutoa utetezi wake, alidai, baadhi ya matukio ambayo alilazimika kutoa fedha zake na kuikopesha TFF mojawapo ni ile ya kulikomboa basi la TFF ambalo lilikuwa linashikiliwa na kampuni ya udalali ya Yono kufuatia amri ya mahakama la kuilipa Kampuni ya Pachi Line iliyokuwa ikitoa huduma za tiketi uwanjani.

Aliendelea kudai kuwa, aliilipa sh milioni 20 kwa kampuni ya udalali ya Yono ambapo TFF ilikuwa ikidaiwa na TRA na walitaka kukamata basi ambalo lilitolewa na wafadhili wao, Kampuni ya Bia ya TBL,Pia alilipia sh.milioni 40 za tiketi za ndege Kampuni ya Ethiopia Airline, za wachezaji wa Tàifa Stars waliokuwa wanakwenda Nchini Nigeria katika Mashindano ya Afrika yaliyokuwa yakufuzu Misri

Aidha aliongeza kudai kuwa aliwahi kuikopesha TFF USD 7000 wakiwa Harale, Zimbabwe baada ya wachezaji waTaifa Stars kutolewa mizigo yao nje ya hoteli waliyokuwa wamefikia kwa sababu Shirikisho la mpira Zimbabwe lilikuwa likidaiwa na hoteli hiyo,  na kusema hata baadhi ya mashahidi waliowahi kutoa ushahidi mahakamani hapa walithibitisha hilo akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa TFF Daniel Masangi.

Aliwataja mashahidi wa upande wa mashtaka waliodhibitisha jambo hilo Mahakamani akiwemo Katibu Mkuu Wilfred Kidao, Hellen Adam na Sareki Yonasi.Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Selestine Mwesigwa


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 15 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya uwamuzi wa kupokelewa kwa kielelezo cha nyaraka ya taarifa ya madeni kati ya TFF na Malinzi ama la.

 
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Selestine Mwesigwa.



Share:

Kesi Ya Tundu Lissu Kupinga Kuvuliwa Ubunge Kusikilizwa Kesho

Kesi ya kupinga kuvuliwa ubunge iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, inatarajiwa kuanza kusikilizwa kesho.

Hati ya kuwaita pande mbili imetolewa jana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikiwaita wahusika kufika katika shauri hilo linalosikilizwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa.

Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Lissu alifungua shauri la maombi  Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo.

Mwombaji huyo anaomba mahakama impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu  alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na masilahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

Mwanasheria huyo Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amekuwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kunusurika katika jaribio hilo la mauaji kwa takribani miaka miwili, tangu  Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa.




Share:

SENGERAMA ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA


Diwani wa kata ya Iselamagazi amechaguliwa  kuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Uchaguzi huo umefanyika Agosti 13,2019 ambapo madiwani 35 wa halmashauri walimpigia kura Sengerema .Pichani ni Isack Sengerema akiwashukuru madiwani kwa kumchagua na kumuamini tena kwa kufikisha kipindi cha miaka mitano kutumikia nafasi  hiyo sasa tangu alipochaguliwa mwaka 2015 alipopata nafasi ya udiwani akiwa mgombea pekee aliyejitokeza. Picha zote na Kareny Masasy Malunde1 blog
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba akisoma ajenda za mkutano wa baraza la madiwani la kufunga mwaka wa 2018/2019 ambapo miongoni  ajenda zilizokuwepo ni uchaguzi wa makamu mwenyekiti ikiwa Isack Sengerema alipigiwa kura na kuchaguliwa na wajumbe 35 waliopiga kura.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakipiga kura kuchagua makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo
Madiwani wakiwa katika baraza la robo ya kwanza ya mwaka wakimsikiliza mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ngassa Mboje aliyekuwa akiendesha kikao. 
Baraka Balongo aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa makamu mwenyekiti na kamati mbalimbali katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga akikabidhi nyaraka alizokuwa amekabidhiwa baada ya kukamilika uchaguzi na kupatikana mshindi.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zikiibuliwa ndani ya kikao hicho. 
Madiwani wakifuatilia ajenda za kikao na kuperuzi makaburasha. 
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Shinyanga Ngassa Mboje akifunga kikao cha baraza la madiwani baada ya kumpata makamu mwenyekiti ambaye ni Isack Sengerema na kamati ya kudumu ya fedha, kamati za uchumi,ujenzi na mazingira, kamati ya afya ,elimu na maji kamati ya maadili na kamati ya Ukimwi. 
Share:

Mashine ya Ultra sound yaibwa Simiyu

Mashine inayotumika kupima magonjwa ya ndani na kutambua taarifa mbalimbali katika mwili wa binadamu (Ultra sound) imeibiwa katika mazingira ya kutatanisha kwenye Hospitali ya mji wa Bariadi (Somanda) mkoani Simiyu.

