Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amemsimamisha Kazi Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA wilaya Karagwe, Mhandisi Magai Kakuru kwa kushindwa kusimamia miradi ya Maji inayoendelea kutekelezwa Wilayani Karagwe.
Ametoa agizo hilo leo Septemba 11, 2022 wakati alipoambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa kukagua mradi wa maji wa Chanika/Omululama ulipo wilayani humo na kutoridhishwa na hali ya utekelezaji wa mradi huo.
“Mhandisi huyu anajitahidi kufanya kazi lakini haiendani na kasi inayohitajika kwahiyo ataenda kusaidia kwenye kazi nyingi, hapa karagwe nitaleta Meneja Mwingine anayeendana na kasi tunayoitaka” ,amesema Aweso
Waziri Aweso amesema alipokuja wilaya karagwe alitoa maelekezo mahususi kuhusu miradi ya maji, lakini leo baada ya kuona na kupata taarifa amegundua wakandarasi wanachezea fedha za miradi.
Aidha, Aweso ameagiza Mkandarasi ayetekeleza mradi wa maji wa vijijini nane wilayani Karagwe nae aondolewe na mchakato wa kupata Mkandarasi Mwenye Uwezo na atakayetekeleza miradi ya maji ndani ya muda wa mkataba.
Waziri Aweso amesema Serikali hatamvumilia wala kumbembeleza Mhandisi yeyote atakayeshindwa kusimamia miradi ya maji na akawasisitiza kusimamia na kukwamua miradi ya maji, “faraja ya Mhandisi wa Maji ni kuona Wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama”.
Pia, amesisitiza hawezi kukubali kuona Meneja wa Maji wa Mkoa ana zaidi ya shilingi Bilioni 9 kwenye akaunti lakini wananchi wanaendelea kuhangaika na kero ya Maji wakati Rais Samia ameshatoa fedha.
Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Kiu ya Wananchi wa wilaya ya karagwe ni kuona miradi ya maji inakamilika na wanapata maji safi na salama.
0 comments:
Post a Comment