Miradi ya ajira ya muda kwa walengwa wa TASAF ni utaratibu wa utekelezaji miradi ya jamii yenye kutumia nguvu kazi, inayoshirikisha walengwa kufanya kazi na kulipwa ujira.
Miradi hiyo inawezesha jamii kupata rasilmali /miundombinu inayotoa huduma na ujuzi kwa jamii kupitia ushiriki wao katika kutekeleza miradi hiyo.
Washiriki wa kazi zinazotoa ajira ya muda kwa walengwa ni watu wenye uwezo wa kufanya kazi wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 65.
Kila kaya ambayo inashiriki katika ajira za muda kwa walengwa inaandikisha watu wawili, ambapo mtu mmoja kutoka kwenye kaya ndiye atashiriki kazi- kwa wakati mmoja.
Utekelezaji wa miradi ya ajira ya muda huchukua miezi sita ambapo walengwa hufanya kazi kwa siku kumi tu kwa kila mwezi. Kwa siku mlengwa anatakiwa kufanya kazi kwa muda usiozidi masaa manne ili aweze kupata muda wa kufanya shughuli nyingine.
Wazee, watu wenye ulemavu, wakina mama wajawazito na wenye watoto wadogo ambao hawajatimiza miaka miwili hawaruhusiwi kufanya kazi za ajira za muda kwa walengwa.
Wasimamizi wanaopanga kazi za walengwa hawatakiwi kuwapangia kazi watu hao na wanapaswa kutoa taarifa kwa wajumbe wa kamati ya usimamizi wa mradi (CMC) na Waratibu ili majina ya watu hao yaondolewe kwenye orodha ya watu walioandikishwa kufanya kazi za ajira ya muda.
Kaya yenye watu ambao hawaruhusiwi kufanya kazi za ajira ya muda watapokea ruzuku ya msingi.
Uongozi wa TASAF umetoa waraka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Ufuatiliaji kupitia orodha za watu walioandikishwa kufanya kazi kwenye miradi ya ajira za muda na kuwaondoa wale ambao hawaruhusiwi kufanya kazi kwenye miradi hiyo.
Aidha utoaji wa elimu kwa viongozi wa jamii, wasimamizi na walengwa kuhusu taratibu za utekelezaji wa miradi ya ajira za muda kwa kaya za walengwa utaendelea kutolewa katika kipindi chote cha utekelezaji.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Mawasiliano MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII TASAF
0 comments:
Post a Comment