Tuesday, 6 August 2019

Korea Kaskazini yarusha makombora zaidi wakati Korea Kusini ikifanya mazoezi na Marekani

...
Korea Kaskazini imerusha makombora mawili yasiyojulikana, na kufanya idadi ya makombora yaliyorushwa kufikia manne chini ya kipindi cha wiki mbili.

Kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini, makombora hayo yalirushwa kutoka jimbo la kusini la Hwanghae.

Upande wa Kaskazini umeeleza kukerwa kwake baada ya Marekani kuanza mazoezi ya kivita na Kusini jana Jumatatu.

Kaskazini inasema mazoezi hayo yanaenda kinyume na makubaliano waliyofikia na raisi wa Marekani Donald Trump na wa Korea Kusini Moon Jae-in.

Japo mazoezi hasa ya kivita yataanza Agosti 11, maandalizi ya awali yanaendelea.
 
Marekani imeeleza kuwa inaendelea kupiga jicho juu ya kile kinachoendelea huku ikiwasiliana na Korea Kusini na Japani.
 
Taarifa ya kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini inaeleza kuwa ushirikiano wa kijeshi baina ya Kusini na Marekani unawalazimu kuendelea kufanya ugunduzi na majaribio ya silaha mpya.

"Tunalazimika kuendelea, kujaribu na kutumia makombora mazito ambayo ni muhimu kwa kujilinda," imeeleza taarifa ya Kaskazini.

Taarrifa hiyo pia imeeleza kuwa kinachoendelea baina ya Marekani na Korea ya Kusini ni uvunjwaji wa wazi wa mazungumzo ya hivi karibuni baina ya Marekani na Korea Kaskazini (DPRK).

"Tumeshaonya mara kadhaa kuwa mazoezi ya kivita yatazorotesha mahusiano baina ya Marekani na Korea Kaskazini na mahusiano ya Korea zote mbili kwa ujumla na kutufanya tufikirie kurejea tena hatua zetu za awali," inaeleza taarifa ya Kakazini.

Kwa mujibu wa jeshi la Kusini, makombora yaliyorushwa leo jumanne ni ya masafa mafupi yanayoenda mpaka kilomita 450.

-BBC


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger