Saturday, 27 May 2023

KLABU ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MSALALA ZARUDISHA SHULE WANAFUNZI WALIOACHA SHULE NA KUKIMBILIA MACHIMBONI.

...


Jackson Malangalila mwezeshaji katoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) akizungumza na Musa Juma mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Shilela
Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Nyikoboko Jackson Amosi ambaye aliacha shule na kurejea tena baada ya kushawishiwa na klabu ya kupinga ukatili akizungumza kwenye mdahalo wa kupinga ukatili uliondaliwa na mtandoa wa jinsia Tanzania (TGNP)
Juma Mohammed kiongozi wa Klabu ya kupinga ukatili Nyikoboko sekondari ambaye pia ni Mwanafunzi wa kidato cha nne akichangia mada kwenye mdahalo wa kupinga ukatili uliandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP)
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Nyikoboko Kurumna Nicholaus ambaye aliacha shule na kwenda Machimboni akungumza kwenye mdahalo wa kupinga ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP)
Joseph Samweli katibu wa kituo cha taarifa na maarifa cha kata ya Shilela akizungumza na wanafunzi katika mdahalo ulioandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP)
Mwezeshaji kutoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Jackson Malangalila akizungumza na wanafunzi wa Shule Msingi Shilela na Sekondari ya Nyikoboko kuhusiana na masuala ya ukatili

Na Salvatory Ntandu - Msalala

Wanafunzi wawili katika Shule ya Sekondari Nyikoboko Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga waliokuwa wamesitisha masomo kwa sababu mbalimbali na kisha kukimbilia Machimboni hatimaye wamerejea shuleni baada ya kupatiwa ushauri juu ya faida za elimu na klabu ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Hayo yamebainishwa jana na Juma Mohamed Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Nyikoboko ambaye ni kiongozi wa Klabu hiyo,wakati akitoa ushuhuda kwenye Mdahalo wa kupinga ukatili wa Kijinsia uliondaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) katika viwanja vya shule ya Msingi Shilela.

Amesema kuwa walifanikiwa kuwarejesha shule kwa kuwashawishi wanafunzi wenzao ambao walikuwa wamesitisha masomo kwa kipindi ncha miezi minne na kukimbilia Machimboni kutokana na elimu waliyoipata kupitia Midahalo mbalimbali iliwawezesha kujitambua na kujua haki zao.

Wanafunzi hao ni pamoja na Jackson Amosi (19) na Kurumna Nicholaus (18) wawili hao wakiwa ni wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Nyikoboko ambao waliacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mwamko mdogo wa elimu wa wazazi ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji.

“Klabu yetu baada ya kuundwa tuliweka maazimio ya kuhakikisha tunawarejesha wanafunzi walioacha shule na kuwenda kwenye shughuli za uchumbaji wa madini ya dhahabu katika mgodi mdogo wa Madini ya dhahabu wa Nyamishiga ,tulizungumza nao na kisha wazazi wao na kisha wakakubali rudisha shule ,”amesema Mohamedi.

Kurumna Nicholaus ambaye aliacha shule na kwenda Machimboni alisema kuwa baada ya wanafunzi wenzake kumfuata na kumweleza faida za elimu alikubali kurejea darasa ili kutimiza ndoto zake za kulitumikia taifa katika kada ya Uhandisi katika sekta ya Madini.

“Wazazi wangu hawana mwamko wa elimu,ukikaa nyumbani utalazimika kuchunga mifugo au kuozeshwa mimi niliona nitoroke nyumbani ili nikatafute maisha kama mchimbaji lakini kwa umri wangu nilishindwa ndio maana walipokuja wenzangu nikubali kurudi shule,”amesema Nicholaus.

Kwa upande wake John Banda Mwalimu wa Malezi katika Shule hiyo ya Sekondari alisema wameanzisha dawati la Malezi,unasihi, ulinzi na usalama kwa wanafunzi,litakalokuwa na dhima ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili ndani ya eneo la shule na kwenye jamii.

Naye Afisa Mtendaji wa kata ya Shilela Mwanaidi Mzee aliwataka wazazi kuwafichua watu wanaofanya ukatili kwa watoto kwenye ngazi za familia ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa sambamba na kuacha tabia ya kutokubaliana watu wanaobainika kuwapa mimba wanafunzi.

Awali akizungumza na wanafunzi hao Jackson Malangalila Mwezeshaji kutoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) amesema midahalo hiyo imeanza kuleta matokeo chanya baada ya makundi mbalimbali kwenye jamii kutambua, athari za ukatili wa kijinsia na kuanza kutafuta suluhisho ya kuzitatua.

“Wanafunzi wamehamasika na kuanzisha klabu za kupinga ukatili,wanatambua haki zao za msingi ikiwemo kupatiwa elimu kutokana uwepo wa mwamko mdogo wa jamii na kutotoa kipaumbe cha elimu kwa wanafunzi wa kiume na kike,”amesema Malangalila.

Amefafanua kuwa mradi huo Ushirikishwaji wa jamii kupitia midahalo ya una lengo la kutokomeza Ukatili wa Kijinsia na mila na desturi hasi kwa kuyahusisha makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuondoa ukatili wa kijinsia kwa wasichana shuleni na kwenye jamii.


“Mradi huu unatekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) na Shirika la Misaada la Korea Kusini (KOICA),”amesema Malangalila.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger