Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanikiwa kukamata na kuteketeza shehena ya vipodozi na chakula zaidi ya tani tatu zenye viambata sumu na zilizoisha muda wa matumizi ambazo zilikamatwa kupitia ukaguzi maalumu uliofanyika katika maduka mbalimbali Kanda ya Ziwa.
Akizungumza Ijumaa Septemba 09, 2022 wakati wa zoezi la kuteketeza shehena hiyo lililofanyika katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza, Afisa udhibiti ubora TBS Kanda ya Ziwa Arnold Kubingwa amesema hatua hiyo inalenga kuondoa sokoni bidhaa zote zenye zisizofaa kwa matumizi kwani zina madhara kwa watumiaji.
Kubingwa ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa wanazoziagiza na kuziuza zinakidhi matakwa ya viwango ikiwemo kuangalia tarehe ya uzalishaji na mwisho wa matumizi.
Amesema TBS itaendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua bidhaa zilizopigwa marufuku sokoni na kuwa na utamaduni wa kukagua bidhaa kabla ya matumizi na kwamba wafanyabiashara wanapaswa kuwa waaminifu kwa kuteketeza bidhaa zisizofaa.
“Wafanyabiashara wanapaswa kufuata matakwa ya Sheria katika utunzaji wa bidhaa zinazopaswa kuwa sokoni, uhifadhi wake wake katika maghala na uteketezaji wa bidhaa ambazo hazifai kuwa sokoni, wakishindwa kufanya hivyo tutaendelea kuziondoa na kuchukua hatua dhidi yao” amesema Kubingwa.
Naye Afisa usalama wa chakula TBS Kanda ya Ziwa, Elikaneny Minja amesema bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na ambazo zina viambata sumu ni hatari kwa afya ambapo zinaweza kusababisha maradhi ya ngozi ikiwemo kansa kwa watumiaji na kwamba madhara hayo yanaweza kuhamia kwa watoto walio tumboni ikiwa mtumiaji ni mjamzito.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii kuzitambua bidhaa zilizopigwa marufuku na zenye viambata sumu, pia tumeziweka kwenye tovuti ya TBS ili wananchi wazitambue na kujiepusha na matumizi yake” amesema Minja na kuongeza kuwa TBS inashirikiana na maafisa afya na biashara katika ngazi za Halmashauri ili kufanya ukaguzi na kuondoa sokoni bidhaa zisizofaa.
Nao baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza akiwemo Happyness Enock pamoja na Amos Makinga wameipongeza TBS kwa jitihada za kuondoa sokoni bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata sumu na kuongeza kuwa ni vyema wafanyabishara wanaokamatwa wakiuza bidhaa hizo wakachukuliwa hatua kali za kisheria.
0 comments:
Post a Comment