Monday, 5 July 2021

BIDHAA ZA AFRICAB ZAVUTIA WENGI MAONESHO YA SABASABA DAR

...

UWEPO wa viwanda vya vinavyozalisha vifaa mbalimbali vya umeme hapa nchini kikiwemo kiwanda cha Kilimanjaro Cables (AFRICAB) kumesaidia wananchi kutambua ubora wa bidhaa hizo hatua iliyowafanya wengi kutembelea banda la kiwanda hicho liliopo Sabasaba ili kujionea bidhaa zake.

Hayo yamebainishwa na Mratibu na Msimamizi wa mauzo wa kiwanda cha AFRICAB Mhandisi Johnson Mabesa alipokuwa akizungumzia ubora wa bidhaa hizo na mwitikio wa wananchi katika maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Mabesa alisema tofauti na kipindi cha nyuma, kwa sasa kumekuwepo na muamko mkubwa kwa watanzania wanaojitokeza mahali hapo na maeneo mengine ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam kununua bidhaa zao, jambo linaloonyesha wametambua ubora wake wakilinganisha na vifaa vya aina hiyo vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.

“Hakuna ubishi kwamba kwa sasa Tanzania  inazidi kupiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda na hasa upande  huu wa vifaa vya umeme, zamani Serikali ilikuwa inapoteza fedha nyingi kwa kuagiza vifaa kutoka nje ya nchi lakini kwa sasa suala hilo halipo kwa kuwa viwanda vingi  AFRICAB ikiwemo vinafanya vizuri kwa kuzalisha vifaa mbalimbali kwa ubora wa hali ya juu”, amesema Mhandisi huyo

Amesema ubora wa vifaa vinavyozalishwa na kiwanda hicho, siyo unatambulika na wananchi pekee bali hata viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye hivi karibuni alifanya ziara ya kukitembelea kiwanda hicho na kueleza kuridhishwa na ubora wa vifaa inavyovizalisha huku akitoa rai kwa watanzania kuthamini bidhaa za ndani.

Amesema hata ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo miundombinu ya umeme na mengine inayoendelea kujengwa nchini kwa sasa inawezeshwa na vifaa vya umeme vinavyozalishwa na viwanda vya ndani, jambo linaloonyesha wazi kuwa kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo tofauti na miaka ya nyuma.

Amesema kiwanda cha AFRICAB  kinachozalisha nyaya, transfoma na aina zingine za vifaa mbalimbali vya umeme, mbali na kuuza bidhaa zake hapa nchini pia hufanya biashara ya kuuza vifaa hivyo katika nchi mbalimbali ikiwemo Zambia, Malawi, Congo DRC na kwingineko  katika Bara la Afrika.

“Tunazidi kuwahimiza  na kuwakumbusha watanzani kuwa kwa sasa  hakuna ubishi kuwa bidhaa za hapa ndani zina ubora wa hali ya juu kushinda zinazotoka nje ya nchi, tunawakaribisha katika banda letu hapa sabasaba waje kujionea na zaidi tumetoa punguzo maalumu kwa ajili ya sikukuu hii ya sabasaba, hatua hii imelenga kuonyesha kuwa tunawathamini kama watanzania wenzetu” amesema Mhandisi Mabesa











Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger