Wanasheria waaswa kutumia taaluma kulinda maslahi waajiri wao
Mkuu wa wilaya ya Nzega Bi. Jackline Liana amewataka Wanasheria
wanapokuwa wakisimamia mashauri mbalimbali kutumia taaluma zao na
kuweka weledi wa kutosha ili kulinda maslahi ya waajiri wao.
Akifungua kikao kazi cha Wanasheria wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kilichofanyika katika ukumbi wa Chama Cha Walimu Nzega tarehe 18
Februari,2016, Bi. Liana aliwaasa Wanasheria kuacha kuuza kesi kwani
alisema kufanya hivyo ni kuwaumiza wananchi.
Bi. Liana aliwataka wanasheria kuwa wazalendo zaidi kwa kujitoa na
kujitolea wakati wanaposimamia mashauri mahakamani pamoja na kusimamia
ipasavyo mikataba na kujiepusha na rushwa.
Aidha, Mkuu wa Wilaya aliwataka wanasheria kujiepusha na migongano ya
kisheria kwakuwa wengi wao ni mawakili wa kujitegemea na kutambua kuwa
wana wajibu mkubwa wa kulinda maslahi ya waajiri wao.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Wanasheria kutoka Halmashauri za
Mji/Wilaya za Urambo,Tabora,Nzega,Uyui,Mkoa wa Tabora, Nzega, Sikonge,
Igunga na Kaliua.