Tuesday, 13 September 2022

RAIS SAMIA : TUNAWASHUKURU WAKENYA KWA ZAWADI YA AMANI...SASA NI MUDA WA KUIJENGA KENYA

...

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Wakenya kufanya uchaguzi mkuu kwa amani.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 13,2022 wakati William Ruto akiapishwa kuwa Rais wa tano wa Kenya.

“Tunawapongeza sana Ndugu yetu William Ruto na Naibu Rais wake, tunampongeza ndugu zetu Wakenya tunawapongeza kwa ukomavu wa Kidemokrasia .Kama kuna zawadi mmeitoa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni zawadi ya amani wakati wa uchaguzi Mkuu. Tunawashukuru sana kwa zawadi ya amani. Sasa ni muda kujenga Kenya”,amesema Rais Samia.


William Ruto ameapishwa rasmi kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya leo Jumanne Septemba 13,2022 katika uwanja wa Moi Kasarani katika sherehe iliyosimamiwa na msajili Mkuu wa mahakama Anne Amadi mbele ya jaji mkuu Martha Koome.


“Mimi, William Samoei Ruto, kwa kutambua kikamilifu wito wa juu ninaochukua kama Rais wa Jamhuri ya Kenya, naapa kwamba nitakuwa mwaminifu wa kweli kwa Jamhuri ya Kenya", ameapa rais mpya William Ruto akiapishwa na Msajili Mkuu wa Mahakama Anne Amadi, mbele ya Jaji Mkuu Martha Koome.
Mkewe Mama Rachel Ruto alikuwa amesimama kando yake wakati akila kiapo hicho akishuhudiwa na zaidi ya wakuu 20 wa nchi mbalimbali.


Ruto mwenye umri wa miaka 55 amekula kiapo kwa kutumia nakala ya katiba ya Kenya, wiki tano baada ya uchaguzi wa Agosti 9, akichukua hatamu za nchi iliyokumbwa na ukame na mzozo wa gharama ya maisha.


Alitangazwa mshindi mnamo Agosti 15,2022 baada ya kumshinda kiongozi wa Upinzani wa muda mrefu Raila Odinga ambaye baadaye aliomba ushindi huo katika Mahakama ya Juu ambapo kesi hiyo ilitupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger