Wednesday, 7 August 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU AMALIZA MGOGORO WA ARDHI KATI YA PORI LA AKIBA LA SELOUS NA KIJIJI ULIODUMU KWA MIAKA 12 MKOANI LINDI

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akionesha eneo la Pori Tengefu akiwa kwenye kigingi ambacho ni mpaka kati ya eneo la Kihurumira ambalo lilikuwa ni eneo la mgogoro kati ya wananchi wa kijiji cha Kikulyungu na Pori la Akiba la Selous ambalo limekuja kubainika kuwa eneo hilo sio ardhi ya Kijiji hicho na wala sio sehemu ya Pori la akiba la Selous bali ni ardhi ya Pori Tengefu amabalo lilikuwa imetengwa kwa  ajili ya kuzaliana kwa wanyamapori wanaotoka katika Pori la Selous katika wilaya Liwale mkoani Lindi. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa na Mbunge wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka wakiwa kwenye eneo la kigingi huku Mbunge huyo akiomuonesha Naibu Waziri Kanyasu eneo la Kihurumira ambalo lilikuwa ni eneo la mgogoro kati ya wananchi wa kijiji cha Kikulyungu na Pori la Akiba la Selous ambalo limekuja kubainika kuwa eneo hilo sio ardhi ya Kijiji hicho na wala sio sehemu ya Pori la akiba la Selous bali ni ardhi ya Pori Tengefu amabalo lilikuwa imetengwa kwa  ajili ya kuzaliana kwa wanyamapori wanaotoka katika Pori la Selous katika wilaya Liwale mkoani Lindi. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka
 .Mbunge wa Liwale, Mhe.Zuberi Kuchauka akizungumza na wananchi wake kuhusu kumalizika kwa mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 12 baada ya Naibu Waziri Kanyasu kuzungumza na wananchi hao
 Baadhi ya wananchi wakiwa wanatoka eneo lenye mgogoro ambapo walitaka eneo hilo la mto waweze kilitumia kwa ajili ya kulishia mifugo pamoja na kulima  katika mto huo ambapo kutokana na hali hiyo mto huo usingeweza kudumu kwa muda mrefu
 Baadhi ya wananchi wakiwa wanatoka eneo lenye mgogoro ambapo walitaka eneo hilo la mto waweze kilitumia kwa ajili ya kulishia mifugo pamoja na kulima  katika mto huo ambapo kutokana na hali hiyo mto huo usingeweza kudumu kwa muda mrefu
 Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock Msocha ( kulia)  akizungumza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati walipotembelea eneo amvalo lilikuwa na mgogoro kati ya Kijiji cha Kikulyungu na Pori la Akiba la Selous
Aniel Heliem mmoia wa wananchi akimuuliza swali Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Cinstantine Kanyasu mata baada ya kuutangaza kuwa eneo la Kihurumila si sehemu ya Pori la Akiba la Selous na wala sio eneo la Kijiji cha Kikulyungu
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametatua mgogoro uliodumu kwa miaka 12  baina ya Pori la Akiba la Selous na Wananchi  wa kijiji cha Kikulyungu  kilichopo katika  wilaya ya  Liwale mkoani Lindi
Mgogoro  huo wa ardhi ulianza mwaka 2007 ambapo wananchi  walianza kudai kuwa eneo la Kihulumira ambalo linapakana na  Pori la Akiba la Selous kuwa  ni moja ya maeneo yao  ya Asili.

Kufuatia hali ilipelekea uhasama mara kwa mara kati ya wananchi na askari wanyamapori hasa pale wananchi walipokuwa wakikamatwa kwa madai kuwa wameingia ndani ya Hifadhi bila kibali.
Akizungumza na wananchi wa wa kijiji cha Kikulyungu mara baada ya kutembelea eneo lililokuwa na mgogoro,  Kanyasu alisema eneo hilo lilisajiriwa  mwaka 1975 na kijiji kilisajiriwa mwaka 2005 hivyo eneo hilo si sehemu ya kijiji.

Amesema baada ya kuundwa timu hiyo iliyokuwa ikiongozwa na wataalamu wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazo  ilibainika kuwa eneo hilo si la wananchi na  wala  sio sehemu ya   Pori la Akiba la Selous bali  ni Pori  Tengefu ambalo ni mali ya serikali Kuu na linasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Katika hatua nyingine, Kanyasu amewataka wananchi   kuacha  vitendo vya kukata miti ovyo na kuchoma misitu kutoka na uharibifu mkubwa wa misitu aliuona karibu na eneo lililokuwa na mgogoro baina ya pande hizo mbili.
 Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu  amewaagiza viongozi wa vijiji hivyo  kuweka sheria kali ili kudhibiti  hali  ya uharibifu  wa misitu unaoendelea katika maeneo hayo.
Akizungumza  kwa niaba ya wanachi wa wilaya ya Liwale Mbunge Liwale,  Zuberi Kuchauka  ameishukuru serikali kwa hatua iliyofikia kwani mgogoro huo ni wa muda mrefu na ulikuwa haujapatiwa ufumbuzi
Amesema mgogoro huo uliwafanya wananchi wa maeneo hayo kupunguza kasi ya kujiletea maendeleo badala yake wajanja wachache walikuwa wakitumia nafasi ya mgogoro kuendelea kujinufaisha.
" Sitegemei mgogoro mwingine wa ardhi baada ya kumalizika huu, Nawaomba wananchi sasa tuchape kazi" Alisisitiza Kuchauka.
Kutokana na kumalizika kwa mgogoro huo wananchi wa kijiji hicho wameiomba serikali kulitumia eneo hilo kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ili kuinua kipato katika kijiji hicho.

mwisho
Share:

WAFUGAJI WAANGUA KILIO MBELE YA WAZIRI MPINA BAADA YA KUCHOMEWA NYUMBA NA MAZIZI, WAMLILIA RAIS MAGUFULI KUWASAIDIA CHAKULA NA MAHALI PA KUISHI



 Mfugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Dorcas Buyase akilia kwa uchungu mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Vilima Vitatu walioondolewa na kuchomewa nyumba, mazizi na makambi ya uvuvi na kukosa mahali pa kuishi. Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Vilima Vitatu, Mhe. Belela Erasto na Mbunge wa Babati Vijijini, Mhe. Jituson
 Mfugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Nanu Mandaga akizungumza kwa majonzi mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi
 Wafugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara wakimsilikiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi
Wafugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara wakiwa juu ya miti wakimsilikiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi.
Na Mwandishi Wetu, Babati
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesitisha operesheni ya kuwaondoa na kuwachomea nyumba, mazizi ya mifugo, makambi ya uvuvi Wananchi wa Kijiji cha Vilima vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara na kuunda timu ya wataalamu kutoka Wizara 8 kufuatilia utekelezaji wa operesheni hiyo na kuwasilisha ripoti hiyo serikalini kwa maamuzi zaidi.
Operesheni hiyo iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu  imesababisha wananchi  wengi kukosa mahali pa kuishi  kutokana na nyumba zao kuchomwa moto ambapo sasa wanaishi chini ya miti hali iliyosababisha adha kubwa kwa wanawake wajawazito, watoto na wagonjwa.
Pia mifugo yao kuvamiwa na wanyama wakali na mingine kupotea baada ya mazizi kuchomwa moto, shughuli za uvuvi kusimama baada ya makambi na zana za uvuvi kuteketezwa kwa moto hali ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi na kushindwa kujua la kufanya.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika  Kijiji cha Vilimavitatu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu huku idadi kubwa ya wananchi wakiangua vilio mbele ya Waziri Mpina wakionesha masikitiko yao kuhusiana na unyama waliofanyiwa na Serikali ya wilaya hiyo na kumuomba kuwasaidia ili waweze kurudi katika maisha yao ya awali.
Walisema mbali na madhara hayo pia akiba ya chakula walichokuwa nacho majumbani mwao nacho kimechomwa moto hivyo kukosa kabisa chakula na kumuomba afikishe kilio hicho kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli ili wapatiwe msaada wa haraka chakula ili kunusuru wasife kwa njaa katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
Waziri Mpina alihoji iweje operesheni hiyo ifanyike huku kukiwa na katazo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la Januari 15 mwaka huu la kusitisha operesheni zote za kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Waziri Mpina pia ahoji iweje operesheni hiyo ifanyike kwenye eneo hilo huku kukiwa na Hukumu ya Mahakama iliyoliondoa eneo la Kijiji  cha Vilima Vitatu kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyapori Burunge (Juhibu) ambapo hukumu hiyo haikukatiwa rufaa wala kutenguliwa na Mahakama.
Pia Waziri Mpina alihoji iweje operesheni hiyo ya kuondoa mifugo  ifanyike bila kushirikisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama Sheria, Kanuni na miongozo inavyoelekeza hali iliyosababisha mifugo mingi kuteseka kwa kukosa huduma muhimu zikiwemo chanjo, dawa, maji na malisho na kusababisha mifugo kupotea na mingine kufa na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji taifa.
Kwa msingi huo, Waziri Mpina alisema operesheni imefanyika kinyume cha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya mwaka 2008, Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za chakula cha Mifugo namba 13 ya mwaka 2010 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003.
Hivyo alisema wote waliohusika kufanya operesheni hiyo walipaswa kukamatwa na kushtakiwa kutokana na makosa ya kuvunja sheria hizo za mifugo kwani wanalo jukumu la kuzisimamia ili zisivunjwe kwakuwa  mifugo ni rasilimali muhimu kwa Taifa kama zilivyo rasilimali nyingine nchini.
Waziri Mpina alieleza kasoro nyingine za operesheni hiyo kuwa pamoja na  kutokufanya tathmini ya kina ya idadi ya wananchi, kaya, mifugo na mali zingine kabla ya operesheni kufanyika, kukosekana kwa nyaraka muhimu za kuendesha operesheni na mahusiano dhaifu baina ya wafugaji, JUHIBU na Mwekezaji Kampuni ya Chemchem Lorge ya nchini Ufaransa.
Pia Waziri Mpina alisema kasoro nyingine ni kutokamilika kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwani kama ungekamilika ungekuwa ndio muarobaini wa migogoro katika Kijiji cha Vilima Vitatu na vijiji vingine 9 vinavyounda Hifadhi ya Wanyamapori Burunge.
Pia Waziri Mpina aliwaonya viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania kutojihusisha na vitendo kuhamasisha uvunjifu wa sheria za nchi na kama kuna masuala muhimu yanayowahusu wafugaji wafuate njia  sahihi za kukutana na mamlaka husika  kutafuta suluhu, Pia amewataka wafugaji kote nchini kufuata Sheria.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati Vijijini, Filbert  Mdachi alisema CCM imesikia malalamiko ya wananchi wa kuwahakikishia kuwa haki itatendeka na kumshukuru Waziri Mpina kwa kufika eneo hilo ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo ulisababisha adha kubwa kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Kitundu alisema alisema operesheni hiyo ilifanyika baada ya kudaiwa kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo hayo na kukiri kupokea maelekezo kutoka mkoani .
Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano 07 August

























Share:

Tuesday, 6 August 2019

Ndege Yaanguka Rufiji na Kuteketea Kwa Moto

Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Rufiji, Onesmo Lyanga amethibitisha kutokea kwa ajali ya ndege ndogo ya shirika la Tropical, iliyokuwa ikiruka kutoka katika kiwanja cha ndege cha Mafia kuelekea Dar es Salaam.

Kamanda Lyanga amesema ajali hiyo imetokea leo Agosti 6 majira ya saa 4:00 asubuhi, baada kuanguka na kuteketea kwa moto na ilikuwa na abiria  takribani tisa.

”Ndege iyopata ajali ilikuwa inaruka uwanja wa Mafia kwenda uwanja wa Julius Nyerere Dar es salaam, ilikuwa na watu 9 lakini mpaka sasa hivi hakuna aliyefariki na kuna majeruhi 6 na ndege yote imeteketea."-Amesema

Aidha, kamanda amesema kuwa majeruhi wote 6 wamekimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi na kwamba Jeshi la polisi Mkoani humo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.


Share:

Dr. Gwajima Atumia “ Video Conference ” Kutoa Maagizo Kwa Wajumbe 234 Wa Timu Za Uendeshaji Huduma Za Afya Mikoa

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima atumia mfumo wa uendeshaji wa vikao vya kazi kwa njia ya kielektroniki “video conferencing” kufanya mkutano na Wajumbe 234 wa Timu za Uendeshaji Huduma za Afya Mikoa, Wakurugenzi na Walezi wa Mikoa kutoka OR-TAMISEMI.
 
Mkutano huu ambao umefanyika kwa teknolojia hiyo ni wa mara ya kwanza na unalenga kupunguza gharama za safari kwa ajili ya vikao ambavyo, ajenda zake zinaweza kujadiliwa kwa njia ya kielektroniki na hivyo kuboresha ufanisi katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
 
Akiongea kwa njia ya Video Conference kutokea Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa kwenye ziara ya kikazi, Dkt. Dorothy Gwajima amesema, kuanzia sasa atakuwa akitumia njia ya kielektroniki “Video Conference” kwa ajili ya kuwakutanisha wadau wote wa sekta ya afya kujadili masuala yanayowahusu pia kutoa maelekezo na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu.
 
Dkt. Gwajima amefafanua kuwa iwapo angefanya kikao cha siku moja cha wadau  hao wa afya , posho peke yake bila gharama za safari na ukumbi kwa siku moja  ingegharimu takribani Tsh. milioni 30 na ukijumlisha na siku 2 za safari kuja Dodoma ingeweza fikia siyo chini ya Tsh. Milioni 100 au zaidi.
 
Anaendelea kufafanua kuwa, mfumo wa uendeshaji vikao kwa njia ya kieletroniki (video conference) utasaidia kudhibiti matumizi ya fedha nyingi zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa vikao hivyo na kuwezesha kusaidia kutoa maagizo ambayo yatasaidia kufanya maboresho ya haraka na kuleta tija katika Sekta ya Afya nchini.
 
Amesema kuwa, kufanya vikao kwa kutumia mfumo huo kutasaidia kutatua changamoto zilizopo katika Mikoa na Halmashauri kwa kutoa ushauri wa haraka na kupokea taarifa za utekelezaji kwa ufanisi na kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na gharama za safari kwa ajili ya kufanya vikao.
 
Wakati huohuo Dkt. Dorothy Gwajima amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya na Timu za Uendeshaji Huduma za Afya nchini kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina ili, kubaini changamoto wanazozisema kwa takwimu siyo kwa maneno tu ya jumla ambayo yanayoficha uhalisia wa changamoto husika.
 
“Kabla hatujasema upungufu wa watumishi tufanye mahesabu ya uwiano wa uwingi wa kazi kwa kila mtumishi kwa kutumia fomula ya WISN ambayo, tumefundishwa wote. Vinginevyo ukisubiri hadi Wizara ije ifanye basi hapo ni kwamba, RHMT/CHMT mtakuwa mmeshindwa kutekeleza wajibu wenu na badala yake mmegeuka chanzo cha changamoto” Amefafanua Dkt. Gwajima.
 
Dkt Gwajima amaesisitiza kufanya hesabu sahihi ili kuweza kuwapata baadhi ya wataalamu na kuwahamisha waende kwenye upungufu mkubwa zaidi wakati, zoezi la ajira likiendelea.
 
Vilevile, Dkt. Gwajima amewataka wajumbe hao kuhakikisha kabla ya kuandika changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba, ni vyema wakahakiki maeneo yenye akiba ya vifaa ambavyo havitumiki ili vipelekwe maeneo yenye uhitaji mkubwa badala ya kila mara tunawaza kununua hivyo kusababisha baadhi ya vifaa kuharibika au kupotea.
 
Aidha amezitaka RHMT kumiliki taarifa wanazotuma Wizarani na kuhakikisha wanazituma kwa wakati kwa kuwa , kila mmoja atatetea taarifa aliyoituma kupitia vikao hivyo na uwajibikaji wake utawekwa wazi ambapo kwa sasa vikao hivyo vitakuwa vitafanyika kila mwezi kwa pamoja na kila wiki kutakuwa na ratiba ya mikoa kadhaa kuhudhuria vikao hivyo na kuwasilisha taarifa za maendeleo ya uwajibikaji.
 
Wakati huohuo Waganga Wakuu wa Mikoa wameupongeza mpango wa kuendesha vikao kwa njia ya Kielektroniki ambao umesaidia kutoa mtazamo mpya wa jinsi ya kukabiliana na changamoto  mbalimbali za Sekta ya Afya nchini.


Share:

Kesi ya Freeman Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Kuendelea kwa Siku 5 Mfululizo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Dar es Salaam, imekwama kuendelea na kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe kwa sababu Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amefiwa na kaka yake.

Kesi hiyo ilitakiwa kuendelea kusikilizwa jana pamoja na kutolewa uamuzi kuhusu mabishano ya kuangalia picha za video zinazodaiwa kuonyesha wafuasi na washtakiwa wakiandamana.

Wakili Peter Kibatala akiwakilisha washtakiwa, alidai kuwa aliandika barua mahakamani akiomba ruhusa kwa washtakiwa wawili, Mbowe na Heche, kwamba wamefiwa na kaka zao kwa nyakati tofauti, hivyo wanaweza kukwama kufika mahakamani.

“Mheshimiwa tuliandika barua tukidhani wote wangeshindwa kufika mahakamani, lakini kwa bahati mheshimiwa Mbowe ameweza kufika isipokuwa Heche ndio wanazika leo (jana), tunaomba kuahirisha kesi hadi tarehe nyingine,” alidai.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akijibu alidai hana neno la kuongeza katika maombi hayo, isipokuwa alipendekeza kesi ipangwe kwa tarehe za karibu ili shahidi wa sita amalize ushahidi wake.

“Mheshimiwa, shahidi tunamshikilia kwa wiki mbili sasa, anatakiwa kwenda Nairobi kwenye mafunzo, wenzake wameshaenda, tunaomba tarehe ya karibu na mfululizo ili amalize aweze kusafiri,” alidai Nchimbi.

Hakimu Simba alikubali kuahirisha kesi hiyo na kuamuru isikilizwe mfululizo kuanzia Agosti 15, 16, 19, 21 na 22.



Share:

WAZIRI MKUU AISHUKURU TIGO KUWA MDHAMINI RASMI WA INTANETI KATIKA MKUTANO WA 39 WA SADC


 Mkuu wa Mauzo – Tigo Business, Kadambara Maita, akimkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika banda la Tigo, lililopo katika mkutano wa 39 wa jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC unaondelea jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere.


Waziri Mkuu aishukuru Tigo kwa kuwa mdhamini rasmi wa intaneti itakayotumiwa na wageni wanaohudhuria mkutano wa 39 wa jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atembelea banda la Tigo na kuwapongeza kwa kuwa wadhamini rasmi wa intaneti itakayotumika kwenye mkutano wa 39 wa jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC ) unaondelea jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere. Tigo ndio kampuni ya mawasiliano pekee yenye mtandao wa kasi wa 4G+.

Wafanyakazi wa Tigo wakimkaribisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh.Kassim Majaliwa, katika banda la Tigo, lililopo katika mkutano wa 39 wa jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC unaondelea jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Share:

Afikishwa Mahakamani Kwa Kumpa Mimba Mwanafunzi wa Sekondari

Mkazi wa Manzese, Dar es Salaam, Amiri Shekhe (25), amepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni  kwa tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu.

Akimsomea mashtaka jana mbele ya Hakimu Anifa Mwingira, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Hilda Kato alidai kuwa Novemba 10, mwaka huu eneo la Mvuleni Manzese wilayani Ubungo, mshatakiwa alimpa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka wa 17.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na Kato alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine.

Hakimu Mwingira alisema dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa kwa kutakiwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 500,000.

Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi Agosti 19, mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kutajwa tena.


Share:

Waziri Mkuu Awataka Watanzania Kuchangamkia fursa za biashara maonesho ya SADC

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wiki ya maonesho ya nne ya viwanda ya nchi za SADC ni fursa pekee ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 6, 2019) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara ya kukagua mabanda kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Maonesho hayo ambayo yalifunguliwa jana na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, yanafanyika katika maeneo matatu ambayo ni ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, viwanja wa Gymkhana na viwanja vya Karimjee.

“Nimekuja kufanya ufuatiliaji wa maandalizi ya mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC, nimekuta yanaendelea vizuri. Nimekuja kuangalia mwitikio wa wajasiriamali wa pande zote mbili za Muungano pamoja na wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa SADC, na pia mwitikio wa wananchi wetu ukoje,” amesema.

Waziri Mkuu amesema fursa hiyo ni muhimu kwa Watanzania kuonesha bidhaa za ndani ili wageni wanaokuja wajue kuna bidhaa zipi zinazozalishwa nchini. “Tumetoa fursa kwa nchi za SADC zote nao pia waoneshe bidhaa zao. Maonesho haya ni ya wazi, Watanzania wanayo nafasi ya kuja kuona na kujifunza,” amesema.

Amesema mbali ya fursa ya masoko, Tanzania inayo pia fursa ya kupata teknolojia mpya na za Kisasa ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa viwanda vya usindikaji bidhaa mbalimbali. “Tumeona utaalamu unaotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, hii maana yake ni kwamba tunajifunza na teknolojia zinazotumika,” amesema.

“Tunayo fursa ya kukaribisha viwanda kutoka nje ya nchi, wote hapa wameleta bidhaa zao. Pia tunawakaribisha waje waanzishe viwanda kwa ubia na Watanzania. Sisi tunayo ardhi, tunazalisha mazao mengi tu, kwa hiyo mbia wa nje anaweza kuunganisha mtaji na Mtanzania na wakajenga kiwanda hapa nchini,” amesema

Mbali ya fursa za kiuchumi kwao binafsi, Waziri Mkuu amewataka washiriki wa maonesho hayo, watangaze vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambavyo vitasaidia kuwafanya wageni wanaoshiriki mkutano huo watamani kubaki nchini na kuvitembelea.

“Watanzania tutumie nafasi hii kutangaza vivutio vingine tulivyonavyo. Mbuga za wanyama tunazo nyingi, tunao Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika na huwezi kuupanda kutokea popote. Ili uupande, ni lazima uje Tanzania,” amesema.

“Pia tuna eneo maarufu la Olduvai Gorge ambalo ni chimbuko la binadamu wa kwanza duniani, na hili liko eneo liko Ngorongoro. Tuna fukwe nzuri, zenye mchanga mzuri ambazo ukikaa wala huwezi kuchafuka, zina urefu wa zaidi ya km. 1,400 kutokea Tanga hadi Mtwara,” ameongeza.

Mapema, Waziri Mkuu alifanya kikao na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Utumishi na Utawala Bora, Viwanda na Biashara wa SMT, Viwanda, Biashara, Wazee na wa Zanzibar (SMZ), Naibu Mawaziri wa TAMISEMI, Mambo ya Nje na Mifugo na Uvuvina kuwapa maelekezo ya kuboresha maandalizi hayo. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,       


Share:

Nchi za SADC Zatakiwa Kuimarisha Nguvu Ya Pamoja Ya Miundombinu Kukuza Viwanda

Na Mwandishi Wetu-MAELEZO
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuimarisha miundombinu ya Reli, Barabara, Bandari pamoja na Mawasiliano ili kukuza sekta ya viwanda katika Mataifa hayo.

Aliyasema hayo leo Jumanne (Agosti 6, 2019) wakati wa mjadala wa wataalamu uliojadili umuhimu  ya sekta ya miundombinu katika  ujenzi wa uchumi wa Viwanda katika Nchi Wananchama wa SADC,  katika Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za SADC yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Kakoko alisema kwa sasa Tanzania imekuwa nchi ya mfano katika nchi za Ukanda huo, kwa kuwa imekuwa kitovu cha usafirishaji wa bidhaa na malighafi mbalimbali katika nchi za SADC, hatua iliyotokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuimarisha Bandari, Reli na mtandao wa barabara.

“Zipo Nchi chache ndani ya SADC ikiwemo Afrika Kusini ambazo tayari zimepata mafanikio makubwa katika miundombinu yake ikiwemo Bandari ya Durban, hivyo mkutano huu unakuwa chachu kwa Mataifa yote kuweza kubaini changamoto zilizopo ili kuhakikisha tunakuwa na mkakati wa pamoja wa kutuvusha hapatulipo” alisema Kakoko.

Aliongeza kuwa ili kufikia mafanikio hayo Serikali za SADC hazina budi kuweka msisitizo katika kuziwezesha sekta binafsi ikiwemo mashirika ya maendeleo ya kimataifa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya miundiombinu pasipo na kuweka masharti magumu kwa serikali, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuleta manufaa kwa wananchi walio wengi.

Kwa mujibu wa Kakoko alisema Serikali kupitia TPA imeanza kuchukua hatua mbalimbali katika kuimarisha kiwango cha ushindani na Bandari nyingine kubwa Barani Afrika na hivyo kuweza kukuza uchumi wa Nchi pamoja na kuwa kichocheo muhimu katika maisha ya wananchi.

Aidha Kakoko alisema miundombinu ya Nchi za SADC kwa sasa si mizuri kwa kuwa zimekuwa zikitumia gharama kubwa za fedha kwa ajili ya kugharamia miundombinu  hivyo ni  wajibu wa Mashirika na Taasisi za umma na binafsi kujitokeza ili kusaidia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu hiyo na hivyo kurahisisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

MWISHO


Share:

UJENZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM WAENDELEA VYEMA

Maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam yanakwenda vizuri ambapo ujenzi wa magati 2 kati ya 7 yaliyopo umekamilika na kuanza kupokea meli kubwa za mizigo.


Akizungumza leo Agosti 6,2019 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema mradi wa ujenzi wa magati hayo utakaogharimu takribani shilingi Trilioni moja utaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuongeza ufanisi kwa kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo na kupokea meli yoyote duniani zikiwemo meli kubwa za kizazi cha saba (7th Generation).

Mhandisi Kakoko amefafanua kuwa kazi inayoendelea imewezesha kukamilika kwa ujenzi katika gati namba 1 na gati namba 2 ambazo zimeongezwa kina kutoka mita 8 hadi kufikia kati ya mita 15 na 19, kina ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na kina kinahitajika kwa meli kubwa zaidi ambacho ni mita 12.

Aidha, Mhandisi Kakoko amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuamua kujenga gati nyingine ya magari iitwayo RORO ambayo itaiwezesha bandari hiyo kupokea meli hata 2 kwa mpigo zenyewe uwezo wa kuchukua magari 10,000 ikilinganishwa na uwezo wa kuchukua magari 200 kabla ya mradi huo.

“Sasa maana yake nini, magari ni kati ya shehena inayoingiza tozo zaidi, kwa magari pekee yake tunaweza kukusanya tozo mara 2 au mara 3 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ndio maana tunamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutuongezea hiyo gati ya RORO.

Kwa hiyo faida ya kwanza tunaipata katika kuongeza kina kwa maana meli kubwa zitaingia kwa mara moja, na kuna watu wamekuwa wakiona kuna Kijiji cha meli zinazosubiri kuingia bandari kushusha mizigo, hiyo haiwezi kuwepo tena” amesema Mhandisi Kakoko.

Mhandisi Kakoko amesema juhudi hizo zinakwenda sambamba na uboreshaji eneo la nyaraka (clearing) kupitia serikali mtandao ili kuondoa mianya ya udanganyifu ambao husababisha upotevu wa mapato.

“Sasa tutaweza kupata moja kwa moja Bill of Lading na hivyo kuondokana na baadhi ya wafanyabiashara au waagizaji mizigo ambao hudai makontena yana mitumba wakati ndani mna magari” amesema Mhandisi Kakoko na kubainisha kuwa uwekaji wa mfumo wa nyaraka unakwenda sambamba na uwekaji wa mitambo ya ukaguzi (scanner).

Amesema baada ya kukamilika kwa gati namba 1 na gati namba 2, ujenzi kwa sasa unaendelea katika gati namba 4 ambayo inakaribia kukabidhiwa TPA na gati namba 5 ambayo uchorongaji unaendelea.

Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati namba 3 na gati namba 4, ujenzi huo utaendelea kwa gati namba 5,6 na 7 na baada ya hapo kazi itaendelea kwa magati ambayo yapo chini ya Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Makontena Bandarini (TICTS) ambayo tayari Serikali ya Awamu ya Tano imeshafanya mazungumzo ya kurekebisha mkataba na sasa mrabaha unaolipwa ni mara 2 ikilinganishwa na zamani.

Mhandisi Kakoko amesema pamoja na kujenga gati hizo, Serikali pia inanunua mitambo mikubwa ya kupakulia na kupakia mizigo na hivyo kuongeza kasi na ufanisi zaidi wa bandari.

Kufuatia juhudi hizo amesema sasa bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kutumia vizuri faida yake ya kijiografia kukabiliana na ushindani wa bandari zote zilizopo katika ukanda wa bandari ya Hindi na kuwa lango bora na muhimu kwa nchi za Afrika.

Mhandisi Kakoko amesema kazi hii ya uboreshaji wa Bandari a Dar es Salaam iliyopaswa kufanyika miaka 30 iliyopita imesababisha Tanzania kupoteza kiasi kikubwa cha mapato na kwamba kutokana na uboreshaji huu na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imechukua, TPA itaendelea kuongoza katika utoaji wa gawio.

Ameahidi kuwa mwaka huu TPA inatarajia kutoa gawio la kati ya shilingi Bilioni 150 na shilingi Bilioni 200 na kwamba miaka michache ijayo TPA kwa kushirikiana na wadau wengine wa bandari watakuwa na uwezo wa kuzalisha fedha za kugharamia bajeti nzima ya Serikali ambayo ni takribani shilingi Trilioni 30 kwa mwaka.

Halikadhalika Mhandisi Kakoko amesema kazi ya ujenzi wa bandari pia inaendelea katika Bandari ya Mtwara na ujenzi katika Bandari ya Tanga utaanza mwezi huu (Agosti 2019)

Mwisho.

Share:

WAKAMATWA KWA KUUZA JUISI YA TENDE YENYE 'NGUVU ZA KIUME AINA YA 4G'

Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA), imewakamata watu wawili kwa tuhuma za kuuza juisi ya tende iliyochanganywa na dawa ya kuongeza nguvu za kiume, kitendo kilichoelezwa kuwa si cha kibinadamu kwani dawa hizo huwa zinatolewa kwa utaratibu maalumu.


Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa ZFDA Nassir Buheti, ambapo ameyataja maeneo ambayo juice hiyo ilikuwa ikiuzwa kuwa ni Fuoni, Kiembesamaki, Mwanakwerekwe na Magari ya Mawe, na kuwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hamid Salum na Hemed Salum, ambao wamekuwa wakiuza juice hiyo kwa watu mbalimbali.

"Walichofanya ni jambo la hatari kwa afya ya binadamu, lengo lao ni kuwavutia watu kuongeza nguvu za kiume, kumbe wanachanganya na dawa hizi wanaziita '4G kifurushi cha wiki', pia hawana kibali kwa upande wa chakula. Na aina ya dawa wanazoziuza zinatakiwa kutolewa kwa cheti maalumu," amesema Buheti.

Kwa upande wa watuhumiwa hao wamekiri kuchanganya juice ya tende na dawa ya kuongeza nguvu za kiume aina ya 4G - Viagra, ambayo walikuwa wakizinunua kwenye maduka ya dawa kwa lengo la kuwavutia wanaume na walikuwa wakisambaza juice hiyo kwa kutumia gari aina ya Spacio.
Share:

Korea Kaskazini yarusha makombora zaidi wakati Korea Kusini ikifanya mazoezi na Marekani

Korea Kaskazini imerusha makombora mawili yasiyojulikana, na kufanya idadi ya makombora yaliyorushwa kufikia manne chini ya kipindi cha wiki mbili.

Kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini, makombora hayo yalirushwa kutoka jimbo la kusini la Hwanghae.

Upande wa Kaskazini umeeleza kukerwa kwake baada ya Marekani kuanza mazoezi ya kivita na Kusini jana Jumatatu.

Kaskazini inasema mazoezi hayo yanaenda kinyume na makubaliano waliyofikia na raisi wa Marekani Donald Trump na wa Korea Kusini Moon Jae-in.

Japo mazoezi hasa ya kivita yataanza Agosti 11, maandalizi ya awali yanaendelea.
 
Marekani imeeleza kuwa inaendelea kupiga jicho juu ya kile kinachoendelea huku ikiwasiliana na Korea Kusini na Japani.
 
Taarifa ya kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini inaeleza kuwa ushirikiano wa kijeshi baina ya Kusini na Marekani unawalazimu kuendelea kufanya ugunduzi na majaribio ya silaha mpya.

"Tunalazimika kuendelea, kujaribu na kutumia makombora mazito ambayo ni muhimu kwa kujilinda," imeeleza taarifa ya Kaskazini.

Taarrifa hiyo pia imeeleza kuwa kinachoendelea baina ya Marekani na Korea ya Kusini ni uvunjwaji wa wazi wa mazungumzo ya hivi karibuni baina ya Marekani na Korea Kaskazini (DPRK).

"Tumeshaonya mara kadhaa kuwa mazoezi ya kivita yatazorotesha mahusiano baina ya Marekani na Korea Kaskazini na mahusiano ya Korea zote mbili kwa ujumla na kutufanya tufikirie kurejea tena hatua zetu za awali," inaeleza taarifa ya Kakazini.

Kwa mujibu wa jeshi la Kusini, makombora yaliyorushwa leo jumanne ni ya masafa mafupi yanayoenda mpaka kilomita 450.

-BBC


Share:

Makubwa Haya : MWANAMICHEZO MWANAUME AKUTWA NA UJAUZITO


Mwanamichezo wa mpira wa kikapu nchini Marekani Donell Cooper
Mwanamichezo wa mpira wa kikapu nchini Marekani Donell Cooper, amezua gumzo ulimwenguni baada ya kupimwa mkojo na kukutwa mjamizito wakati anafanya vipimo vya afya ili kujiunga na timu nchini Bosnia Herzogovina.

Inadaiwa kuwa mchezaji huyo ametumia mkojo wa mpenzi wake ili kukwepa kupimwa kwa sababu alikuwa anatumiwa dawa za kuongeza nguvu.

Kipimo cha kumgundua mtu anayetumia madawa ya kulevya kiitwacho Human Chorionic Gonadotropin (HGO) kimeonyesha kuwa mchezaji huyo ni mjamzito.

Baada ya kugundulika kuwa ametumia mkojo wa mpenzi wake Donell Cooper amesema hata yeye alikuwa hajui kama mpenzi wake ni mjamzito na amefanya hivyo ili kukwepa kugundulika kama anatumia dawa ya kuongeza nguvu.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Monaco na Ohio kwa sasa amefungiwa miaka 2 na chama cha mpira wa kikapu duniani (FIBA) kutojiuhusisha na mchezo huo.
Share:

Marekani yazuia mali zote za Venezuela.

Utawala wa Rais Donald Trump umezuia mali zote za serikali ya Venezuela zilizopo nchini Marekani. 

Amri hiyo inazihusu mali zote za serikali ya Venezuela pamoja na zile zinazoweza kumilikiwa na mtu yoyote aliyeko nchini Marekani. 

Utawala wa Trump pamoja na serikali kadhaa za nchi za Amerika ya Kati zinamtaka Rais Nicolas Maduro ajiuzulu ili kumwezesha kiongozi wa upinzani, Juan Guaido achukue madaraka.

 Amri ya Rais Trump imetolewa kutokana na kuendelea kwa mgogoro wa haki za binadamu nchini Venezuela. 

Watu wa Venezuela zaidi ya milioni 4 wameshaondoka nchini humo kutokana na shida za kiuchumi na uhaba wa chakula. 

Wakati huohuo Rais wa Colombia Ivan Duque ametangaza kuwa nchi yake itawapa uraia watoto 24,000 waliozaliwa na wazazi kutoka Venezuela kuanzia mwezi Agosti mwaka 2015. 

Watu zaidi ya milioni 1.4 kutoka Venezueka walivuka mpaka na kuingia Colombia ili kuepuka athari za mgogoro na uhaba sugu wa mahitaji muhimu.


Share:

NDEGE YAPATA AJALI IKITOKEA MAFIA KWENDA DAR

Ndege Tropical iliyokuwa ikitokea Mafia kuelekea jijini Dar es Salaam imepata ajali leo majira ya saa 5 asubuhi Agosti 6, 2019 na kuungua. Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali wamesema kuwa ajali hiyo imesababishwa baada ya rubani kugonga fensi ya ukuta. Habari kamili zitawafikia punde.

Share:

Serikali Yaandaa Mpango Kazi Kupunguza Matumizi ya Zebaki Nchini

Na Lulu Mussa, Tarime
Serikali imeandaa Mpango-Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao umeainisha fursa mbalimbali zitakazowezesha sekta ya wachimbaji wadogo kuendelea na shughuli za uzalishaji wa dhahabu bila kuathiri sekta ya Mazingira nchini.
 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira katika Wilaya ya Tarime Mkoani Mara hususan maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu.
 
Amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na Upatikanaji wa masoko ya Dhahabu kupitia masoko ya madini ya mikoa yanayojengwa katika mikoa yote nchini; Upatikanaji wa mikopo midogo na ya kati kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu na Kuwezesha vikundi vya kinamama wanaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu kwa kutoa mafunzo kuhusu uchenjuaji salama na rafiki kwa mazingira na mikopo.

Naibu Waziri amesema Ofisi yake inaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu kuhusu madhara ya zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira na kuwataka wachimbaji wadogo kuchenjua dhahabu kupitia vituo mahiri saba (7) vya mafunzo na uchenjuaji wa dhahabu vinavyojengwa katika mikoa ya Simiyu, Mara, Kagera, Katavi, Mbeya, Ruvuma and Tanga na Geita chini ya Wizara ya Madini.

Amesema, Serikali imeona umuhimu wa kuungana na jumuiya ya kimataifa ili kuweza kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo na kuwaelimisha kutumia katika njia salama na rafiki wa mazingira ikiwemo matumizi ya ”gloves” wakati wa ukamatishaji na matumizi ya vigida wakati wa uchomaji wa dhahabu ili kudhibiti athari za mvuke wenye zebaki unaotokana na uchomaji wa dhahabu.
 
Akiwa katika Kata ya Kenyamanyori Mtaa wa Kebaga Naibu Waziri Sima amepata fursa ya kujionea shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kwa kutumia zebaki ambayo imebainika kuwa na athari kwa afya za binadamu na mazingira kwa ujumla.
 
Akizungumza na wakazi wa Mtaa wa Kebaga Naibu Waziri Sima amesema zebaki inasababisha magonjwa ya ngozi, Moyo, Figo na kuharibu mfumo wa neva za fahamu endapo watumiaji hawatazingatia miongozo iliopo.
 
“Sisi kama Serikali lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunawaelimisha wananchi wetu kwa kuwaambia madhara ya matumizi ya zebaki na kuwashawishi kutotumia zebaki kwa shughuli za uchenjuaji dhahabu” Sima alisisitiza.
 
Amesema njia kuu ambazo zinaweza kusababisha binadamu adhurike na Zebaki ni kupitia ngozi hususan wakati wa uchenjuaji wa dhahabu; kuvuta mvuke wa Zebaki; na kunywa maji na kula vyakula vilivyochafuliwa na Zebaki kwa kuwa hudumu katika mazingira kwa muda mrefu. 
 
Zebaki ni metali pekee iliyo katika hali ya kimiminika ambayo hutumika katika sekta ya afya  katika vifaa tiba, tiba ya meno na uhifadhi wa chanjo; uzalishaji viwandani kama vile vipodozi, viutatilifu na bidhaa mbalimbali ikiwemo betri, swichi, taa za umeme; na madini katika uchenjuaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger