Tuesday, 6 July 2021

Serikali Na Unesco Wazindua Mradi Mpya Wa Kisayansi Utakaosaidia Nchi Kimaendeleo

...


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amesema kuwa mpaka sasa hakuna sera ya sayansi , teknolojia na ubunifu zaidi ya kuwa na sera ya sayansi ilitungwa mwaka 1996 ambayo ndio inatumika kwa sasa.

Prof. Mdoe aliyasema hayo jana mjini Morogoro wakati akizindua mradi wa kuboresha mifumo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswidi (SIDA) kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknololojia pamoja na Tume ya Taifa ya UNESCO.

Alisema kuwa kama nchi na kwa kutambua umuhimu wa sayansi, teknolojia na ubunifu kwa sasa mchakato wa kuandaa sera ya sayansi, teknolojia na ubunifu unaendelea na kwamba wizara iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukamilisha uandaaji wa sera hiyo.

“Covid imetufundisha tuwe tunajitegemea wenyewe kwa kuwekeza kwenye tafiti za kisayansi na kama nchi mradi huu utasaidia tuko wapi na tunaelekea wapi,” alisema Prof. Mdoe.

Awali akitambulisha mradi huo Mkuu wa kitengo cha Sayansi asilia kutoka UNESCO Keven Robert alisema kuwa mradi huo utawezesha kusaidia nchi kuimarisha mifumo ya sayansi, teknolojia na utafiti.

Aidha mradi huo pia utasaidia kuimarisha taasisi za kisayansi kufanya tafiti na kuweka mazingira wezeshi ya kufanya tafiti za kisayansi ambazo zitasaidia katika kutatua changamoto za wananchi, kukabiliana na majanga yakiwemo magonjwa mbalimbali na pia kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Robert alisema kuwa mradi huo utakuwa na maeneo10 ya utekelezaji ambapo baadhi ya maeneo ni pamoja na kuangalia uwekezaji katika tafiti za kisayansi ambapo matokeo ya tafiti hizo zinapouzwa zinaweza kuimarisha uchumi ya nchi.

“Mfano katika kipindi hiki cha janga la Corona yapo mataifa yaliyofanya tafiti za kisayansi na kutengeneza chanjo hivyo zinapouzwa mataifa hayo yamekuwa yakipata fedha na kukua kiuchumi,” alisema Robert.

Alitaja maeneo mengine yatakayoangaliwa katika mradi huo kuwa ni kwa namna gani tafiti za kisanyansi zinasaidia wananchi na kwa namna gani wananchi wanashirikishwa kwenye tafiti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi mkazi wa UNESCO Faith Shayo alisema kuwa mradi huo utakuwa wa awamu mbili na matarajio ya mradi huo ni kuona nchi inazingatia maazimio 10 ambayo yaliazimiwa mwaka 2017 baada ya maazimo ya awali ya mwaka 1974 kufanyiwa maboresho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger