Dk.Bilal,Waziri Magufuli wanusurika ajali ya chopa
Baadhi ya watu wakiangalia helikopta iliyokuwa
imembeba Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed
Gharib Bilal, muda mfupi baada ya ndege hiyo kuanguka eneo la Uwanja wa
Ndege Terminal One jijini Dar es Salaam jana.Picha: Mpigapicha Wetu
Wengine walionusurika katika ajali ya helikopta hiyo iliyokuwa imebeba watu 11 ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, waandishi wa habari wawili, walinzi wawili na maofisa wengine wa serikali.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Khamis Suleiman,akizungumza na NIPASHE alisema kuwa ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 3:15 asubuhi katika eneo la uwanja wa ndege wa Air Wing unaotumiwa na jeshi.
Suleiman alisema viongozi hao baada ya kupata ajali hiyo walikimbizwa hospitali ambayo hakuitaja jina kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, taarifa ambazo NIPASHE ilizipata zilieleza kuwa viongozi hao baada ya kupata ajali hiyo walipelekwa katika hospitali ya usalama wa Taifa iliyopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Kamanda Suleiman alisema viongozi hao walipata ajali hiyo wakati wanakwenda kukagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko ya mvua zilizonyesha tangu juzi jijini Dar es Salaam.
Alisema helkopita hiyo muda mfupi baada ya kuruka katika uwanja huo wa Air Wing, ilipata hitilafu ikiwa angani na kuanguka.
Aliongeza kuwa hali za viongozi hao zinaendelea vizuri, na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk.Harrison Mwakyembe, alipoulizwa na NIPASHE alisema taarifa za tukio hilo amezipata na kwamba ajali hiyo haijatokea upande wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere (JNIA) kama ambavyo baadhi ya watu wanaeleza.
“Kimsingi taarifa za tukio hili unaweza kuzipata zaidi kutoka kwa watu wa jeshi maana ajali imetokea upande wa air wing,”alisema Dk.Mwakyembe.
Wakati huo huo, Kurugenzi ya Habari ya JWTZ, imesema helikopta hiyo ilipata ajali katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere (JNIA) kwa upande wa Jeshi wakati ilipokuwa katika hatua ya kuanza kuruka.
Katika taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa JWTZ, Kanali Erick Komba imeeleza kuwa mbali na viongozi hao, wengine waliokuwemo ni Dk. Mnzava ambaye ni msaidizi wa Makamu wa Rais, Msaidizi wa Kamanda Kova na waandishi wa habari watatu.
Alisema ujumbe wa Makamu wa Rais ulikuwa katika safari ya kuzungukia maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kufuatia mvua hizo zilizoanza kunyesha kuanzia Aprili 11, mwaka huu.
Komba alisema Makamu wa Rais pamoja na ujumbe wake hawakupata majeraha katika ajali hiyo. Aidha, rubani na wasaidizi wake pia wametoka salama.
Aliongeza kuwa uchunguzi wa ajali hiyo umeanza mara moja kwa ajili ya kubaini chanzo cha ajali hiyo.