Mashine hiyo inadaiwa kuibiwa pamoja na kifaa chake cha kudurufu picha (printer) ambapo ilikuwa maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya akina mama wajawazito na iliibiwa ikiwa kwenye wodi hiyo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, amekiri kuibiwa kwa mashine hiyo ambapo amesema hadi sasa bado haijapatikana.

Mabimbi amesema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo waliweza kutoa taarifa jeshi la polisi, ambapo watu 17 wakiwemo wauguzi walikamatwa kwa ajili ya mahojiano.

“Ni kweli mashine hiyo ambayo ilitolewa na wadau wa maendeleo UNFPA kwa ajili ya wodi ya akina mama tu iliibiwa katika mazingira ya kutatinisha, tayari taarifa tulitoa na polisi wanaendelea na uchunguzi,” amesema.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Mwanaidi Churu, amesema mazingira ya kuibiwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma waliokuwepo wodini siku hiyo kila mmoja kudai hajui.

Credit: Mtanzania


Share:

Rais mstaafu Benjamin Mkapa kueleza uzoefu wake SADC Kesho

Mwenyekiti  mstaafu wa SADC na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, atatoa mhadhara kwa umma kesho kuhusu uzoefu wake katika jumuiya hiyo.

Mhadhara huo utakaowashirikisha wasomi, wachambuzi wa masuala ya kikanda, wanasiasa, wachumi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida, utafanyika katika jengo jipya la maktaba la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano 14 August
























Share:

Tuesday, 13 August 2019

DED KYERWA AWATAKA VIJANA KUWA WABUNIFU,KUTAMBUA VIPAJI VYAO



Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Shedrak Mohamed

Vijana wilayani Kyerwa mkoani Kagera wametakiwa kuwa wabunifu katika  masuala mbali mbali ya  kiuchumi kuliko kusubiri ajira kutoka serikalini.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 13,2019,na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Shedrak Mohamed katika mwendelezo wa wiki ya uwekezaji Kagera yenye lengo la kutangaza fursa za mkoa wa Kagera.

Mohamed amesema vijana wanatakiwa kubuni na kutambua vipaji walivyonavyo kuliko kukaa bila kazi huku baadhi wakisubiri ajira kutoka serikalini.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika wilaya yake ya Kyerwa kipaumbele ni kwa vijana ili kujenga taifa imara na lenye nguvu.

Amesema vijana wanatakiwa kuchangamkia  fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa na halmashauri.

Hata hivyo ametoa wito kwa jamii kufanya kazi bila kubagua ili kujikombia kiuchumi kutokana na mkoa wa Kagera kuwa na fursa mbalimbali.
Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog Kagera








Share:

Wananchi Rukwa kushiriki kuchangia Damu kusaidia Majeruhi ajali ya Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa mkoa huo kushiriki katika zoezi la kuchangia damu litakalofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 14 hadi 18.8.2019 katika halmashauri nne za mkoa, ili kusaidia majeruhi walioungua na moto uliosababishwa na kulipuka kwa lori la Mafuta katika ajali iliyotokea eneo la Msavu mkoani Morogoro, na kusababisha vifo vya watu 76 na majeruhi 54.

Mh. Wangabo amesema kuwa zoezi hilo litawajumuisha Waendesha Bodaboda na Bajaji, Madereva wa Magari, Vijana, Watumishi wa Serikali, Wanafunzi, Vyama za Siasa, Madhehebu ya Dini, Viongozi mbalimbali na wale wote wenye mapenzi mema na moyo wa kujitolea kwaajili ya majeruhi hao.

“Nafahamu kuwa mtu yeyote aliyeungua sehemu yoyote ya mwili, miongoni mwa madhara makubwa anayoyapata ni pamoja na kupoteza kiasi kikubwa cha maji mwilini (Dehydration) na kupungukiwa damu mwilini (Anaemia).  Kwa hiyo natoa wito na kuwaomba Wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuchangia Damu kwa ajili ya wenzetu majeruhi wanaoendelea na matibabu.  Damu hiyo pamoja na salamu zetu za pole tutaiwasilisha kwa Dkt. Kebwe Steven Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,” Alisema.

Aidha Mh. Wangabo kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa anaungana na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Viongozi wa Mkoa huo, Familia za Marehemu, Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa kuondokewa na Wapendwa wao.  Na kumuomba Mwenyezi Mungu awape Moyo wa Subira na Uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Mungu awape pumziko la milele waliopoteza uhai na awaponye Majeruhi wote wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.  ‘Bwana Alitoa na Bwana Alitwaa Jina lake lihimidiwe’.” Alimalizia.

Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini.


Share:

Kiongozi Mbio Za Mwenge Agoma Kuzindua Mradi Wa Maji Dodoma.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa  kwa mwaka 2019 Mzee Mkongea Ally amegoma kuzindua mradi wa maji wa Mzase uliopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma  kutokana na kasoro mbalimbali za mradi huo, ikiwamo kukosekana kwa vielelezo vya  majibu ya vipimo vya mabomba kutoka maabara ya serikali.
 
Akizungumza  mara baada ya kukagua miundombinu ya mradi huo Mkongea amesema baada ya ukaguzi wao wameona kuna baadhi ya vitu walivyoomba kwenye mradi huo havipo lakini fedha zinaonyeshwa zilitengwa.
 
“ Tulifanya ukaguzi kwa pamoja tumeona kuna baadhi ya vitu vielelezo vyake havipo kama test za nondo kutoka maabara ya serikali haipo,test za zege haipo,test za bomba kutoka maabara ya serikali hazipo,ubaya wa hapa ni kwamba kazi hazikufanyika lakini kwenye certificate fedha zimelipwa,”amesema Mkongea.
 
Amesema kutokana na kasoro hizo inaonyesha utaratibu ulikiukwa kwa kufanya malipo hewa hivyo Mwenge wa Uhuru 2019 hauwezi kuzindua mradi huo.
 
Kutokana na kasoro hizo amemtaka  mkuu wa Wilaya hiyo Jabir Shekimweri kumpa taarifa za mradi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa(TAKUKURU)wilaya ili ajiridhishe na matumizi ya pesa zilizotumika.
 
“Tunajua mkuu wa wilaya hili sio kosa lako  wala sio kosa la waheshimiwa wabunge,kuna wataalam ambao wanataalum ya injinia kuweza kusimamia miradi hii ndio wanakiuka utaratibu,mh mkuu wa wilaya tunakukabidhi taarifa ya mradi ili umkabidhi afisa Takukuru,kila eneo liangaliwe ili kujiridhisha matumizi ya fedha na baada ya wiki mbili taarifa itumwe makao makuu ya Takukuru,”amesema.
 
Pamoja na kasoro hizo Mkongea amesema wameangalia ubora wa maji kwa mujibu wa vipimo vya maabara na vimeonyesha kwamba maji ni salama kwa matumizi hivyo wananchi waendelee  kuyatumia.
 
Kwa upande wake waziri wanchi ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira George Simbachawene amesema kitendo hicho kimekuwa ni fundisho kwa wao wanaoongoza jamii na kwa wataalam ili wanapoyasikia mapungufu hayo waweze kusema na katika vikao vya halmashauri.
 
Simbachawene ambaye ni mbunge wa Kibakwe ametumia nafasi hiyo kusisitiza wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa kuheshimu sheria iliyopo ya kutofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji.
 
Akizungumza baada ya maelekezo hayo mkuu wa Wilaya Ya Mpwapwa  Jabir  Shekimweri amesema wamepokea taarifa ya ukaguzi na watazingatia maelekezo yaliyotolewa na kuyafanyia kazi.
 
Mradi huo umegharimu kiasi cha sh mil 432.2 ukihusisha baadhi ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa kisima,nyumba ya mashine,ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji,ujenzi wa mlango,ofisi ya jumuiya ya watumiaji maji na njia ya umeme mpaka eneo la kisima.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger