Monday, 1 February 2016

Zari ahofia kuishi Bongo!

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
zariiiMwandani wa Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady.
Stori: MUSA MATEJA, WIKIENDA
Dar es Salaam: Ubuyu! Tumbuatumbua ya majipu ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ inadaiwa kumtisha mwandani wa Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kuja kuishi Bongo ikidaiwa kisa ni utajiri mkubwa alionao wenye shaka juu ya malipo ya ushuru na mapato.
Habari kutoka kwenye chanzo cha ndani cha familia ya Diamond, zimeeleza kuwa Zari alikuwa na mpango wa kuhamishia miradi na makazi yake rasmi Dar mwanzoni mwa mwaka 2016 lakini ndoto hiyo inaonekana kuyeyuka.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, familia ya Diamond imekuwa ikimshinikiza jamaa huyo amshawishi Zari kuwekeza Bongo lakini kwa sasa mpango huo umefutika kwani mwanadada huyo anaogopa kutumbuliwa majipu.
zari1
….Akipozi.
“Unajua Zari anafuatilia kila kitu kinachoendelea nchini. Kwa hiyo usidhani hajui mambo ya TRA (Mamlaka ya Mapato) yalivyochachamaa.
“Unajua anasema akihamia Bongo itabidi aingize nchini yale magari yake ya kifahari anayotembelea akiwa Sauz (Afrika Kusini) au Uganda lakini anahofia tumbua majipu ya Magufuli.
“Wewe fikiria kama lile Range (Rover) la Wema (Sepetu) limekamatwa na TRA, itashindikana nini kukamata Hummer au Lamborghini ya Zari?
“Nafikiri ishu ni utajiri wake. Nilishasoma kwenye vyombo vya habari vya Uganda kuwa utajiri wake wa ghafla umekuwa ukiibua sana maswali na yeye huwa hapendi kuzungumzia vyanzo vya utajiri wake,” kilinyetisha chanzo chetu.
ZARI47817Baada ya kumwagiwa ubuyu huo, mwanahabari wetu alithibitisha kuwa kweli Zari hayupo Bongo yupo Sauz hivyo alimsaka Diamond ambaye alikuwa na haya ya kusema: “Zari ana miradi mingi, muda wa kuwekeza Bongo ukifika atakuja kufanya hivyo.
uhusu mheshimiwa (Magufuli) mimi nampongeza kwa kutumbua majipu kwa sababu tulikuwa tunahitaji kiongozi kama yeye,” alisema Diamond na kuongeza kuwa mpango wa Zari wa kuja kuishi Dar upo palepale.
Share:

Serikali Yakataa Maombi Yote Ya Shule Binafsi Kupandisha Ada Mwaka Huu

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Kamishna wa Elimu nchini amekataa maombi yote ya shule za msingi na sekondari zisizo za Serikali kupandisha ada katika mwaka huu wa masomo na ameagiza shule zilizopandisha ada kinyume cha tamko la Serikali kusitisha ada hizo mpya.

Kutokana na uamuzi huo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeziagiza shule zote za binafsi ambazo zimepandishia ada kiholela bila kupata kibali cha wizara hiyo, kurejesha ada waliyokuwa wanatoza mwaka jana, la sivyo hatua kali zitachukuliwa kwa shule itakayokaidi.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ithibati ya Shule, Hadija Mcheka amesema baada ya tangazo la wizara hiyo kuzitaka shule binafsi zinazotaka kupandisha ada kuwasilisha maombi kwa Kamishna wa Elimu na kutoa sababu za kupandisha ada, ni shule 45 tu zilipeleka maombi ya kupandisha ada wakati shule zingine 900 ziliomba ziendelee kutoza ada ya mwaka jana.

“Hizi shule 45 hazikupata kibali cha kupandisha ada maana sababu walizozitoa hazikumridhisha Kamishna wa Elimu hivyo akaamuru zibakie na ada ya mwaka jana,” alisema Mcheka. 

Tanzania ina jumla ya shule za msingi 14,000 na kati ya hizo shule binafsi ni 1,000.

Kwa upande wa sekondari, shule binafsi ziko zaidi ya 1,400 kati ya sekondari 4,000. Mcheka alifafanua kuwa baadhi ya shule zilitoa sababu kuwa wanapandisha ada kwa sababu wana ujenzi, jambo ambalo kamishna aliona halimhusu mzazi.

“Mwingine anasema anataka kupandisha ada kwa vile anataka kuajiri walimu kutoka nje ya nchi, hili nalo halimhusu mzazi ndio maana tumewanyima kibali cha kupandisha ada,” alieleza.

Pia alisema shule zingine zilinyimwa ruhusa ya kupandisha ada kwa sababu hazikutoa sababu yoyote zaidi ya kueleza kuwa wanataka kupandisha ada kutokana na gharama za uendeshaji.

“Sababu zote hizi hazikumridhisha kamishna ndio maana tumewataka watii agizo la Serikali hadi hapo baadaye.” Alifafanua. 
Mcheka alisema hatua ya kuzitaka shule zote zibaki na ada ya mwaka jana ni kutokana na wizara hiyo kumwajiri mtaalamu mwelekezi anayefanya kazi ya kujua gharama za kumsomesha kila mwanafunzi ili kuisaidia Serikali kuweka ada elekezi.

Alisema ada elekezi hiyo ndio itakayoisaidia wizara kupanga ada elekezi kwa shule binafsi. 

Aliwaonya wamiliki wa shule binafsi ambao wamepuuza agizo hilo kwa kisingizio kuwa hawajapelekewa barua na wizara husika kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria zilizoainishwa wakati shule inaposajiliwa.

Alisema Serikali inafanya kazi kupitia waraka, matamko na maagizo ambayo lazima wahusika wanaohusika kuyatiii na sio kusubiri kuandikiwa barua. 
“Katika hili hatutanii kama zipo shule ambazo hazikutii tamko lile la Serikali na wakapandisha ada naomba wasitishe ada hizo mpya,” alionya.

Mcheka aliwataka wazazi na walezi walioanza kulipa ada hiyo mpya kusitisha malipo hayo mara moja na kwamba wahakikishe kuwa ada yote watakayolipa kwa mwaka huu ifanane na ile iliyolipwa mwaka jana na sio vinginevyo.

“Kama mwaka jana alilipa Sh milioni 1.5 na mwaka huu amepandishiwa hadi Sh milioni 1.8, na kwa kuwa mzazi analipa kwa term (muhula)na tayari ameshalipa term ya kwanza, naomba atakapolipa muhula wa pili alipe pesa pungufu ya kile alicholipa term (muhula) ya kwanza ili zitimie Sh milioni 1.5 na sio Sh milioni 1.8,” alisema Mcheka.

Aliwataka wazazi na walezi kutoa taarifa wizarani na ofisi za elimu za wilaya kwa shule ambazo zitakaidi agizo hilo ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Share:

Mkoa wa Dar es Salaam Kuwa na Wilaya 5

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Rais Dk. John Magufuli ameidhinisha kuwepo kwa wilaya tano katika jiji la Dar es Salaam, badala ya tatu zilizokuwepo awali, ili kuleta maendeleo ya haraka hususan katika elimu.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki, alisema juzi kuwa, waliwasilisha ombi la ugawaji wa wilaya za Kinondoni na Temeke kwa rais, ambapo ameshaliidhinisha.

“Hatua hii ya kuwepo kwa wilaya tano italiwezesha jiji la Dar es Salaam, kupata maendeleo ya haraka kwa kugawanywa kwa wilaya hizo, ambapo kutakuwa na usimamizi thabiti na hakutakuwa na kisingizio cha kuelemewa kwa majukumu kwa watendaji,”alisema.

Aliomba katika ugawaji wa wilaya hizo, rasilimali zilizopo na mipaka igawanywe kwa manufaa ya wananchi wa wilaya hizo. 
Aidha, alisema kinachosubiriwa ni ugawaji wa mipaka na kutangazwa rasmi kuongezeka wilaya mbili ya Kigamboni na Ubungo na kufikisha idadi ya wilaya tano katika jiji la Dar es Salaam.

Akizungumzia ombi la ugawaji wa wilaya za Kinondoni na Temeke, Sadiki alisema hadi kufikia juzi, ombi hilo lilishaidhinishwa na rais, hivyo Kinondoni itakuwa na wilaya mbili za Kinondoni na Ubungo huku wilaya ya Temeke ikiwa na wilaya za Temeke na Kigamboni
Share:

Jaji Mkuu: Maharti ya Dhamana Mahakama za Mwanzo Kupunguzwa

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Jaji mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Othman Chande amesema idara ya mahakama ipo katika mchakato wa kuangalia upya masharti ya dhamana yanayotolewa katika mahakama za mwanzo baada ya kubainika kuwa ni magumu hali inayochangia mlrundikano wa mahabusu katika magereza yote nchini.

Jaji Chande aliyasema hayo jana jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa wiki ya elimu ya sheria nchini katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo alisema sharti la dhamana sio adhabu kwa mtuhumiwa na kusisitiza kuwa tayari mahakimu katika ngazi za Mahakama za Mwanzo, Wilaya na mikoa wameanza kutafuta njia ya kupunguza idadi ya mahabusu.

Aidha katika uzinduzi huo idara ya mahakama imesema inaangalia uwezekano wa kutoa adhabu mbadala kwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha chini ya miaka mitatu ikiwemo vifungo vya nje kwa kufanya kazi za kijamii zinazosimamiwa na idara ya ustawi wa jamii.
Share:

Askofu Mpya KKKT Aonya Utumbuaji MAJIPU.......Amtahadharisha Rais Kutumbua Majipu kwa Haki, Asema Bunge Halipaswi Kulindwa na Jeshi

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
(Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo (kulia) na Askofu Mkuu wa KKKT Mstaafu Alex Malasusa baada ya ibada ya kumuingiza kazini Askofu Shoo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la KKKT mjini Moshi Januari 31, 2016. )
***

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo ameitahadharisha Serikali kuhusu zoezi la Utumbuaji Majipu linaloendelea akiitaka kuzingatia misingi ya haki na busara ya Ki-mungu ili kutowapa nafasi watu wasio waaminifu kuitumia vibaya kufanya ukandamizaji.

Askofu Shoo aliyasema hayo jana  mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro, katika ibada maalum ya kuingizwa kazini iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alisema kuwa Kanisa lina imani na Serikali ya Awamu ya Tano na kupongeza juhudi zake katika kupambana na watumishi wa wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali za umma pamoja na mafisadi, lakini zoezi la kutumbua majipu linapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka uonevu.

“Utumbuaji huu ufanyike katika misingi ya haki na kwa busara kwani watu wengine wanaweza kutumia mwanya huu kuonea wenzao wasiokuwa na hatia,” alisema Askofu Shoo.

Katika hatua nyingine, Askofu Shayo alielezwa kusikitishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya wabunge wanapokuwa Bungeni.

“Tunahitaji kuona Bunge linajadili vikao vyake kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia. Kanisa linasikitishwa sana na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyoendelea bungeni. Tunapenda kuona hoja zinajadiliwa kwa ustaarabu,” alieleza.

Kadhalika, Askofu Shayo aliionya matumizi ya jeshi la Polisi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza kuwa Bunge ni sehemu ya Demokrasia na kamwe haipaswi kulindwa na jeshi. Aliongeza kuwa Bunge linapaswa kuendeshwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na uwazi.

Aliihakikishia serikali kuwa Kanisa litaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo ikiwa ni pamoja ikiwemo sekta ya elimu na afya. Aliishauri Serikali kuangalia upya sera ya elimu bure na kuboresha utoaji wa elimu hiyo.

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizishukuru taasisi za dini kwa kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo kupitia sekta mbalimbali na kuzihimiza kuendelea kuwekeza katika maeneo muhimu yakiwemo ya Afya na elimu.

“Napenda kutumia fursa hii kuyashukuru madhehebu ya dini ambayo yamekuwa mstari wa mbele kusaidia Serikali katika kufikisha huduma hizi za afya karibu zaidi na wananch. Wito wangu kwa hili, naombeni mjitahidi kutoa huduma hizi kwa gharama nafuu ili wananchi wengi waweze kuzitumia,” Waziri Mkuu Majaliwa ananukuliwa.

Ibada hiyo maalum ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Share:

Mahakama Yashusha Rungu kwa Majangili,Yawapiga Kifungo cha Miaka 20 na Faini ya Milioni 270

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, imewahukumu mtu na kaka yake, kutumikia kifungu cha miaka 20 kila mmoja na kulipa fidia ya sh. milioni 270, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kukutwa na meno ya tembo, silaha na risasi kinyume cha sheria.

Washitakiwa hao ni Nicodem Mchongareli na Festol Mchongareli, ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 13 ya mwaka jana. 
Wanadaiwa kukutwa na meno ya tembo mawili yenye thamani ya sh. milioni 27, bunduki tatu zikiwemo za aina ya Riffle, risasi 25 na maganda yake 15.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Joyce Minde, baada ya upande wa Jamhuri uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Salim Msemo na ule wa utetezi kufunga ushahidi.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Joyce alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa jamhuri ulileta mashahidi watano na washitakiwa baada ya kuonekana wana kesi ya kujibu walijitetea wenyewe.

“Mahakama imewaona washitakiwa hao wana hatia baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote,” alisema.

Hakimu huyo aliwapa adhabu washitakiwa hao kwa kukutwa na meno ya tembo, kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja na kulipa serikali sh. milioni 270. 
Pia shitaka la pili wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya sh. milioni 333 na makosa mengine kutumilia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya sh. milioni mbili kwa kila shitaka.

Adhabu za vifungo zinakwenda sambamba, hivyo washitakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja
Share:

Jini Mauti-20

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nilisema huku nikilia mno. Hawakuniambia kitu chochote kile zaidi ya kuondoka. Katika kipindi chote hicho sikuwa nikijua kwamba bibi yangu aliniwekea jini mauti mwilini mwangu na kwamba kwa kila mwanaume ambaye ningefanya naye mapenzi ilikuwa ni lazima afariki dunia. Endelea….
Siku iliyofuata, nilikwenda shuleni kama kawaida, nilipofika, nikaanza kusikia vilio kutoka kwa wanafunzi mbalimbali, moyoni niliumia mno, nilijua fika kwamba kile kilichokuwa kikiwaliza ni kuhusu kifo cha Mudi aliyefariki dunia mbele ya macho yangu.
Nikashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kunibubujika, nilihisi moyo wangu kuwa na maumivu makali mno. Sikuamini kama nilikabidhiwa umalkia ambao ulinifanya kumuua mwanaume yeyote ambaye ningelala naye.
Moyo wangu ukakosa amani kabisa, nilipokuwa nikiwaangalia walimu na wanafunzi waliokuwa wakilia, moyo wangu ulijisikia hukumu sana. Wengi walijua kwamba nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mudi lakini hakukuwa na aliyefahamu kama jana usiku tulikuwa wote hivyo kuona kwamba nisingeweza kugundulika.
Kitu kilichonishangaza ni wanafunzi wengi kuanza kuninyooshea vidole. Kwanza nikashangaa, haikuwa kawaida hata kidogo, kwa nini sasa waninyooshee vidole? Niliwafanya nini mpaka kunifanyia kitu kama hicho, kila nilichojiuliza, nikakosa majibu kabisa.
Sikutaka kujali sana, nikazidi kuendelea mbele mpaka nilipoingia darasani, huko nako kila mwanafunzi aliogopa kunisogelea ni marafiki zangu wawili tu ndiyo walionifuata, alikuwa Anita na Maria.
“Mbona watu wananikimbia na kuninyooshea vidole?” niliwauliza huku nikilia.
“Wanasema wewe ndiye umemuua Mudi,” alinijibu Anita.
“Mimi nimuue Mudi?”
“Ndiyo! Wanasema haukuanza kuua hapo, hata ulipokuwa na Thomas, ilikuwa hivyohivyo, alikufa kifo kama hiki, tena chumbani kwake,” alisema Maria, maneno yale yakaniongezea uchungu.
“Yaani mimi nimuue Mudi?” niliuliza kwa sauti ya juu na kuanza kulia.
Ndiyo nilimuua lakini sikujua nilimuua vipi. Wanafunzi waliniogopa sana na wengi wakayaamini maneno aliyokuwa akiyapakaza Agape kwamba nilikuwa mchawi. Kuanzia siku hiyo sikuwa na amani na hata nilipotaka kwenda mazishini na wanafunzi wengine, wote wakanitenga.
Niliachwa shuleni nikilia peke yangu, kilio changu kilikuwa ni kumlilia bibi yangu kwa kile alichokuwa amenifanyia. Sikutaka kabisa kuua, watu wote waliokuwa wamefariki dunia walikuwa wale niliowapenda kwa moyo wa dhati.
Hakukuwa na wa kunibembeleza tena, kila mtu alinikimbia na hawakutaka hata kunisogelea. Nilijisikia aibu kubwa, shule ikawa chungu, kuanzia siku hiyo nikajuta kuwa mchawi, sikuwa na uhuru hata kidogo, sikuwa na uhuru wa kuwa na mwanaume yeyote.
Wakati nikikaa hapo darasani huku nikilia tena shule nzima kukiwa hakuna mtu yeyote zaidi ya mlinzi, ghafla nikaanza kusikia kizunguzungu kikali, nikajikaza lakini ikashindikana kabisa, kizunguzungu kile kikanipelekesha mno, nikajaribu kusimama, nikashindwa, nikaangukia viti na hapohapo nikaanza kuona giza, sikujua tena ni kitu gani kiliendelea.
***
Nilikuja kupata fahamu na kujikuta nikiwa kitandani, dripu ilikuwa ikining’inia juu yangu na maji yalikuwa yakiingia taratibu katika mshipa wangu. Macho yangu yalikuwa mazito, kitendo cha kuiona dripu ile tu nikajua kwamba mahali nilipokuwa palikuwa ni hospitalini.
Nikaanza kuangalia huku na kule mle chumbani nilimokuwa peke yangu. Nikaanza kuvuta kumbukumbu ilikuwaje mpaka nikafika hapo pale.
Itaendelea wiki ijayo.
Share:

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-39

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Basi wewe nenda.”
Mlinzi akatoka. Mimi niliogopa kurudi chumbani, nikaenda kukaa sebuleni. Niliogopa kurudi chumbani kwa sababu nilijua mke wangu alikuwa akinisubiri anishambulie kwa maneno na ugomvi wake ungekuwa mkubwa.
Pale sebuleni nilifungua TV, nikawa ninatizama taarifa mbalimbali za nje. Usingizi ulikuwa umeniruka.SASA ENDELEA…
Wakati nimekaa hapo nilisikia sauti ya mke wangu akizungumza kwenye simu chumbani. Sikuweza kujua alikuwa akizungumza na nani.
Alizungumza kwa muda mrefu kisha akatoka akiwa amembeba mwanaye. Kilichonishangaza ni kuwa alikuwa amevaa nguo zake za kutokea kama vile alikuwa anataka kwenda mahali.
Nikatazama saa iliyokuwa ukutani. Ilikuwa ikikaribia kuwa saa kumi na moja na nusu.
Kwa jinsi uso wake ulivyokuwa ameukunja sikuweza kumuuliza kitu.
Aliketi kwenye kochi kisha akaniambia.
“Baba Mkanga mimi naondoka kwenye nyumba hii.”
“Unataka kwenda wapi saa hizi?” nikamuuliza huku macho yangu yakiwa kwenye skriini ya TV.
“Ninakwenda kwetu. Siwezi kuendelea kuishi na wewe. Nakuacha uendelee na mambo yako.”
“Niendelee na mambo yangu yapi mke wangu?”
“Haya matatizo yote yanayotokea hapa nyumbani tangu juzi umeyasababisha wewe…” mke wangu alikuwa akiendelea kusema, nikamkatiza.
“Nimeyasababisha mimi kivipi?”
“Usinifanye mimi ni mjinga mume wangu. Mimi nimeshajua kuwa wale watu wanaokuja ni wenzako kama walivyosema wenyewe, wanatoka kwenu Nzega!”
“Wakitoka kwetu Nzega ndiyo wenzangu. Inawezekana wametumwa tu na maadui zangu waje waniharibie kazi.”
“Jana kuna mmoja alisema wazi kuwa mlikuwa mnafukua makaburi pamoja. Kufukua makaburi maana yake nini?”
“Wewe mwenyewe unaona kuwa hayo maneno hayaeleweki. Mimi waziri mzima nifukue makaburi?” nikajidai kumuuliza.
“Wale ni wachawi na wewe ni mwenzao kama walivyosema wenyewe. Mlikuwa mnafukua makaburi pamoja usiku ukienda huko kwenu.”
Mke wangu aliponiambia hivyo niliona aibu nikaugeuza uso wangu kuelekea kwenye sikriini ya TV.
“Umeahidi kumtoa mtoto wako kama kafara kwa wachawi wenzako, sasa leo unajidai kuwageuka wenzako!” Mke wangu aliendelea kuniambia kwa hasira. Machozi yakaanza tena kumtoka.
“Hayo ni maneno yako wewe, mimi si mchawi. Wale watu wametumwa kuja kunichafua tu kwa sababu zao.”
“Mume wangu wewe ni mchawi, usikatae!” Mke wangu akaniambia kwa mkazo na kwa sauti ya juu.
“Nitakataa, nisikatae kwa nini makatio mimi si mchawi.”
“Kabla ya hawa wachawi kuja hapa nilikwisha kutilia shaka. Kumbuka kuna siku niliamka usiku nikawa nakutafuta nikakukuta uko uchi uani umeufungua ule mkoba wako. Juzi tena huyu msichana wa kazi akaukuta ule mkoba chini ya uvungu wa kitanda. Nikakuuliza huu mkoba ni wa nini ukajidai kuniambia ulipewa na babu yako…”
Hapo nikanyamaza. Kule kunyamaza kwangu kukampa nafasi ya kuendelea kunichamba.
“Mkoba una hirizi, una mkono wa mtoto mchanga umekauka, kama si uchawi ni kitu gani? Basi huyo babu yako pia alikuwa mchawi ndiyo maana alikupa ule mkoba. Usinidanganye mume wangu, wewe ni mchawi. Na sasa mtoto wako anatakiwa na mimi sitakuwa tayari achukuliwe. Nitakuumbua!”
Maneno ya mke wangu yalikuwa yakiniingia akilini na kunichoma moyo. Nilibaki kunyamaza huku nikichezea rimoti ya TV.
Sikujua kama aliona ule mkono wa mtoto mchanga uliokuwa kwenye mkoba wangu. Inaelekea aliuchunguza sana.
Alikuwa na ushahidi wa kutosha wa kunitia katika hatia, ilinipasa ninyamaze tu. Kwanza ule mkono wa mtoto mchanga kama utaonekana na polisi ninaweza kushitakiwa na kupoteza uwaziri wangu pamoja na ubunge. Isitoshe mke wangu alikuwa ameyakariri vyema maelezo ya wale wachawi yanayoashiria kuwa mimi pia ni mchawi.
“Sasa mimi naondoka na mwanangu. Siwezi kuendelea kuishi na wewe. Mwanangu atachukuliwa, mtoto mwenyewe ameshalegea, sijui wameshamchukua kivuli?”
Niliona kunyamaza zaidi kutampa nguvu mke wangu na kuendelea kuamini moja kwa moja kuwa mimi ni mchawi. Nikamwambia.
“Unanituhumu bure tu, mimi si mchawi na wala sijapanga kumtoa mtoto wangu kwa wachawi. Usidhani mimi sina akili nizae mtoto kisha niwape wachawi wamle!”
“Uliwaahidi, hivi sasa umewageuka wenzako ndiyo maana wanakufuata nyumbani,” mke wangu alisisitiza.
Nikanyamaza tena kwa sababu alichosema kilikuwa ni cha ukweli na ukweli ukidhihiri, uongo hujitenga.
“Leo atachukuliwa mtoto na kesho nitachukuliwa mimi, bora nijiepushe mapema. Naenda kwetu.”
Akilini mwangu nilikuwa ninawaza jinsi ya kuepukana na aibu ile.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.
Share:

Baba P… Baba Pili… Baba Pilima!-16

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Mimi sijui,” alijibu baba Pilima. Alishaanza kuwa na wasiwasi sasa. Akashika simu na kuandika namba ya rafiki yake Juma wa Mbezi-Beach ili amuulize kisa cha kutoa namba yake kwamba anawajua wateja wa mbao wakati anajua yeye si mfanyabiashara.
JIACHIE MWENYEWE SASA…
Baba Pilima mwenyewe alitaka kumzuia, lakini moyoni akasema aache tu, atapambana mpaka mwisho na vile mkewe yuko njiani, mshindi atakuwa yeye tu…
“Haloo Juma…” alianza kwa kuita baba Pilima feki…
“Haloo, niambie…”
“Eti unamfahamu jamaa anaitwa…”
Kabla hajamaliza kusema, simu yake ilikatika kwa sababu ya mtandao, akapiga tena.
Simu iliita sana, lakini haikupokelewa upande wa pili.
Simu ya baba Pilima mwenyewe ikaita, mkewe alishafika…
“Nipo hapa nje ya Baa ya Sewa…”
“Ingia ndani sasa.”
“Poa.”
Mama Pilima alizama ndani na kushtuka kumwona baba Pilima mumewe akiwa amekaa na baba Pilima feki…
“Ha!” alihamaki mama Pilima, akaanguka tena.
Baba Pilima feki alishtuka sana. Alishtuka kwa mambo mawili. Kwanza kwa kumwona mama Pilima, pili kwa kuanguka…
“He! Huyu mwanamke namfahamu, ni mwanamke wangu, sasa sijui imekuwaje tena na sijui amekuja kufuata nini hapa?” alihoji baba Pilima feki huku akimtumbulia macho mama Pilima pale chini…
“Wewe ni mwanamke wako, mimi ni mke wangu,” alisema baba Pilima mwenyewe. Baba Pilima feki naye akaanza kuweweseka huku jasho jembamba likimtoka…
“Ina…ina…ina maana…ina maana,” alisema baba Pilima feki ambaye kwenye simu ya mama Pilima aliseviwa kwa jina la Baba P…
“Usisumbuke sana ndugu, kaja hapa kwa sababu yangu na mimi nimekutafuta wewe kwa sababu ya yeye. Wewe ndiye Baba P, unatembea na mke wangu huku ukijua ana mume…muda si mrefu nimetoka kwa Baba Pili…nadhani ni mapacha maana hata sura zenu zinafanana,” alisema baba Pilima huku akiwa amekasirika sana.
Watu walimzunguka mama Pilima, baba Pilima mwenyewe akiwa anamsaidia mkewe akae kwenye kiti maana safari hii hakupoteza fahamu kama kule DDC-Kariakoo…
“Pole sana jamani…pole,” watu walimpa pole mama Pilima akiwa amekaa kwenye kiti…
“Baba Pilima mume wangu,” aliita mama Pilima kwa sauti ya chini sana ikiashiria kuchoka na mambo yalivyokwenda…
“Nini?” baba Pilima alimjibu hivyo mke wake…
“Nimekukubali mume wangu. Hata kama leo utanipa talaka lakini nitakuheshimu kuliko mwanaume yeyote hapa duniani. Najua kukutana wewe na yule mwanaume Kariakoo ilikuwa mbinu yako, lakini pia kukutana na huyu hapa pia ni mbinu yako japokuwa mimi nimejikuta nikiingia kichwakichwa…
“Sikutaka kukusaliti. Imetokea tu! Lakini si kwamba sikupendi na huenda labda ni kwa sababu ya mambo yetu ya siri nyumbani…nisamehe kwa utangulizi lakini uamuzi ni wako ingawa mimi kama mimi ningependa unisamehe,” alisema mama Pilima huku akiona aibu kwa watu waliokuwa wakimsikiliza.
Baba Pilima alimwangalia mkewe kwa macho ya kumshangaa sana kisha akasema…
“Umemaliza kusema?”
“Nimemaliza baba Pilima mume wangu.”
“Kwa hiyo kama kuna matatizo nyumbani ndiyo ukaamua kutembea na mapacha?”
“Hiyo nayo ni stori ndefu mume wangu, inataka nafasi ya kusimulia kwa mapana,” alisema mama Pilima huku akizidi kuona aibu.
Baba Pilima alisimama, akamuaga baba P kwamba anaondoka huku akisema…
“Mkubwa mimi sifanyi biashara yoyote. Sina mbao wala miti. Ila nilitaka kukuona. Nimejikaza sana katika hii ishu.
Ningekuwa mwanaume mwingine nadhani ningeua mtu au ningeua watu. Lakini mjue kwamba mimi ni binadamu kama binadamu wengine, sijapenda mlichonifanyia. Nasema sijapenda kwa sababu wote mlijua huyu ni mke wa mtu japokuwa hata yeye alitakiwa kujijua kwamba ni mke wa mtu. Naye ana nafasi yake ya lawama.”
Wakati baba Pilima akimalizikia kutoka nje ya baa hiyo, mama Pilima kule ndani aliangua kilio huku naye akisimama…
“Nilishasema mimi sijawahi kusaliti jamani. Sijui shetani gani amenikuta katika kipindi hiki cha kuelekea uzeeni. Kwani kama ningemvumilia mume wangu na udhaifu wake nini kingenipata mama Pilima!”
Watu waliojua kisa hicho walimzomea mama Pilima huku baba P akibaki kushangaa. Simu yake ikaita, alipiga baba Pili…
“Haloo,” alipokea baba P…
“Ndugu yangu yamenikuta mazito,” alisema baba Pili…
“Nadhani hayo yako ni madogo, mimi zaidi…mwenzako si nimefumaniwa na mume wa mama Pilima…” alisema baba P.
yaani we acha tu…haya wewe mwenzangu yamekupata makubwa yapi?” alisema baba P…
“He! Mume wa mama Pilima?”
“Ndiyo…”
“Mbona hata mimi pia imekuwa hivyo…”
“Wewe lini?”
“Muda si mrefu ndugu yangu.”
Simu ya mama Pilima iliita akiwa nje ya baa hiyo, alipoangalia mpigaji ni mume wake…
Je, unajua nini kilitokea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.
Share:

True Memories Of My life – 46

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Wiki iliyopita niliishia nilipokuwa nasema kuwa bunduki sizilaumu kwa uhalifu unaoendelea nchini, maana hazina uwezo wa kujifyatua, bali nalaumu mikono ya vijana wetu inayozigusa bunduki hizo na kufyatua! ninachoiomba serikali ya awamu ya tano ni kufanya kile kila kinachowezekana kutengeneza mazingira ya vijana kufanikiwa, tuendelee kubana matumizi, ufisadi lakini pia tutengeneze njia za kuleta mzunguko wa fedha. SASA ENDELEA…
Watu wa Ruangwa, jimboni kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wapo katika hali mbaya, mvua kubwa imenyesha na mafuriko yametokea, pamoja na nyumba nyingi kubomolewa na nyingine kuezuliwa mapaa! Ni tukio baya ambalo limewafanya watu zaidi ya 500 kukosa makazi. Tukio hili lilitokea takribani wiki mbili zilizopita.
Januari 28, 2016, nipo ofisini kwangu nikimsubiri Mzee Hanga, ambaye ni mmoja wa wanakamati iliyoundwa kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo zitawasaidia watu wa Ruangwa kwenye tatizo lililokuwa limewakuta, mimi pia ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambayo pia yumo Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mama Mtima.
Pamoja na kazi nyingi ofisini kwangu, siku hizi ni lazima nitenge muda kwa ajili ya kuzunguka kwenye ofisi mbalimbali jijini Dar es Salaam kuomba msaada, juzi tu nilikuwa Ofisi za Kampuni ya Bia na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, kote huko kutafuta misaada kwa ajili ya wananchi wa Ruangwa ambao hivi sasa wanateseka.
Namsubiri Mzee Hanga kwa sababu tuna ahadi ya kwenda pamoja ofisi za MMI Steel, watengenezaji wa mabati, misumari, vinywaji vya Sayona, maji ya kunywa na pia wanamiliki Hoteli za Sea Cliff, White Sands na majengo mengi jijini Dar es Salaam.
Tuna ahadi ya kuonana na mmiliki wa kampuni hiyo, Bw. Subash Patel, ambaye kwa miaka mingi nimesikia juu ya utajiri wake lakini hata siku moja sikuwahi kukutana naye ana kwa ana! Ambacho nafahamu kutoka kwa watu wengine kuhusu mtu huyu ni mpole, mkarimu, mwenye kujishusha ambaye hafanani kabisa kama ukikutana naye barabarani na utajiri alionao, nina hamu kubwa ya kukutana na mtu huyo, ahadi yetu ni kukutana naye saa kumi kamili ofisini kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam, mita kama mia mbili hivi kutoka ofisini kwangu.
Saa tisa na nusu napigiwa simu na sekretari wangu ambaye ananitaarifu kuwa Mzee Hanga amekwishafika, nilichokifanya ni kumuomba amlete ofisini kwangu! Mzee huyu ni mcheshi na anapenda utani, alipoingia ofisini kwangu akiwa ameongozana na Subira ambaye ni sekretari wangu, alifanya matani mawili matatu na binti huyo kabla hajaketi na kuanza kuongea.
“Swahiba, nashukuru sana bwana dua zako zimesaidia ule mfupa ulionikwama umeondoka!” ndiyo maneno aliyoanza nayo baada ya kusalimiana.
Mzee Hanga alipatwa na tatizo la kukwamwa na mfupa wa samaki kooni, tatizo ambalo lilimsumbua kwa muda katika hospitali kadhaa, aliponieleza mimi niliongea kwa kujiamini kwamba “Mfupa huo kwa jina la Yesu kesho hautakuwepo!” Ingawa kesho yake ulikuwa bado upo kooni, siku iliyofuata ambayo ndiyo alikuwa ameketi mbele yangu mfupa ulitoka wenyewe.
Tuliongea mengi kuhusu kazi tuliyokuwa tukiifanya ya kukusanya misaada ya kuwasaidia watu wa Ruangwa, saa tisa na dakika arobaini na tano ndipo tuliondoka ofisini kwangu moja kwa moja hadi MMI Steel, ambako tulikaribishwa ofisini kwa Bw. Subash ambaye hakika alitupokea kwa furaha kubwa tofauti kabisa na matajiri wengi niliowahi kukutana nao.
Mambo yote yaliyokuwa yakiongewa kuhusu Subash yalikuwa ni kweli, alikuwa mpole, mcheshi, asiye hata na chembe ya dharau pamoja na utajiri wote aliokuwa nao! Moyoni mwangu nikajisemea “Laiti matajiri wote wangekuwa hivi…” Tuliongea naye juu ya lengo la kumuona, akatuhakikishia kwamba angewasaidia watu wa Ruangwa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. milioni hamsini! Moyoni nikamshukuru Mungu, nilijua angetusaidia lakini sikuwa nimewaza kwamba Mungu angemuongoza atusaidie kiasi kikubwa namna hiyo.
Tulimshukuru kwa moyo wake wa kuwa tayari kutumia utajiri wake na watu ambao hawajabarikiwa kama yeye, kama ilivyo kawaida yangu, kila ninapokutana na tajiri huwa ni lazima nimuulize jinsi ya kuwa kama yeye, siwezi kuondoka bila kujifunza kitu kwa sababu mimi sikukaa sana darasani kujifunza kama ilivyo kwa wasomi wengi.
“Naomba nikuulize swali Subash, unawezaje kuzisimamia mali zote ulizonazo na bado ukaendesha maisha ya furaha?”
“Siku zote namuweka Mungu mbele, yeye ndiye kila kitu katika maisha yangu, naswali asubuhi na jioni nikimuomba anisaidie katika kazi zangu, lakini pia nafanya kazi na watu waaminifu na wenye akili huku nikiwalipa vizuri na kuwafuatilia!”
“Kama ungekuwa unaanzisha kiwanda leo, ungeanza na kutengeneza bidhaa gani?”
“Nitaangalia mahitaji yaliyopo, kisha nitaanza kidogo na baadaye kuendelea kukua, start small, think big and grow rich!” alisema Bw. Subash kwa sauti ya unyenyekevu.
Baada ya hapo tuliongea mambo mengi kuhusu biashara na nchi yetu kwa jumla, nikagundua nilikuwa naongea na Mtanzania anayeipenda nchi yake pamoja na kuwa ana asili ya India, nilishangaa aliponiambia yeye ni mzaliwa wa Chalinze, Kijiji cha Lugoba ambako alisoma mpaka darasa la nne na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete.
Tuliondoka ofisini kwa Subash tukiwa na furaha mno kwamba matatizo ya watu wa Ruangwa hatimaye yalikuwa yanakwenda kutatuliwa kwa misaada tuliyokuwa tukiikusanya, wakati naingia ofisini kwangu kutoka ofisini kwa Subash ilikuwa tayari saa kumi na mbili kasoro, sikuwa tena na nguvu za kufanya kazi, nilishachoka tayari na mambo ambayo nilishayafanya siku nzima.
Hata hivyo, sikuondoka ofisini, nilibaki nikisoma baruapepe na kujibu barua za mashabiki wangu mpaka saa mbili za usiku nilipoondoka kwenda nyumbani kwa mama yangu kabla sijaelekea nyumbani kwangu Kijitonyama, mke wangu alinipokea vizuri nikamweleza habari za siku nzima, alishangaa ukarimu wa Subash Patel, mtazamo wake kuhusu Waasia ukabadilika.
Kwa sababu ya kuchoka sana siku hiyo niliingia kitandani mapema, kabla sijasinzia, majira ya saa nne hivi usiku, simu yangu iliita, nikanyanyuka na kwenda kuiangalia, kwenye kioo nilisoma maandishi “Mrisho” hili ni jina la Meneja Mkuu wa kampuni yetu, moyo ukashtuka sana kwa sababu mimi na Mrisho huwa hatuna tabia ya kupigiana simu na kuelezana mambo ya kipuuzi, ni kazi tu!
“Mungu wangu, sijui kuna nini!” nilisema mke wangu akisikia.
“Nini?”
“Mrisho!” nikajibu, kumbukumbu zikanijia kichwani kwamba Mrisho aliondoka ofisini mapema sana siku hiyo akinitaarifu kuwa kaka yake, Dawood Mrisho alikuwa mgonjwa na alipelekwa Hospitali ya Tumaini kwa matibabu.
“Pokea tu!”
“Lazima kuna tatizo, kaka yake alikuwa mgonjwa, isije kuwa kimetokea kitu kibaya!” nilisema na kuipokea simu hiyo.
Alichonielezea Mrisho kwenye simu ni kwamba hali ya kaka yake ilikuwa imebadilika na kuwa mbaya, hivyo alikuwa akiniulizia kama nilimfahamu daktari yeyote Hospitali ya Muhimbili ili wamhamishe Hospitali ya Tumaini ambako huduma zilikuwa mbaya.
“Nakuja kaka, tukutane Muhimbili Idara ya Wagonjwa wa Dharura!” nilisema.
Nilichokifanya ni kuvaa haraka na kumuaga mke wangu ambaye alitaka kuongozana na mimi lakini nilimkatalia kwa sababu bado alikuwa akiumwa kichwa na pia siku iliyofuata alikuwa na kazi nyingi sana za kufanya ofisini kwake, alichokifanya ni kunisindikiza hadi mlangoni, akanipiga busu la shavuni, nami nikafanya hivyo tukaagana.
Nikaingia kwenye gari na kuwasha, walinzi wakafungua lango na nikatoka kwa kasi na kuendesha hadi Muhimbili ambako nilimkuta Mrisho na kaka yake, Dawood wakiendelea kufanyiwa vipimo, alikuwa kwenye mashine ya oksijeni ambayo alidai ilikuwa haisaidii chochote katika kuhema, pumzi ilikuwa haitoshi!
Daktari aliyekuwa akimtibu alikuwa kijana mdogo, ambaye alikiri kwamba wakati akisoma shule ya msingi alikuwa msomaji sana wa maandishi yangu na alifurahi mno kuniona siku hiyo. Tukampeleka mgonjwa kufanya kipimo cha X-Ray ya kifua na kumrejesha tena wodini, mpaka kila kitu kinakamilika na kupewa dawa kisha kupelekwa Wodi ya Mwaisela kulazwa, ilikuwa ni saa kumi za usiku!
Ndipo nikarejea nyumbani kupumzika, saa kumi na mbili nilikuwa macho tayari kwa kuwapeleka watoto wangu shule, nilitamani kuendelea kulala lakini haikuwezekana, haraka nikakimbia bafuni nikajimwagia maji ili kuondoa usingizi! Saa moja na nusu nilishawafikisha watoto shule na kuelekea ofisini ambako niliendelea na kazi mpaka saa tatu na nusu, Mrisho aliponipigia simu akinitaarifu kuwa, kaka yake Dawood hatimaye alikuwa amefariki dunia.
“Nakuja kaka!” ndiyo maneno pekee niliyosema na kukata simu.
Nikaondoka ofisini na Mhariri Mtendaji, Richard Manyota, Mhariri wa Gazeti la Championi Ijumaa, John Joseph, Mhariri wa Gazeti la Risasi Jumamosi, Erick Evarist na Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Muhimbili ambako nilimkuta Mrisho, tukakumbatiana na wote tukalia kwa uchungu, kifo cha Dawood kilikuwa kimemuumiza kila mmoja wetu kwa namna yake.
Share:

Namna ya kudumisha uhusiano wa mbali (Distance Relationship)

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Why-Long-Distance-Relationships-Are-Usually-DoomedKaribu tena mpenzi msomaji wa XXLove kwa ajili ya mada nyingine murua inayozungumzia ‘Namna ya Kuweza Kudumisha Uhusiano wa Mbali wa Kimapenzi (Distance Relationship)’ kwa wapenzi wanaoishi mbalimbali.
Ni sehemu ndogo sana ya wapenzi wanaoishi mbalimbali ambao hudumu katika uhusiano wao kwa muda mrefu. Hiki kinaonekana kuwa ni kitendawili kigumu sana kwa wapenzi wengi kuvumiliana kwenye uhusiano bila kusalitiana.
Ninapozungumzia umbali namaanisha wilaya na wilaya, wilaya na mkoa au mkoa na mkoa au nchi na nchi au bara na bara.
Ninaamini miongoni mwetu ama tumeshuhudia au kusikia au kuona au kuadithiwa kuwa kuna mwanaume au mwanamke ambaye alikuwa na mpenzi, mara mpenzi wake akapata nafasi ya kwenda kusoma mkoa mwingine au nchi nyingine lakini mwisho wa siku ukasikia wapenzi wale wamemwagana baada ya mmoja kupata mpenzi mwingine huko aliko.
Inawezekana mpenzi wako alihamishwa kikazi nje ya wilaya uliyopo lakini mwisho wa siku ukabaini kuwa mwenzio amepata mtu mwingine na mapenzi kwako yameanza kupungua au yamepungua kama siyo kwisha kabisa.
Najua wengi huwa mnajiuliza ni nini huwa kinachangia? Zifuatazo ni baadhi ya sababu;
UAMINIFU
Kutokuwa na uaminifu miongoni mwenu, kama wapenzi mtakuwa ni waaminifu katika uhusiano wenu basi kila unapoingiwa na pepo wa usaliti unakumbuka uzuri wa mpenzi wako basi unaacha na kujizuia kumshinda pepo huyo.
UZALENDO
Kutokuwa mzalendo kwa mpenzi wako. Jaribu kumpenda kwa kuwa ndiye uliyemchagua kuwa naye, kila siku Tanzania inasema watumishi wake wawe wazalendo, siyo wao tu hata mapenzi yanahitaji uzalendo.
Uzalendo wa kupenda kitu chako, kumpenda mpenzi wako, mkeo, mumeo au mchumba wako. Lazima ujivunie, ujisifie kuwa naye kisha mthamini.
10-naughty-games-for-long-distance-relationshipsSUBIRA
Kutokuwa na subira au uvumilivu. Hili nalo huchangia mapenzi ya mbali kuvunjika. Kama ilivyo subira ya kila mtu kuamini kuwa ipo siku ataondoka kwenye shida na ugumu wa maisha alio nao, basi amini na kuwa na subira au uvumilivu kwa mpenzi wako ili mfikie ndoto zenu.
MAZINGIRA
Jiepushe sana na mazingira ambayo yanaonekana kabisa yanaweza kukusababisha ukaingia kwenye uhusiano usio rasmi tena, pengine kwa mtu ambaye huna ndoto naye.
Tatizo la kujiingiza kwenye uhusiano kwa sababu za kimazingira linaweza kukufanya ukajikuta umezama kwenye huba na mtu ambaye hana mapenzi na wewe na mwisho wa siku ukajikuta unaumia sana.
MAWASILIANO
Kutokuwa na mawasiliano ya mara kwa mara nayo huchangia sana kuvunjika kwa mapenzi ya mbali au kupoteza ladha, lakini kama mtu anakupenda, anakupenda tu, anaweza kukupigia simu na kukutumia SMS kibao lakini akawa bado ni tatizo.
TAMAA
Kama utaishi kwa kutamani vitu usivyokuwa na uwezo navyo ni dhahiri utajikuta unamsaliti mpenzi wako kwa kuwa tu uko mbali na unaona hawezi kukubana wala kukufuatilia. Ingawa ningeshauri ufanye kitu kwa kujiongoza na siyo kwa kuongozwa na tamaa au kwa kuwa mpenzi wako hayuko karibu nawe.
MKUMBO
Acha maisha ya kufuata mkumbo kama mwenzako amefanya kitu f’lani basi eti na wewe unataka ukifanye au ukipate ili uonekane wa kisasa au mjanja.
Kumbuka kuwa mwisho wa siku mtamaliza chuo na mengineyo, kila mtu atasambaa, kama uliharibu kwa mpenzi wako, mwenzio hatokuwepo.
Msomaji tafadhali tuma maoni yako kuhusu mada hii na yatatoka wiki ijayo. Pia usikose ku-like ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na Group la WhatsApp.
Share:

Tofauti ya kuwa na virusi vya Ukimwi na kuwa na Ukimwi

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

HIV-patient
Wasomaji wengi wa safu hii wamekuwa wakiniuliza nini tofauti kati ya kuwa na virusi vya Ukimwi na mtu kuwa na Ukimwi.Ukweli ni kwamba kuna tofauti kati ya mtu mwenye virusi vya Ukimwi na yule ambaye ana Ukimwi, jambo ambalo wengi hawalijui. Mtu anapokuwa ameambukizwa virusi vya Ukimwi haanzi kuugua mara moja na badala yake huweza kuishi na virusi hivyo kwa muda mrefu hata zaidi ya miaka 10 bila kuonesha dalili zozote.
Tofauti yake na mtu mwenye Ukimwi ni kwamba huyu ambaye anatajwa kuwa anao dalili za magonjwa nyemelezi hujitokeza haraka kutokana na kinga yake ya mwili kupungua kupita kiasi kutokana na kuharibiwa na virusi.
Magonjwa ambayo yatajitokeza ni pamoja na kuharisha, kuvimba tezi mbalimbali mwilini mwake hasa shingoni, kukohoa, kutokwa na malengelenge ya neva za ngozi au kupatwa na mkanda wa jeshi au kuwa na utando mweupe mdomoni. Hata hivyo, siyo kila anayeumwa maradhi hayo tuliyoyataja hapo juu ni mwathirika wa Ukimwi, hujulikana kuwa ameathirika baada ya kupimwa na kuthibitishwa kwa vipimo.
MTU ANAAMBUKIZWAJE UKIMWI?
Bahati nzuri wengi siku hizi wanajua jinsi Ukimwi unavyoambikizwa. Kuna njia nyingi za mtu kuweza kuambukizwa Ukimwi lakini hapa kuna nne muhimu. Virusi vya Ukimwi huishi kwenye majimaji kama vile yale yaliyo sehemu za siri za mwanamke, mbegu za kiume, maziwa ya mama, majimaji ya vidonda, usaha, damu na kadhalika. Lakini majimaji haya huhitaji njia ya kupita ili maambukizi yatokee.
Hivyo basi, mtu anaweza kuambukizwa VVU akiguswa na majimaji ya mwenye Ukimwi kupitia kujaamiiana kwa njia ya kawaida na kinyume cha maumbile au kwa njia ya mdomo (oral sex), hasa kama atakuwa amechubuka sehemu za siri. Pili, mama mzazi anaweza kumuambukiza mtoto wake Ukimwi wakati akiwa tumboni, wakati wa kujifungua au akiwa anamnyonyesha.
Tatu, mtu anaweza kuambukizwa Ukimwi kwa kupewa damu iliyo na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na nne kwa kuchangia sindano au nyembe ambazo zimetumika na mtu mwenye maambukizo. Takwimu zilizotolewa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi zinaonesha kuwa maambukizi kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye maambukizi ni asilimia 82.1. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa njia ya kunyonyesha au wakati wa kujifungua ni asilimia 5.9.
Wanaopata maambukizi kutokana na kuongezewa damu yenye virusi vya Ukimwi ni asilimia 0.3 wakati wanaokumbwa na maradhi hayo kwa njia nyingine kama vile kuchangia sindano, nyembe ni asilimia 1.7. na wale ambao wanapata Ukimwi bila kufahamu chanzo ni asilimia 10.
Ni vyema wasomaji wakafahamu njia ambazo haziambukizi kabisa Ukimwi. Mtu hawezi kuambukizwa kwa kuumwa na mbu au kwa kupiga chafya au kukohoa kunakofanywa na mwenye virusi vya Ukimwi. Mtu hapati maradhi hayo kwa kula, kulala kitanda kimoja, kuogelea bwawa moja, kutumia vikombe au sahani moja kwa chakula au kuchangia choo na mtu mwenye virusi vya Ukimwi.
USHAURI
Mtu aliye na Ukimwi inatakiwa apate mahitaji muhimu ya lishe na jamii ifundishwe kuachana na tabia ya kuwanyanyapaa au kudhani kuwa aliye na Ukimwi ni mzinifu au amekosa maadili.
Share:

The angel of darkness – 43

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.
Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.
Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa ameanza kuchanganya bangi na Cocaine kwa lengo la kupunguza msongo wa mawazo, jambo linalosababisha mabadiliko makubwa kwenye tabia yake. Diego naye anaanza kumshawishi wamuibie Msuya na kutoroka. Safari hii anatumia vitisho ambapo Arianna anakosa ujanja zaidi ya kukubaliana naye. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Kesho yake asubuhi, Msuya aliwahi kuondoka kuelekea kwenye shughuli zake kama kawaida. Alipoondoka tu, Arianna naye aliamka na kumfuata Diego, mkononi akiwa na funguo za gari moja la kifahari la Msuya.
Kwenye mkoba wake mdogo, alikuwa amebeba kadi za benki (ATM) karibu tano, zote akiwa tayari anajua namba zake za siri. Akamuamsha Diego na kumpa funguo za gari, wakawadanganya wafanyakazi kwamba wanaenda kliniki kwa sababu Arianna hakuwa anajisikia vizuri. Wakatoka Diego akiwa ndiyo dereva.
Breki ya kwanza ilikuwa ni kwenye benki ya kwanza, Arianna na Diego wakateremka kwenye gari na kwenda mpaka kwenye mashine ya ATM na kutumbukiza kadi ya kwanza. Baada ya kuingiza namba za siri, Arianna alibonyeza kitufe cha ‘kutazama salio’.
Akaunti hiyo moja tu ya Msuya, ilikuwa na jumla ya shilingi milioni 47 za Kitanzania, wote wakashusha pumzi ndefu na kutazamana.
“Tuzitoe hizi kwanza mengine yatafuatia baadaye,” alisema Diego huku akionesha kuwa na papara zisizo za kawaida.
“Lakini si unajua hatuwezi kuzitoa zote mara moja, kwa leo tunaruhusiwa kutoa mpaka shilingi milioni mbili tu, tena kwa awamu, huo ndiyo utaratibu wa kutoa fedha ATM,” alisema Arianna na kuanza kumfafanulia Diego ambaye alikuwa mgeni na matumizi ya mashine za ATM.
“Basi siyo mbaya, leo tutoe hapa kidogo, tuhamie kwenye benki nyingine nako tukatoe kidogo mpaka tuzimalize kisha tutarudi tena kesho mpaka tutoe zote,” alisema Diego, wakakubaliana ambapo walitoa shilingi laki tanotano kwa awamu nne, jumla ikawa shilingi milioni mbili, wakarudi kwenye gari na kuhamia kwenye benki nyingine.
“Hebu angalia salio? Maana nahisi kama nashindwa kuzisoma hizo namba,” alisema Arianna baada ya kuwa wameshaingiza namba za siri kwenye mashine ya ATM. Salio lilisomeka kuwa shilingi milioni mia moja na laki mbili, wote wakapigwa na butwaa tena.
“Mh! Huyu mzee ana pesa nyingi kiasi hiki? Kumbe biashara ya madini inalipa namna hii?” Diego alisema akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona. Kama walivyofanya kwenye ATM ya kwanza, walichukua shilingi milioni mbili na kuhamia kwenye benki nyingine. Mpaka wanakamilisha mizunguko yao, tayari walikuwa na shilingi milioni kumi mfukoni.
“Umeangalia chumbani kwenu kama kuna fedha na madini kama nilivyokwambia?”
“Daah! Nilisahau ujue, turudi nyumbani sasa hivi nikaanze kupekua kabla muda wa Msuya kurudi haujafika,” alisema Arianna, wakaingia kwenye gari na kuziweka vizuri shilingi milioni kumi walizokusanya siku hiyo na kurejea nyumbani.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, Arianna alienda moja kwa moja mpaka chumbani kwao na kuanza kupekua kila sehemu. Kama Diego alivyokuwa amehisi, ndani kulikuwa na shehena ya madini ya Tanzanite iliyokuwa imehifadhiwa kwenye kabati gumu chumbani humo.
“Whaoo! Madini mengi kiasi hiki?” alisema Arianna na kurudisha kila kitu mahali pake harakaharaka, akaendelea kupekua ambapo aligundua fedha nyingine nyingi, zaidi ya shilingi milioni sitini zikiwa kwenye droo ya kitanda. Ndani ya droo hiyo, pia Arianna alikutana na bastola ambayo bila hata kuuliza, alijua ni ya mumewe anayotumia kujilinda.
Hakutaka kupoteza muda, alitoka haraka na kwenda mpaka kwenye chumba cha Diego, akatazama huku na kule na alipohakikisha hakuna aliyekuwa anamuona, aliingia mpaka ndani. Akamueleza Diego kila kitu alichokiona.
“Mungu wangu, kumbe pia ana bastola? Sasa akigundua kwamba tunamfanyia njama si atatuua? Unaaonaje tutoroke leoleo?”
“Mh! Acha papara Diego, yaani wewe ukishaona pesa akili zinahama kabisa,” alisema Arianna, ikabidi Diego atulie.
“Kwanza jana aliniambia kwamba ndani ya siku chache hizi anaweza kusafiri kwenda New York, Marekani kibiashara, huoni huo ndiyo utakuwa muda muafaka wa sisi kuondoka?” alisema Arianna, kauli ambayo Diego alikubaliana nayo.
Baada ya kumaliza kuzungumza na Diego, Arianna alitoka na kurudi chumbani kwake, akajifungia na kuanza kuvuta madawa ya kulevya kama ilivyokuwa kawaida yake. Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa akielea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa, akauchapa usingizi mzito palepale alipokuwa amekaa.
Alikuja kuzinduka baadaye, alipotazama saa yake tayari ilikuwa ni saa kumi na mbili za jioni, harakaharaka akaficha ushahidi wote wa madawa aliyovuta, akapulizia ‘air freshner’ ili kusafisha hewa ya chumbani humo kisha akaenda kuoga na kuanza kujipodoa kama kawaida yake.
Muda mfupi baadaye Msuya alirejea na kumkuta mkewe amejilaza kitandani, akamkumbatia kimahaba na kumbusu bila kujua kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia.
“Mbona leo umetulia sana? Unaumwa?” Msuya alimuuliza mkewe kwani haikuwa kawaida yake kutulia na kuwa mpole kiasi kile. Swali hilo lilimshtua Arianna, ikabidi azuge kwamba hakuwa akijisikia vizuri.
“Asubuhi ilibidi niende kliniki, alinipeleka kaka Diego,” Arianna alijihami kwa kuongea uongo, Msuya akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye lakini akarudia kumsisitiza kwamba muda wowote anapojisikia vibaya, ni bora apige simu ili mumewe ndiyo ampeleke hospitali.
“Sawa nimekuelewa mume wangu, nakupenda sana mwenzio na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele naona hata mwanao naye anazidi kukupenda,” alisema Arianna huku akilishika tumbo lake, Msuya akapiga magoti kwa furaha na kulibusu tumbo la Arianna.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.
Share:

Nelly Muosha Magari wa Posta-24

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale fundi Yassin alipomfahamisha Doreen kwamba kwa siku ile walimaliza kazi ndipo mtoto huyo wa kishua aliwapa pole akaingia ndani alikochukua bahasha ya khaki na kumkabidhi fundi huyo. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na chombezo hili lisiloisha utamu…
Kwa vile alijua ulikuwa ‘mpunga’ wa maana, fundi Yassin alitabasamu na kumshukuru Doreen aliyemwambia asijali, kama ilivyokuwa kwa fundi, Zakayo, Haruni na Nelly nao walitabasamu kwani walijua mifuko yao ingetuna.
Baada ya kuagana na Doreen, fundi na vijana wake waliondoka lakini kabla ya kufika kituo cha daladala alifungua ile bahasha na kukuta ilikuwa na shilingi lakini 250,000.
Alimpatia Haruni shilingi 40,000, Zakayo 40,000 na Nelly shilingi 30,000 kisha vijana hao wakiwa na furaha walielekea kituo cha basi walikopanda gari, wa kwanza kuteremka alikuwa Haruni na walipofika Tegeta Kibaoni Zakayo kabla ya kumuaga fundi Yassin alisema:
“Kaka mkubwa kama nilivyokwambia, usipoufanyia kazi ushauri wangu kesho nikija itakuwa mara yangu ya mwisho kufanya kazi.”
Maneno ya Zakayo yalimwingia barabara fundi Yassin ambaye hakuwa tayari kumpoteza dogo huyo mchapakazi aliyekuwa akiijua kazi yake na wakati mwingine alipokuwa na dharura alikuwa akifanya kazi zake bila tatizo.
“Sawa kaka mkubwa nimekuelewa,” fundi Yassin alimwambia Zakayo bila Nelly kujua kama jambo hilo lilimhusu yeye.
“Kaka mkubwa, kwani Zakayo kakupa ushauri gani ambao anasema usipoufanyia kazi kesho ndiyo itakuwa mara yake ya mwisho kufanya kazi?” Nelly alimwuliza fundi Yassin.
“Ni mambo tu ya kawaida, nitakuambia,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Walipofika Kituo cha Kwa Ndevu, Nelly na fundi Yassin walipanda daladala la kwenda Ubungo ili pale waunganishe la Tandika, kwa kuwa walipandia mwanzo walikaa katika siti moja.
Safari yao ilikuwa nzuri sana kwani haikuwa na foleni hadi Ubungo walikopanda gari la Tandika, njiani walikuwa wakizungumza mambo mchanganyiko yakiwemo ya mademu lakini fundi Yassin hakupenda kumuweka wazi kuhusu jambo alilokuwanalo moyoni.
Walipoteremka Tandika, fundi Yassin alimpeleka sharobaro Nelly kwenye baa moja ambapo alimwambia aagize kinywaji chochote alichohitaji pamoja na chakula.
Nelly aliagiza kilevi alichokuwa akitumia pamoja na chipsi na mishkaki mitatu, fundi Yassin aliangiza soda na kongoro pamoja ndizi mbili wakaanza kujiburudisha.
“Dogo, samahani kuna jambo nataka kuzungumza na wewe lakini lichukulie kawaida kwani ndiyo changamoto za maisha,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Nelly alipoambiwa hivyo, alishtuka na kumwuliza fundi Yassin ni jambo gani hilo ndipo akamwambia anashukuru kwa kuwa pamoja naye kule site kwa siku mbili lakini siku ile ilikuwa ya mwisho kuendelea kufanya kazi kule.
Nelly alipoambiwa hivyo alimwuliza kwa sababu gani ndipo fundi huyo akamwambia kila kitu kuhusu uwezo wake kikazi na jinsi alivyomzoea haraka Doreen na nyumba ya bosi wake jambo ambalo lilikuwa hatari kwake.
“Kama ulivyomsikia Zakayo akisema kama sitaufanyia kazi ushauri wake ataacha kazi, jambo lenyewe ndiyo hili ninalokueleza ndiyo maana nimeona nikwambie ukweli mdogo wangu,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
“Yaani aliyependekeza unifukuze kazi ni Zakayo si ndiyo?” Nelly alimwuliza fundi wake.
“Siyo kapendekeza, tumeona hatari iliyopo mbele yetu kwa bosi, wewe kuwa mpole kama hela za matumizi nitakuwa nakupa wakati ukiangalia nini cha kufanya,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Pamoja na kauli ya fundi Yassin, Nelly alimmaindi sana Zakayo kwani alijua yeye ndiye aliyemchongea na kujisemea moyoni kwamba ‘watu wengine bwana wana roho mbaya, yaani mimi kuzoeana na mtoto wa bosi kuna ubaya gani?’
“Oke bro kwa kuwa umeamua hivyo poa tu!” Nelly alimwambia fundi Yassin.
“Siyo nimeamua, wewe kuwa mpole kama nilivyokwambia wala usimmaindi mtu yeyote,” fundi Yassin alimwambia.
Kufuatia alichoelezwa na fundi wake, Nelly alikosa raha hata bia aliyokuwa akinywa aliiona chungu, akawa anamfikiria Doreen huku akijisemea moyoni kwamba ndiyo atamkosa.
Kwa vile jambo hilo lilimchanganya akasahau kabisa kama alikuwa amepewa simu na binti huyo wa kishua hadi aliposhtuliwa na fundi Yassin aliyemwita.
“Dogo naona uko mbali kabisa,” fundi Yassin alimwuliza.
“Bro we acha tu, unajua tayari nilishaanza kuizoea kazi na kuifurahia sasa umenikatili sana wewe hujui tu!” Nelly alimwambia fundi Yassin huku moyoni akiwa na lake jambo.
“Usiwaze sana mdogo wangu, nitakapoanza kazi site nyingine tutaenda wote,” fundi Yassin alimwambia.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, ushauri nicheki kwa namba hiyo juu.
Share:

Wabogojo atoboa kwa kucheza kwenye maji China

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

wabogoji (2)Athuman Ford ‘Wabogojo.
Na Gabriel Ng’osha
Nani amekwambia Mbongo hawezi kutengeneza fedha nchini China? Sasa sikia hii, Athuman Ford ‘Wabogojo’ au Wabo kwa Macau ni Mbongo mwenye kipaji cha kutumia mwili wake kwa kuukunja atakavyo. Aling’ara kwa mara ya kwanza katika Wimbo wa Kikulacho wa mkali wa Tekeu, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’ miaka ya 2000.
Kwa sasa Wabogojo amelamba shavu la kucheza shoo inayofahamika kwa jina la The House of Dancing Water huko Macau nchini China.
MACAU
Macau ni kisiwa kikongwe chenye ukubwa wa kilomita za mraba 8.5, lugha kubwa inayotumika kisiwani humo ni Kireno huku fedha wanayotumia inafahamika kama Macanese Pataca. Kisiwa hiki ni maarufu kwa kumbi na casino mbalimbali za starehe.
SHOO YA KWENYE MAJI
Hii ni shoo maalum inayochezwa ndani ya maji na inaitwa The House of Dancing Water na inafanyika kwenye Kasino inayofahamika kama City of Dream.
SHOO YA WATU 400
Shoo nzima huhusisha watu 400 katika vitengo tofauti ila wanaokuwa stejini ni watu kati ya 70 hadi 80 na miongoni mwao ni Waafrika 12 ambao ni Watanzania, waliobaki ni kutoka mataifa mengine.
WATANZANIA HAO NI KINA NANI?
Mbali na Wabogojo wengine hawafahamiki sana ambao ni Kevin, Halfan, Mfaume, Hussein, Godfrey, Said, Kimaya, Vuai, Stanley, Stevin na Adam.
SHOO 2 KILA WIKI
Kila wiki hufanyika shoo mbili kwa kiingilio cha Pataca 580 zaidi ya Sh. laki moja na hamsini (150,000) za Kibongo. Viti maalum ni Pataca 1,500 zaidi ya Sh. laki nne (400,000) za Kibongo kwa shoo moja.
MWAKA MMOJA WA MAZOEZI
Katika maandalizi ya shoo hiyo, huchukua mwaka mmoja kukamilika kwa mazoezi yake yaliyokuwa yakifanyika nchini Ubelgiji.
FAMILIA YA WABOGOJO
Wabogojo ana ndugu zake lakini pia ana mtoto mmoja aliyezaa na Mtanzania anayemiliki mashamba, usafiri na vitu vingine ambavyo hakupenda kuviweka wazi.
Pia jamaa hupenda kuwatembelea sana Watanzania waliofungwa katika Magereza ya Macau akiwemo modo maarufu wa Bongo, Jacqueline Patrick aliyefunga huko kwa msala wa kukamatwa na madawa ya kulevya.
Kupitia Wabogojo tunajifunza kuwa inawezekana kutimiza ndoto zako, haijalishi unayoyapitia, haijalishi una kipaji kinachodharauliwa au lah! Amini katika uwezo na kipaji chako.
Share:

magazeti ya leo jumatatu february tarehe 1/2/2016

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Share:

Sunday, 31 January 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI “UVUMI WA AJIRA ZA MADAKTARI JWTZ”

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

jwtz
Hivi karibuni kumekuwa na uvumi unaoeleza kuwa JWTZ limetoa nafasi za kazi kwa vijana wenye fani ya Udaktari na kuwataka vijana hao kuripoti Makao Makuu na vyeti vyao kwaajili ya usaili.
Habari hizo si za kweli,JWTZ kama zilivyo taasisi nyingine za serilikali lina mfumo rasmi wa kutangaza habari zake hivyo jeshi linawaomba wananchi wazipuuzie taarifa hizo.
Aidha JWTZ linawataka wamiliki wa mitandao ya kijamii kutotoa taarifa za jeshi bila kuwasiliana na Makao Makuu ya jeshi kinyume na utaratibu huu,unawasababishia wananchi usumbufu usio wa lazima.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu JWTZ.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger