Moja ya miundombinu ya maji wilayani Kakonko
Madiwani wa Kakonko wakisikiliza kwa makini wakati kikao kikiendelea.
***
Na Daniel Limbe,Kakonko
LICHA ya Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) wilayani Kakonko mkoani kigoma kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa usambazaji wa bora wa maji, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mbizi kata ya Kakonko wameshindwa kutumia huduma hiyo kutokana na imani potofu.
Hayo yamebainishwa kwenye baraza la madiwani wa halmashauri hiyo na Kaimu Meneja wa Ruwasa,Denis Manji,wakati akijibu swali lililoulizwa na diwani wa kata ya Kakonko,Masumbuko Linze,aliyetaka kujua ni lini wananchi wake satanufaika na huduma ya maji safi.
Pamoja na mambo mengine,Manji amesema Kijiji cha Mbizi kimewekewa vituo vitatu vya kutolea maji lakini wananchi wameshindwa kuvitumia badala yake wameendelea kutumia maji ya chemichemi hali iliyosababisha kushusha bei ya maji kutoka shilingi 50 kwa ndoo moja ya lita 20 hadi kufika shilingi 20.
Amesema kuwa wakala hiyo, imefanikiwa kusambaza maji kwa aslimia 87 kwenye wilaya ya Kakonko huku vijiji vinne pekee ndiyo vikiwa vimesalia kupata huduma hiyo.
Amevitaja vijiji hivyo kuwa ni Kabale,Nyamtukuza, Huruhuru pamoja na Nyakiyobe na kwamba ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu mamlaka hiyo itakuwa imeunganisha mtandao wa maji kwa aslimia 91.
Hata hivyo,Manji amewataka Madiwani hao kuwasisitiza wananchi wao kuvuta maji majumbani pamoja na kulipa gharama za utumiaji kwa lengo la kusaidia huduma hiyo kuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Fedelis Ndelego, ameipongeza Ruwasa wilaya ya Kakonko kwa jitihada kubwa za kusambaza maji vijijini na kwamba waendelee kusambaza hadi kwenye vijiji vilivyosalia ili kuvuka malengo waliojipangia.
0 comments:
Post a Comment