Wednesday 16 August 2023

AFYA CHECK , OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA TANGA KUZINDUA KAMBI MAALUMU YA MATIBABU BURE

...


MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mapema leo
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo akizungumza wakati wa mkutano huo

Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo akizungumza




TAASISI ya  Afya Check kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga wanatarajia kuzindua kambi maalum ya kupima afya  bure kwa wananchi wa Jiji la Tanga  kwa siku tano ikiwa ni mpango wa kuihamasisha  jamii kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara ili pale wanapogundulika kuwa na matatizo mbalimbali waweze kupata matibabu ya haraka.


Akizungumza na waandishi wa Habari leo Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema kambi hiyo itafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Augost 21 ambapo wananchi 5000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi katika magonjwa ya Kisukari,  shinikizo la damu, Saratani ya tezi dume,saratani ya mlango wa kizazi.

Waziri Ummy amesema magonjwa yatayopimwa ni yale yanayoambukiza na yasiyoambukizwa na endapo mtu atakutwa na ugonjwa atapatiwa tiba bure na kwa wale ambao watakuwa na magonjwa yatakayohitaji  upasuaji watapatiwa tiba watakapokuja madaktari bingwa huku akiipongeza banki ya CRDB ambao ndio wadhamini wakuu wa kambi hiyo. 

"Takwimu inaonesha wapo watu laki mbili ambao hawajajitambua afya zao katika upimaji wa vvu, tunawashauri na kuwahamasisha watu kupima na kama watu wote ambao wana maambukizi wangekuwa wanafuata masharti ya kumeza dawa tunaweza kuutokomeza kabisa" amesema.

"Niwapongeze sana sana wadau wetu wakubwa CRDB, benki yetu kwa kujitolea na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan,  katika kufadhili huduma zinazowasaidia wananchi" amebainisha.

"Sasa, nitoe wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza, wilaya zote kujitokeza kuja kupima katika viwanja vya shule ya sekondari ya Usagara, lengo ni watu 5000 lakini hata tukipata zaidi itakuwa vizuri" amesisitiza.

Awali akizungumza Mratibu mkuu wa Afya check Isack Maro amesema lengo la kuweka kambi mkoani hapa ni kutaka kuwajengea wananchi tabia ya kupima afya kwa hiyari mara kwa mara na hii ni mara baada ya kumaliza mkoani Dar es salaam ambapo zaidi ya wananchi 9324 walifanyiwa vipimo.

"Kitakwimu watanzania tunatumia gharama kubwa sana kujitibu na mara nyingi ni kwa sababu tumechelewa kugundua tatizo sasa kampeni hizi zilianzishwa kuhakikisha kwamba watanzania  wanajenga tabia ya kuoenda kupima afya zao mara kwa mara na hii inaonyesha kuyokana na matukio tunayoyaona  kutokana na hizi kambi ambazo tumezifanya kwa muda mrefu"

"Kwa  sasa hivi ndio tumetoka kumaliza vipimo kwa wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na wilaya zake zote na tukafanikiwa kuwapatia huduma za afya za bure wananchi takriban 9324 walifanikiwa kupatiwa  huduma zote za kibingwa pamoja na hufuma za kawaida  bila kusahau wakapatiwa dawa na vipimo"
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger