Thursday, 22 September 2022

ELIMU YA URAIA ITOLEWAYO SHULENI INA MCHANGO MDOGO KUSAIDIA VIJANA WA KITANZANIA

...
Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa akiwa na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari akizindua ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchin, hafla hiyo imefanyika leo Septemba 22,2022 Jijini Dar es Salaam. Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa akiwa na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari wakionesha ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchin, hafla hiyo imefanyika leo Septemba 22,2022 Jijini Dar es Salaam.Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchini iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.Kaimu Mkurugenzi Mkuu HakiElimu Bw.Godfrey Bonventure akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchini iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.Mwasilishaji wa Matokeo ya Utafiti, Dkt.Perpetua Kalimasi akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchini iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa elimu nchini wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchini iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchini iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

*******************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na asasi ya HakiElimu mwaka 2022 kwa lengo la kuangalia mchango wa Elimu ya Uraia shule za sekondari katika kumwandaa kijana kujifunza na kushiriki vema michakato ya kidemokrasia nchini umeonesha kuwa Elimu ya Uraia itolewayo shuleni ina mchango kidogo katika kumsaidia kijana wa Kitanzania kujifunza na kushiriki shughuli za kisiasa na demokrasia.

Ameyasema hayo leo Septemba 22,2022 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu HakiElimu Bw.Godfrey Bonventure katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa ‘Elimu ya Uraia’ Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia Nchini.

"Kwa mujibu wa utafiti huu, uliofanyika katika Wilaya za Mkuranga, Tabora, Ukerewe, Kilwa, Sumbawanga and Arusha; unaonesha ushiriki hafifu wa vijana katika mifumo ya kidemokrasia ndani na nje ya shule; unachangiwa na mapungufu yaliyopo katika mtaala wa elimu ya uraia itolewayo shule za sekondari, namna ya ufundishaji pamoja na mifumo ya ukuzaji demokrasia kama vile utawala na uongozi shuleni, namna ya uendeshaji vyumba vya madarasa na mtazamo hasi wa jamii juu ya shughuli za kisiasa na kidemokrasia kwa ujumla". Amesema

Amesem utafiti umebaini kuwepo kwa changamoto kubwa katika mtaala wa somo la uraia shule za sekondari ambao kwa kiwango kikubwa haumpi mafunzo stahiki mwanafunzi yatakayomfanya aelewe vyema na kushiriki shughuli za kidemokrasia katika ngazi mbalimbali kwa nafasi yake.

Aidha amesema kwa upande wa walimu, utafiti umeonesha kuwa sehemu kubwa ya walimu ambao wanafundisha somo la uraia hawana maarifa stahiki yanayowawezesha kuwafundisha na kuwaaandaa vijana kuelewa maana ya siasa safi na umuhimu wa ushiriki wao katika mifumo ya kidemokrasia katika ngazi ya shule, familia na jamii.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa utafiti huo vijana wanatarajia kuwa shule ndio chanzo kikuu cha kujifunza na kujengewa uzoefu katika michakato ya kidemokrasia ukilinganisha na radio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na kujisomea vitabuni.

Hata hivyo amesema pamoja na matarajio makubwa ya kujifunza siasa na demokrasia kupitia elimu ya uraia itolewayo shuleni; matokeo ya utafiti huu yanaonesha bado kuna mapungufu katika utoaji wa Elimu ya Uraia shuleni na ushiriki wa vijana katika michakato ya kidemokrasia.

Amesema katika ngazi ya shule, utafiti unaonesha asilimia 44.4 ya wanafunzi hawaelewi maana ya demokrasia, asilimia 85.5 hawajawahi kushiriki au kushirikishwa katika vikao rasmi vya shule vinavyofanya maamuzi kuhusu mapato na mgawanyo wa rasilimali za shule.

Huku asilimia 68.9 hawajawahi kugombea au kuonesha nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ngazi ya shule, asilimia 44 hawashiriki katika chaguzi za uongozi wa wanafunzi, asilimia 26 hawajawahi kushiriki kabisa midahalo na mijadala ya hoja kama sehemu ya kuwajengea uwezo wa ushawishi na demokrasia.

Amesema Utafiti pia umeonesha kuwa asilimia 47 ya viongozi wa wanafunzi shule za sekondari hawapatikani kwa njia ya chaguzi za kidemokrasia bali kwa kuteuliwa na uongozi wa shule 11% kwa kujitolea na asilimia 42 pekee ndio ambao hupatikana kwa kufanyika uchaguzi ambao wanafunzi wenzao hupata fursa ya kupiga kura na kuchagua.

"Hali hii inaelezwa kuchangia kwa kiasi kukubwa kudumaza ushiriki wa vijana katika shughuli za kidemokrasia katika maisha yao". Amesema

Amesema katika ngazi ya jamii, zaidi ya asilimia 80 ya vijana waliko shuleni hawajawahi na hawahamasishwi kushiriki mikutano ya kampeni na siasa; asilimia 67.8 hawajawahi kuhudhuria mikutano ya Kijiji au mtaa na asilimia 67.5 hawajawahi na hawaoni umuhimu wa wao kushiriki shughuli za kijamii husasani zinazohusu maendeleo ya vijiji au mtaa kwa kujitolea.

"Sehemu kubwa ya jamii bado inashidwa kuoanisha elimu ya uraia na maandalizi ya viongozi na siasa safi za baadae; hali hii imechangia jamii kutoa hamasa kidogo kwa vijana kushiriki katika shughuli za siasa na demokrasia wakiwa bado shuleni". Amesema

Ameeleza kuwa kwa ujumla matokeo ya utafiti huo yanaonesha kutoridhika kwa vijana na namna mfumo wa elimu na jamii unavyowaandaa kuelewa na kushiriki katika mfumo wa siasa na demokrasia.

Amesema kuwepo kwa sheria kama za uchaguzi zinazolazimisha vijana kuanza kupiga kura katika umri wa miaka 18, zinatajwa kuchangia katika kuchelewesha vijana kuanza kushiriki katika masuala ya demokrasia.

Hata hivyo amesema Utafiti unapendekeza mapitio ya mtaala wa elimu ya uraia ili kutilia mkazo maudhui na mbinu za ufundishaji vinavyomwandaa kijana katika mawanda mapana ya ufahamu juu ya maana na umuhimu wa ushiriki wao katika medani za siasa na uga wa demokrasia angali mapema.

Pamoja na hayo amesema Katika ngazi ya familia, wazazi na walezi wanashauriwa kuachana na mfumo wa malezi usiowashirikisha au unao watenga Watoto,katika maamuzi ya kifamilia na maslahi yao.

Kwa upande wake Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema ili kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu shughuli za demokrasia ni vyema Elimu ya uraia ikaanza kutolewa katika ngazi ya awali ili kuwaandaa mapema zaidi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger